Mtoto wa bilionea wa Kiarabu akiri kwa BBC kuhusika katika mauaji ya mwanafunzi wa kike

Chanzo cha picha, ODD PETTER
Mtoto wa kiume wa bilionea huyo, ambaye alikimbilia Yemen saa chache baada ya mauaji ya mwanafunzi huko London miaka kumi na tano iliyopita, amekiri kwa BBC kwamba alihusika katika mauaji yake.
Mwili wa Martin Vic Magnussen, mwenye umri wa miaka 23, uligunduliwa ukiwa umefukiwa chini ya vifusi katika sehemu ya chini ya nyumba kwenye Mtaa wa Great Portland mwaka wa 2008.
Tangu wakati huo, familia yake imekuwa ikitafuta haki.
Farouk Abd al-Haq, ambaye anaongoza katika orodha inayosakwa na polisi wa Uingereza, na ambaye hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake imetolewa, hajawahi kuzungumza katika kesi hii.
Aliambia BBC kwamba kifo cha Martin Vik Magnussen kilitokana na "ajali ya ngono iliyokwenda mrama".
Hata hivyo, Abdul Haq, ambaye alisoma na Vic Magnussen, pia alisema hayuko tayari kurejea Uingereza kuzungumza na polisi, kwa kuwa "amechelewa".
Nilikuwa mwanafunzi wakati mwili wa Martine ulipopatikana, na nilipata mshtuko mkubwa, haswa wakati niliposikia madai kuwa mshukiwa mkubwa wa mauaji yake alikuwa Myemen - na mimi pia natoka Yemen.
Kwa hiyo simulizi hii ilikuwa moja ya nilizozipa kipaumbele nilipojiunga na BBC kama mwandishi wa habari mwaka wa 2011.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lengo langu kuu wakati huo lilikuwa kupata majibu kutoka kwa familia ya Martine, wanaoona mauaji yake kama mtihani wa sheria za kimataifa, hasa kwa vile hakuna makubaliano kati ya Uingereza na Yemen ya kubadilishana wafungwa na wale waliofunguliwa mashtaka kisheria.
Hata hivyo, sikuweza kuwasiliana na Farouk Abdelhak hadi mwaka jana.
Nilianza kuwasiliana naye kwenye mitandao ya kijamii.
Mamia ya waandishi wa habari wamejaribu kuwasiliana naye katika kipindi cha miaka kumi na minne iliyopita, lakini amewapuuza wote.
Hata hivyo, malezi yetu ya pamoja ya Wayemeni yalinisaidia kupata imani yake.
Baada ya siku kumi za mawasiliano kati yetu, alinitumia ujumbe wa kwanza ambao ungebadilika na kuwa jumbe nyingi za ufichuzi.
"Nilifanya jambo nilipokuwa mdogo, na lilikuwa kosa," aliandika katika mojawapo ya barua hizo.
Kupitia maelfu ya ujumbe wa maandishi na maelezo ya sauti aliyonitumia kwa muda wa miezi mitano, hakuwahi kutumia jina la Martine, wala hakurejelea kifo chake, akipendelea kutumia neno "ajali."
Hata hivyo, ripoti ya kitaalamu ilifafanua maelezo ya kifo cha kikatili cha mwanafunzi huyo wa Norway - kutokana na kushinikizo shingoni, ambayo ina maana kwamba "huenda alinyongwa, kubanwa chini kwa nguvu na kushindwa kupumua."
Mwili wake ulikuwa na majeraha na mikwaruzo 43 aliyopata, "baadhi ya hayo yanaonyesha wazi kuwa alishambuliwa au aliyopata wakati wanakabiliana."

Farouk na Martine wote walisoma katika Shule ya Biashara ya Regent huko London, na Martine alitarajia kupata kazi katika sekta ya fedha na biashara katika mji mkuu.
Mara ya mwisho marafiki zake walimwona akiwa hai ilikuwa mapema Machi 14, 2008, katika klabu ya usiku ya kipekee ya Maddox huko Mayfair London, ambapo yeye na Farouk walikuwa wakisherehekea kumalizika kwa mitihani.
Marafiki wanasema kuwa Farouk alijitolea kuandaa tafrija katika nyumba yake kwenye Mtaa wa Great Portland katikati mwa London.
Marafiki walikuwa wamechoka, lakini wanasema Martine alitaka kuendelea kusherehekea - kamera za usalama zinaonyesha aliondoka na Farouk saa 2:59 asubuhi. Hakuna mashahidi wa kilichotokea baadaye.
Na kabla ya jua kuchomoza, Martine alikuwa ameaga dunia - ingawa mwili wake haukugunduliwa hadi baada ya saa 48 baadaye.
Kufikia wakati huo, Farouk alikuwa ameondoka Uingereza kwa ndege kuelekea Cairo. Kisha akapanda ndege binafsi ya baba yake, kuelekea Yemen.
Wakili wake anasisitiza kuwa hana hatia ya mauaji hayo.
Farouk hakuwa raia wa kawaida wa Yemen. Alikulia kati ya Marekani na Misri.
Yeye ni mtoto wa Shaher Abdulhak, - mmoja wa Wayemen tajiri zaidi na wenye mamlaka nchini humo.
Alikuwa na himaya ya biashara ya sukari, vinywaji baridi, mafuta na biashara ya silaha, na pia alikuwa rafiki wa karibu wa rais wa Yemeni wakati huo, Ali Abdullah Saleh.
Nilipojaribu kuwasiliana na Farouk kwa mara ya kwanza katika mwaka wa elfu 2011, nilitumia miezi mingi nchini Yemen kumtafuta. Lakini nililazimika kuondoka mamlaka iliponiambia niachane na simulizi hiyo.
Mnamo Februari mwaka wa 2022, niliamua kusikiliza kesi hiyo tena, kutoka London. Wakati huo, Baba yake Farouk alikuwa amefariki na Rais Saleh alikuwa amepinduliwa. Nilijiuliza iwapo nitafanikiwa kumtafuta Farouk aongee.
Lakini pia nilijua haingekuwa rahisi. Rafiki yangu alipofanikiwa kupata nambari yake, nilimtumia ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutumia programu nyingi za simu, lakini hakujibu. Kisha rafiki yangu akagundua kuwa Farouk alikuwa akitumia Snapchat.

Nilimtumia ujumbe, na baada ya sekunde chache nikapata jibu lake. Swali lake la kwanza kwangu lilikuwa kuhusu mahali nilipo. Nilimpa jina la kitongoji jirani huko Yemen ambacho nilikulia nikihisi kuwa na yeye pia alikuwa akiishi huko.
Nikawa nimegonga ndipo na papo hapo nikaona ile hamu ya yeye kutaka kuzungumza na mimi tena ikawa imeisha lakini udadisi wake ukaongezeka.
Sasa kwa kuwa nilikuwa nimeanzisha mazungumzo naye, ilikuwa ni swala la muda tui li kupata Imani yake tena, hasa kwa vile sikuwa nimeficha kazi yangu tangu mwanzo.
Aliponiuliza nilichokuwa nafanya mwanzo kabisa nilimjibu moja kwa moja kuwa mimi ni mwandishi wa habari.
Ujumbe wetu wa kwanza ilikuwa juu ya tajriba yetu ya pamoja. Licha ya utajiri wake, kwa namna fulani tulikuwa na mengi tunayoendana.
Tulibadilishana simulizi kuhusu kuteleza kwenye theluji katika eneo moja la mapumziko la Uswizi, kusoma katika shule zilizo na mitaala ya kimataifa, na maeneo ambayo sisi sote tunapenda kutembelea London.
Na hapa ilianza kufunguka kidogo kidogo.
"Nilifanya kitu nilipokuwa mdogo, na ilikuwa makosa ...", aliandika katika moja ya ujumbe wake. "Nimekuambia jina langu halisi, siwezi kurudi Uingereza kwa sababu ya kitu kilichotokea huko."
"Sababu pekee ya mimi kuogopa kukueleza ni kwa kuwa uliniambia wewe ni mwandishi wa habari."
"Wewe ndiye mtu wa mwisho ninayehitaji kuzungumza naye."
Kasi ambayo alinipa ujasiri kuwa ataniamini inaweza kuonekana ya lakini ikumbukwe kwamba Farouk ametengwa sana.
Familia yake yote inaishi nje ya Yemen, ikiwa ni pamoja na mke wake wa zamani na binti yake, ambaye alitoroka nchi kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo, yeye hawezi kumtembelea yeyote kati yao kwa kuhofia kukamatwa.
Hakuna hata mmoja wa rafiki zake niliyezungumza naye wakati wa uchunguzi wangu amewahi kuwasiliana naye tangu alipokimbia.
Hata hivyo, walikubaliana kwa kauli moja kuonesha mshtuko waliposoma kuhusu kifo cha Martine wakati huo, na walisema kwamba madai ya kuhusika kwake yalionekana kuwa ya ajabu kwa utu wake.

Chanzo cha picha, CECILIE DAHL
Sasa kwa kuwa Farouk alikuwa tayari kuzungumza na kufichua zaidi, nilimwambia kwamba nilifanya kazi BBC na nilitaka kuripoti kuhusu kisa chake.
Cha kushangaza ni kwamba, hii haikumzuia kuzungumza.
Kwa hivyo, kikamwomba aeleze ujumb uliyotangulia kwamba alikuwa na "majuto makubwa," alijibu:
"Kwanza, ninajutia tukio hilo la kusikitisha lililotokea. Pili, ninajuta kwamba nilikuja hapa [Yemen], wakati nilipaswa kusalia huko na kulipa nilichokitenda."
Wakati huohuo, nilikuwa pia nikiwahoji watu waliohusika katika kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na baba ya Martine na marafiki zake wa karibu.
Hii ilifanya uchunguzi huu kuwa moja ya yenye changamoto zaidi ambayo nimefanya katika kazi yangu hadi hii leo.
Nikiwa nazungumza na wale ambao maisha yao yalivurugika kutokana na kifo cha Martine, na ambao walikuwa wamekata tamaa ya kupata majibu, simu yangu iliendelea kupokea ujumbe kutoka kwa Farouk.
Nina Brantzig na Cecile Daal ni marafiki wawili wa Martine ambao walikuwa naye kwenye klabu ya Maddox usiku wa kifo chake. Cécile aliwahi kukutana na Farouk na Martine hapo awali, na anasema walikuwa marafiki.
Lakini anaongeza kuwa usiku huo alikuwa tofauti, na kwamba alikasirika wakati mmoja wao alipiga picha yake na Martine, ingawa Martine hakuonekana kujua chochote kisicho cha kawaida.
Rafiki mwingine wa Martine, Tala Lassen, anasema anafikiri Farouk aliwahi kujaribu kumbusu Martine, lakini akamwambia kwamba hapendezwi na uhusiano huo.
Kwa hakika, anasema kwamba Martine kwa kawaida alilala kwenye nyumba ya Farouk kwa sababu ilikuwa katikati ya jiji.
Kamera za uchunguzi zinaonyesha kwamba aliondoka kwenye klabu ya usiku akiwa ameshikana mkono na Farouk.
Wakati Martine hakurudi nyumbani siku iliyofuata, marafiki zake waliandikisha ripoti kwamba alikuwa ametoweka, lakini polisi hawakuchukua hatua kali hadi walipogundua kuwa Farouk alikuwa amefuta akaunti yake ya Facebook.
Walipekua nyumba ya Farouk, na polisi wakagundua mwili wa Martine ukiwa nusu uchi kwenye eneo la chini ya ghorofa.
Wakati huo, Farouk alikuwa ameondoka Uingereza.
Polisi walijua kwamba alikuwa ameondoka kwa ndege ya kibiashara kutoka London hadi Cairo, lakini hawakuwa na maelezo zaidi ya kutoroka kwake.

Chanzo cha picha, CECILIE DAHL
Niliweza kuwafikia marafiki wa karibu wa baba yake Farouk huko London mtu ninayempa jina Samir.
Aliniambia kuwa alipokea simu kutoka kwa Farouk asubuhi ya tarehe 14 Machi ikimtaka amtumie kiasi cha pesa, akidai kuwa na dharura ilimlazimu kwenda nyumbani Cairo lakini kadi zake za mkopo hazifanyi kazi.
Samir aliongeza kuwa akiwa nje ya nyumba yake kutoa pesa, Farouk alizimia kwenye kochi, jambo ambalo lilimlazimu kummwagia maji ya barafu usoni ili kumwamsha.
“Ilionekana kana kwamba alikuwa na kitu kinachomsumbua,” Samir alinieleza.
Aliongeza kuwa Farouk alinunua tikiti kwenye ndege ya karibu zaidi kuelekea Cairo, na kutoka hapo tunajua kwamba baba yake alimpeleka Yemen, mahali ambapo Farouk alikuwa hajawahi kuishi kabisa, lakini ambapo haiwezekani kumrudisha kutoka huko ili kuja kuhukumiwa kwa makosa aliyotenda.
Nilizungumza kuhusu hili kwa undani zaidi na rafiki mwingine wa baba yake Farouk, mfanyabiashara wa Jordan Abdul Hay al-Majali.
"Mtoto wake wa kiume alitaka kurudi London na kufika mahakamani kujitetea," aliniambia (Abdul Hayy). "Lakini baba yake alimshauri asijihusishe (katika kesi hiyo) na badala yake asalie Yemen milele."
Jessica Wadsworth, afisa wa polisi aliyeongoza uchunguzi wa kesi hiyo, anakiri kwamba alisikitika sana alipotambua mahali Farouk alikuwa ameenda.
"Kwa sababu, bila shaka, ulikosa fursa. Sijawahi kufanya uchunguzi wa mauaji... ambapo unagundua baada ya siku tatu au nne kwamba mshukiwa hawezi kufikiwa," Jessica alisema.

Polisi walikutana na wanafamilia wa Martine muda mfupi baada ya ndege yao kutoka Norway kutua na kuwaeleza habari hizo.
Baba yake, Odd Peter Magnussen, aliniambia kuhusu hofu aliyohisi alipoenda kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kutambua mwili wa binti yake.
"Kama mzazi, huo ndio wakati mgumu zaidi maishani mwangu. Sikuweza kukata tamaa kwa Martine. Sikuweza kumuacha. Kwa hiyo nilikaa naye [katika chumba cha kuhifadhia maiti] kwa dakika tano zaidi. Nilikuwa nikimuaga."
Kama baba mwenye kiu ya haki, Odd Butter alimwandikia Malkia Elizabeth II mwaka 2010, na yeye akapeleka kesi hiyo ya mauaji kwa Meya wa London wa wakati huo, Boris Johnson.
Bw. Peter amepokea matoleo kadhaa ya kujitolea kwa serikali kumsaidia katika kesi hiyo. Niliendelea kuwasiliana naye mara kwa mara katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, kila mara akiahidi kutafuta majibu kuhusu nini kilimtokea binti yake.
Na hatimaye nilipata fursa ya kusikia maelezo ya Farouk ya kile kilichotokea usiku ule, nimekuwa nikijaribu kwa njia ya mawasiliano kwa takriban mwezi mmoja sasa kuuchambua ukweli hatua kwa hatua.
Nawal: "Unataka kuniambia kilichotokea?"
Farouk: "Sijui ni nini kilitokea, kila kitu hakiko sawa kwangu."
Farouk: "Ninapata kumbukumbu mara kwa mara."
Farouk: "Nikinusa manukato ya wanawake fulani, sijisikii vizuri."
Hatimaye nikazungumza naye kwa njia ya simu. Nilimuuliza kama atakuwa tayari kurudi Uingereza kukabiliana na matokeo ya mauaji ya Martine.
"Sidhani haki itatendeka," aliniambia mara moja. "Nadhani mfumo wa haki ya jinai huko [Uingereza] unapendelea sana. Pia nadhani wanataka kunitolea mfano mimi mtoto wa Mwarabu na pia kama mtoto wa tajiri... hilo limechelewa,” alisema.
Nilisafiri kwenda Yemen kujaribu kukutana naye ana kwa ana, lakini baada ya kufika huko aliniambia angependelea kukutana nami nyumbani kwake - hatari ambayo singeichukua.
Nilimweleza jinsi baba yake Martine anavyosubiri kwa hamu na ghamu kutaka kujua na kupata majibu kuhusu kilichotokea.
"Kama mwanaume, kama mwanadamu, kama mtu mwenye maadili, nadhani napaswa kufanya hivyo," aliniambia kwa njia ya simu. Lakini aliendelea: "Kuna mambo ambayo ni bora kutosema. Kwa kweli, ikiwa sitakumbuka kile kilichotokea, hakika hakuna cha kusema."
Niliporudi London, nilijaribu tena kupata ukweli, nikamtumia ujumbe mfupi wa simu kuwa ningetaka kujua kilichotokea.
Kisha akajibu,
"Ilikuwa ajali tu. Hakuna jambo la kuudhi lililotokea. Tukio la kufanya tendo la ngono ambalo lilimalizika vibaya," aliendelea.
"Hakuna anayejua kwa sababu nilishindwa kuunganisha na kujua kilichotokea," alisema.
Nilipomuuliza kwa nini, alijibu kwa neno moja tu: "kokeini."
Nikamuuliza kama amewahi kuongea na mwanasheria hapa (Uingereza). Alisema alikuwa amefanya hivyo.
"Niamini, mimi kisheria nina [makosa]," alituma ujumbe mfupi.
[Kwa sababu] ya "kuondoka nchini na kuhamisha mwili."
Nilimuuliza sababu iliyomsukuma kuuhamisha mwili kutoka mahali ulipokuwa.
"Sikumbuki," alijibu kwa kutuma ujumbe mfupi.
Kisha nikamuuliza ikiwa aliwahi kufikiria kujisalimisha, na akasema kwamba wanasheria walimshauri asichukue hatua hiyo, kwa sababu sasa "aliwajibika kwa adhabu kali."
"Hilo limeshapita Nawal."
Nilimwomba mara nyingi katika mazungumzo yetu kurekodi mahojiano yetu, lakini alikataa.












