DRC na Rwanda zasisitiza utekelezaji wa mkataba wa Washington

Jeshi la Jamhuri ya demokrasi ya Congo limeimarisha kampeni yake ya kutaka waasi wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kutoka Rwanda linaloendesha shughuli zake nchini DRC, kujisalimisha kwa mamlaka za Congo au kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO)

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Seif & Martha Saranga

  1. Iran: Marekani ilipe fidia kamili kutokana na Shambulio la Israel

    azx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Balozi wa kudumu wa Iran katika umoja wa mataifa UN Amir Saeed Irvani,ameomba fidia na marekebisho kutoka kwa Marekani kwa waathiriwa,majeruhi na uharibifu uliosababishwa katika taifa lake,kupitia barua yake kwa baraza la usalama.

    Katika barua yake Balozi Irvani alitaja taarifa ya hivi karibuni ya rais Trump kama sababu ya kuhusika kwake moja kwa moja na mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran akisema

    “Marekani na Israel zinawajibika kikamilifu na kwa pamoja kwa vitendo vyao vya uchokozi na matokeo yanayotokana navyo dhidi ya Iran.”

    Aidha Irvani aliandika kwamba Donald Trump alieleza katika mkutano na vyombo vya Habari November 6 kwamba alikuwa na “udhibiti kamili” wa shambulio la Israel dhidi ya Iran.

    Aidha Balozi Irvani pia anazitaja kauli za Trump kuwa tata na kukinzana na za Waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Rubio,ambaye 13 June alikanusha Marekani kuhusika katika shambulizi la Israel dhidi ya Iran.

    Soma Zaidi:

  2. DRC na Rwanda zasisitiza utekelezaji wa mkataba wa Washington

    AXD

    Chanzo cha picha, AFP

    Jeshi la Jamhuri ya demokrasi ya Congo limeimarisha kampeni yake ya kutaka waasi wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kutoka Rwanda linaloendesha shughuli zake nchini DRC, kujisalimisha kwa mamlaka za Congo au kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO).

    Maafisa wa polisi na jeshi la FRDC wamekuwa wakitumia vipaza sauti katika eneo la Walikale, jimbo la Kivu Kaskazini, kuwahimiza waasi hao wajisalimishe.

    Matangazo ya redio na vipeperushi vinavyorushwa kutoka kwenye helikopta pia vinatumika katika kampeni hiyo.

    Oparesheni hiyo pia katika eneo la Pinga, mpakani mwa Masisi, ambako kunatajwa kuwa baadhi ya makundi ya FDLR yanapiga kambi huko.

    Kuwapokonya silaha waasi wa FDLR ni mojawapo ya masuala makuu yanayosababisha mvutano kati ya DRC na Rwanda, na pia ni kipengele muhimu katika makubaliano ya amani yaliyosainiwa kati ya nchi hizo mbili jijini Washington.

    Hata hivyo, mpaka sasa, FDLR haijatoa kauli yoyote kuhusu mpango huo wa amani.

    Wakati huo huo, wawakilishi kutoka Jamuhuri ya demokrasia ya Congo na Rwanda wametia saini Mfumo wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa kikanda (REIF), chini ya usimamizi wa maafisa wa Marekani, katika Mkutano wa Nne wa kamati ya Pamoja ya usimamizi wa Mkataba wa Amani uliofanyika siku ya Ijumaa.

    Kamati hiyo ilieleza wasiwasi wake kuhusu kusuasua kwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Washington, na kuwataka pande husika kuongeza juhudi.

    Hata hivyo, Qatar ilibainisha kuwa mazungumzo yanayoendelea kati ya DRC na AFC/M23 yamepiga hatua katika maeneo muhimu, ikiwemo kubadilishana wafungwa.

    Soma Zaidi:

  3. Maandamano Tanzania: Zaidi ya watu 400 washtakiwa katika mikoa mbalimbali

    .

    Mamia ya watu wamefikishwa mahakamani jana ijumaa katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania, na kufunguliwa mashtaka yaliyohusianishwa na maandamano ya uchaguzi yaliyofanyika wiki iliyopita nchini humo.

    Katika jiji kuu la kibiashara Dar es Salaam watu 240 walipandishwa kizimbani na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

    Katika jiji la pili kwa ukubwa la kibiashara Mwanza watu 172 walipandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma moto na uharibifu wa mali sawa na watu 11 walioshtakiwa katika mkoa wa Kigoma.

    Aidha makao makuu ya nchi Dodoma watu 25 walifunguliwa mashtaka miongoni mwao ya uhaini na wengine ya uharibifu wa mali.

    Katika mashtaka hayo yote uhaini ndio tuhuma nzito zaidi ambayo mtu akipatikana na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.

    Hata hivyo Tanzania haijashuhudia mtu yeyote akinyongwa tangu mwanzoni mwa 1990. BBC haijapata taarifa rasmi kutoka mikoa mingine, lakini ndugu wa karibu wa mwandishi wa habari wa kituo cha Millard Ayo, Godfrey Thomas, wamethibitisha kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka mkoani Arusha.

  4. Afrika Kusini yasikitishwa na uamuzi wa Trump kutohudhuria mkutano wa G20

    AXC

    Chanzo cha picha, AFP

    Afrika Kusini kupitia wizara ya masuala ya kigeni imeelezea masikitiko yake kuhusu uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump, wa kutotuma mwakilishi yeyote wa serikali katika mkutano ujao wa G20.

    Mkutano huo wa kila mwaka huwaleta pamoja viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani, ambapo mwaka huu unafanyika jijini Johannesburg.

    Rais Trump ametangaza kwamba hatahudhuria mkutano huo, akirejelea madai kwamba wakulima wazungu wananyanyaswa nchini Afrika Kusini madai ambayo mara kadhaa yamepuuzwa na wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo.

    Awali, Rais Trump alisema kwamba makamu wake, JD Vance, angehudhuria mkutano huo wa G20, lakini taarifa mpya kutoka Washington zinasema hakuna afisa yeyote wa Marekani atakayeshiriki.

    Wizara ya Mambo ya kigeni nchini Afrika Kusini imepinga madai ya Rais Trump kuhusu unyanyasaji dhidi ya wakulima wazungu, ikiyaita ni ya uongo na yasiyo na msingi.

    Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umeendelea kushuhudia mvutano, huku Rais Trump akikosoa sera ya mageuzi ya ardhi ya Afrika Kusini na hatua ya Pretoria kuishtaki Israel katika Mahakama ya kimataifa ya haki (ICJ) kwa tuhuma za mauaji ya kimbari.

    Aidha, Rais Trump ameweka ushuru wa forodha wa hadi asilimia 30 kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka Afrika Kusini ikiwa ni kiwango cha juu zaidi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara wakati ambapo Pretoria inajiandaa kukabidhi uenyekiti wa G20 kwa Marekani.

    Soma Zaidi:

  5. Israel yasema mwili wa Lior Rudaeff umerudishwa Kutoka Gaza

    azd

    Chanzo cha picha, Hostages and Missing Families Forum

    Jeshi la Israel limesema kuwa limeutambua mwili uliokabidhiwa kutoka Gaza kuwa wa Lior Rudaeff, raia wa Israel mwenye asili ya Argentina.

    Limearifu kwamba Rudaeff aliyekuwa na umri wa miaka 61 aliuawa alipokuwa akijaribu kulinda Kijiji cha Kibbutz Nir Yitzhak wakati wa shambulio la Hamas kusini mwa Israel Oktoba 7 2023, na mwili wake ulikuwa mikononi mwa kundi la wapiganaji wa PIJ.

    Kundi la PIJ limesema lilipata mwili huo siku ya Ijumaa mjini Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

    Kufikia sasa Hamas imerudisha mateka hai 20 na miili ya watu 23 kati ya 28 waliokuwa wamefariki, chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa Oktoba 10.

    Watu wanne kati ya watano waliosalia ambao miili yao haijarudishwa ni raia wa Israel, na mmoja wa Thailand.

    Israel imeikosoa Hamas kwa kushindwa kurudisha miili yote, lakini Hamas imesema ni vigumu kuipata kutokana na kufukiwa na vifusi.

    PIJ ni kundi la kijeshi linaloshirikiana na Hamas, na lilihusishwa katika shambulio la Oktoba 7 pamoja na kuwahi kuwashikilia baadhi ya mateka raia wa Israeli.

    Jukwaa linalofuatilia mateka na familia zilizopotea, limeunga mkono kurejeshwa kwa mwili wa Rudaeff.

    “Kurudishwa kwa mwili wa Lior kunaleta faraja kidogo kwa familia ambayo imeishi katika maumivu na mashaka kwa zaidi ya miaka miwili,” ilieleza sehemu ya tamko la jukwaa hilo. “Hatutapumzika hadi kila mateka atakaporejeshwa nyumbani.”

  6. Kufungwa kwa Serikali Marekani: Maelfu ya safari za ndege zaahirishwa

    acx

    Chanzo cha picha, BBC / Kwasi Asiedu

    Zaidi ya safari 5,000 za ndege nchini Marekani zilisitishwa au kucheleweshwa jana baada ya mashirika ya ndege ya Marekani kuagizwa kupunguza safari za anga wakati wa kufungwa kwa serikali.

    Safari za ndani katika viwanja 40 vya ndege vilivyo na shughuli nyingi zaidi nchini humo zimeathiriwa huku maafisa wakijaribu kupunguza mzigo kwa waongoza ndege.

    Viwanja vya ndege vinakabiliwa na uhaba wa waongoza ndege kutokana na likizo za ugonjwa na ufanyaji kazi bila malipo wakati wa kufungwa kwa serikali ya Marekani.

    Muungano wa wafanyakazi, ambao unawakilisha wahudumu 55,000 wa ndege nchini Marekani, ni sehemu ya kundi lililotoa wito wa kusitishwa ufungwaji wa shughuli za serikali, likisema usalama wa wafanyakazi wa anga uko hatarini.

    “Sababu pekee sekta ya usafiri wa anga inaendelea kufanya kazi wakati wa kufungwa kwa serikali ni kutokana na waongoza ndege wa Marekani na maafisa wa usafiri wanafanya kazi bila malipo.

    Wakati huohuo, kila mtu anayesaidia kazi yao ya kutuhakikishia usalama na ulinzi amerejeshwa nyumbani bila malipo,” alisema Sarah Nelson, rais wa Chama cha Wahudumu wa Ndege

    Soma Zaidi:

  7. Trump aipatia Hungary msamaha dhidi ya vikwazo vya mafuta na gesi

    avx

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameipatia Hungary mwaka mmoja wa msamaha wa vikwazo vinavyohusiana na ununuzi wa mafuta na gesi kutoka Urusi, afisa wa Ikulu ya White House amethibitishia BBC.

    Awali, Trump alisema angefikiria kutoa msamaha huo wa vikwazo, ambavyo vinalenga kusaidia kumaliza vita vya Ukraine, kwa Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban.

    Akizungumza Ijumaa wakati wa ziara ya Orban Ikulu ya White House, Trump alisema huenda kukatolewa kibali maalum kwa sababu “ni vigumu sana kwa Orban kupata mafuta na gesi kutoka maeneo mengine.”

    Kauli hizo zinakuja baada ya Marekani kuwekea vikwazo makampuni mawili makubwa ya mafuta ya Urusi mwezi uliopita, na kutishia kuchukua hatua dhidi ya wale watakaonunua mafuta kutoka kwao.

    Baada ya mkutano huo, Waziri wa Mambo ya kigeni wa Hungary, Péter Szijjártó, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba Marekani imeipa Budapest “msamaha kamili na usio na mipaka dhidi ya vikwazo vya mafuta na gesi.”

    Uamuzi huu wa Trump unachukuliwa kuwa ushindi mkubwa kwa Orban, ambaye awali alisema kuwa vikwazo hivyo vingedhoofisha uchumi wa nchi yake.

    Soma Zaidi:

  8. Wanaharakati wa Kenya Bob Njagi na Nicholas Oyoo waachiliwa baada ya siku 38

    .

    Chanzo cha picha, Bobi Wine/X

    Maelezo ya picha, Wanaharakati hao wa Kenya walikuwa wakisaidia kampeni ya Bobi Wine

    Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Faith Odhiambo, ameunga mkono kuachiliwa kwa wanaharakati Nicholas Oyoo na Bob Njagi, ambao waliachiliwa huko Busia Alhamisi usiku baada ya siku 38 za kutoweka kwa lazima.

    Katika taarifa yake kuhusu X, Odhiambo alisema kuwa pamoja na VOCAL Africa na Amnesty Kenya, wanakaribisha kuachiliwa kwao.

    Alisema wawili hao walikuwa wametoweka kwa zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kuachiliwa, na hivyo kuashiria kile alichokitaja kuwa wakati muhimu kwa watetezi wa haki za binadamu katika eneo hilo.

    "Tunakaribisha kuachiliwa kwa Nicholas Oyoo na Bob Njagi jana usiku huko Busia baada ya siku 38 za kutoweka kwao," taarifa hiyo ilisoma.

    Odhiambo aliwashukuru wale waliofanya kampeni ya kuachiliwa kwao, ikiwa ni pamoja na familia za wanaharakati, Chama Huru cha Kenya, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, na wizara za mambo ya nje nchini Kenya na Tanzania.

    "Tunatoa shukrani zetu kwa familia zao, wenzao wa harakati Huru ya Kenya, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, wizara za mambo ya nje nchini Kenya na Tanzania, na raia wote watendaji ambao wamefanya kampeni bila kuchoka kwa wakati huu," alisema.

    Soma Zaidi:

  9. Mwanajeshi wa zamani wa Uingereza akamatwa kwa madai ya mauaji ya mwanamke Mkenya mwaka 2012

    .

    Chanzo cha picha, COURTESY

    Maelezo ya picha, Marehemu Agnes Wanjiru, ambaye alidaiwa kuuawa na afisa wa Jeshi la Uingereza mwaka wa 2012.

    Mwanajeshi wa zamani wa Uingereza anakabiliwa na kesi nchini Kenya kuhusiana na madai ya mauaji ya mwanamke mwenye umri wa miaka 21 nchini humo mwaka wa 2012.

    Shirika la Kitaifa la kushughulikia Uhalifu (NCA) lilisema Robert James Purkiss alikamatwa huko Tidworth, Wiltshire mnamo Novemba 6 na akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu

    Mkazi ya Westminster Ijumaa. Alikamatwa na maafisa maalum kutoka Kitengo cha Kitaifa cha a NCA kuhusiana na mauaji ya Agnes Manjiru baada ya hati kutolewa mwezi Septemba, shirika hilo liliongeza.

    Bw. Purkiss, mwenye umri wa miaka 38, aliiambia mahakama kwamba alikusudia kupinga kesi hiyo ya kupelekwa Kenya na aliwekwa kizuizini kabla ya kufikishwa tena katika mahakama hiyo hiyo mnamo Novemba 14.

    Mawakili wake waliiambia mahakama kwamba "anakana vikali" shutuma za mauaji dhidi yake.Mwili wa Bi. Wanjiru uligunduliwa kwenye tanki la maji taka karibu na hoteli katika mji wa Nanyuki, yapata maili 200 kaskazini mwa Nairobi, miezi mitatu baada ya kupotea mnamo Machi 31, 2012.

    Alikuwa na mtoto wa miezi mitano wakati huo.

    Mwili wake ulipatikana karibu na kambi ya mafunzo ya jeshi la Uingereza. Usiku aliouawa, inasemekana alikuwa kwenye baa na marafiki ambapo wanajeshi wa Uingereza pia walikuwepo.

    Soma Zaidi:

  10. Israel yapokea jeneza, Hamas yasema lina mwili wa mateka wa Gaza

    .

    Chanzo cha picha, MOHAMMED SABER/EPA/Shutterstock

    Maelezo ya picha, Shirika la Msalaba Mwekundu lilisaidia tawi la kijeshi la Hamas kutafuta miili ya mateka tarehe 5 Novemba

    Israeli imepokea jeneza ambalo Hamas na Palestina Islamic Jihad walisema lina mwili wa mateka, jeshi la Israeli linasema.

    Hamas walisema mwili huo ulipatikana Ijumaa huko Khan Younis kusini mwa Gaza. Mwili huo umesafirishwa hadi Israel kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu kwa ajili ya utambuzi.

    Kabla ya makabidhiano haya, Hamas ilikuwa imewarudisha mateka wote 20 walio hai na mateka 22 kati ya 28 waliokufa chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza tarehe 10 Oktoba.

    Watano kati ya mateka sita waliokufa ambao bado wako Gaza walikuwa Waisraeli na mmoja alikuwa rais wa Thailand. Israel imeikosoa Hamas kwa kutorudisha miili yote. Hamas inasema ni vigumu kuwapata chini ya vifusi.

    Soma Zaidi:

  11. Waziri wa Ulinzi wa Pakistan: Mazungumzo na serikali ya Taliban huko Istanbul 'yamefeli'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Khawaja Muhammad Asif anasema duru ya tatu ya mazungumzo ya Istanbul imeshindwa kwa sababu, kulingana naye, wawakilishi wa nchi yake hawakuweza kutatua "tofauti kubwa" na serikali ya Taliban nchini Afghanistan.

    Ameongeza kuwa usitishaji vita kati ya nchi yake na serikali ya Taliban utaendelea kuwepo maadamu hakuna mashambulizi yoyote yatakayotekelezwa kutoka ardhi ya Afghanistan.

    Duru ya tatu ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa pande hizo mbili, iliyoanza mjini Istanbul siku ya Alhamisi kwa upatanishi wa Uturuki na Qatar, iliendelea kwa siku ya pili mfululizo hapo jana.

    Wakati huo huo, Tahir Hussain Andrabi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba "hakuna mkwamo" katika mazungumzo ya amani yanayoendelea na serikali ya Taliban nchini Afghanistan.

    Kwa upande mwingine, saa chache kabla ya matamshi ya Bwana Asif, Noorullah Noori, Waziri wa Mipaka na masuala ya Kikabila wa serikali ya Taliban, alionya Pakistan kutokuwa na "kiburi" kwa kuwa na teknolojia ya hali ya juu.

    Soma Zaidi:

  12. Mahakama ya Uturuki yatoa vibali vya kukamatwa kwa Netanyahu na waziri wake

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Hatua hii ya kiishara inakuja wakati serikali ya Marekani inatambua jukumu muhimu la Türkiye katika kusaidia kuwapokonya silaha Hamas.

    Mamlaka ya mahakama ya Uturuki imetoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wake wa ulinzi na maafisa wengine 35 wakuu wa Israel kwa tuhuma za "uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari."

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Istanbul ilisema hukumu hizo zinahusiana na vitendo vyao huko Gaza na dhidi ya kundi la kimataifa ambalo lilikuwa likijaribu kutoa msaada kwa Wapalestina waliozingirwa. Israel imekanusha vikali tuhuma za kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza.

    Hatua hiyo ya kiishara inakuja wakati serikali ya Marekani imezidi kukiri jukumu muhimu la Uturuki katika kusaidia kuwapokonya silaha Hamas na uwezekano wa kushiriki katika kikosi cha kimataifa cha kuunganisha mpango wa amani wa Donald Trump huko Gaza.

    Ripoti zinaonyesha kuwa uamuzi wa mamlaka ya mahakama ya Uturuki ulifanywa ndani ya mfumo wa uchunguzi wa "uhalifu uliofanyika" wakati wa mashambulizi ya Israel dhidi ya raia, hospitali, na misafara ya misaada, hasa "Global Solidarity Convoy" huko Gaza.

    Soma Zaidi:

  13. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja