Kwa nini makubaliano ya kuipa Ethiopia njia ya kuingia baharini ni muhimu

Chanzo cha picha, Getty
- Author, Kalkidan Yibeltal, Esther Kahumbi na Aaron Akinyemi
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Addis Ababa na London
Somalia imeelezea pingamizi kali kwa mpango uliopendekezwa ambao utaipa Ethiopia ufikiaji wa bandari muhimu katika jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland.
Katika kujibu mkataba wa maelewano (MOU), nchi hiyo imemwita haraka balozi wake kutoka Ethiopia.
Msemaji wa serikali alisema ilikataa vikali pendekezo lililokiuka mamlaka yake na uadilifu wa eneo - Somalia inaiona Somaliland kama sehemu ya eneo lake.
Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre alisema: "Ninataka kuwasihi watu wa Somalia watulie, nataka kuwahakikishia kwamba tumejitolea kuilinda nchi yetu. Hakuna sehemu ya ardhi yetu, bahari yetu na hewa yetu inayoweza kukiukwa, na tutaitetea kwa kila njia ya kisheria. Na nina hakika kwa msaada wa watu wetu iwe kaskazini au kusini tunaweza kuilinda nchi yetu”
Somaliland ilijitenga kutoka Somalia mwaka 1991 lakini haitambuliwi kimataifa kama taifa huru, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika. Kwa hiyo hatua yoyote kuelekea kutambuliwa rasmi- hasa kutoka kwa taifa lenye ushawishi mkubwa wa AU kama Ethiopia - inaweza kuwa muhimu kwa mustakabali wake.
Ikumbukwe kuwa hadi sasa, hakuna mpango wowote ambao umerasimishwa kisheria. Hakuna mkataba. Ingawa maafisa wa serikali ya Ethiopia walipendekeza kwa waandishi wa habari kuwa unaweza kukamilika mwezi ujao.

Chanzo cha picha, Getty
Hakuna shaka mpango wowote kama huo utaipa Ethiopia ufikiaji wa kona ya kimkakati na yenye faida kubwa ya ulimwengu. Inaweza kumaanisha nini kwa majirani zake?
Ethiopia
Ufikiaji wa kilomita 20 tu wa ukanda wa pwani huenda usichukuliwe kama jambo kubwa lakini kwa Ethiopia isiyo na bandari, ufikiaji wa bandari ni muhimu kwa hali yake ya kifedha. Ni nchi yenye watu wengi zaidi duniani ambayo haina ukanda wa pwani - na hii inatoa changamoto za wazi kwa ukuaji.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Zaidi ya 95% ya biashara ya kimataifa ya Ethiopia inategemea nchi jirani ya Djibouti, ambayo ina 31km ya ukanda wa pwani. Waziri Mkuu Abiy Ahmed anaelezea hitaji la nchi yake la kupata ufikiaji zaidi wa bandari kama suala "suala muhimu kwa uwepo wa nchi yake", na alisema katika hotuba ya televisheni mnamo Oktoba mwaka jana kwamba bandari ya Bahari Shamu ni muhimu kuwaondoa raia wake milioni 120 kutoka "gerezani la kijiografia"
Biashara inaweza isiwe sababu pekee. Nchi hiyo ilikuwa kigogo baharini yenye bandari mbili - Massawa na Assab. Lakini Ethiopia ilipoteza maeneo haya pamoja na maeneo mengine ya pwani wakati Eritrea ilipojitenga na kuunda nchi mpya mwaka 1993.
Kulingana na Balozi wa zamani wa Marekani nchini Ethiopia David Shinn, sababu ya msingi ya bandari ya Bahari ya Shamu ya Ethiopia na mkataba wake wa MOU na Somaliland ni kuanzisha kituo cha wanamaji mahali fulani katika Bahari ya Shamu au Ghuba ya Aden.
Aliambia kipindi cha Newsday cha BBC: "Somaliland imesema itakodisha kilomita 20 za ufuo wa pwani kando ya Ghuba ya Aden ili Ethiopia iweze kuanzisha kituo kama hicho. Pia huenda itatumika , au angalau kuruhusu Ethiopia kutumia bandari ya Berbera, ambayo ni bandari muhimu ya Somaliland, kwa matumizi ya kuagiza na kuuza bidhaa zake nje ya nchi. Ingawa sioni hiyo kama sababu kuu ya hii. Nadhani inahusiana zaidi na hamu ya kuwa na kituo cha jeshi la majini.
Michael Shurkin, mwenzake wa Kituo cha Afrika cha Baraza la Atlantiki: "Ni hatari iliyotathminiwa na Ethiopia, na ambayo ina mambo ya kweli. Ethiopia inatamani sana kupata ufikiaji mkubwa wa bahari, na kwa njia hii inaweza kuwa na mwelekeo mdogo wa kuanzisha vita na Eritrea. Zaidi ya hayo inaipa Somaliland utambuzi inayostahili . Bila shaka, pia inaikasirisha Somalia, lakini hiyo ni hatari ndogo kuliko makabiliano na Eritrea."

Chanzo cha picha, Getty Images
Somalia
Wadau wakuu wa kisiasa wa Somalia wanaamini kuwa hatua hiyo inaweza kutishia uthabiti wa eneo hilo la Pembe. Inakuja siku chache baada ya Somalia na Somaliland kufikia mwafaka wa kuanza tena mazungumzo yenye lengo la kutatua mvutano wa kisiasa. Mjumbe maalum wa Somalia katika Somaliland Abdikarim Hussein Guled alisema mpango uliopendekezwa unaonyesha "kutozingatia waziwazi kwa Ethiopia kanuni za kimataifa" na kufichua maendeleo yaliyopatikana kati ya Mogadishu na mji mkuu wa Somaliland Hargeisa.
Rais wa zamani wa Somalia Mohamed Farmaajo alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X, MOU hiyo ni "wasiwasi mkubwa kwa Somalia na Afrika nzima". Aliongeza: "Heshima kwa mamlaka na uadilifu wa eneo ndio nguzo ya utulivu wa kikanda na ushirikiano wa nchi mbili. Serikali ya Somalia lazima ijibu ipasavyo.”
Mohamed Mubarak mwenyekiti wa zamani wa Taasisi ya Hiraal, mdau wa masuala ya usalama katika Pembe ya Afrika alisema kuna maelfu ya wanajeshi wa Ethiopia kusini mwa Somalia. Ikiwa uhusiano utazidi kuwa mbaya, Ethiopia inaweza kujiondoa, na hivyo kuzidisha hali ya ukosefu wa usalama huko.
"Abiy amekuwa akisema kwa miezi mingi kwamba angeiwezesha Ethiopia kupata bahari," Bw Mubarak alisema. "Hicho ndicho amefanya [uwezekano] na mpango huu. Yuko tayari kufanya chochote kinachohitajika bila kujali athari zake kwa amani na utulivu wa eneo hilo.

Kenya
Miongoni mwa nchi ambazo Ethiopia imekuwa katika mazungumzo nazo ili kubadilisha upatikanaji wa bandari yake ni Kenya. Mnamo Agosti 2023, maafisa wa Ethiopia walitembelea bandari ya Lamu. Bandari hiyo ni sehemu ya mradi wa usafiri wa kikanda kati ya Ethiopia, Kenya, na Sudan Kusini uitwao LAPSSET.
Kupitia Lamu, Kenya ilitarajiwa kupunguza sehemu ya Djibouti ya mahitaji ya ndani ya Ethiopia kwa 15% kulingana na Ripoti ya Benki ya Dunia. Kwa hivyo mkataba wowote mpya wa bandari na Somaliland au kuchelewa kupanua Lamu kunaweza kupelekea Kenya kushindwa kuufanikisha mradi huo. Mnamo 2020, Somalia ilikata uhusiano na Kenya kwa muda mfupi baada ya kuwa mwenyeji wa kiongozi wa Somaliland Muse Bihi.
Kenya inasema kwamba inatambua Somaliland kama serikali ya kikanda ndani ya Somalia, lakini kama Ethiopia, Kenya inaendesha ubalozi mdogo huko Hargeisa.
Misri
Mhusika mkuu kwenye Pwani ya Bahari ya Shamu Misri ina idadi kubwa ya bandari zikiwemo bandari 8 za kibiashara na bandari tano za mafuta, madini na watalii.
Kumekuwa na wasiwasi katika kanda kuhusu muda ambao Waziri Mkuu Bw. Abiy Ahmed yuko tayari kwenda kupata ufikiaji wa Bahari ya shamu.
Amenukuliwa akielezea ufikiaji kama "suala linaloamua uwepo wa nchi yake". Wachambuzi wanasema maoni yake kuhusu hili hayana tofauti sana na yale alipoamua kuendelea na ujenzi wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (Gerd). Mkataba wa 1929 uliwapa Misri na Sudan haki kwa karibu maji yote ya Mto Nile lakini Ethiopia na Misri bado hazijakubaliana juu ya sheria za uendeshaji wa bwawa hili.
Njia ya kupitia Berbera inaweza kuifanya Ethiopia ikijiunga na mataifa mengi (pamoja na Misri,) ambayo yamekuza uchumi wao kwa kiasi kikubwa kutokana na kufikia Bahari ya Shamu.

Chanzo cha picha, Getty
Djibouti
Taifa hilo dogo la Kiafrika ni lango la kuelekea kwenye Mfereji wa Suez, mojawapo ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za meli duniani. Bandari yake ya thamani ndiyo moyo wa uchumi wake, ikitoa chanzo kikubwa zaidi cha mapato na ajira katika nchi ambayo haina kipato kingine. Kama lango kuu la biashara kwa jirani yake mkubwa mpango wowote wa biashara zaidi kupitia Berbera unaweza kuhatarisha hali yake.
China
Mbali zaidi, China inaweza pia kuwa na nia ya dhati katika mpango wowote - Somaliland imepokea msaada kutoka kwa Taiwan na kwa upande wake China inaunga mkono Somalia. Zikishirikiana mwaka wa 2020, Somaliland na Taiwan zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na kuwakasirisha majirani zao wakubwa. Wote hawatambuliki kimataifa na wote wana majirani - Somalia na China - ambazo zinasisitiza kuwa ni sehemu ya maeneo yao.
Na taarifa ya ziada kutoka kwa Angela Henshall.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












