Wizi wa fedha zinazosafirishwa waleta hofu katika barabara za Afrika Kusini

Na Daniel De Simone
BBC News, Johannesburg
Uhalifu wa kimabavu unazidi kuongezeka nchini Afrika Kusini, huku wizi wa pesa katika magari yanayosafirisha fedha ukiwa jambo la kawaida na kiwango cha mauaji kikiwa juu kwa miaka 20.
Kwa serikali - na wale wote wanaoishi hapa - rekodi hii mbaya ni tatizo kubwa.
Ni mwaka wa uchaguzi, wenye ushindani mkubwa zaidi tangu kuzaliwa kwa demokrasia mwaka 1994, na uhalifu ni suala muhimu.
Kulingana na takwimu za hivi punde za kila mwaka, zaidi ya watu 27,000 waliuawa kwa mwaka mmoja. Lakini idadi ya kesi zilizotatuliwa imeshuka hadi chini, ni 12% tu.
Kuua bila kukamatwa imekuwa kawaida.
Mchanganyiko wa viwango vya juu vya uhalifu, umaskini na ukosefu wa ajira hufanya ukosefu wa usalama kuwa wasiwasi mkubwa katika jamii.
Kujiamini na jeuri ya wahalifu kunaonyeshwa na jinsi wanavyoiba pesa zinazosafirishwa mchana peupe .
Magari ya usalama yaliyobeba pesa yamevamiwa kutoka kwa barabara zenye shughuli nyingi mchana kwa mashambulizi ya kimakusudi na magari, huku walinzi wakiwa wamezidiwa nguvu na watu wenye silaha kali wanaotumia mabomu kulipua sehemu za ulinzi.
Ujambazi unaweza kudumu kwa muda mrefu, huku msongamano wa magari ukiendelea kama kawaida upande wa pili wa barabara huku magenge yakitengeneza vilipuzi vyao na kuzunguka-zunguka kwa kutumia silaha za kiotomatiki, wakati mwingine hurekodiwa na watazamaji.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wahl Bartmann, mkuu wa kampuni ya usalama ya ADT Fidelity, anasema magenge hayo "ni kama kundi la kigaidi".
"Njama hizi sasa zimepangwa kijeshi, zimetekelezwa vyema, na ikiwa unaona jinsi wanavyopanga ujambazi huu, ni vigumu sana kwa timu zetu kukomesha hilo."
Anataka usaidizi zaidi kutoka kwa serikali, akisema huduma za CIT(Usafirishaji wa fedha ) ni muhimu - hulipa ruzuku ya kijamii kila mwezi, na kuhamisha fedha taslimu kwa benki na wauzaji reja reja.
Walinzi 15 wa kampuni hiyo waliuawa mwaka jana wakati wa wizi.
Lenience, mlinzi aliyenusurika kutekwa nyara hivi majuzi, anasema "kama binadamu ninaogopa" na kwamba yeye huomba kila asubuhi ili aokoke siku hiyo.
"Huenda nisirudi - lakini hayo ni maisha kwa kila mtu katika CIT," anasema, hataki kutumia jina lake la pili.
Hulka ya maisha nchini Afrika Kusini ni idadi kubwa ya maafisa wa usalama wa kibinafsi, wanaoshika doria katika magari yenye nembo ya kampuni zao, na katika baadhi ya maeneo karibu kila nyumba na jengo huwa na ishara inayoonyesha ni kampuni gani inaitegemea.
Sasa walinzi wa kibinafsi wanazidi wenzao wa polisi.
Lizette Lancaster, wa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama ya Afŕika Kusini, anasema kumekuwa na 'ubinafsishwaji wa usalama wa maeneo ya umma'
"Wananchi wengi wa Afrika Kusini hawawezi kumudu huduma hizi lakini wanahisi polisi wamewafelisha'
"Kwa hivyo mara nyingi huunda vikundi vyao vya kujisaidia - makundi ya kujitetea katika jamii zao.
Nilijiunga na timu kutoka ADT Fidelity usiku mmoja huko Johannesburg. Mara kwa mara huwakabili majambazi wenye silaha, wakicpigwa risasi na kuvunja utekaji nyara unaoendelea.
Wakiwa wamejihami kwa bunduki ikitokea matatizo ya ghafla, msafara mdogo uliondoka na tahadhari ikafika haraka - gari lilikuwa limeibiwa.
Kama magari mengine ambayo yana usajili wa usalama wa kibinafsi, gari lililoibiwa lilikuwa na kifuatiliaji kidogo cha kielektroniki kilichofichwa ndani, ambacho majambazi hujaribu sana kupata, wakijua kwamba timu zilizo na silaha zinaweza kulifuata kwa usahihi mradi tu libaki salama.
Baada ya kukimbizana kuelekea kusini mwa jiji, timu hiyo iliwaona wanaume wawili wakikimbia kutoka mahali ambapo gari hilo lilidhaniwa kuwa na wakakamatwa wakiwa wamenyooshea bunduki.
Lakini hawakuwa wanyang'anyi na waliachiliwa. Gari hilo lilipatikana muda mfupi baadaye, likiwa limeachwa kwa "kipindi cha kutafakariwa" ambacho huwaruhusu wezi kuangalia kama wanafuatwa.
Polisi waliitwa na kuja kuchukua gari - baada ya kupatikana na timu ya usalama.

Tishio la kila siku la uhalifu linamaanisha chama tawala cha African National Congress, nchini Afrika Kusini ambacho kiliingia madarakani miaka 30 iliyopita mwezi Aprili, kinakabiliwa na shinikizo kubwa kuchukua hatua.
Kiwango cha mauaji kilishuka katika miaka baada ya mwisho wa ubaguzi wa rangi, na kufikia kiwango cha chini karibu muongo mmoja uliopita. Tangu wakati huo, imeongezeka 62% hadi kiwango cha sasa - hadi ambapo ilikuwa miaka 20 iliyopita.
Viwango vya kusuluhisha kesi za uaji vimepungua hadi chini ya 55% tangu 2012, na kusababisha hali ambapo mauaji machache sana yanatatuliwa.
Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali inaajiri maelfu ya maafisa wapya wa polisi, huku 20,000 wakijiunga katika kipindi cha miaka miwili iliyopita katika matukio ya hadhi ya juu.
Katika hafla moja huko Pretoria mnamo Disemba, maafisa wapya waliandamana mbele ya umati wa watu waliokuwa wakishangilia, wakiniambia kuwa wasingeweza kusubiri kutoka mitaani kupambana na uhalifu.
Bheki Cele, waziri wa polisi, anakubali kwambacuhalifu ni suala kubwa na anasema viwango vya uhalifu wa kimabavu "havifurahishi hata kidogo".
Anasisitiza kuwa serikali inazidi 'kupambana na hali' na kwamba uhalifu ni "jambo la kimataifa", akitoa mfano wa wizi wa hivi karibuni wa mchezaji wa kandanda wa West Ham Kurt Zouma nchini Uingereza kuonyesha kwamba uhalifu wa kimabavu hutokea katika "kila nchi".
Lakini viwango vya uhalifu wa kimabavu hapa ni vya juu sana kwa viwango vya kimataifa.
Katika hali ya sasa ya ukosefu wa usalama nchini Afrika Kusini, wimbi la ghasia halitazimwa haraka .
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












