Wanajeshi majeruhi 200 wa SADC wakiwemo Watanzania warejeshwa nyumbani

Wanajeshi hao waliondoka Goma na kuvuka mpaka na kuingia Rwanda kuelekea Kigali kwa ajili ya kupata ndege za kuwarejesha makwao.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Yusuf Mazimu & Mariam Mjahid

  1. Shukran kwa kufuatilia matangazo yetu ya moja kwa moja. Usiku mwema

  2. COP 16 2025: Hazina ya Fedha ya kufadhili Bio-Anuwai yazinduliwa mjini Roma

    Mikutano ya kilele ya Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai hufanyika kila baada ya miaka miwili - mwaka huu huko Cali, Colombia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mikutano ya kilele ya Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai hufanyika kila baada ya miaka miwili - mwaka huu inafanyika huko Cali, Colombia

    Na Sarafina Robi

    BBC Swahili

    Hazina ya fedha ya Cali ya kufadhili bio-anuwai imezinduliwa rasmi mjini Roma, Italia, huku kongamano la bio-anuwai la Umoja wa Mataifa la COP 16 likingoa nanga tena kwa mara ya pili.

    Kongamano hili linakuja kufuatia makubaliano yaliyofikiwa mwaka uliopita mjini Cali, Colombia.

    Kikao hiki cha pili, kinachofanyika katika makao makuu ya Shirika la Chakula Duniani (FAO), kimeandaliwa baada ya mkutano wa mwaka jana kushindwa kufikia malengo yaliyokuwa yamejiri kutokana na kutokuwa na idadi ya kutosha ya washirika wa kimataifa.

    Kongamano hili linajadili masuala muhimu kuhusu bio-anuwai chini ya kauli mbiu “Amani na Mazingira,” likilenga kuangazia utekelezaji wa mfumo wa Kunming-Montreal na mikakati ya kufadhili bio-anuwai.

    Lengo kuu la kongamano hili ni kujadili jinsi ya kufikia ufadhili wa dola bilioni 200 kila mwaka hadi kufikia 2030, ili kusaidia kutekeleza malengo ya kupunguza uharibifu wa bio-anuwai na kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali za kinasaba.

    Pia, linalenga kupunguza madhara ya uharibifu wa bio-anuwai kwa dola bilioni 500.

    Rais wa COP 16, Susana Muhamad, na Katibu Mkuu, Astrid Schomaker, wamezitaka nchi ambazo hazijaweza kuwasilisha mikataba yao ya NBSAP kuhakikisha wanatuma mikataba hiyo mara moja.

    Masuala mengine yatakayozungumziwa ni pamoja na umuhimu wa kuhamasisha ufadhili na rasilimali kwa bio-anuwai, na kuwezesha mataifa yanayoendelea kupata msaada katika utekelezaji wa protokali za kimataifa kama ya Nagoya kuhusu upatikanaji wa rasilimali za kinasaba na mgao wa mapato.

    Mataifa ya Afrika na Asia yameonyesha changamoto zao katika kupata ufadhili kutoka mifumo ya sasa, wakieleza vikwazo vinavyowazuia kupata fedha, na kupendekeza kuwepo kwa mfumo mpya wa ufadhili.

    Nchi kama Brazil na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimesema kuwa ni muhimu kuundwa mfumo mwingine, lakini Umoja wa Ulaya, Canada na Ufaransa wamepinga pendekezo hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Putin aahidi kuipatia Marekani madini adimu ya Urusi na Ukraine

    gg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema kuwa Urusi iko tayari kutoa fursa kwa Marekani kupata madini adimu, ikiwa ni pamoja na kutoka maeneo ya Ukraine yanayoshikiliwa na Urusi.

    Haya yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kushinikiza kwa muda mrefu Ukraine itoe baadhi ya madini yake kama sehemu y amakubaliano ya kusaidiwa na Marekani.

    Putin alisema katika mahojiano ya televisheni kwamba Urusi itashirikiana na washirika wa Marekani katika miradi ya uchimbaji, ikiwemo maeneo ya mashariki mwa Ukraine yaliyoshikiliwa na Urusi.

    Aliongeza kuwa Urusi ina rasilimali nyingi zaidi kuliko Ukraine na iko tayari kuvutia washirika wa kigeni kwa “mikoa mipya” ya kihistoria ambayo imejiunga na Shirikisho la Urusi.

    Pendekezo hili linaweza pia kuona nchi hizi mbili zikishirikiana katika uchimbaji wa alumini huko Krasnoyarsk, Siberia na usambazaji wake kwa Marekani ili kuimarisha bei .

    Maoni hayo ya Putin yalifuatia mkutano wa baraza la mawaziri kuhusu rasilimali asili za Urusi.

    Hatua ya Putin inakuja wakati Ukraine ikikabiliwa na shinikizo la Marekani kusaini makubaliano ya kutoa madini yake, huku Trump akisema Marekani inahitaji madini ya Ukraine yenye thamani ya dola bilioni 500.

    Hata hivyo, Rais Volodymyr Zelensky ameipinga takwimu hiyo na anasisitiza kuwa makubaliano yatakuwa na dhamana za usalama.

    Umoja wa Ulaya pia unashauri ushirikiano wa madini na Ukraine ambayo Kamishna wa Viwanda wa Umoja wa Ulaya, Stephane Sejourne, aliita ''ushindi kwa pande zote''.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Mzozo wa DRC: Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC awasili Congo kufanya uchunguzi

    Karim Khan Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai tangu 2021.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Karim Khan Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai tangu 2021.

    Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Karim Khan, amewasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuimarisha ahadi ya Mahakama hiyo kuchunguza uhalifu unaoendelea katika mikoa ya mashariki mwa nchi.

    Ziara hii inakuja huku ghasia zikizidi kuongezeka, ambapo mamia ya watu wameuawa na maelfu kujeruhiwa.

    Khan atakutana na maafisa wa serikali, wawakilishi kutoka MONUSCO, waathirika, na mashirika ya kiraia kujadili hali inavyoendelea na hatua za kuchukua kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.

    “Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya mashariki mwa Congo,” alisema Khan.

    “Hali ni ngumu, na tunajua kuwa mamia ya watu wamepoteza maisha. Ujumbe wetu ni wazi: hakuna kundi lolote lenye silaha au majeshi yanayoshirikiana nalo yatakayokosa kuwajibishwa. Lazima waheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.”

    Alisisitiza umuhimu wa kutekeleza Mkataba wa Roma na kuhakikisha kwamba wahusika wanawajibishwa.

    “Hakuna mtu anayeweza kushambulia raia au kuwajeruhi na asichukuliwe hatua. Huu ni wakati wa kuona kama ICC itasimama na kutimiza matakwa ya watu wa DRC ya utekelezaji wa sheria kwa usawa,” alsema Khan.

    Mwendesha mashitaka huyo pia alielezea kuwa hali ya DRC ni kama mizozo mingine duniani, akitaja mfano wa Palestina, Ukraine, na Israel, ambapo watu wa DRC wanastahili haki na usawa kama watu wengine duniani.

    Khan atafanya mazungumzo na Rais wa Congo Félix Tshisekedi na maafisa wa serikali kuhusu hatua za zitakazofuata.

    Pia atakutana na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo kesho Jumanne.

    Ziara hii inaonyesha juhudi za ICC katika kutafuta haki na kuwawajibisha wale wanaohusika na uhalifu unaoendelea mashariki mwa Congo.

    Mnamo Oktoba 2024, BwKhan alitangaza kwamba ofisi yake ilianza kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa katika jimbo la Kivu Kaskazini mnamo Januari 2022.

    Rais wa DRC Felix Tshisekedi pia aliwasilisha rufaa kwa ofisi ya mwendesha mashtaka mnamo Mei 2023 kuhusu uhalifu unaodaiwa kufanywa katika jimbo la Kivu Kaskazini na wanachama wa vikundi na vikosi mbalimbali vya waasi tangu Januari 1, 2022.

    ICC ina mamlaka tu juu ya makosa yaliyofanywa baada ya Mkataba wa Kirumi kuanza kutumika tarehe 1 Julai 2002.

    Na DRC imeshuhudia wababe wengi wa vita wakihukumiwa akiwemo Jean Pierre Bemba, Thomas Lubunga na Bosco Ntaganda.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Sayari saba zitaonekana angani kwa mara ya mwisho hadi 2040

    gg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wiki hii, sayari saba - Mars, Jupiter, Uranus, Venus, Neptuni, Mercury, na Saturn - zitakuwa zikionekana kwa kifupi angani, tukio linalojulikana kama ‘mchakato wa sayari’.

    Hii itakuwa mara ya mwisho kwa sayari saba kuonekana kwa pamoja hadi mwaka 2040.

    Fursa bora ya kuziona sayari hizi itakuwa mara tu baada ya jua kuzama, Jumanne, Jumatano, na Alhamisi.

    Sayari nne - Mercury, Venus, Jupiter, na Mars - zitaonekana kwa macho ya kawaida, lakini sayari ya Saturn itakuwa ngumu kuiona na Uranus na Neptune zitahitaji darubini.

    Dkt. Edward Bloomer, mtaalamu wa angani, anashauri kutafuta eneo lenye upeo wazi wa angani na kuepuka mwanga wa miji ili kuongeza nafasi ya kuziona.

    Anasema, “Chukua muda kidogo ili macho yako yazoee mwanga na epuka kutazama simu yako.”

    Ni fursa ya kipekee kufuatilia mabadiliko angani na kushuhudia mifumo ya mfumo wa jua ikifanya kazi.

    Pia unaweza kusoma:

  6. AI kuchukua kazi nyingi ambazo kwa sasa zinafanywa na binadamu nchini Singapore

    gg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Benki kubwa ya Singapore, DBS, imetangaza kupunguza ajira 4,000 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kutokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI).

    Kupunguzwa kwa ajira kutatokea kwa njia ya mabadiliko ya asili, ambapo kazi za muda na mikataba zitakoma, na wafanyakazi wa kudumu hawatarajiwi kuathirika.

    Hata hivyo, benki inatarajia kuunda ajira 1,000 zinazohusiana na AI.

    DBS ina wafanyakazi 41,000, na kati yao 8,000 hadi 9,000 ni wa muda na mikataba.

    Benki hiyo imekuwa ikifanya kazi na AI kwa zaidi ya muongo mmoja na inatarajia athari ya kiuchumi ya AI kufikia dola bilioni 1 za Singapore (S$1bn) ifikapo mwaka 2025.

    DBS inakuwa miongoni mwa benki kubwa za kwanza kutoa maelezeo kuhusu jinsi AI itakavyoathiri shughuli zake.

    Hata hivyo haijasema ni ajira ngapi zitapunguzwa Singapore au ni kazi zipi zitakazoathirika.

    AI inatarajiwa kugusa takriban asilimia 40% ya ajira duniani, na IMF imeonya kuwa inaweza kuimarisha usawa wa kiuchumi.

    Hata hivyo, Gavana wa Benki ya Uingereza, Andrew Bailey, alisema AI ina “uwezo mkubwa” licha ya hatari zake.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Vita mpakani mwa Ethiopia na Kenya: Takriban watu 30 wauawa

    GG

    Chanzo cha picha, OTHER

    Watu kadhaa wameuawa katika mapigano yaliyozuka mpakani mwa Ethiopia na Kenya, kati ya jamii za wafugaji wa mifugo na wafugaji wa samaki katika mkoa wa Dasenech, unaopakana na kaunti ya Turkana, Kenya.

    Mapigano haya yalishuhudiwa mapema wiki hii.

    Maafisa wa mkoa wa Dasenech wamesema kuwa raia 13 wa Ethiopia wameuawa, huku mamlaka za Kenya zikisema takriban watu 22 hawajulikani waliko tangu mgogoro ulipoanza.

    Wanasiasa wawili kutoka eneo hilo wamelalamikia wanamgambo wa Ethiopia kwa kuvamia kijiji chao na kuua watu 20.

    Chifu wa mkoa wa Dasenech, Tadele Hasie, aliiambia BBC kwamba mgogoro huu ni wa pili kati ya jamii hizo ndani ya wiki chache.

    Alidai kwamba mauaji ya wavuvi wawili wa Ethiopia katika Ziwa Turkana yaliwachochea wafugaji kuanzisha vita.

    Takriban watu 10,000 kutoka Dasenech wamekimbia makazi yao kwa hofu ya usalama wao, alisema.

    Naibu Kamishna wa Turkana Kaskazini, George Orina, alisema maafisa wa usalama wamepelekwa eneo la tukio na wanazungumza na waathiriwa wa mapigano hayo.

    Eneo hili limekuwa na migogoro ya mara kwa mara, hasa kuhusu mashamba ya malisho na maeneo ya kuvua samaki.

    Bwana Tadele alielezea mgogoro huu kama mmoja wa kali zaidi, na alidai kuwa wavuvi 32 kutoka Kenya na maboti 5 walizuiliwa na baadaye kuachiliwa.

    Soma pia:

  8. Uganda yachunguza kifo cha mwanasoka wa Nigeria kilichotokea nchini humo

    Lawal amekuwa akiichezea klabu ya Vipers ya Uganda tangu 2022

    Chanzo cha picha, Vipers Sports Club/X

    Maelezo ya picha, Lawal amekuwa akiichezea klabu ya Vipers ya Uganda tangu 2022

    Polisi wa Uganda wanachunguza kifo cha mchezaji wa soka kutoka Nigeria, Abubakar Lawal, aliyedaiwa kuanguka kutoka ghorofa ya tatu ya jumba la Voicemall Shopping Arcade jijini Kampala.

    Lawal mwenye umri wa miaka 29, alikuwa amekwenda kumtembelea rafiki yake kutoka Tanzania, Omary Naima, ambaye alimuacha akiwa anajiandaa kutengeneza chai kabla ya tukio.

    Alikimbizwa hospitalini ambapo alithibitishwa kuwa amekufa, polisi walisema.

    Lawal alikuwa mshambuliaji wa timu ya Vipers Sports Club ya Uganda tangu Julai 2022 na alikuwa na historia ya kuchezea AS Kigali ya Rwanda.

    Klabu ya Vipers imetuma risala za rambi rambi kwa kifo chake, wakisema alikuwa mtu mkarimu na mwenye moyo mkubwa.

    ''Ni vigumu kuamini kuwa haupo tena, Lawal. Mtu mwenye huruma, kipaji na upendo.Tutakutamani daima,'' alisema mchezaji wa Uganda, Mustafa Kizza.

    Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti awali kuwa alikufa katika ajali ya pikipiki, lakini polisi wamesema wanachunguza mazingira halisi ya kifo hicho.

    Wamesema wanaendelea kupata video za CCTV na kufanya uchunguzi ili kubaini kilichotokea.

    Vitu vya Lawal, ikiwa ni pamoja na simu, viatu na vifaa vya mazoezi, vimepatikana na vitatumika katika uchunguzi zaidi.

    Taarifa zaidi zitatolewa kadri uchunguzi unavyosonga mbele.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Kenyatta, Obasanjo na Desalegn wateuliwa kuwa waratibu wa mzozo wa DRC

    Uhuru Kenyatta, Oluseguna Obasanjo na Hailemariam Desalegn
    Maelezo ya picha, Uhuru Kenyatta, Oluseguna Obasanjo na Hailemariam Desalegn

    Marais wa zamani wa Kenya na Nigeria, pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia wameteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC), kuongoza mchakato wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

    Kupitia taarifa iliyotolewa na Rais wa Kenya William Ruto ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC alisema walifikia uamuzi wa pamoja kwamba Uhuru Kenyatta wa Kenya, Olusegun Obasanjo wa Nigeria na Hailemariam Desalegn wa Ethiopia wataongoza mikakati ya EAC na SADC ya kupata amani Mashariki mwa Congo.

    Makubaliano ya uteuzi huo yalifanyika katika Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC uliofanyika Dar es Salaam tarehe 8 Februari 2025, ukiongozwa na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Rais Ruto wa Kenya, kujadili hali ya usalama nchini DRC.

    Haya yanajiri baada ya Rais wa Angola João Lourenço kutangaza kuwa majukumu aliyonayo yatamzuia kuendelea kuwa mpatanishi wa mzozo wa DRC unaoendelea.

    Kikundi Kazi cha EAC kilifanya majadiliano kuhusu hali ya usalama, na kutoa mapendekezo muhimu, ikiwa ni pamoja na kusitisha mapigano mara moja na kutoa msaada wa kibinadamu.

    M23 na wahusika wote wanahimizwa kusitisha mapigano na kutii mapatano ya amani yaliyotangazwa.

    Serikali ya DRC na waasi wa M23 wamelaumiana kwa kukiuka makubaliano ya Luanda, ambayo yaliwania kurejesha amani Congo na badala yake migogoro imeshuhudiwa kwa zaidi ya miaka 30.

    Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri wa masuala ya kigeni wa Rwanda , Olivier Nduhungirehe. serikali ya Rwanda imekaribisha uamuzi huu ukiutaja kama mkakati wa uhakika wa utekelezwaji wa mpango wa amani wa EAC na SADC.

    Tangu kuzuka kwa vita hivi, Rais wa Congo, Felix Tshisekedi, ameendelea kuziomba nchi rafiki kumsaidia kukabiliana na waasi wa M23, lakini hadi sasa hajafanikiwa.

    Mnamo mwaka 2022, Makubaliano ya Nairobi yaliagiza kupelekwa kwa Kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) mashariki mwa Congo ili kusaidia kutatua mzozo huo kwa njia ya upatanishi.

    Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka 2023, serikali ya Congo iliiomba EACRF kujiondoa, ikituhumu kikosi hicho kwa kutokuwa na manufaa, huku Rais Tshisekedi akiomba msaada wao katika vita dhidi ya M23.

    Wakati huo, serikali ya Tshisekedi ilifanya maombi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kusaidia kupambana na waasi hao huku nchi za Afrika Kusini, Tanzania na Malawi zilituma wanajeshi, ambao walishirikiana na wanajeshi wa Burundi katika vita dhidi ya M23.

    Hata hivyo, hatua hii haikupokelewa vyema na Rwanda, inayoshutumiwa kwa kuunga mkono M23, kama ilivyothibitishwa na serikali ya Congo, Umoja wa Mataifa na nchi jirani.

    Pamoja na juhudi hizo, M23 waliendelea kupanua maeneo waliyodhibiti, na hivi karibuni waliteka miji ya Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, na Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Choo cha dhahabu cha jumba alikozaliwa Churchill kiliibiwa kwa dakika tano, mahakama yaambiwa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kesi inaendelea Oxford kuhusu wizi wa choo cha dhahabu kilichokuwa katika jumba alikozaliwa Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Churchill Winston ambapo mwendesha mashtaka Jumatatu alielezea kwa undani jinsi wizi huo ulivyofanyika.

    Choo hicho chenye dhahabuya thamani ya hadi dola milioni sita kiliibwa kutoka Blenheim Palace karibu na Oxford kwa dakika tano pekee. Vyombo vya habari duniani viliripoti juu ya wizi huu katika msimu wa vuli wa 2019.

    Mwendesha mashtaka Julian Christopher alisema genge la wanaume watano lilivamia magari mawili kwenye lango la Jumba la Blenheim usiku wa Septemba 14, kisha wakavunja dirisha na kuingia ndani ya jumba lenyewe.

    Baada ya kuvunja choo kwa nyundo, waliacha nyundo kwenye eneo la uhalifu na kukimbia.

    Operesheni nzima ya wizi iliwachukua wahalifu kama dakika tano.

    Unaweza pia kusoma:

  11. Wanajeshi majeruhi 200 wa SADC wakiwemo Watanzania wanarejeshwa nyumbani kupitia Rwanda

    g

    Chanzo cha picha, SAMIDRC

    Maelezo ya picha, Mwishoni mwa 2023, Afrika Kusini ilituma maelfu ya wanajeshi kusaidia vikosi vya serikali ya DR Congo kupambana na vuguvugu la M23.

    Takriban wanajeshi 200 wanaohitaji wakihitaji huduma ya matibabu wakiwemo wale wa Afrika Kusini, Malawi na Tanzania walioko katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa ujumbe unaojulikana kwa jina la SAMIDRC waliondoka Goma na kuvuka mpaka na kuingia Rwanda kuelekea Kigali kwa ajili ya kupata ndege za kuwarejesha makwao.

    Waziri wa ulinzi wa Afrika Kusini alitangaza wikendi iliyopita kwamba wanajeshi wao waliojeruhiwa katika mapigano na M23 nchini DRC wataanza kurejeshwa makwao wiki hii.

    Donatien Mugabo, mkazi wa Gisenyi nchini Rwanda, ambaye ameshuhudia magari yaliyokuwa yamewabeba askari hao yakiondoka mpakani kwa upande wa Rwanda, ameiambia BBC kuwa walikuwa kwenye mpaka huo kwa saa kadhaa.

    g

    Walifika mpakani Jumatatu saa sita mchana, na waliondoka mpakani baada ya saa kumi na mbili jioni, Donatien anasema.

    Haijabainika ni nini kilisababisha wacheleweshwe mpakani.

    Vyombo vya habari vya Goma - jiji linalodhibitiwa na M23 na nchini Rwanda vilipigwa marufuku kupiga picha au kuzungumza na wanajeshi, kama ilivyokuwa wakati mamluki wa Ulaya walipoondoka Goma kupitia Rwanda.

    Magazeti ya Rwanda yanaripoti kuwa wanajeshi 129 wanatoka Afrika Kusini, 40 kutoka Malawi na 25 kutoka Tanzania.

    Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi walikotoka askari hao hawajazungumzia kuachiliwa kwa askari hao wanaotajwa kuhitaji matibabu.

    Unaweza pia kusoma:

  12. Marekani yaungana na Urusi katika maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Kaimu mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Marekani, Dorothy Camille Shea, akipiga kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

    Marekani imeungana mara mbili na Urusi katika kura kwenye Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha mwaka wa tatu wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ikionyesha mabadiliko ya serikali ya Trump kuhusu vita.

    Kwanza nchi hizo mbili zilipinga azimio lililoandaliwa na Ulaya la kulaani vitendo vya Moscow na kuunga mkono uadilifu wa eneo la Ukraine, ambalo lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York.

    Kisha wakaunga mkono azimio lililoandaliwa na Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa kwa mzozo huo lakini halikukuwa na ukosoaji wowote dhidi ya Urusi.

    Azimio la Baraza la Usalama lilipitishwa lakini washirika wawili wakuu wa Marekani, Uingereza na Ufaransa, hawakupiga kura baada ya majaribio yao ya kurekebisha baadhi ya masuala kupingwa.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Mzozo wa DRC: Takriban wanajeshi watoro 60 wahukumiwa na mahakama ya kijeshi DRC

    g

    Kesi dhidi ya wanajeshi sitini watoro wa vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) na washirika wawili wa kike imefunguliwa leo.

    Watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama ya kijeshi ya Butembo mjini Musienene, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

    "Watuhumiwa wanashtakiwa na mahakama ya kijeshi ya Butembo kwa kumkimbia adui, wizi, ubakaji, unyang'anyi na makosa mengine katika maeneo ya Lubero-Centre, Kimbulu na Musienene," Seros Muyisa, mwandishi wa habari wa eneo hilo ambaye alikuwepo katika kikao hicho, aliiambia BBC.

    h

    Waasi wa M23 wamekuwa wakiyateka maeneo ya mashariki mwa DRC tangu kuanza kwa mashambulizi makali mwezi Januari.

    Wiki iliyopita, waliingia Bukavu, mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa nchi, na kuchukua udhibiti wa ofisi ya gavana.

    Kabla ya Bukavu kuangukia mikononi mwa waasi hao, takriban wanajeshi 80 wa Congo na wanamgambo wa Wazelendo walikuwa wamekamatwa na kuzuiliwa katika gereza la mji huo wakisubiri kufikishwa mahakamani.

    Lakini baada ya shambulio la waasi wa M23, wafungwa kutoka gereza la Bukavu walitoroka, wakiwemo wanajeshi, mamlaka imesema.

    Walishutumiwa kwa mauaji na uporaji katika maeneo ya Kabare na Bukavu baada ya kuacha mstari wa mbele, Mkoa wa Kivu Kusini.

    Pia unaweza kusoma:

  14. 'Nchi inakaribia kulipuka kwasababu ya vita' - Kabila anazungumza baada ya miaka mitano ya 'ukimya'

    h

    Chanzo cha picha, Joseph Kabila - PR

    Maelezo ya picha, Joseph Kabila ameonekana mara chache sana katika siasa tangu aondoke madarakani mwaka 2019, baada ya tangazo lake Jumapili, msemaji wake alisema, "Joseph Kabila atangaza kurejea kwake."[hadharani]

    Baada ya takriban miaka mitano ya kuwa kimya kwa kiasi kikubwa katika siasa na vyombo vya habari, Joseph Kabila, rais wa zamani wa DR Congo, ametangaza kuwa nchi hiyo "iko karibu kulipuka kutokana na vita vya ndani" ambavyo vinaweza kuyumbisha kanda nzima.

    Félix Tshisekedi, ambaye alimrithi mwaka wa 2019 - katika makabidhiano ya kwanza ya amani ya mamlaka katika historia ya DR Congo - mwezi huu alisema Kabila ndiye "mtu halisi nyuma ya haya yote", akimshutumu kulisaidia vuguvugu la M23.

    Tangu mwaka 2019 Joseph Kabila ambaye ni seneta amekuwa akizungumziwa na msemaji wake Barbara Nzimbi, lakini wiki hii gazeti la Sunday Times la Afrika Kusini lilichapisha maoni ya Bwn. Kabila hukusu mzozo wa DRC.

    Alimshutumu Bw Tshisekedi kwa kukiuka mara moja mikataba mipya ya kisiasa ambayo ilikuwa imekubaliwa mara tu baada ya kukabidhiwa madaraka.

    Ameongeza kuwa hali "imekuwa mbaya zaidi. Hadi kufikia hatua ambayo nchi iko kwenye hatihati ya kulipuka kutokana na migogoro ya ndani, inaweza hata kuyumbisha eneo lote."alisema.

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Tshisekedi (kulia) alimshutumu mrithi wake Kabila (pichani akikabidhi madaraka mwaka wa 2019) kwa kuwa nyuma ya kile kinachoendelea Mashariki mwa DRC

    Rais Tshisekedi yuko vitani na vuguvugu la M23, ambalo kwa sasa linadhibiti sehemu kubwa za majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Anamtuhumu Kabila, na Rwanda, kuwa nyuma ya M23, na wikendi hii aliahidi kupanga upya jeshi kukabiliana na kundi hilo.

    Joseph Kabila alitangaza kwamba "ikiwa migogoro hii na mizizi yake haitashughulikiwa ipasavyo, juhudi za kuimaliza zitakuwa bure".

    Kabila anasema tatizo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sio tu kuhusu vuguvugu la M23 - anamshutumu Tshisekedi kwa "kujaribu kudhihirisha kulielezea kundi hilo kama la kigeni ambalo halina sababu halali za kupigania", jambo ambalo sio ukweli.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Amani sio lazima imaanishe kuisalimisha Ukraine, anasema Macron akiwa na Trump

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema makubaliano yoyote ya amani nchini Ukraine lazima yaje na dhamana ya usalama. Macron ameyasema hayo alipokutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House kwa mazungumzo kuhusu vita.

    "Amani hii lazima isiwe kujisalimisha kwa Ukraine, haipaswi kumaanisha kusitishwa kwa mapigano bila dhamana," alisema wakati viongozi hao wawili wakifanya mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari baada ya mkutano wao wa Jumatatu.

    Trump, ambaye hakutaja hakikisho la usalama mwenyewe, alisema gharama na mzigo wa kupata amani nchini Ukraine lazima zilipwe na mataifa ya Ulaya na sio Marekani pekee.

    Macron alijibu kwamba Ulaya inaelewa hitaji la "kushiriki kwa usawa mzigo wa usalama", na akaongeza kuwa mazungumzo ya maadhimisho ya mwaka wa tatu wa uvamizi wa Urusi yameonyesha njia ya kusonga mbele.

    Wakati wawili hao wakirushiana maneno ya makali Jumatatu nzima, baadhi ya tofauti za wazi ziliibuka kuhusu suala la kumaliza vita nchini Ukraine walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya rais wa Marekani ya Oval na kisha kufanya mkutano wa wa dakika dakika 40 na waandishi wa habari baadaye mchana.

    Unaweza pia kusoma:

  16. Zelensky anamatumaini kumaliza vita vya Ukraine mwaka huu

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema "tunatumai kwamba tunaweza kumaliza vita hivi mwaka huu" katika kumbukumbu ya mwaka wa tatu wa uvamizi kamili wa Urusi.

    Lakini ameonya kuwa Ukraine inahitaji dhamana ya usalama ili kuizuia Moscow kurejea, akipendekeza uanachama wa EU na Nato kwa nchi yake utasaidia. Urusi imepinga mara kwa mara wazo la Ukraine kujiunga na Nato.

    Hapo awali, Zelensky alisema makubaliano ya amani na Urusi yanaweza kuanza kwa ubadilishanaji "kamili" wa wafungwa wa vita.

    Zelensky alikuwa akizungumza katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya, pamoja na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, ambao walikuwa Kyiv kuonyesha uungaji mkono wao kwa taifa hilo.

    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Zelensky aliulizwa nini matumaini yake kwa Ukraine na watu wake baada ya miaka mitatu ya vita.

    "Tunatumai kuwa tunaweza kumaliza vita mwaka huu," alijibu, akiongeza kuwa vimekuwa "vigumu sana" kwa taifa zima.

    Alisema Ukraine Ukraine inahitaji dhamana ya usalama katika muda mfupi ili kuizuia Urusi kurejea katika miaka ijayo.

    Kujiunga na EU na Nato hivi karibuni "kutatusaidia sana", aliongeza.

    Unaweza pia kusoma:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya Jumanne ya tarehe 25.02.2025, tukikuletea taarifa za kikanda na kimataifa kadri zinavyojiri