Francis Atwoli: Je Kiongozi huyu wa Leba anaweza kuwa ndiye tosha katika kipute cha urais Kenya?

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya
- Author, Yusuf Juma na Seif Abdalla
- Nafasi, BBC Swahili
Kenya inapojitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022 viongozi mbali mbali wamejitokeza kutangaza nia ya kumrithi rais Uhuru Kenyatta.
Viongozi hao ni pamoja na naibu wake William Ruto , Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi , Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ,Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula ,kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi miongoni mwa wengine.
Wa hivi punde kujitosa katika kipute hicho ni gavana wa Mombasa Hassan Joho na Aliyekuwa mkuu wa UNCTAD Mukhisa Kituyi .
Francis Atwoli na muungano wa COTU

Chanzo cha picha, Atwoli/Twitter
Hata hivyo kiongozi ambaye jina lake na kauli zake kuhusu siasa za 2022 zimekuwa zikigonga vichwa vya habari na ambaye wengi hawajamchukulia kama anayeweza kuamua atakayechukua usukani ama hata kuchukua usukani mwenyewe ni katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini Kenya COTU Francis Atwoli .
Atwoli amekuwa akitoa kauli zake kuhusu uchaguzi mkuu ujao na hakuna ambaye amekuwa akiweka katika darubini uwezekano wake kujipata katika meza kuu ya uongozi ama ile ya kuamua mrithi wa rais Uhuru Kenyatta .
Kiongozi huyo wa muungano wa wafanyikazi nchini ana historia ya muda mrefu na chama cha Kanu na endapo ataamua kugombea kiti cha urais basi atakuwa na uzito wake na kubadilisha kabisa mkondo wa kisiasa nchini Kenya .

Chanzo cha picha, Atwoli/Twitter
Mwanzo ,Atwoli anatoka magharibi mwa Kenya ambapo jamii ya Waluhya ina idadi kubwa ya watu na wapiga kura ambao akiweza kuwashawishi kuweka kura zao katika kapu moja zitampa ushawishi wa kujadiliana na vigogo wengine wa kisiasa kutoka jamii nyingine za Kenya .
Atwoli pia ana wafuasi wake wengi hasa miongoni mwa vyama vya wafanyakazi na mtandao wake wa kimataifa pia unaweza kumsaidia sana katika kupata raslimali za kufanya kampeini ya kumrithi rais Uhuru Kenyatta .

Chanzo cha picha, Atwoli/twitter
Viongozi wanaowaunga mkono rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekuwa wakionekana kumtegmea sana Atwoli kwa mikutano inayoandaliwa kwake , na semi zake kuhusu mwelekeo wa siasa pia zinaungwa mkono na makundi hayo mawili .
Amenukuliwa akisema kwamba hajui ni nani atakayekuwa rais wa Kenya katika uchaguzi mkuu ujao lakini anajua kwamba Naibu wa rais William Ruto siye atakayekuwa rais ,usemi ambao umemfanya kushambuliwa vikali na washirika wa kisiasa wa Ruto .
Kinachomfanya Atwoli kuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kutumiwa kama mgombeaji wa kushtukiza katika uchaguzi mkuu ujao ni kwamba wagombeaji wengine wakuu wana madhaifu yao mbali mbali ambayo yanawazuia kujitokeza kama watu wenye uwezo na ushawishi huru wa kuendesha kampeini za kuchukua usukani wa serikali .

Atwoli ni nani ?
Francis Lumasayi Atwoli alizaliwa miaka 71 iliyopita katika kaunti ya Kakamega na ndiye kiongozi wa muda mrefu zaidi wa muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini Kenya.
Amekuwa akihudumu katika nafasi hiyo tangu mwaka wa 2001 na uzoefu wake katika masuala ya leba na siasa za Kenya unamfanya kuwa miongoni mwa viongozi wachache wa enzi zake kuwa na utajiri wa ufahamu wa mengi kuhusiana na utawala na mwelekeo wa kisiasa wa Kenya .

Chanzo cha picha, Atwoli/Twitter
Atwoli ametambulika kwa kuwa mtu asiyeficha kusema lililo moyoni mwake na hili limechukuliwa kama ujasiri miongoni mwa wafuasi wake.
Atwoli pia hatopata tatizo la kuuzwa ama kutambulishwa kwa wakenya endapo atajipata katika debe la uchaguzi kwani semi zake na kauli zake kuhusu masuala mbali mbali nchini Kenya kwa miaka mingi zimejulikana na wengi na Sherehe za leba nchini Kenya huwa kama siku yake ya kupewa ukumbi wa kuzungumza na umma .
Tangu kuanza kwa siasa za urithi wa rais Uhuru Kenyatta ,Atwoli amekuwa kama ghundi inayowaleta pamoja viongozi mbali mbali wa kisiasa ambao wanapinga ari ya Ruto kuwa rais n ahata wakati mmoja aliwahi kupendekeza kwamba rais Kenyatta azidishe muda wake uongozini kwani alikuwa na umri 'mdogo' kustaafu muda wake hatamuni utakapokwisha .
Atwoli pia ana bahati kwamba mirengo miwili muhimu ya kisiasa inayowaunga mkono viongozi wakuu -Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga inampa sikio . Misururu ya mikutano ambayo makundi hayo yamekuwa yakifanya imekuwa ikumhusisha Atwoli hatua inayompa nafasi ya kujua n ahata kutoa mwelekeo mwenyewe kuhusu mambo ya siasa .

Chanzo cha picha, Atwoli/Twitter
Ukakamavu wake pia unaweza kumsaidia kuwapiga kumbo viongozi wengine hasa kutoka eneo la magharibi walioonekana hapo mwanzoni kama ndio vogogo wa jamii hiyo .
Iwapo Atwoli atajipata kama mgombeaji wa kutumiwa kama mtu wa 'wastani' katika uchaguzi mkuu ujao ama kujithibitisha kabisa kama muamuzi wa atakayechukua hatamu za serikali ,jukumu na wajibu wake katika siasa za kabla ya kuondoka kwa rais Uhuru haliwezi kupuuzwa .
Francis Atwoli huenda ndiye chambo cha pembeni kinachoweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa siasa za Kenya mwaka mmoja kabla ya Kenya kufanya uchaguzi wake .
Je ,huenda Atwoli ndiye akawa matokeo ama mafao ya mwafaka wa maridhiano(BBI)? Na iwapo hilo litatimia hivyo ,hatma ya wagombeaji wengine waliojitokeza mapema itakuwa gani?












