Mahakama yasema rais Uhuru Kenyatta alikiuka katiba katika kuanzisha mchakato wa BBI Kenya

Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake wa kisiasa, Raila Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Rais Uhuru Kenyatta alitumia nguvu zaidi ya uwezo wake kikatiba alipoanzisha mchakato wa kubadilisha katiba kupitia mpango wa BBI , mahakama kuu mjini Nairobi imeamuru.

Katika uamuzi mkali dhidi ya mchakato huo wa amani nchini Kenya , majaji watano wamesema kwamba rais Uhuru Kenyatta alifanya makosa kadhaa ya kikatiba wakati alipokuwa akianzisha mpango huo wa mabadiliko ya kikatiba.

Mahakama , katika uamuzi uliosomwa kupitia kanda ya video kwa zaidi ya saa nne, imesema kwamba jopo la wanachama 14 lililobuniwa kuongoza mchakato huo lililoongozwa na aliyekuwa seneta wa Garissa , marehemu Yussufu Haji lilikuwa kinyume na sheria .

Majaji hao walioongozwa na Jaji Joel Ngugi walisema kwamba rais alifanya makosa ya kisheria katika kujaribu kubadili katiba , njia ambayo hana uwezo kutumia. Wanasema kwamba angetumia bunge kupitia mwanasheria mkuu kuamua kuhusu mabadiliko yanayohitajika, ulisema uamuzi wa mahakama hiyo.

Kura ya maoni

Mahakama ilisema kwamba hakuna njia nyengine ya kubadili katiba isipokuwa kupitia bunge ama kura ya maoni.

Waliutaja mchakato wote wa BBI kama uliosimamiwa na rais badala ya kusimamiwa na bunge ama raia.

''Rais hawezi kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba , ilisema mahakama ikiongezea kwamba BBI imegubikwa na mgongano wa maslahi''.

Kwa wale waliodai kwamba rais Uhuru Kenyatta alikuwa akichukua hatua hiyo kukuza umoja wa kitaifa, mahakama ilisema kwamba hoja hiyo inamsaliti na ukweli ni kwamba kamati simamizi ya BBI iliundwa na rais na inawajibika kwake.

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga
Maelezo ya picha, Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

''Ukweli ni kwamba mchakato wote wa BBI ni mpango wa rais kitu ambacho ni kinyume na kifungo cha 257 cha katiba. Kamati ilioundwa kusimamia mchakato wote iliundwa kinyume na sheria .Ilikuwa kamati haramu tangu mwanzo'', walisema majaji.

Pia walishutumu hoja kwamba rais mstaafu Mwai Kibaki alianzisha mabadiliko ya kikatiba mwaka 2005 na2010. Majaji hao wanasema kwamba rais Kibaki alifanya hivyo kupitia katiba ya zamani.

Katika katiba ya sasa, walisema kwamba , inasema ni nani anayeweza kuanzisha mpango wa kubadili katiba , walisema.

''Katiba inasema ni nani anayeweza kufanya mabadiliko na rais ama chombo cha serikali sio kati ya wanaopatiwa fursa hiyo''.

Wakuzaji wa BBI waliambia mahakama kwamba rais alikuwa akitumia uwezo wake kikatiba alipoanzisha mchakoto wa BBI.

Lakini mahakama ilisema kwamba bwana Kenyatta alifeli kulinda katiba na hivyobasi akakiuka katiba katika masuala ya uongozi na maadili.

''Huku juhudi zake za kuunganisha taifa zikipongezwa , katika majukumu yake hawezi kuanzisha mpango wowote wa kufanyia marekebisho katiba kinyume na katiba.Hana uwezo kama huo'', mahakama hiyo ilisema.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Waliongezea kwamba mchakato huo tangu mwanzo haukufuata sharia.

Mahakama hiyo pia ilisema kwamba rais aliyepo madarakani anaweza kushtakiwa binafsi iwapo ataenda kinyume na sheria kwa vitendo vyake.

Je umma ulishirikishwa?

Majaji walisema kwamba rais Kenyatta aliorodheshwa kama mtuhumiwa na alishirikishwa katika kesi hiyo hadi mwisho. Hivyobasi kuhusu mahakama hiyo iliamuru kwamba shughuli yote ilikwenda kinyume na sheria kwasababu wakuzaji wa BBI walishindwa kuwashirikisha Wakenya.