Hatujapokea mpango wa amani wa Marekani kuhusu Ukraine- Urusi
Mpango huo wa Marekani uliovujishwa, unapendekeza Ukraine ikubali kuachia baadhi ya maeneo ya Donetsk, kupunguza ukubwa wa jeshi, na kutokuwa mwanachama wa NATO mapendekezo yanayoonekana kuipendelea Urusi.
Muhtasari
- Waasi wanaohusishwa na Dola la Kiislamu waua raia 89 DR Congo
- Uefa yawaamuru mashabiki wa Scotland kuondoa video za sherehe za ushindi
- Urusi haijapokea mpango wowote wa amani wa Marekani kuhusu Ukraine
- Palmer wa Chelsea avunjika kidole cha mguu baada ya kujigonga na mlango
- Viongozi wa G20 waanza kukusanyika Afrika Kusini huku Trump akisusia
- Pogba kurejea uwanjani wikiendi hii kwa mara ya kwanza tangu afungiwe
- Tetemeko la ardhi laua watano na kujeruhi karibu 100
- Mshiriki aliyeondoka katika shindano la ulimbwende ashinda
- Serikali ya Tanzania kutoa majibu kwa makala ya CNN juu ya mauaji wakati wa uchaguzi
- Venezuela yasema Machado atahesabiwa amekimbia nchi ikiwa atawenda kupokea tuzo ya Nobel
- Wanaume waliojifanya ni maafisa wa benki kuu waiba dola 800,000 mchana
- Wanafunzi wengine watekwa nyara Nigeria
- DRC na Rwanda zajadili awamu ya pili ya operesheni za kuondoa FDLR
- Mzozo wa Tigray: Kenya yaripotiwa kusuluhisha mgogoro kati ya Abiy na Isaias
- Australia inapiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya miaka 16
- Wanawake wa Afrika Kusini watoa wito wa maandamano kupinga ukatili wa kijinsia
- Kiongozi wa vuguvugu la kujitenga nchini Nigeria ahukumiwa kifungo cha maisha kwa ugaidi
- Trump anasema ujumbe wa Democrats kwa wanajeshi ni kitendo cha uasi kinachoweza kuadhibiwa kwa kifo
- Watu 41 wafariki kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Vietnam
- Zelensky kuzungumza na Trump baada ya Marekani kupendekeza mpango wa amani kati ya Urusi na Ukraine
Moja kwa moja
Rashid Abdallah
Waasi wanaohusishwa na Dola la Kiislamu waua raia 89 DR Congo

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) wakipiga doria dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) karibu na Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini, Desemba 31, 2013. Waasi wanaohusishwa na Islamic State wamewaua raia 89 katika mashambulizi mengi katika eneo la Lubero mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati, kinachojulikana kama MONUSCO, kimesema Ijumaa.
Mashambulizi hayo yalitekelezwa na wapiganaji wa Allied Democratic Forces (ADF) katika maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu Kaskazini kati ya Novemba 13 na Novemba 19, na 89 waliouawa ni pamoja na wanawake 20 na idadi isiyojulikana ya watoto, imesema MONUSCO katika taarifa.
Katika moja ya mashambulizi hayo, waasi hao walishambulia kituo cha afya kinachoendeshwa na Kanisa Katoliki huko Byambwe, na kuua watu wasiopungua 17 wakiwemo wanawake waliokuwa wamekwenda kupata huduma ya uzazi na kuzichoma moto wodi nne za wagonjwa.
Pia waasi hao wamefanya utekaji nyara na uporaji wa vifaa vya matibabu, imesema ripoti hiyo.
"MONUSCO inaitaka Congo kuanzisha uchunguzi huru na wa kuaminika mara moja ili kuwabaini wahusika na washirika wa mauaji haya na kuwafikisha mahakamani," ilisema taarifa hiyo.
Maafisa wa eneo hilo wameliambia shirika la habari la Reuters, mwezi uliopita watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa ADF wamewaua raia 19 katika shambulio la usiku katika kijiji cha Mukondo katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Mwezi Septemba, ADF ilidai kuhusika na moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika miezi ya hivi karibuni ambayo yaligharimu maisha ya zaidi ya raia 60 katika mazishi mashariki mwa Congo.
ADF walianza uasi nchini Uganda lakini wameweka makao yake katika misitu ya nchi jirani ya Congo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, na wametangaza utiifu kwa Islamic State.
Jeshi la Congo na vikosi vya Uganda hufanya operesheni dhidi ya ADF, lakini mashambulizi ya kundi hilo yanaendelea.
Maeneo mengine ya jimbo la Kivu Kaskazini yako chini ya udhibiti wa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda baada ya kuyateka mwaka huu.
Wapatanishi wakiwemo Marekani na Qatar wanajaribu kuleta amani katika mzozo huo, ambao Washington inatumai kuwa utawezesha uwekezaji wa nchi za Magharibi katika sekta ya madini.
Pia unaweza kusoma:
Uefa yawaamuru mashabiki wa Scotland kuondoa video za sherehe za ushindi

Chanzo cha picha, PA Media
Maelezo ya picha, Scotland iliishinda Denmark katika ushindi wa 4-2 na kufuzu Kombe la Dunia Mashabiki wa Scotland wameikosoa Uefa baada ya video za mashabiki wao wakiisherehekea timu yao kufuzu Kombe la Dunia kuondolewa kwenye mitandao ya kijamii.
Chama cha Wafuasi wa Soka cha Scotland (SFSA) kilipokea barua pepe kutoka kwa bodi inayosimamia soka ya Ulaya ikisema kuwa mashabiki wamechapisha video zinazoonyesha mchezo wa Scotland v Denmark kwenye X bila ruhusa.
Ni mechi ya Jumanne usiku, ambapo Scotland ilipata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1998.
Video nyingi zimeondolewa kwa sababu ya ukiukaji wa hakimiliki na akaunti ya SFSA pia imefungwa.
Mwanzilishi mwenza wa SFSA Paul Goodwin alitilia shaka haki ya dai hilo.
Alisema: “Ni vigumu kuamini kuwa Uefa wameishiwa nguvu kiasi cha kuitaka X iondoe picha za mashabiki waliokuwa na furaha kwenye baa za Glasgow, Stirling na Dundee ambako baadhi ya wanachama wetu walikuwa wakisherehekea jioni hiyo tukufu kwa taifa.
Scotland ilifuzu kwenda Kombe lao la Dunia mara ya kwanza 1998 kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Denmark huko Hampden.
Uefa huondoa mara kwa mara video za YouTube kwa sababu ya sheria kali za hakimiliki.
Bodi hiyo inayosimamia soka la Ulaya inamiliki haki za matangazo kwa mechi zake na kwa ujumla linazuia kweka video za mechi kwa chaneli zisizo rasmi na za mashabiki.
Urusi haijapokea mpango wowote wa amani wa Marekani kuhusu Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imesema haijapokea rasmi mpango wa amani kutoka Marekani, licha ya Rais Zelensky kusema yuko tayari kufanya kazi na serikali ya Trump kumaliza vita.
Mpango huo wa Marekani, uliovujishwa, unapendekeza Ukraine ikubali kuachia baadhi ya maeneo ya Donetsk, kupunguza ukubwa wa jeshi, na kutokuwa mwanachama wa NATO mapendekezo yanayoonekana kuipendelea Urusi.
Zelensky hakuyakataa moja kwa moja mapendekezo hayo, akisema anathamini juhudi za Trump kurejesha usalama barani Ulaya. Ofisi yake ilisema mpango huo unaweza kufufua diplomasia, na Zelensky atazungumza na Trump hivi karibuni.
Wakati huohuo, Urusi inaendelea na mashambulizi na kuripoti mafanikio madogo mashariki mwa Ukraine, huku Ukraine ikikabiliwa na kashfa ya ufisadi inayohusisha maofisa wakuu. Marekani imekanusha madai kuwa Ukraine ilitengwa katika maandalizi ya mpango huo, ikisema mazungumzo na afisa Rustem Umerov yalichangia marekebisho muhimu.
Kremlin imesema bado haijapokea chochote rasmi kutoka Marekani lakini milango iko “wazi kwa mazungumzo ya amani,” ingawa inaendelea kushikilia madai ambayo Ukraine huyaona kama masharti ya kujisalimisha.
Palmer wa Chelsea avunjika kidole cha mguu baada ya kujigonga na mlango

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Cole Palmer hajacheza tangu Chelsea iliposhindwa na Manchester United tarehe 20 Septemba Mchezaji wa Chelsea, Cole Palmer hatakuwepo uwanjani kwa wiki nyingine baada ya kuvunjika kidole cha mguu alipokibamiza na mlango siku ya Jumatano usiku.
Mshambulizi huyo wa kimataifa wa Uingereza alitarajiwa kuanza tena mazoezi ya kikosi cha kwanza wiki hii baada ya kuwa nje kwa miezi miwili kutokana na jeraha la paja.
Lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 atakaa nje kwa muda mrefu zaidi kwa sababu ya jeraha la kidole kidogo cha mguu wake wa kushoto.
Atakosa mechi tatu zijazo za The Blues - mechi ya Jumamosi ya Ligi Kuu ya Uingereza huko Burnley, mechi ya Jumanne ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona na mechi ya wikendi ijayo nyumbani dhidi ya Arsenal.
Meneja wa Chelsea Enzo Maresca amesema, "kwa bahati mbaya, alipata ajali nyumbani ambapo alikigonga kidole chake cha mguu. Hatarejea wiki ijayo."
Mechi ya mwisho ya Palmer ni wakati Chelsea ilipochapwa 2-1 na Manchester United tarehe 20 Septemba.
The Blues wamecheza michezo 11 katika mashindano yote tangu wakati huo - wakishinda nane na kupoteza miwili - na kushika nafasi ya tatu kwenye jedwali la Ligi Kuu England.
Viongozi wa G20 waanza kukusanyika Afrika Kusini huku Trump akisusia

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amewasili Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa mkutano wa viongozi wa dunia katika mkutano wa kila mwaka wa G20.
Mkutano huo unazileta pamoja nchi 20 zenye uchumi mkubwa, ingawa Donald Trump wa Marekani, ameamua kutohudhuria kutokana na madai yake ya uongo kuwa Wazungu wananyanyaswa nchini humo.
Sir Keir, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wanatarajiwa kuzungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky baadaye kando ya mkutano huo.
Trump hatahudhuria mkutano huo, baada ya kutangaza kuwa ni "aibu kubwa" katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, na kurudia madai yake ya uongo kwamba Waafrika Wazungu wanateswa nchini Afrika Kusini.
Wazungu wa Afrika Kusini wamepewa hadhi ya ukimbizi nchini Marekani na utawala wa Trump, na kwa sasa wanapewa kipaumbele kuliko watu wengine.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema kutokuwepo kwa Marekani katika G20 ni "hasara" na kuongeza kuwa "siasa za kususia hazifanyi kazi."
Hakuna chama hata kimoja kati ya vyama vya siasa nchini Afrika Kusini - ikiwa ni pamoja na vile vinavyowakilisha Waafrikana na jumuiya ya wazungu - vimedai kuwepo kwa mauaji ya kimbari nchini Afrika Kusini.
Pogba kurejea uwanjani wikiendi hii kwa mara ya kwanza tangu afungiwe

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Paul Pogba alisaini mkataba wa miaka miwili na Monaco msimu uliopita Kiungo wa kati wa Monaco, Paul Pogba anatarajiwa kurejea uwanjani wikiendi hii baada ya kupigwa marufuku kwa kutumia dawa za kusisimua misuli.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alijiunga na klabu hiyo ya Ligue 1 msimu uliopita wa kiangazi, baada ya marufuku yake ya miaka minne kwa kutumia dawa za kusisimua misuli kupunguzwa hadi miezi 19 na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (Cas).
Mara ya mwisho Pogba kucheza mechi ni Septemba 2023, alipoichezea Juventus katika mechi ya Serie A dhidi ya Empoli.
Pogba sasa anatarajiwa kutajwa kwenye kikosi cha Monaco kitakachomenyana na Rennes siku ya Jumamosi.
Alipigwa marufuku kutojihusisha na soka mwezi Februari 2024, kufuatia kipimo cha dawa za kuongeza nguvu mwilini mwezi Agosti 2023.
Pogba alijitetea kuwa hilo lilikuwa kosa la kupewa dawa bila kujua ilikuwa na kemikali iliyopigwa marufuku.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, mshindi wa Kombe la Dunia 2018, aliruhusiwa kurejea kwenye soka mwezi Machi kufuatia uamuzi wa kupunguza marufuku yake.
Iwapo Pogba atacheza mechi yake ya kwanza ya Monaco dhidi ya Rennes, itakuwa ni mechi yake ya kwanza kabisa ya Ligue 1.
Akitokea Manchester United Pogba alijiunga na Juventus kwa uhamisho wa bure mwaka 2012, kabla ya kurejea Old Trafford kwa pauni milioni 89m miaka minne baadaye.
Alirejea Juventus baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa miaka sita na United mwaka 2022, lakini alicheza mechi 12 pekee kabla ya mkataba wake kukatishwa.
Pogba alifunga katika fainali wakati Ufaransa ilipoilaza Croatia 4-2 katika fainali ya Kombe la Dunia 2018.
Pia unaweza kusoma:
Tetemeko la ardhi laua watano na kujeruhi karibu 100

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wakaazi wamesimama kwenye kichochoro baada ya kuondoka kwenye nyumba zao kufuatia tetemeko la ardhi huko Dhaka, Bangladesh, Novemba 21, 2025. Takriban watu watano, ikiwa ni pamoja na mtoto, wamefariki na karibu 100 kujeruhiwa wakati tetemeko la ardhi la kipimo cha 5.7 lilipopiga Bangladesh siku ya Ijumaa, serikali imesema, na majengo kuharibiwa katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Dhaka.
Mitetemeko ilisikika katika majimbo ya mashariki katika nchi jirani ya India ambayo inapakana na Bangladesh, lakini hakukuwa na ripoti za uharibifu mkubwa, imesema serikali.
Muhammad Yunus, mkuu wa serikali ya mpito ya Bangladesh amesema waliojeruhiwa ni pamoja na wanafunzi wa chuo kikuu cha Dhaka, wafanyakazi wa kiwanda katika mji wa Gazipur na wakaazi wa Narsingdi, kitovu cha tetemeko hilo.
Majeruhi kadhaa waliopelekwa hospitalini kutoka Narsingdi, yapata kilomita 40 (maili 25) mashariki mwa Dhaka, walikuwa katika hali mbaya, mshauri wa afya Nurjahan Begum aliwaambia waandishi wa habari.
Wakazi wa Dhaka walikimbia kutoka katika nyumba zao huku majengo yakitetemeka na baadhi ya majengo yalipoporomoka, mashahidi wameliambia shirika la habari la Reuters.
Idara ya zimamoto imesema baadhi ya watu wamejeruhiwa wakati matofali na zege zilipoanguka kutoka katika majengo yaliyokuwa yakijengwa.
Serikali inafuatilia kwa karibu tukio hilo na imeiagiza Idara ya zimamota kuimarisha shughuli za uokoaji katika maeneo yaliyoathiriwa, ofisi ya Yunus ilisema katika taarifa hiyo.
Pia unaweza kusoma:
Mshiriki aliyeondoka katika shindano la ulimbwende ashinda

Chanzo cha picha, Getty Images
Mlimbwende kutoka Mexico, Fatima Bosch ametawazwa kuwa Miss Universe katika hafla iliyofanyika Bangkok, Thailand kuashiria mwisho wa msimu wa mashindano hayo yaliyojaa vimbwanga.
Mshiriki huyo mwenye umri wa miaka 25 aliondoka katika hafla hiyo mapema mwezi Novemba baada ya afisa wa Thailand kumkemea hadharani mbele ya makumi ya washiriki na kutishia kuwaondoa katika shindano wale wanaomuunga mkono.
Tukio hilo la kushangaza lilikuja wiki moja baadaye na kujiuzulu kwa majaji wawili, ambapo mmoja wao aliwashutumu waandaaji kwa kulihujumu shindano hilo.
Haya yanajiri huku shindano hilo lililodumu kwa muda mrefu zaidi duniani likikabiliwa na maswali kuhusu umuhimu wake na kupungua kwa hadhira.
Matokeo ya hivi punde ya shindano hilo yameongeza utata, huku habari za ushindi wa Miss Mexico zimeleta maoni mseto mtandaoni.
Wamexico wengi wanasherehekea ushindi wake. Lakini wengine wamejiuliza ikiwa waandaaji walimpa taji ili kufidia kashfa ya awali.
Miss Thailand Praveenar Singh alishika nafasi ya pili huku Miss Venezuela Stephany Abasali akishika nafasi ya tatu, akifuatiwa na Miss Ufilipino Ma Ahtisa Manalo na Miss Cote d'Ivoire Olivia Yace.
Pia unaweza kusoma:
Serikali ya Tanzania kutoa majibu kwa makala ya CNN juu ya mauaji wakati wa uchaguzi

Chanzo cha picha, AP
Maelezo ya picha, Waandamanaji katika mitaa ya Arusha, Tanzania, siku ya uchaguzi, Jumatano, Oktoba 29, 2025. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema imefuatilia makala iliyochapishwa na chombo cha habari cha CNN kutoka Marekani kuhusu matukio ya tarehe 29 Oktoba, 2025 na siku zilizofuata.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika mitandao ya kijamii, imesema, “tunachambua na kuhakiki maudhui yaliyomo katika makala hiyo na tamko la Serikali litakuja baada ya kukamilika kwa uhakiki huo.”
Makala ya uchunguzi ya CNN, iliyopeperushwa leo inaangazia kuhusika kwa vikosi vya usalama nchini Tanzania katika mauaji ya waandamanaji kuanzia siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29.
Makala hiyo imefichua uwezekano wa uwepo wa makaburi ya halaiki, kupitia uchunguzi wa video, picha za satalaiti, na kuzungumza na zaidi ya Watanzania 100.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema, yanasema zaidi ya watu 1000 waliuawa kuanzia Oktoba 29, huku serikali ya Tanzania ikiwa bado haijatoa idadi ya waliouawa licha ya kukiri watu walipoteza maisha.
Siku ya jana Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan alizindua tume ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi, na matokeo ya ripoti hiyo yanatarajiwa kuanza kutolewa miezi mitatu ijayo.
Pia unaweza kusoma:
Venezuela yasema Machado atahesabiwa amekimbia nchi ikiwa atawenda kupokea tuzo ya Nobel

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, María Corina Machado amekuwa mafichoni tangu mwanzo wa mwaka Kiongozi wa upinzani wa Venezuela atahesabiwa kuwa 'amekimbia nchi' ikiwa atasafiri kwenda Norway kuchukua tuzo yake ya Amani ya Nobel, mwanasheria mkuu wa taifa hilo amesema.
Tarik William Saab ameliambia shirika la habari la AFP kwamba María Corina Machado - ambaye amekuwa akiishi mafichoni ili kukwepa kukamatwa - anashutumiwa kwa "vitendo vya kula njama, kuchochea chuki na ugaidi."
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 58 alishinda tuzo hiyo mwezi Oktoba, akipongezwa kwa juhudi zake za kupigia debe "mabadiliko kwa njia amani kutoka kwenye udikteta na kwenda kwenye demokrasia."
Kwa muda mrefu ameishutumu serikali ya Rais Nicolás Maduro kuwa ya "wahalifu" na kuwataka raia wa Venezuela kuungana ili kuiondoa. Mataifa mengine yanauona utawala wa Maduro kuwa si halali.
Machado - ambaye kwa muda mrefu amekuwa mmoja wa watu wanaoheshimika katika upinzani wa Venezuela - alizuiwa kugombea katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana, ambapo Maduro alishinda muhula wa tatu wa miaka sita madarakani.
Uchaguzi huo ulikosolewa kwa kiasi kikubwa katika jukwaa la kimataifa kuwa haukuwa huru na wa haki, na ulizusha maandamano kote nchini.
Licha ya kuzuiwa kwake, Machado aliweza kuunganisha upinzani wa Venezuela ili kumuunga mkono mrithi wake kwenye uchaguzi, Edmundo González.
Baraza la Taifa la Uchaguzi linalodhibitiwa na serikali lilimtangaza Madurulo kuwa mshindi - ingawa hesabu kutoka vituo vya kupigia kura zilionyesha González alishinda kwa kishindo.
González baadaye alikimbilia Uhispania, akihofia ukandamizaji, kufuatia majaribio ya kuwaweka kizuizini maafisa wengine wa upinzani.
Kamati ya Nobel, wakati inamtangaza katika Taasisi ya Nobel ya Norway huko Oslo, ilimsifu Machado kama "ni mifano wa kuvutia wa ujasiri wa raia katika Amerika ya Kusini."
Mwenyekiti wa Nobel Jørgen Watne Frydnes alisema wakati huo anatumai Machado ataweza kuhudhuria hafla ya tuzo huko Oslo Disemba 10, lakini anaelewa hali mbaya ya usalama anayokabiliana nayo.
Miongoni mwa viongozi waliompongeza wakati huo ni Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye pia alikuwa anawania tuzo hiyo huku mivutano yake na serikali ya Maduro ikizidi kuongezeka.
Mwanasheria Mkuu Saab pia amesema Machado yuko chini ya uchunguzi kwa kusaidia kutumwa vikosi vya kijeshi vya Marekani katika Caribbean.
Utawala wa Trump ameanzisha mashambulizi yanayolenga boti za mihadharati, katika visiwa vya Caribbean, ambaozo inazishutumu kusafirisha dawa za kulevya kutoka Amerika Kusini hadi Marekani. Zaidi ya watu 80 wameuawa, wengi wao wakiwa raia wa Venezuela.
Trump amemshutumu Maduro kwa kuwa kiongozi wa shirika la kuuza dawa za kulevya, jambo ambalo kiongozi huyo wa Venezuela amelikanusha.
Maduro anamshutumu Trump kwa kujaribu kuanzisha vita ili kupata udhibiti wa hifadhi ya mafuta ya Venezuela, lakini hivi karibuni alisema yuko tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wawakilishi wa utawala wa Trump.
Pia unaweza kusoma:
Wanaume waliojifanya ni maafisa wa benki kuu waiba dola 800,000 mchana

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Polisi wameanzisha msako mkali kuwatafuta watu hao Watu wenye silaha waliojifanya ni maafisa kutoka benki kuu ya India wameiba rupia milioni 70 sawa na dola za kimarekani 800,000 katika gari lililokuwa likisafirisha pesa hizo katika jimbo la kusini la Karnataka, wanasema polisi.
Operesheni kubwa imeanzishwa kuwatafuta wanaume hao walioiba katikati mwa jiji la Bengaluru.
Wizi huo ulitokea Jumatano mchana. Wanaume sita waliokuwa kwenye gari la SUV walilisimamisha gari la kubeba pesa kwenye barabara yenye magari mengi lilipokuwa likisafirisha pesa kati ya matawi ya benki, kamishna wa polisi wa Bengaluru Seemant Kumar Singh aliambia BBC.
Gari hilo lilikuwa limembeba dereva, mtunza pesa na walinzi wawili wenye silaha.
Bw Singh anasema majambazi hao waliwaambia watu waliokuwa kwenye gari hilo kuwa wao ni maafisa kutoka Benki Kuu ya India na walihitaji kuthibitisha ikiwa wana hati sahihi za kusafirisha kiasi hicho kikubwa cha pesa.
Genge hilo liliwaambia Walinzi waache silaha zao kwenye gari na kuingia kwenye SUV, wakati dereva akiagizwa kuendelea kuendesha gari hilo, polisi wanasema.
Gari hilo aina ya SUV lililifuata gari la pesa kwa kilomita chache kabla ya genge hilo kumlazimisha dereva kutoka nje ya gari hilo, na kumlazimisha mlinzi wa pesa na walinzi kutoka nje ya SUV, na kuhamisha pesa hizo kwa mtutu wa bunduki, na kukimbia.
Eneo hilo lina kamera chache za CCTV, na polisi wanachunguza ikiwa genge hilo lilitumia magari mengine katika operesheni hiyo.
Kampuni ya huduma ya uchukuzi wa pesa imefungua kesi polisi.
Gari hilo aina ya SUV lililotumika katika wizi huo lilikuwa na nambari bandia za usajili na kibandiko kinachosomeka "Serikali ya India," afisa wa polisi aliiambia BBC kwa sharti la kutotajwa jina.
Afisa huyo aliongeza kuwa polisi pia wanachunguza ikiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wana uhusiano wowote na wizi huo.
Waziri Mkuu wa jimbo la Karnataka, Siddaramaiah amewaambia waandishi wa habari polisi wamelipata gari la SUV lililotumika katika wizi huo.
Lakini Waziri wa Mambo ya Ndani, G Parameshwara amesema bado haijabainika ni gari gani washukiwa walilitumia kutoroka.
"Imethibitishwa kuwa walibadilisha magari na kuhamisha pesa," aliwaambia wanahabari.
Alisema ana imani polisi watashughulikia kesi hiyo, kama walivyofanya katika matukio mengine ya wizi wa benki huko Karnataka.
Mwezi Mei, kilo 59 za dhahabu zenye thamani ya rupia milioni 532.6 ziliibiwa kutoka benki ya wilaya ya Vijayapura kwa kutumia ufunguo unaofanana.
Polisi walifanikiwa kupata kilo 39 za dhahabu na pesa taslimu, na kuwakamata watu 15, wakiwemo wafanyakazi wawili wa zamani.
Pia unaweza kusoma:
Wanafunzi wengine watekwa nyara Nigeria

Chanzo cha picha, Twitter
Serikali ya jimbo la kati la Niger nchini Nigeria inasema watu wenye silaha wamewateka nyara wanafunzi na wafanyakazi katika shule ya bweni ya Wakatoliki.
Wakazi katika jamii ya Papiri wanaamini karibu wanafunzi na wafanyakazi 100 wamechukuliwa wakati watu wenye silaha walipovamia Shule ya St Mary's mapema Ijumaa.
Shule hiyo, inayoendeshwa na Kanisa Katoliki, ilishambuliwa majira saa nane usiku kwa saa za huko.
Polisi wanasema "majambazi wenye silaha walivamia shule na kuwateka nyara wanafunzi kutoka hosteli yao," na kuongeza kuwa vitengo vya polisi, wanajeshi na mashirika mengine ya usalama "wanapiga msako katika msitu kwa lengo la kuwaokoa wanafunzi waliotekwa nyara."
Serikali ya jimbo la Niger imethibitisha kwamba mashirika ya usalama yameanzisha "uchunguzi" lakini haikubainisha ni wanafunzi wangapi wamepotea.
Serikali ya Jimbo hapo awali ilitoa agizo la kusimamishwa shughuli zote za ujenzi na kuagiza kufungwa kwa muda kwa shule zote za bweni ndani ya eneo lililoathiriwa kama hatua ya tahadhari.
“Kwa bahati mbaya, Shule ya St Mary iliendelea na shughuli zake na kuendelea na masomo bila ya kutoa taarifa au kuomba kibali kutoka kwa Serikali ya Jimbo, na hivyo kuwaweka wanafunzi na wafanyakazi katika hatari inayoweza kuepukika," imesema serikali ya jimbo hilo.
Utekaji nyara huu unakuja siku tano tu baada ya zaidi ya wasichana 20 wa shule kutekwa nyara katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Serikali katika jimbo jirani la Kebbi. Tukio ambalo limesababisha huzuni kitaifa na mjadala mpya kuhusu uwezo wa Nigeria kulinda shule zake.
Wakati huo huo Nigeria bado inaomboleza shambulio la Jumanne usiku kwenye kanisa katika jimbo la Kwara, ambapo watu wenye silaha waliwaua watu wawili na kuwateka nyara wengine kadhaa.
Baada ya shambulio hilo Serikali ya jimbo la Kwara imefunga zaidi ya shule 50 katika baadhi ya wilaya za vijijini kama tahadhari.
Pia unaweza kusoma:
DRC na Rwanda zajadili awamu ya pili ya operesheni za kuondoa FDLR

Chanzo cha picha, WHITEHOUSE
Maelezo ya picha, Mfumo wa Uratibu wa Usalama wa Pamoja unaendelea kukutana mjini Washington kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini Juni (6) mwaka huu kati ya Olivier Nduhungirehe wa Rwanda (kushoto) na Thérèse Kayikwamba wa DR Congo, ambayo yalipokelewa na Rais Donald Trump (katikati). Serikali ya Marekani imetangaza kuwa mkutano wa nne wa Kikundi cha Usimamizi wa Pamoja (Joint Steering Group – JSG) juu ya utekelezaji wa Makubaliano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda ulifanyika Washington DC siku ya Jumatano na Alhamisi, ukilenga kujadili awamu ya pili ya utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa Juni mwaka huu.
Mikutano hii inahusisha kikundi kinachojulikana kama Mfumo wa Kuratibu Usalama wa Pamoja (Joint Security Coordination Mechanism – JSCM), likijumuisha wawakilishi wa DRC, Rwanda, Marekani, Togo, na Umoja wa Afrika.
Lengo ni kutekeleza mpango wa kuondoa kundi la FDLR, linalopinga serikali ya Kigali, na kushughulikia hatua za usalama zilizochukuliwa na Rwanda, kama ilivyokubaliwa kwenye makubaliano.
Washington imesema kuwa duru ya awali ya mikutano ya JSCM ilijumuisha kubadilishana taarifa za kijasusi na kutoa taarifa kuhusu jitihada za serikali ya DRC za kuwashawishi wanachama wa FDLR kuacha silaha na kurudi nyumbani.
Kauli ya pamoja iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema kuwa mkutano wa nne wa JSCM uliofanyika siku mbili zilizopita ulianza kujadili awamu ya pili ya mpango huu, ikiwemo utekelezaji wa kuondolewa kwa FDLR na kufutwa kwa hatua za kizuizi zilizochukuliwa na Rwanda.
Katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali katika Wilaya ya Walikale, Mkoa wa Kivu Kaskazini, kumekuwa na ripoti za vikosi vya serikali vikihimiza wapiganaji wa FDLR kuacha silaha, kujisalimisha kwa MONUSCO, na kurudishwa nyumbani.
Serikali ya Rwanda inaishutumu Kinshasa kwa kusaidia harakati za FDLR, madai ambayo Kinshasa inakataa.
Kuhusu kufutwa kwa hatua za usalama zilizochukuliwa na Rwanda, serikali ya Kinshasa inaeleza kuwa ni “Rwanda ikiondoka na majeshi yake kutoka kwenye eneo la Kongo”, ambapo inadai walifika kusaidia harakati za M23.
Umoja wa Mataifa, Kinshasa, na baadhi ya nchi za Magharibi wanasema hawana shaka kuwa Rwanda ilituma majeshi kusaidia M23, jambo ambalo serikali ya Rwanda inakataa.
Hayo yakijiri, mapigano makali kati ya harakati za M23 na wapiganaji wa Wazalendo walioko pamoja na vikosi vya serikali yameongezeka hivi karibuni katika Wilaya ya Masisi, hasa katika maeneo ya Osso Banyungu na Katoyi, yanayopakana na Wilaya ya Walikale.
Kila upande unashutumu lingine kwa kushambulia na kutoheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa Doha, huku mazungumzo ya makubaliano ya amani ya kudumu yakiendelea.
Soma Zaidi:
Mzozo wa Tigray: Kenya yaripotiwa kusuluhisha mgogoro kati ya Abiy na Isaias

Maelezo ya picha, Kauli na hotuba zinazotolewa na maafisa wa Ethiopia na Eritrea zinaambatana na matusiano ya maneno ambayo yanaweza kuwapeleka kwenye vita. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy anaripotiwa kuiomba Kenya kusuluhisha mvutano unaoongezeka kati yao na Eritrea kuhusu msukumo wa taifa lake kupata ufikiaji wa Bahari Shamu.
Kwa mujibu wa chombo cha habari binafsi, Ethio Forum, kilichoripoti tarehe 19 Novemba mwaka huu, Rais William Ruto inasemekana alituma ujumbe maalumu kwenda Asmara.
Ujumbe huo wa Kenya, unaodaiwa kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Taifa (NIS), Noordin Haji, ulifanya mazungumzo na Rais Isaias pamoja na maafisa wengine wa serikali.
Ethio Forum iliripoti kwamba, “Rais wa Eritrea anaripotiwa kuomba agano [kutoka kwa msuluhishi],” ikinukuu vyanzo vya kidiplomasia visivyotajwa majina.
Iliongeza kwamba vyanzo hivyo vilisema Abiy alimpigia Ruto simu wiki mbili zilizopita kuomba msaada wake.
Waziri Mkuu alinukuliwa akisema: “Siko tayari kwenda vitani na Eritrea. Yeye [Isaias] anapaswa kusitisha maandalizi yake [ya vita]. Najua anajiandaa kuanzisha vita dhidi yangu [Ethiopia].”
Hadi sasa, hakuna upande wa Eritrea wala Ethiopia uliotoa maoni kuhusu taarifa hizo.
Madai ya Ethiopia kuhusu bandari ya Assab nchini Eritrea yameibua hofu ya kutokea kwa vita kati ya mataifa hayo jirani.
Bandari ya Assab ilikuwa lango kuu la biashara la Ethiopia kabla ya Eritrea kujipatia uhuru mwaka 1993 na kukatisha upatikanaji huo.
Soma pia:
Australia kupiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya miaka 16

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuanzia tarehe 10 Desemba, kampuni za mitandao ya kijamii zitakuwa na wajibu wa kuchukua "hatua zinazofaa" kuhakikisha kwamba watoto wenye umri chini ya miaka 16 nchini Australia hawawezi kuanzisha akaunti kwenye majukwaa yao na kwamba akaunti zilizopo zifutwe au kuzimwa.
Serikali inasema marufuku hiyo, sera ya aina yake duniani iliyopendwa na wazazi wengi, inalenga kupunguza "shinikizo na hatari" ambazo watoto wanaweza kukabiliana nazo kwenye mitandao ya kijamii, zinazotokana na "vipengele vya muundo vinavyowahamasisha kutumia muda mwingi kwenye skrini, huku pia vikionesha maudhui yanayoweza kuharibu afya na ustawi wao."
Utafiti ulioagizwa na serikali mwanzoni mwa mwaka huu ulionesha kuwa asilimia 96 ya watoto wenye umri wa miaka 10-15 walitumia mitandao ya kijamii na kwamba saba kati ya kumi kati yao walikuwa wamethibitishwa kuathirika na maudhui na tabia hatarishi.
Tabia hizi zilijumuisha kutoka kwenye maudhui ya ubaguzi dhidi ya wanawake, video za mapigano, hadi maudhui yanayohimiza matatizo ya kula na kujiua.
Mtoto mmoja kati ya saba pia aliripoti kuathirika na tabia za ukandamizaji kutoka kwa watu wazima au watoto wakubwa, na zaidi ya nusu walisema kuwa walikuwa wahanga wa unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying).
Serikali ya Australia hadi sasa imeorodhesha majukwaa kumi yatakayojumuishwa kwenye marufuku: Facebook, Instagram, Snapchat, Threads, TikTok, X, YouTube, Reddit na majukwaa ya mtiririko wa video ya Kick na Twitch.
Pia ipo chini ya shinikizo la kupanua marufuku hadi kwenye michezo ya mtandaoni.
Wakiwa na hofu ya kuwa wanaweza kuingizwa kwenye marufuku, majukwaa ya michezo kama Roblox na Discord hivi karibuni yameanzisha ukaguzi wa umri kwenye baadhi ya vipengele kwa lengo la kujaribu kuepuka kuingizwa kwenye marufuku hiyo.
Serikali imesema itaendelea kukagua orodha ya majukwaa yaliyoathirika, na itazingatia vigezo vikuu vitatu wakati wa kufanya hivyo.
Unaweza kusoma;
Wanawake wa Afrika Kusini watoa wito wa maandamano kupinga ukatili wa kijinsia

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Makundi ya watetezi wa haki za wanawake nchini Afrika Kusini yanatoa wito wa maandamano ya nchi nzima ili kudai kuwa ukatili wa kijinsia (GBV) utangazwe kuwa janga la kitaifa katika nchi ambako mashambulizi dhidi ya wanawake yamekuwa ya kawaida.
Kampeni hiyo ilianza kupitia harakati zilizovuma kwenye mitandao ya kijamii na itafikia kilele chake kwa “mgomo” wa taifa zima siku ya Ijumaa, kabla ya Mkutano wa G20 utakaofanyika Johannesburg.
Watu mashuhuri, wananchi na mataifa mbalimbali wameonesha mshikamano wao kwa kubadilisha picha za wasifu wao kwenye mitandao ya kijamii na kuwa rangi ya zambarau, rangi ambayo mara nyingi inahusishwa na uelimishaji kuhusu unyanyasaji wa kijinsia (GBV).
Afrika Kusini ina viwango vya juu zaidi vya GBV duniani, huku kiwango ambacho wanawake wanauawa kikiwa mara tano zaidi ya wastani wa kimataifa, kulingana na shirika la UN Women.
Kati ya Januari na Machi mwaka huu, wanawake 137 waliuawa na zaidi ya 1,000 kubakwa, kulingana na takwimu za uhalifu za Afrika Kusini.
Siku ya Ijumaa, wanawake wanahimizwa kujiepusha na kwenda kazini au shuleni, "kujiondoa katika uchumi kwa siku moja", na kulala chini kwa dakika 15 saa 12:00 saa za huko (10:00 GMT) kwa heshima ya wanawake waliouawa nchini humo.
Pia wanahimizwa kuvaa nguo nyeusi kama ishara ya "maombolezo na upinzani". Maandamano hayo, yaliyopewa jina la Kufungwa kwa Wanawake wa G20, yameandaliwa na Women for Change, ambayo pia imekuwa ikiongoza kampeni ya mtandaoni.
Pia kumekuwa na ombi la mtandaoni, lililosainiwa na zaidi ya watu milioni moja, likiitaka serikali kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya janga hili.
Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Maafa (NDMC) kimekataa wito wa kutangaza GBV kuwa janga la kitaifa, kikisema hakiingii ndani ya mahitaji ya kisheria.
Unaweza kusoma;
Kiongozi wa kundi linalotaka kujitenga Nigeria ahukumiwa kifungo cha maisha

Chanzo cha picha, Reuters
Mahakama nchini Nigeria imempata kiongozi wa vuguvugu la kujitenga, Nnamdi Kanu, na hatia ya ugaidi na mashtaka mengine kufuatia kesi ya zaidi ya miaka kumi iliyojaa misukosuko.
Amehukumiwa kifungo cha maisha mara nne, pamoja na vifungo vingine vitakavyotumikiwa kwa pamoja.
Upande wa mashtaka ulikuwa umetaka adhabu ya kifo, lakini Jaji James Omotosho amesema kwamba sasa “adhabu ya kunyonga haipendelewi”.
Katika uamuzi wake, alisema ameridhika kwamba Kanu alifanya matangazo kadhaa yaliyochochea vurugu na mauaji kama sehemu ya kampeni yake ya kutaka kuanzisha taifa tofauti kusini mashariki mwa Nigeria, linalojulikana kama Biafra.
Kanu alipatikana na hatia katika mashtaka yote saba aliyokabiliwa nayo. Mbali na ugaidi, mashtaka hayo yalijumuisha uhaini na ushiriki katika harakati iliyopigwa marufuku.
Kanu amekuwa akikana mashtaka hayo kila wakati na alipinga mamlaka ya mahakama. Mwanzoni mwa kesi, aliwafukuza mawakili wake lakini alikataa kujitetea.
Hakuwa mahakamani wakati hukumu inatolewa, baada ya kuondolewa kutokana na tabia isiyodhibitika.
Usalama uliongezwa kuzunguka jengo la mahakama katika mji mkuu, Abuja, kabla ya hukumu kutolewa iwapo kungetokea maandamano kutoka kwa wafuasi wa Kanu.
Akiwa mtu ambaye hapo awali hakujulikana sana, alijipatia umaarufu kitaifa mwaka 2009 alipoanzisha Radio Biafra, kituo kilichokuwa kikitoa wito wa kuanzishwa kwa taifa huru la watu wa Igbo, kikirusha matangazo yake kuelekea Nigeria kutoka London.
Unaweza kusoma
Trump asema ujumbe wa Democrats kwa wanajeshi ni kitendo cha uasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Donald Trump amewalaumu wabunge sita wa Democratic kwa “tabia ya uhaini, inayostahili adhabu ya kifo,” baada ya wao kutoa video iliyoitaka jeshi la Marekani kukataa maagizo yasiyo halali.
“Hii ni mbaya sana, na ni Hatari kwa Nchi Yetu. Maneno yao hayawezi kuruhusiwa. TABIA YA UHAINI KUTOKA KWA WASALITI!!! WAFUNGWE JELA???,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
Wabunge hao sita, ambao wote wametumikia katika jeshi au katika taasisi za ujasusi, walisema matamshi ya Trump ni hatari na kwamba yanamaanisha vitisho dhidi ya viongozi waliochaguliwa.
“Hakuna tishio, vitisho, au wito wa vurugu utakaotuzuia kutimiza wajibu huo muhimu,” walisema katika taarifa ya pamoja.
Video hiyo ya Democrats, ambayo ilichapishwa na Seneta wa Michigan Elissa Slotkin, inamshirikisha Seneta wa Arizona Mark Kelly na Wawakilishi Chris DeLuzio wa Pennsylvania, Maggie Goodlander wa New Hampshire, Chrissy Houlahan wa Pennsylvania na Jason Crow wa Colorado.
Seneta Kelly, ambaye aliwahi kutumikia katika Jeshi la Wanamaji na pia ni mwanaanga wa zamani, anasema: “Sheria zetu ziko wazi. Unaweza kukataa maagizo yasiyo halali.”
Wabunge hao wanasema kwenye video: “Hakuna mtu anayelazimika kutekeleza maagizo yanayokiuka sheria au katiba yetu.”
Video hiyo inasema: “Serikali hii inawapandisha mabega wanajeshi wetu na wataalamu wa jumuiya ya ujasusi dhidi ya raia wa Marekani. Kama sisi, nyote mliapa kiapo cha kulinda na kutetea Katiba hii. Kwa sasa, vitisho vinavyokabili Katiba yetu havitoki tu nje ya nchi bali kutoka hapa nyumbani.”
Majibu kutoka kwa Trump Alhamisi asubuhi yalikuja kupitia misururu ya machapisho kwenye Truth Social.
Katika moja ya machapisho, aliandika: “Hii inaitwa TABIA YA UHAINI KIWANGO CHA JUU. Kila mmoja wa wasaliti hawa wa Nchi Yetu anapaswa KUKAMATWA NA KUFIKISHWA MAHAKAMANI. Maneno yao hayawezi kuruhusiwa kusimama. Hatutakuwa na Nchi tena!!! Mfano LAZIMA UWEKWE.”
Kisha akaendelea kusema: “Hii ni mbaya sana, na ni Hatari kwa Nchi Yetu. TABIA YA UHAINI KUTOKA KWA WASALITI!!! WAFUNGIWE JELA???”.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, katibu wa habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alikataa mapendekezo kwamba Trump alikuwa akitoa wito wa kuuawa kwa wabunge hao. "Wengi katika chumba hiki wanataka kuzungumzia kuhusu majibu ya rais, lakini si kile kilichomfanya rais kujibu kwa njia hii," alisema, akiwashutumu wabunge kwa kuwahimiza wanajeshi kukataa "amri halali".
Watu 41 wafariki kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Vietnam

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Miji ya pwani ya Hoi An na Nha Trang ni miongoni mwa miji iliyoathiriwa zaidi na mvua na mafuriko ya hivi karibuni. Mvua zisizokoma na mafuriko vimesababisha vifo vya takribani watu 41 katika Vietnam ya kati tangu mwisho wa wiki, huku juhudi za kusaka watu tisa ambao hawajulikani walipo zikiendelea, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Mafuriko hayo yamezika zaidi ya nyumba 52,000 na kuacha kaya na biashara nusu milioni bila umeme, kwa mujibu wa ripoti.
Kiwango cha mvua kimezidi mita 1.5 katika maeneo kadhaa ndani ya siku tatu zilizopita, kikifikia hadi juu kuliko kilele cha mafuriko ya mwaka 1993 cha mita 5.2 katika sehemu nyingine.
Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni pamoja na miji ya pwani ya Hoi An na Nha Trang, pamoja na ukanda muhimu wa uzalishaji wa kahawa katika nyanda za juu za kati, ambako wakulima tayari wanakabiliwa na mavuno yaliyokwama kutokana na dhoruba za awali.
Hali mbaya ya hewa imeikumba Vietnam katika miezi ya hivi karibuni. Kimbunga Kalmaegi na Bualoi vimeacha mfululizo wa vifo na uharibifu ndani ya kipindi cha wiki chache.
Majanga ya asili nchini Vietnam yamesababisha hasara inayofikia dola bilioni 2 kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, kwa mujibu wa makadirio ya serikali.
Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani zinaonesha watu wakiwa wamekwama juu ya paa huku maji ya mafuriko yakitanda majumbani mwao, wakati video inayosambaa mtandaoni inaonesha daraja la kamba katika mkoa wa Lam Dong liking’oka kutoka kwenye nguzo zake.
Mkoa huo umetangaza hali ya dharura baada ya maporomoko ya udongo kuharibu barabara kuu na njia za magari.
Usafiri ulisimama kabisa baada ya sehemu ya Mlima Mimosa, njia muhimu ya kuingia katika jiji maarufu la utalii la Da Lat, kuporomoka na kutumbukia korongoni, shirika la habari la AFP liliripoti.
