Kwa nini Marekani iliikamata ndege ya Rais Maduro huko Dominika?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka nchini Marekani imeikamata ndege inayotumiwa na Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kutoka Jamhuri ya Dominika na kuipeleka Florida Kusini.
Wizara ya Sheria ilisema ndege hiyo ilikamatwa kwa ombi la Marekani baada ya kukiuka vikwazo.
Akijibu hatua hiyo ya Marekani , Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela Yvan Gil aliishutumu Marekani kwa kufanya "uhalifu wa mara kwa mara ambao hauwezi kuelezewa kama kitu kingine chochote isipokuwa uharamia."
Aliongeza kuwa Venezuela "inahifadhi haki za kuchukua hatua zozote za kisheria" kurekebisha uharibifu uliosababishwa na Marekani kwa hatua hii.
Habari za kukamatwa kwa ndege hiyo zilitolewa katika taarifa ya Wizara ya Haki nchini Marekani kwa vyombo vya habari ambapo Mwanasheria Mkuu Merrick B. Garland alisema: “Leo asubuhi (Septemba 2), Wizara ya Haki ilikamata ndege ambayo tunadai ilinunuliwa kinyume cha sheria kwa dola milioni 13 kupitia kampuni bandia na kusafirishwa nje ya Marekani kwa matumizi ya Nicolás Maduro na waandani wake.”
Garland aliongeza kuwa uchunguzi utaendelea "kuwazuia kutumia rasilimali za Marekani kudhoofisha usalama wa taifa la Marekani."
Hatua hiyo inajiri mwezi mmoja tu baada ya uchaguzi wa Julai 28, ambapo Maduro alitangazwa mshindi bila kuonyesha rekodi za upigaji kura na licha ya madai ya udanganyifu kutoka kwa upinzani.
Serikali ya Rais Joe Biden haitambui ushindi wa Maduro, baada ya mgombea wa upinzani, Edmundo González, na kiongozi María Corina Machado, kuchapisha 81.7% ya ushindi ambao unaunga mkono upinzani.

Chanzo cha picha, EPA
"Ununuzi haramu"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Taarifa ya Wizara ya Sheria ilieleza kwamba mwishoni mwa 2022 na mapema 2023, "watu wanaohusishwa na Maduro walidaiwa kutumia kampuni bandia iliopo katika eneo la Caribbean kuficha kuhusika kwao katika ununuzi haramu wa ndege ya Dassault Falcon 900EX kutoka kwa kampuni hiyo ya Kusini mwa Florida."
Baadaye, Aprili 2023, ndege hiyo ilidaiwa kusafirishwa kinyume cha sheria kutoka Marekani hadi Venezuela kupitia visiwa vya Caribbian. Tarehe hiyo hiyo ndege hiyo iliwasili Caracas baada ya kupita Kingston, huko Saint Vincent na Grenadines, kulingana na data kutoka kwa tovuti ya Flightradar24, kwa mujibu wa BBC News.
Haijabainika ni lini ndege hiyo iliwasili katika Jamhuri ya Dominika. Data ya njia ya ndege inayopatikana inaonyesha ilipaa Jumatatu kutoka Uwanja wa Ndege wa La Isabela karibu na Santo Domingo na kuwasili muda mfupi baadaye kwenye Uwanja wa Ndege wa Fort Lauderdale huko Florida.
"Tangu mwezi Mei 2023, ndege hiyo aina ya Dassault falcon , yenye nambari ya mkia T7-ESPRT , imekuwa ikisafiri mara kwa mara kuelekea na kutoka kambi ya kijeshi nchini Venezuela na imetumiwa kwa manufaa ya Maduro na wawakilishi wake, ikiwa ni pamoja na kumsafirisha Maduro katika ziara za nchi nyingine. ”
Mnamo Agosti 2019, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alitoa amri ya Utendaji nambari 13884 , ambayo inakataza Wamarekani kujihusisha katika miamala na watu ambao wamehusishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa niaba ya serikali ya Venezuela, pamoja na kuwa wanachama wa serikali ya Maduro.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ujumbe ulio wazi"
"Acha ukamataji huu utume ujumbe ulio wazi: ndege iliyopatikana kwa njia haramu nchini Marekani kwa manufaa ya maafisa wa Venezuela haiwezi tu kupaa angani itakavyo," ilisema Idara ya Biashara Chini ya Katibu wa Udhibiti wa Mauzo ya Nje Matthew S. Axelrody, kulingana na wizara ya Sheria .
"Haijalishi ni ndege ya aina gani iwe ya kibinafsi au kifahari au ya watu wenye uwezo, tutafanya kazi bila kuchoka na washirika wetu hapa na kote duniani kutambua na kurejesha ndege yoyote iliyosafirishwa kutoka Marekani kinyume na sheria," aliongeza.
Mwanasheria wa Marekani katika Wilaya ya Kusini mwa Florida, Markenzy Lapointe alisema ukamataji huo uliwezekana kwa ushirikiano wa serikali ya Jamhuri ya Dominika, ambayo Maduro alivunja uhusiano nayo baada ya kukataa tangazo la ushindi wake.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah












