Je, uwezo wa kijeshi wa Venezuela ni upi na inawezaje kujibu mashambulizi ya Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuwasili kwa meli inayobeba ndege za kijeshi ya Marekani USS Gerald Ford katika maji ya Amerika Kusini kumeashiria awamu mpya katika mvutano kati ya Marekani na Venezuela.
Hili ndilo jeshi kubwa zaidi la Marekani katika eneo hilo tangu uvamizi wa Panama mwaka 1989. Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, kama Rais wa wakati huo wa Panama Manuel Antonio Noriega, anakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya, ambayo anayakanusha.
Kwa kutuma chombo kikubwa zaidi na cha kisasa zaidi cha kubeba ndege karibu na pwani ya Venezuela, Washington imezua utata kuhusu nia yake ya kweli, lakini huko Caracas kila kitu kinaonyesha maandalizi ya makabiliano.
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino Lopez wiki iliyopita alitangaza "utumaji mkubwa" wa vikosi vya ardhini, baharini, anga, mito na makombora, pamoja na wanamgambo maarufu wa kujitolea, kote nchini ili kukabiliana na kile alichokiita vitisho kwa serikali ya Maduro.
Lopez alisema katika ujumbe wake wa televisheni kwamba Maduro aliamuru kutumwa kwa askari "karibu 200,000" kama sehemu ya operesheni hiyo.
Kuwasili kwa meli ya kubeba ndege ya Marekani USS "Abernathy" katika eneo hilo kunaonekana na wengi kama kuongezeka kwa kampeni ya kijeshi ya utawala wa Donald Trump dhidi ya kile inachokiita "makundi ya madawa ya kulevya yanayofanya kazi nchini Venezuela." Kampeni hii hadi sasa imegharimu maisha ya zaidi ya watu 75 kwenye boti na meli.
Lakini wachambuzi kadhaa wanaamini kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana unaolenga kuidhoofisha au hata kuiangusha serikali ya Maduro, ambayo Washington inaiona kuwa isiyo halali baada ya uchaguzi wa mwaka jana uliokumbwa na utata na madai ya ulaghai uliofanywa na vikosi vya upinzani na mashirika ya kimataifa.
Je, jeshi la Venezuela chini ya Nicolas Maduro linaweza kustahimili mashambulizi kutoka kwa nguvu kubwa zaidi ya kijeshi duniani?
'Jeshi ni kivuli cha lilivyokuwa zamani'
Maduro alitangaza mnamo Septemba kwamba zaidi ya watu milioni nane wamejiandikisha kuitetea Venezuela na hata akadokeza kwamba anaweza kuwapa silaha wanamgambo wa idadi sawa na hiyo.
Wataalam wameelezea mashaka makubwa juu ya nambari hizi.
"Hiyo si kweli. Idadi halisi ni ndogo zaidi. Maduro hakupata hata kura milioni nne mwaka jana. Wanajeshi pia wana kiwango kikubwa cha watu wasiojiweza," James Story, afisa mkuu wa zamani wa Venezuela katika ubalozi wa Marekani huko Bogota (2020-2023), aliambia BBC Mundo.
Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, Venezuela ina takriban wanajeshi 123,000 walio hai, wanajeshi 220,000 na askari wa akiba 8,000.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
James Story anasema jeshi la Venezuela kwa ujumla halifundishwi mara kwa mara, vifaa vyake havitunzwi mara kwa mara, na wanamgambo wengi wanaoiunga mkono serikali hawana hata silaha: "Kunaweza kuwa na vitengo vichache vyenye uwezo vilivyosalia jeshini, lakini kama jeshi la mapigano, havifanyi kazi sana."
Anaongeza kuwa jeshi la Venezuela ni "kivuli tu cha siku zilizopita," lakini anakubali kwamba nchi hiyo ina "rasilimali za kipekee katika eneo hilo."
Ingawa jeshi la Marekani lina nguvu zaidi kuliko lile la Venezuela, Caracas bado inaonekana kuwa na uwezo wa kufikia zana za juu zaidi za kijeshi.
Mbali na takriban ndege 20 za kivita za Sukhoi ambazo Hugo Chavez alinunua kutoka Urusi mwaka wa 2006, Venezuela pia ilipokea ndege 10 za kivita aina ya F-16 kutoka Marekani katika miaka ya 1980. Wakati huo, Caracas ilikuwa moja wa washirika wa karibu wa Washington katika eneo hilo.
"Ndege za kijeshi za Sukhoi ni bora kuliko ndege nyingine yoyote katika kanda (Amerika ya Kusini) na baadhi yao bado zinafanya kazi. Kati ya F-16s, pengine kuna moja au mbili ambazo bado zinafanya kazi," anasema Storey.
Makombora ya kuzuia ndege na droni

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwishoni mwa Oktoba, katika kilele cha mvutano na Marekani, Maduro alitangaza kwamba Venezuela ilikuwa imetuma makombora 5,000 ya ndege ya Igla-S ya Kirusi katika "nafasi muhimu za ulinzi wa anga."
"Kila jeshi duniani linafahamu uwezo wa Igla-S," alisema katika hafla ya kijeshi iliyoonyeshwa kwenye televisheni.
Makombora ya Igla-S ni mifumo ya ulinzi wa anga ya masafa mafupi, ambayo yanaweza kulenga makombora yaliorushwa, ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege zinazoruka anga ya chini.
Venezuela pia ina magari ya kivita ya Uchina aina ya VN-4 na katika miaka ya hivi karibuni imekuwa nchi pekee ya Amerika Kusini yenye ndege zisizo na rubani zenye silaha, ambazo Nicolas Maduro alizionyesha kwenye gwaride la kijeshi la 2022.
Ndege zisizo na rubani za "Antonio José de Sucre 100 na 200" zimetengenezwa Venezuela na zimeundwa kulingana na matoleo mapya ya ndege zisizo na rubani za Irani.
Venezuela pia imepokea boti za mashambulizi ya haraka za "Pickup-3" zilizotengenezwa na Iran zenye vifaa vya kurushia makombora.
Kando ya hizi ni mifumo ya makombora yanayorushwa kutoka ardhi hadi angani ya Pantsir-S1 na Buk-M2A, ambayo, kulingana na Alexei Zhuravlev, mbunge wa Urusi na naibu mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Duma, hivi karibuni walisafirishwa hadi Caracas ili kupeleka ndege.
Lakini kulingana na Andrey Serbin-Pont, mchambuzi wa mahusiano ya kimataifa katika uwanja wa sera za kigeni na ulinzi na mkuu wa "Mratibu wa Kikanda wa Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii", sehemu kubwa ya vifaa hivi vipo kwenye karatasi tu.
"Kuna tofauti kubwa kati ya kile Venezuela inacho kwenye karatasi na vifaa vinavyofanya kazi," aliiambia BBC Mundo.
Mfumo ambao unaweza "kuondolewa" kwa urahisi
Wakati baadhi ya ripoti zinaonyesha uwezekano wa mashambulizi ya moja kwa moja katika ardhi ya Venezuela, mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo imepewa kipaumbele zaidi kuliko hapo awali.
Hatahivyo, Andrei Serbin-Pont anasema kwamba sehemu kubwa ya mtandao huu haitumiki au "imebadilishwa kwa urahisi" na teknolojia ya Marekani, pamoja na mifumo ya makombora ya ulinzi wa anga ya Pechora iliyotengenezwa na Urusi, ambayo teknolojia yake ilianza miaka ya 1960.
Venezuela pia ina mifumo ya makombora ya Buk iliyosambazwa karibu na Caracas, ambayo ni mizuri zaidi, lakini kulingana na Serbin Pont, haitakuwa vigumu kwa Marekani kuizuia pia.
"Aidha, utayari wa mifumo hii ni mdogo sana kutokana na uhaba wa vipuri," anafafanua.
Kuhusu makombora 5,000 ya Igla-S ambayo Maduro alizungumzia mwishoni mwa Oktoba, Serbin Pont anasema idadi iliyotangazwa ni sahihi.
"Lakini ina takriban milingoti 700 tu ya kurusha Igla-S, ambayo bado ni idadi kubwa na jambo la kutia wasiwasi kwa sababu ikiwa itaangukia mikononi mwa makundi yenye silaha yanayoiunga mkono serikali, inaweza kuwa hatari sana. Sio lazima kwa operesheni za Marekani, lakini kwa ndege za kiraia au helikopta yoyote na ndege zinazoruka katika miinuko ya chini."

Chanzo cha picha, Getty Images
"Vita vita vya muda mrefu"
Kulingana na Serbin Pont, mkakati wa sasa wa serikali ya Maduro ni kupendekeza kwamba silaha hizo zinaweza kusambazwa miongoni mwa watu wa Venezuela baada ya uwezekano wa shambulio la Marekani.
Baadhi wana wasiwasi kuwa silaha hizi zitaishia katika makundi yenye silaha kama vile Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa au matawi yaliyojitenga ya FARC.
Lengo la mkakati huo ni kutishia kuleta ukosefu wa utulivu na machafuko nchini Venezuela kwa serikali yoyote ya mpito ya siku zijazo.
Wachambuzi wengi wanaamini kwamba Maduro na mduara wake wa ndani wanajiandaa kwa "vita vya msituni."
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela Diosdado Cabello alitishia mnamo Septemba kwamba nchi yake iko tayari kwa "vita vya muda mrefu."
Muda mfupi baadaye, serikali ya Maduro iliamuru Jeshi la Kitaifa la Venezuela kutoa mafunzo kwa wakaazi wa maeneo masikini kutumia silaha.
Lakini balozi wa zamani wa Marekani James Story anaona kuwa haiwezekani kwamba umma utajiunga na kampeni kama hiyo: "Maduro si maarufu sana miongoni mwa wanajeshi au miongoni mwa umma, kwa hivyo sidhani kama umma ungemfuata au kumuunga mkono katika vita vya msituni."
Anatukumbusha tena kwamba Maduro "hakuweza hata kupata kura milioni nne katika uchaguzi uliopita."
Kwa mujibu wa "Baraza la Taifa la Uchaguzi", ambalo linafanya kazi chini ya usimamizi wa serikali, Nicolas Maduro alipata takriban kura milioni 6.4, lakini takwimu hii imetiliwa shaka na baadhi ya upinzani na taasisi nyingi za kimataifa.
Je, Venezuela imejiandaa vipi kwa mzozo?
Licha ya serikali ya Venezuela kuzidi kuwa na uhasama na chuki dhidi ya Marekani, Andrei Serbin Pont anaamini kuwa jeshi la nchi hiyo haliko tayari kwa mzozo.
Anafafanua kuwa kwa miaka 25 iliyopita, vikosi vya jeshi vya kitaifa vimeendesha dhana ya kijeshi inayoitwa "vita vya awamu," ambayo inachukulia kwamba mzozo unaendelea hatua kwa hatua na katika awamu au hatua kadhaa zinazoweza kudhibitiwa.
Katika hatua ya kwanza, kipindi cha kutokuwa na utulivu wa ndani kinaendelea, ambayo serikali inadai unasababishwa na kuingilia kati kwa nguvu ya kigeni. Katika hatua ya pili, nchi jirani inahusika, na kuunda "mgogoro kati ya pande mbili zinazofanana," hali ambayo inaweza hatimaye kusababisha kuingilia kati kwa Marekani.
"Mchakato huu unapelekea hatua ya nne, upinzani wa muda mrefu wa wananchi, ambapo vikosi vya kijeshi vinatarajiwa kusambaratika na makundi mengine ya kijamii yanatarajiwa kuchukua silaha na kutawanyika miongoni mwa watu ili kuendesha vita vya msituni dhidi ya uvamizi wa Marekani," anasema Serbin Pont.
"Katika mzozo na nchi jirani - kwa mfano, Colombia au Brazil - mifumo ya kawaida ya silaha ya Venezuela inaweza kuwa muhimu sana," anaendelea.
Lakini anasisitiza kuwa silaha hizi "hazina tishio kubwa" kwa Marekani.















