UAE imefadhili mauaji ya kisiasa nchini Yemen, uchunguzi wa BBC

Chanzo cha picha, JACK GARLAND/BBC
- Author, Nawal al-Maghafi
- Nafasi, BBC
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umefadhili mauaji yanayochochewa kisiasa nchini Yemen, uchunguzi wa BBC umegundua, na hivyo kuzidisha mzozo unaohusisha serikali ya Yemen na kundi la Houthi.
Mafunzo ya kukabiliana na ugaidi yanayotolewa na mamluki wa Marekani kwa maafisa wa Imarati nchini Yemen, yametumika kutoa mafunzo kwa wenyeji.
BBC pia imegundua kuwa lengo la mamluki wa Marekani ni kuangamiza vikundi vya wanajihadi vya al-Qaeda na Islamic State (IS) kusini mwa Yemen, lakini UAE imeendelea kuwaajiri wanachama wa zamani wa al-Qaeda katika kikosi cha usalama ili kupambana na waasi wa Houthi na vikundi vingine vyenye silaha.
Serikali ya UAE imekanusha na kueleza kuwa madai kwamba imeuwa watu wasio na uhusiano na ugaidi "ni ya uwongo na hayana mashiko".
Vita vya Yemen
Nimekuwa nikiripoti kuhusu mzozo katika nchi yangu ya asili ya Yemen tangu ulipoanza mwaka wa 2014. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisha serikali kupoteza udhibiti wa eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kwa Wahouthi.
Mwaka 2015, Marekani na Uingereza ziliunga mkono muungano wa mataifa Kiarabu yakiongozwa na Saudi Arabia - na UAE kama mshirika mkuu - kupigana.
Muungano huo uliivamia Yemen kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali ya Yemen iliyo uhamishoni na kupambana na ugaidi. UAE ilipewa dhamana ya usalama kusini, na ikawa mshirika mkuu wa Marekani katika kukabiliana na ugaidi katika kanda ambayo - al-Qaeda imekuwepo kwa muda mrefu kusini.
Wakati wa safari zangu za kuripoti mara kwa mara - nilishuhudia wimbi la mauaji ya ajabu katika maeneo ya kusini yanayodhibitiwa na serikali ya Yemen.
Chini ya sheria za kimataifa, mauaji yoyote ya raia bila kufuata utaratibu yatahesabiwa kuwa ni haramu. Wengi wa waliouawa walikuwa wanachama wa Islah - tawi la Yemen la Muslim Brotherhood.
Ni vuguvugu maarufu la kimataifa la Kiislamu la Sunni ambalo halijawahi kuainishwa na Marekani kama shirika la kigaidi, lakini limepigwa marufuku katika nchi kadhaa za Kiarabu - ikiwa ni pamoja na UAE ambapo harakati zake za kisiasa na uungawji - unaonekana na familia ya kifalme ya nchi kama tishio kwa utawala wao.
Mamluki wa Marekani

Chanzo cha picha, JACK GARLAND/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Video iliovuja ya ndege zisizo na rubani katika operesheni ya kwanza ya mauaji zilinipa mahali pa kuanzia ambapo nitachunguza mauaji haya. Iliwekwa Desemba 2015 na ni video ya wanachama wa kampuni ya kibinafsi ya usalama ya Marekani iitwayo Spear Operations Group.
Hatimaye nilikutana na mmoja wa watu waliohusika na operesheni iliyoonyeshwa kwenye video katika mkahawa mmoja huko London mwaka wa 2020.
Isaac Gilmore, alikuwa mwanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani, Navy Seal, ambaye baadaye alikuja kuwa afisa mkuu wa uendeshaji wa Spear. Alikuwa mmoja wa Waamerika kadhaa ambao waliajiriwa kutekeleza mauaji huko Yemen na UAE.
Alikataa kuzungumza kuhusu mtu yeyote ambaye alikuwa kwenye "orodha ya kuuwawa" iliyotolewa kwa Spear na UAE – isipokuwa atazungumzia tu opereseheni yao ya kwanza:
Ansaf Mayo, mbunge wa Yemen ambaye ni kiongozi wa Islah katika mji wa bandari wa kusini wa Aden, mji mkuu wa muda wa serikali tangu 2015.
Nilimkabili Gilmore juu ya ukweli kwamba Islah hajawahi kuainishwa kama gaidi na Marekani.
"Migogoro ya kisasa kwa bahati mbaya ni siri nyingi," alisema. "Tumeona hilo nchini Yemen - kiongozi wa kiraia wa mtu mmoja na mhubiri, ni kiongozi wa kigaidi kwa mtu mwingine."
Gilmore, na mfanyakazi mwingine wa Spear nchini Yemen wakati huo - Dale Comstock - waliniambia operesheni zao Yemen ziliisha mwaka 2016. Lakini mauaji kusini mwa Yemen yaliendelea. Kwa hakika yalizidi kuongezeka, kulingana na wachunguzi kutoka kundi la haki za binadamu la Reprieve.
Walichunguza mauaji 160 yaliyotekelezwa nchini Yemen kati ya 2015 na 2018. Walisema idadi kubwa ya mauaji yalitokea kuanzia 2016 na ni watu 23 tu kati ya 160 waliouawa walikuwa na uhusiano na ugaidi.
Mauaji yote yalikuwa yametekelezwa kwa kutumia mbinu zile zile ambazo Spear walikuwa wakitumia - ulipuaji wa kilipuzi cha ovyo, na kufuatiwa na shambulizi.
Mauaji ya karibuni zaidi ya kisiasa nchini Yemen, kulingana na wakili wa haki za binadamu wa Yemen, Huda al-Sarari, yalitokea mwezi uliopita tu - ya imamu aliyeuawa huko Lahj kwa njia hiyo hiyo.
Gilmore, Comstock, na mamluki wengine wawili kutoka Spear ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walisema Spear ilihusika kuwafunza maafisa wa Imarati katika kambi ya kijeshi ya UAE huko Aden.
Mwandishi wa habari ambaye aliomba jina lake lisitajwe pia alituambia ameona picha za mafunzo hayo.
Afisa wa Yemen azungumza

Chanzo cha picha, JACK GARLAND/BBC
Mamluki hawakuweza kueleza kwa undani kile walichofanya huko, lakini afisa mkuu wa kijeshi wa Yemeni kutoka Aden, ambaye alifanya kazi moja kwa moja na UAE, alinipa maelezo zaidi.
“Mamluki hao walitoa mafunzo mafunzo kwa maafisa wa Imarati, ambao nao waliwafundisha Wayemeni wa eneo hilo kulenga shabaha," afisa wa kijeshi wa Yemeni aliniambia.
Pia tulizungumza na vyanzo vingine zaidi ya kumi na mbili Yemeni ambavyo vilisema ndivyo ilivyokuwa. Waliwataja wanaume wawili ambao walisema walifanya mauaji ambayo hayakuhusiana na ugaidi, baada ya kupewa mafunzo ya kufanya hivyo na askari wa Imarati.
Kufikia 2017, UAE iliunda kikosi cha wanamgambo kama sehemu ya Baraza la Mpito la Kusini mwa Imarati (STC), baraza la usalama linaloendesha mtandao wa makundi yenye silaha kote kusini mwa Yemen.
Kikosi hicho kilifanya kazi kusini mwa Yemen bila ya serikali ya Yemen, na kilipokea tu maagizo kutoka UAE. Wapiganaji hawakufunzwa tu kupigana kwenye mstari wa mbele - kilifunzwa pia kufanya mauaji, mtoa taarifa wetu alituambia.
Mtoa taarifa huyo alituma waraka wenye majina 11 ya waliokuwa wanachama wa al-Qaeda ambao sasa wanafanya kazi katika STC, baadhi yao tuliweza kujithibitisha wenyewe.
Wanachama wa al-Qaeda
Wakati wa uchunguzi wetu pia tulikutana na jina la Nasser al-Shiba. Wakati mmoja alikuwa mtendaji wa cheo cha juu al-Qaeda, alifungwa jela kwa ugaidi lakini baadaye aliachiliwa.
Waziri wa serikali ya Yemen tuliyezungumza naye alituambia al-Shiba alikuwa mshukiwa anayejulikana katika shambulio la meli ya kivita ya Marekani USS Cole, ambalo liliua mabaharia 17 wa Marekani Oktoba 2000.
Vyanzo vingi vilituambia kwa sasa ni kamanda wa moja ya vitengo vya kijeshi vya STC.
Wakili Huda al-Sarari amekuwa akichunguza ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi hivi vinavyoungwa mkono na UAE.
Na mara nyingi alikuwa akipokea vitisho vya kuuawa. Lakini ni mtoto wake Mohsen mwenye umri wa miaka 18 ambaye alilipa gharama kubwa.
Alipigwa risasi kifuani Machi 2019 akiwa safarini kwenye kituo cha mafuta cha eneo hilo, na akafa mwezi mmoja baadaye. Huda aliporejea kazini baada ya kifo chake, anasema alipokea ujumbe wa kumuonya. "Je, mwana mmoja hajatosha? Unataka tumwue mwingine?"
Uchunguzi uliofuata wa mwendesha mashtaka wa umma wa Aden uligundua kuwa Mohsen aliuawa na mwanachama wa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi kinachoungwa mkono na UAE, lakini mamlaka haijawahi kufungua mashtaka.
Wajumbe wa ofisi ya mwendesha mashtaka - ambao hatuwezi kuwataja kwa sababu za usalama - walituambia mauaji yaliyoenea yamezua hali ya hofu - inamaanisha hata wao wanaogopa sana kutafuta haki katika kesi zinazohusisha vikosi vinavyoungwa mkono na UAE.
Reprieve imepokea hati iliyovuja ya UAE inayoonyesha Spear ilikuwa bado inalipwa hadi 2020, ingawa haijabainika ni kwa kiwango gani.
Tulimuuliza mwanzilishi wa Spear, Abraham Golan, ikiwa mamluki wake walitoa mafunzo kwa Imarati ya mbinu za mauaji, lakini hakujibu.
Nayo serikali ya UAE ilisema si kweli kwamba ililenga watu wasio na uhusiano wowote na ugaidi. Inaunga mkono operesheni za kukabiliana na ugaidi nchini Yemen kwa mwaliko wa serikali ya Yemen na washirika wake wa kimataifa.
Tuliomba Idara ya Ulinzi ya Marekani na Wizara ya Mambo ya Nje kuzungumza nasi kuhusu Kundi la Spear, lakini walikataa.
Na shirika la kijasusi la serikali ya Marekani lilisema katika taarifa yake: "Wazo kwamba CIA ilitia saini operesheni hiyo ni ya uongo."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












