ADF: Fahamu kundi hili la wapiganaji la Uganda linaloshirikiana na IS kufanya mashambulizi Uganda

Mahambulio ya ADF/IS karibu na eneo la Beni yamekuwa yakiongezeka kuanzia Mei 2020

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mahambulio ya ADF/IS karibu na eneo la Beni yamekuwa yakiongezeka kuanzia Mei 2020

Eneo la Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo limekuwa katika vita kwa muda mrefu baina ya makundi yenye silaha yanayopigana utawa la nchi hiyo , nchi za Rwanda , Burundi na Uganda.

Moja ya makundi yanayofahamika sana kwa kutekeleza vitendo vya ukatili zaidi ni kikundi hiki kutoka Uganda -Allied Democratic Forces ADF kinachoendesha harakati zake mashariki mwa DRC.

Kikundi hiki chenye itikadi za Kiislamu kilianzishwa ya1990, na kilifahamika katika mzozo wa ndani ya Uganda. Hatahivyo kilipofika DRC kilianza vitendo vya ugaidi na kutangaza kuwa vitendo hivyo vinaendeshwa na Islamic State (IS).

Mnamo Jumanne wiki hii, kulikuwa na mashambulio ya ugaidi katika mji mkuu wa Uganda Kampala, yaliyowauwa watu sit ana kuwajeruhi wengine zaidi ya 30. IS ilitangaza kupitia Telegram yake pamoja na gazeti lake Amaq, ikidai kuwa wapiganaji wake ndio waliotekeleza shambulio hilo.

Vingozi wa Uganda walikuwa tayari wamekwishasema kuwa kikundi hicho cha ADF, kilichojiunga na IS mwaka 2019 ndicho kilichotekeleza shambulio hilo

ADF ilianza vipi?

Kikundi cha ADF kilianzishwa magharibi mwa Uganda ambapo kiliundwa na wanajeshi waliokuwa wakimuunga mkono rais wa zamani wa nchi hiyo Idi Amin, na kuanzisha vita vya kupambana na utawala wa rais wa sasa, Yoweri Museveni, kikundi hicho kikidai kuwa kuwa utawala huo umekuwa ukiwafanyia maasi.

Picha ya Propaganda za IS baada ya shambulio la Ituri

Chanzo cha picha, Propaganda IS

Maelezo ya picha, Picha ya Propaganda za IS baada ya shambulio la Ituri

Kikundi hiki kiliposhindwa na jeshi la Uganda mwaka 2001, kilihamia katika Kivu Kusini katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Baada ya kipindi kirefu cha kusitisha harakati zake, ADF ilisikika tena mwaka 2014 ilipoanza mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya raia wa Congo.

Mwaka 2015, ndipo Musa Seka Baluku alipochukua uongozi wa kundi hili baada ya mtangulizi wake Jamil Mukulu kukamatwa .Bakulu alitangaza kujiunga na IS mwaka 2016.

Hatahivyo kikundi IS kilianza kutangaza kuwa inaendesha harakati zake katika eneo hilo Aprili 2019, ambapo lilikiri kuwa lilitekeleza mashambulio kwenye ngome za kijeshi karibu na mpaka wa Uganda.

IS katika propaganda zake hatahivyo haijawahi kutangaza wazi kuwa IS na ADF waliungana . Mwezi Septemba 2020, Baluku alitangaza kuwa kikundi cha ADF hakipo tena.

Alisema: "Sisi kwa sasa tuko jimbo, jimbo la Afrika ya kati, mojawapo ya maeneo yanayounda Islamic State ".

Hali ikoje katika DRC ?

Kulingana na Shirika la wakimbizi la Umoaja wa Mataifa UNHCR kuanzia mwezi Januari 2021, ADF kimekwisha kuwauwa mamia ya raia wa nchi hiyo wasio na hatia na kuwafurusha makwao wengine zaidi ya 40.000 katika eneo la Beni.

Kundi hilo la wapiganaji limeshindwa kudhibitiwa na vikosi vya serikali ya DRC na vile vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani vilivyopo DRC -Monusco.

Tangia IS iiingie DRC, mashambulio ya mara kwa mara yalianza kuongezeka.

Mashambulio ya IS yamekuwa yakijitokeza katika maeneo yenye harakati za ADF kama vile Beni , Kivu kusini na wakati mwingine mashambulio hayo hufanyika katika jimbo la Ituri kweney mpaka na Kivu kusini.