Maandamano Tanzania: Zaidi ya watu 600 washtakiwa katika mikoa mbalimbali

.
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mamia ya watu wamefikishwa mahakamani jana ijumaa katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania, na kufunguliwa mashtaka yaliyohusianishwa na maandamano ya uchaguzi yaliyofanyika wiki iliyopita nchini humo.

Kwa mujibu wa chama cha wanasheria Tanganyika TLS waliofikishwa mahakamani ni watuhumiwa 641, wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo uhaini.

Mmoja wa mawakili wa TLS William Maduhu amewaambia waandishi wa habari kwamba mkoa wa Dare es salaam unaongoza kwa watuhumiwa zaidi ya 400.

Aidha amesema Mwanza ina zaidi ya watuhumiwa 200, Kilimanjaro 312, Mbeya zaidi ya 300, Njombe 12 na Tabora 5.

Katika jiji la pili kwa ukubwa la kibiashara Mwanza watu 172 walipandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya unyang'anyi wa kutumia silaha, kuchoma moto na uharibifu wa mali sawa na watu 11 walioshtakiwa katika mkoa wa Kigoma.

Aidha makao makuu ya nchi Dodoma watu 25 walifunguliwa mashtaka miongoni mwao ya uhaini na wengine ya uharibifu wa mali.

BBC haijapata taarifa rasmi kutoka mikoa mingine, lakini ndugu wa karibu wa mwandishi wa habari wa kituo cha Millard Ayo, Godfrey Thomas, wamethibitisha kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka mkoani Arusha.

Kwa upande wa mfanyabishara Jenipher Jovin maarufu kama Niffer Pamoja na mashtaka ya njama za uhaini na uhaini pia anashtakiwa kwa uchochezi wa kuhamasisha umma kununua barakoa za kuzuia moshi wa kutoa machozi wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi wa Oktoba 29,2025.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anatuhumiwa Kutenda kosa hilo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar Es Salaam kati ya August 01 mpaka Oktoba 24, 2025.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania mashtaka ya uhaini hayana dhamana na adhabu yake kwa atakayekutwa na hatia ya kosa hilo ni kifo.

Hata hivyo Tanzania haijashuhudia mtu yeyote akinyongwa tangu mwanzoni mwa 1990.

Katika maandamano yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi, watu kadhaa wamepoteza maisha, wakitaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki.

Bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu tathmini ya madhara yaliyotokea kutokana na maandamano hayo makubwa zaidi kuwahi kutokea kuhusu uchaguzi tangu nchi hiyo ipate uhuru miongo zaidi ya sita iliyopita.

Maandamano hayo yaliyoanzia jijini Dar es Salaam na kusambaa katika maeneo mengine ikiwemo majiji ya Arusha, Mwanza, Mbeya, na Dodoma, na maeneo ya mikoa mingine yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya umma na binafsi, ikiwemo vituo vya Polisi, ofisi za umma zikiwemo za chama tawala (CCM), vituo vya mafuta na maduka kadhaa.