Marufuku ya Pogba: Huu ndio mwisho wa nyota wa Juventus na Ufaransa?

Chanzo cha picha, NurPhoto
Taaluma ya Paul Pogba inaweza kufikia kikomo baada ya kufungiwa kwa miaka minne kwa kutumia dawa za kusisimua misuli huku ikionekana kuwa kiungo huyo wa kati wa Juventus mwenye umri wa miaka 30 hakuwahi kuutendea haki uwezo wake.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, ambaye alishinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa, alikuwa na kipaji cha hali ya juu na kwa kishindo alionekana kuwa mshindi kabisa, lakini hakuwahi kudhihirisha hivyo mara nyingi.
Tayari amesema atakata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, lakini hilo likishindikana, hadi kufikia wakati atastahili kucheza tena, Agosti 2027, atakuwa na umri wa miaka 34 na atakuwa hana klabu.
Kwa hivyo litakuwa changamoto kubwa kwa mchezaji ambaye hajacheza mechi 22 kamili za ligi kwa msimu mmoja tangu 2018-19 kukaa hali nzuri na kuwa na motisha kwa kipindi kirefu kama hicho.
Mwandishi wa habari wa soka wa Ufaransa Julien Laurens alisema kwenye kipindi cha Ligi ya Euro cha BBC Radio 5 Live: "Nakumbuka nilimwona akiwa na umri wa miaka 15 na alikuwa kitu bora zaidi sikuwahi kuona.
"Alikuwa mzuri sana, talanta ya kizazi, mwenye akili kabisa.
"Alikuwa na taaluma nzuri, alishinda mataji manne ya Serie A na Kombe la Dunia. Ni taaluma nzuri sana. Lakini alikuwa mzuri sana hivi kwamba nilidhani hakuna kikomo.
“Nilidhani atafika kileleni, atashinda Ballons d’Or, atashinda mataji zaidi na kuwa mchezaji bora zaidi duniani.
"Mwishowe tutaangalia nyuma katika taaluma yake kila wakati na yeye tukijiuliza nini kilipaswa kuwa."
Nini sasa kwa Pogba?

Chanzo cha picha, NurPhoto
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Pogba alisimamishwa kwa muda mwezi Septemba baada ya kipimo cha dawa kilichochukuliwa baada ya mchezo wa ufunguzi wa msimu kupatikana viwango vya juu vya testosterone kwenye mfumo wake.
Siku ya Alhamisi, mahakama ya kitaifa ya kupambana na dawa za kusisimua misuli ya Italia (Nado) ilithibitisha kusimamishwa kwa miaka minne, ambayo ni ya tarehe 20 Agosti 2023 alipofeli mtihani huo.
Pogba alisema uamuzi huo "si sahihi" na hatawahi "kujua au kwa makusudi kutumia dawa". Alithibitisha kuwa atakata rufaa na kuongeza "ninapokuwa huru na vikwazo vya kisheria, hadithi kamili itakuwa wazi".
Laurens alisema: "Kisa kinachosimuliwa ni kwamba ana rafiki yake ambaye ni daktari huko Miami ambaye alimpa virutubisho vya chakula ambavyo alichukua bila kujua kilichomo ndani yake na hiyo ndiyo iliyosababisha yote haya.
"Angeweza kusema kwa urahisi 'nilikuwa mjinga, sikuzingatia na nilipaswa kutaja kwa madaktari wa Juventus' na labda adhabu ingepunguzwa.
"Kwa yeye kutarajia chini ya miaka minne kwa sababu alisema 'sikujua nilikuwa nikiichukua na nikitarajia bora', naona ni ujinga kidogo."
Mtaalamu wa kandanda wa Italia Mina Rzouki alisema: "Adhabu yake inaweza kupunguzwa ikiwa mwanariadha anaweza kuthibitisha kwamba dawa yake haikukusudiwa au sampuli zao zilichafuliwa - au ikiwa mchezaji atatoa msaada mkubwa kusaidia wachunguzi.
"Kwa hivyo inategemea kama hataweza kudhibitisha kuwa hii haikuwa ya kukusudia na basi kuna uwezekano tunaweza kuona marufuku hiyo ikipunguzwa hadi miaka miwili ambayo inaweza kumaanisha kuwa anaweza kurejea tena."
"Nadhani miaka minne inamaliza kazi yake. Ana karibu miaka 31. Unaongeza miaka minne. Kwa miezi 18 amecheza kwa shida sana kwa sababu ya majeraha. Kwa hivyo sio miaka minne tu bila mpira, ni karibu miaka sita.” Laurens alisema.
"Sina uhakika angetaka akiwa na umri wa miaka 35 awe tayari kwenda tena. Nadhani hivi ndivyo itakavyoisha ikiwa marufuku hii itazingatiwa. Ikiwa ni miaka miwili kuna nafasi ya akiwa miaka 33 mtu kumpa kandarasi ya mwisho."
Juventus wanadhaniwa kupunguza mshahara wake hadi takriban pauni 2,000 kwa mwezi - kama sehemu ya makubaliano ya pamoja kati ya klabu na muungano wa wachezaji.
Pogba alikuwa akipokea pauni milioni 6.9 kwa mwaka. Juve wana chaguo la kufuta kandarasi yake, ambayo itaendelea hadi Juni 2026 - zaidi ya mwaka mmoja kabla ya marufuku ya miaka minne kukamilika.
Mwandishi wa kandanda wa Italia James Horncastle alisema: "Juventus haijatoa taarifa. Mkurugenzi wao wa michezo, alipoulizwa mara ya mwisho, alisema wangesubiri matokeo ya mwisho ya mchakato huo.
"Bado kuna rufaa ya kwenda kwa CAS. Bila hiyo kumalizika hatutakuwa na taarifa rasmi kutoka kwa Juventus kuhusu hatua wanazoweza kuchukua."
Je, taaluma ya Pogba ilifikia matarajio?

Kwa vipimo vingi, Pogba alikuwa na taaluma yenye mafanikio makubwa.
Alianza maisha yake ya soka katika klabu ya Manchester United kabla ya kuhamia Juventus, ambako alishinda Serie A katika kila misimu yake minne ya kwanza klabuni hapo.
Kisha akarejea United kwa rekodi ya dunia ya pauni milioni 89 mwaka wa 2016. Katika msimu wake wa kwanza United alishinda Ligi ya Europa na Kombe la FA.
Pogba, ambaye aliichezea Ufaransa mechi 91, kisha kuisaidia Les Bleus kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia 2018, akifunga bao katika ushindi wao wa fainali wa 4-2 dhidi ya Croatia nchini Urusi.
Katika misimu miwili kila upande wa Kombe la Dunia, alihusika katika mabao 38 ya Ligi Kuu ya United (mabao sita na asisti 10 msimu wa 2017-18 na mabao 13 na asisti tisa msimu wa 2018-19).
Lakini kwa mchezaji ambaye alitajwa kuwa gwiji, hakuwahi kukaribia kabisa Ballon d'Or - na mataji hayo mawili mwaka 2017 akiwa na United yangekuwa mawili ya mwisho ya maisha yake ya klabu.
Majeraha yalikatiza misimu yake mitatu ya mwisho akiwa United, huku ukosefu wa ubora ukiwa haujasaidia pia, na kurejea kwake kama wakala huru kwa Juventus miezi 18 iliyopita kulikusudiwa kuwa mwanzo mpya.
Lakini majeraha zaidi, na kisha kupigwa marufuku wakati huu alikuwa sawa, inamaanisha kuwa amecheza dakika 213 tu kwa kilabu cha Italia.
"Ilitakiwa kuwa muungano wa kusimulia hadithi mpya, mwana mpotevu akirejea Juventus. Majira haya ya joto kila mtu alifikiri huu ungekuwa mwaka na angefanya kitu maalum," alisema Rzouki.
"Klabu na mchezaji walitaka kuandika hadithi ya kurejea kwa ushindi kwa nyota huyo. Badala yake, tutabaki tukijiuliza nini kitatokea kwa mchezaji ambaye hajawahi kutimiza uwezo wake wa kweli."
Laurens aliongeza: "Alipata kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani, 2018 ilikuwa kilele cha maisha yake huko Urusi akiwa na Ufaransa, lakini sio kwa kiwango cha juu kama alivyopaswa kuwa. Atakubaliana na hilo.
"Njia pekee ambayo ningetumia neno kupoteza kwake na kipaji chake ni kwa sababu alipaswa kuwa na taaluma bora zaidi kuliko aliyokuwa nayo."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Lizzy Masinga.












