Uchaguzi Kenya 2022: Musalia Mudavadi kujiunga na naibu rais William Ruto itabadilisha siasa za Kenya?

Chanzo cha picha, Mudavadi/facebook
- Author, Joseph Kioko
- Nafasi, Mchambuzi Kenya
Haijawahi kutokea katika siasa ya Kenya watu kusubiri tangazo la kisiasa kama lile lililoahidiwa na kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi katika mkutano wa wajumbe wa chama hicho siku ya Jumapili tarehe 23 Januari 2021.
Tangazo hili kwa mujibu wa utabiri wa Mudavadi, lingesababisha tetemeko la ardhi la kisiasa ambalo lingepanga upya na kurekebisha hali ya kisiasa ya nchi tunapojiandaa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022.
Mbali na kuwa kiongozi wa chama cha ANC nchini Kenya , ni miongini mwa viongizi wakuu wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA), ambao ni muungano wa waliokuwa wanachama wakuu wa National Super Alliance (NASA), jukwaa la kampeni ambalo lilitumika katika uchaguzi wa 2017..
Viongozi hao ni pamoja na aliyekuwa Makamu wa Rais Mhe. Kalonzo Musyoka -kiongozi wa chama cha Wiper, Mhe. Seneta Moses Wetangula, kiongozi wa Ford-Kenya na Mheshimiwa Seneta Gideon Moi, kiongozi wa KANU.
Kuundwa kwa OKA kulitokana na kutoaminiana na dhuluma ambazo viongozi hawa waliamini zilisababishwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na mshirika wao wa NASA.
Uongozi wa OKA uliamini kuwa wangeweza kuweka waziwazi njia mbadala ya kisiasa, mbali na siasa zinazodhaniwa kuwa sumu ambazo zilikuwa zikiwazunguka Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.
Kama sehemu ya kujenga moyo wa urafiki na mshikamano miongoni mwa vyama vinavyounda OKA, viongozi wa chama hicho walikubali kuhudhuria na kushuhudia kila mkutano mkuu wa wajumbe wa vyama hivyo (NDC).
Mkutano wa NDC umekuwa chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi katika chama chochote cha siasa ambacho kingewapa viongozi wa chama mamlaka mapya ya kutafuta washirika wapya wa kisiasa katika harakati za kupata urais/mamlaka ya kisiasa. Kwa hivyo walihudhuria mikutano ya NDC ya kila mmoja wao kama walivyokubaliana.
Hivyobasi kwa upande wa ANC, kama ilivyokuwa katika vyama vingine, wakuu wa muungano wa OKA walialikwa na kama kawaida walihudhuria
Je tetemeko la kwanza liliwaathiri wakina nani
Hatahivyo ni wakati wa mkutano huo wa NDC ndiposa zilizala ya kwanza ya kisiasa ilitokea.
Uhudhuriaji wa wanachama wengi wa chama cha UDA na mseneta uliofuatiwa na ujio wa naibu wa Rais William Ruto ambaye ndiye kiongozi wa UDA , uliwashangaza wengi , waliokuwa katika ukumbi wa Bomas n ahata wale waliokuwa wakitazama kupitia vyombo tofauti vya Habari.
Mudavadi kutokana na kuwaalika Naibu Rais William Ruto na waandamizi wake wa UDA aliwaonyesha wana siasa kwamba hakuna kitu cha kudumu isipokuwa maslahi katika siasa.
Alikuwa amedhihirisha kwamba wakati Rais Uhuru na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Naibu Rais William Ruto alikuwa adui wa kisiasa; kwa Wetangula na yeye, William Ruto alikuwa mshirika bora na mwaminifu wa kisiasa na kwa hivyo Rais Uhuru hangeweza kumchagulia marafiki zake wa kisiasa.

Chanzo cha picha, Musalia/facebook
Huku ikiwa imesalia miezi minane kabla ya uchaguzi mkuu, hatua hiyo ya Mudavadi pia imeanzisha kipindi cha rais kilema kisiasa, ambapo uwezo wa Rais anayeondoka madarakani wa kutumia nguvu, kulazimisha au kushawishi miungano ya kisiasa unapungua polepole na kwa kasi.
Wanasiasa wengi huenda wakatiwa moyo na kitendo hiki cha Mudavadi na Wetangula.
Je Hatua hiyo iliathiri vipi Muungano wa OKA?
Kuingia kwa Naibu Rais na wapambe wake pia kulipelekea wakuu wa OKA (Kalonzo na Moi) kuondoka kwenye hafla hiyo. KANU kisha ilitoa taarifa ambayo ilishutumu muungano wa OKA na ANC na washirika wake wapya UDA.
Huku wakuu wawili pekee (Moi na Kalonzo) wakiondoka na wengine wawili wakisalia katika mkutano huo (Mudavadi na Wetangula), tetemeko la pili la kisiasa lilikuwa limetokea; huku chama ambacho kilionekana kuwa mbadala wa tatu kwa Jina OKA ulikuwa unasambaratika.
Uchaguzi Mkuu wa kitaifa bila shaka utakuwa wa mbio za farasi wawili kati ya mrengo wa kisiasa unaomuunga mkono Raila Odinga (Azimio) na mrengo mpya wa kisiasa unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto akiungwa mkono na Musalia Mudavadi na Moses Wetangula.
Wakuu wawili waliosalia OKA kwa hivyo watalazimika kuchagua upande gani wa mgawanyiko wa kisiasa kuunga mkono.
Na je kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga atafaulu bila Mudavadi?
Miungano ya kisiasa nchini Kenya inategemea uungwaji mkono wa kikanda kupitia viongozi wa kikabila/kieneo. Kwa upande wa magharibi mwa Kenya Mhe. Mudavadi na Mhe. Wetangula wamekuwa nguzo thabiti ya msingi kwa usaidizi mkuu wa Rt. Mhe. Raila Odinga kutoka uchaguzi Mkuu wa 2007, 2013 (isipokuwa Mudavadi) na 2017.

Chanzo cha picha, Musalia Mudavadi/facebook
Wawili hawa kwa pamoja walihusika na msaada wa zaidi ya 85% ambao Mhe. Raila Odinga alifanikiwa kupata katika eneo la magharibi na pia katika maeneo mengine yalio na watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Kuondoka kwa vigogo hao wawili kutoka Muungano wa NASA na taarifa yao waliotoa katika mkutano huo wa wajumbe wa chama cha ANC kwamba watatafuta washirika wapya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 , na sio muungano wa Azimio , lilikuwa tetemeko la tatu la siku.
Kufuatia taarifa hiyo , lile ambalo lilionekana kuwa ngome ya Raila , ilibadilika na kuwa eneo ambalo naibu war ais Wiiliam Ruto atapigania kuliweka katika kikapu chake kupitia usaidizi wa Musalia Mudavadi Moses Wetangula.
Kule mashinani, wafuasi wa Naibu Rais Ruto wanahisi kutiwa nguvu baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Musalia na Wetangula .
Kufikia mwisho wa mkutano huo wa NDC, ilikuwa wazi kwamba vyama vya ANC/Ford-Kenya vingeingia katika muungano mpya wa kisiasa na UDA na kwa pamoja vingeendesha mikutano ya kisiasa ili kuwaeleza wafuasi wao kile ambacho mpango huo mpya unamaanisha.
Madhara halisi ya kuendesha mikutano hii ni kuuunda muungano mpya wa kisiasa na pia kudumisha muonekano wa kisiasa kwamba Raila Odinga ndiye anayepoteza majenerali wazuri wa "kisiasa", huku Naibu Rais ndiye anayepata na kusonga mbele.
Kama tunavyojua Siasa ni kuhusu mtazamo, suali ni je,
Mitetemeko hii itasababisha tetemeko kubwa la ardhi kisiasa?…….Ni muda ndio muamuzi













