William Ruto: Muuza kuku aliyepanda ngazi hadi kuwa rais wa Kenya

th

Chanzo cha picha, Getty Images

William Ruto - ambaye ameapishwa kuwa rais mpya wa taifa la kenya alikuwa na maisha ya utotoni ambayo ni mfano wa maisha ya Wakenya wengi maskini.

Alienda shule ya msingi bila viatu, akiwa amevaa jozi yake ya kwanza ya viatu akiwa na umri wa miaka 15. Pia aliuza kuku na karanga kando ya barabara katika maeneo ya mashambani ya Bonde la Ufa.

Kwa hivyo haikushangaza kwamba alijionyesha kama mtetezi wa maskini alipokuwa akiwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Bw Ruto alishindania hilo chini ya bendera ya Kenya Kwanza, kwa ahadi ya kukuza uchumi.

Kiwango rasmi cha ukosefu wa ajira miongoni mwa wale wenye umri wa kati ya miaka 18 na 34 ni karibu 40%, na uchumi hautengenezi ajira za kutosha kunyonya vijana 800,000 wanaojiunga na nguvu kazi kila mwaka.

Kwa hiyo akabuni msemo "Hustler nation" kurejelea vijana wanaohangaika kutafuta riziki.

Bw Ruto ameahidi kuboresha uchumi kuanzia chini kwenda juu kwa jina 'Bottom up' , akisema utawanufaisha maskini ambao wanabeba mzigo mkubwa wa shida ya maisha ambayo imekumba ulimwengu kufuatia janga la coronavirus na vita nchini Ukraine.

Hili lilikuwa jaribio la kwanza kwa Ruto mwenye umri wa miaka 55 kugombea urais, na aliwashangaza wakosoaji wake kwa kupata ushindi - ingawa katika hali ya kushangaza, wajumbe wengi wa tume ya uchaguzi wamekataa matokeo hayo huku kukiwa na madai ya wizi na ugomvi kwenye kituo cha kujumlisha kura cha kitaifa mjini Nairobi.

Hata hivyo mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki kwani alimtangaza Bw Ruto kuwa mshindi kwa kupata asilimia 50.5 ya kura.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Bw Ruto alijiunga na siasa 1992, baada ya kufuata mfano , anasema wa aliyekuwa Rais wa wakati huo Daniel arap Moi.

Bw Ruto alikuwa sehemu ya mrengo wa vijana wa chama cha Bw Moi kilichowahi kutawala zaidi cha Kanu, na alikuwa miongoni mwa wanaharakati waliotwikwa jukumu la kuhamasisha wapiga kura kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini uliofanyika mwaka huo huo.

Ana sifa ya kuwa mzungumzaji mwenye nguvu ambaye alivutia umati mkubwa kwenye mikutano ya hadhara na kuweka utendaji mzuri katika mahojiano ya vyombo vya habari.

Mara nyingi huanza kuzungumza kwa kusema "Rafiki yangu", ambayo humsaidia kupata ukaribu na wapiga kura na kuwapokonya wakosoaji silaha.

Miungano inayobadilika

Baada ya kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri - ikiwa ni pamoja na elimu na kilimo - alipanda hadi naibu rais baada ya uchaguzi wa 2013.

Bw Ruto aligombea uchaguzi huo kama mgombea mwenza wa Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta, na kuwashangaza Wakenya wengi kwa vile walikuwa katika pande tofauti za siasa katika uchaguzi uliopita.

Ulikuwa ni muungano wa manufaa kwa pande zote kwani wote wawili walikuwa wameshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu baada ya kutuhumiwa kuchochea ghasia baada ya uchaguzi uliokuwa na mzozo mkubwa wa 2007, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa.

Katika kura hiyo, Bw Ruto alikuwa amemuunga mkono mgombeaji wa upinzani Raila Odinga - ambaye ameshindwa naye wakati huu - huku Bw Kenyatta akimuunga mkono aliyekuwa Rais Mwai Kibaki katika azma yake ya kuchaguliwa tena.

Muungano wao uliopewa jina la 'bromance' ulizaa matunda huku watu hao wawili wakiingia madarakani, na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuepusha tishio lao na ICC - jambo ambalo walifanikisha wakati upande wa mashtaka ulipoondoa mashtaka dhidi ya Rais Kenyatta mwaka wa 2014 na majaji walitupilia mbali kesi dhidi ya Bw Ruto mnamo 2016.

th

Chanzo cha picha, AFP

Hata hivyo, muungano wao ulivunjika mwaka wa 2018 wakati Bw Kenyatta - katika hatua nyingine ya kushangaza - alipopatana na Bw Odinga, na hivyo kuondoa matumaini ya Bw Ruto kwamba rais anayeondoka angemwidhinisha kama mrithi wake katika kampeni za sasa za uchaguzi.

Washirika wa rais walimshutumu Bw Ruto kwa kukosa utiifu madai ambayo alikanusha, lakini alikiri mpasuko huo kwa kusema kuwa yeye na rais "wanaona siasa tofauti".

Bw Ruto alisalia afisini, hata hivyo, kwa hisani ya vipengee vya kikatiba vinavyohakikisha muda wa kuwa naibu rais.

Katika uchaguzi wa sasa, Bw Kenyatta alimfanyia kampeni vikali Bw Odinga, akisema Bw Ruto "haaminiki" na hawezi kukalia kiti cha juu zaidi cha ardhi.

Bw Ruto alijibu akisema Bw Kenyatta alitaka Bw Odinga amrithi kwa sababu anataka "rais kibaraka".

Katika muda wote wa kampeni, alijionyesha kama "mkorofi", akipambana na kile alichokiona kama jaribio la nasaba mbili za Kenya - akina Kenyatta na Odinga - kung'ang'ania madarakani.

Mmiliki mkubwa wa ardhi na mkulima shupavu

Uaminifu wa kikabila una jukumu kubwa katika siasa za Kenya na Bw Ruto anatoka katika kabila la tatu kwa ukubwa, Wakalenjin, ambalo limetoa rais mwingine mmoja tu, marehemu Bw Moi, ambaye alikuwa mtawala wa muda mrefu zaidi wa Kenya. Yeye sasa, bila shaka, ni mfalme wa kisiasa wa jumuiya.

Bw Ruto ameolewa na Rachael, ambaye alikutana naye mara ya kwanza kwenye mikutano ya vijana wa kanisa.

Wana watoto sita. Mwana wao mkubwa, Nick, aliwahi kubarikiwa na wazee wa Kalenjin, jambo lililochochea uvumi kwamba alikuwa akiandaliwa kwa ajili ya nafasi ya kisiasa, huku binti yao, June, akifanya kazi katika wizara ya mambo ya nje.

th

Chanzo cha picha, KENYA DEPUTY PRESIDENT OFFICE

Bw Ruto ana uchu wa kilimo, jambo ambalo limemfanya kujitosa katika kilimo cha mahindi, maziwa na kuku.

Anamiliki sehemu kubwa ya ardhi magharibi na pwani ya Kenya na pia amewekeza katika sekta ya hoteli

Bw Ruto amekuwa akihusishwa na kashfa za ufisadi serikalini na chanzo cha utajiri wake ni suala la uvumi mwingi.

Mnamo Juni 2013, Mahakama Kuu ilimwamuru kusalimisha shamba la ekari 100 (hekta 40), na kufidia mkulima ambaye alikuwa amemshtaki kwa kunyakua ardhi wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Anakanusha makosa yoyote, na alitoa wito kwa wapiga kura kwa ahadi ya kuwapa fursa ya kuboresha maisha yao, kama alivyofanya.