Wenyeji wa Afcon 2027 Tanzania na Uganda wapangwa katika kundi moja Morocco

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ivory Coast ndio mabingwa watetezi baada ya kubeba kombe la Afcon 2023 katika ardhi ya nyumbani kufuatia ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Nigeria katika fainali.
Muda wa kusoma: Dakika 3

Mabingwa watetezi wa Afcon Ivory Coast wamewekwa katika kundi moja na Cameroon katika hatua ya makundi ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 nchini Morocco.

Katika hafla iliyosheheni mbwembwe za akila aina mjini Rabat, Tembo walipangiwa Kundi F, ambapo pia watamenyana na timu ya Pierre-Emerick Aubameyang Gabon na Msumbiji.

Kinyang'anyiro hicho cha Afrika kitaaanza tarehe 21 Desemba na kuendelea hadi Januari 18 2026. Mechi ya ufunguzi itazikutanisha wenyeji Morocco dhidi ya Comoro.

Nigeria, ambayo ilishindwa na Ivory Coast katika fainali ya Afcon 2023, itakuwa Kundi C pamoja na Tunisia.

Katika kundi moja, Uganda na Tanzania, wawili kati ya waandaji wenza wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2027, watachuana.

Katika mashindano mengine ya kikanda yenye mvuto, timu tatu za kusini mwa Afrika zitashiriki Kundi B, huku Afrika Kusini, Angola na Zimbabwe zikiwa zimepangwa pamoja na Misri ya Mohamed Salah.

Sudan, ambayo ilifuzu kwa Afcon 2025 licha ya nchi hiyo kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, itamenyana na Algeria katika Kundi E.

Gwiji wa Morocco Mustapha Hadji alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri wa kandanda waliokuwepo kusaidia katika droo hiyo.

Kando yake alikuwa mlinzi wa zamani wa Nottingham Forest na Tottenham Serge Aurier, mshindi mara mbili wa Afcon akiwa na Ivory Coast.

Joseph Yobo, nahodha wa timu ya Nigeria iliyoshinda Afcon mwaka 2013, pia alikuwepo kuzichagua timu hizo.

Kocha wa zamani wa Senegal aliyeshinda Afcon, Aliou Cisse, ambaye aliiongoza Simba ya Teranga kushinda 2021, pia alisaidia, huku taifa lake likipangwa Kundi D pamoja na DR Congo.

Timu 24 zimegawanywa katika vikundi sita. Washindi na washindi wa pili katika kila kundi, pamoja na timu nne bora zilizoshika nafasi ya tatu, zitafika awamu ya muondoano.

Droo ya Afcon 2025 yafanyika Morocco

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Droo ya Afcon 2025 ilifanywa na (kutoka kushoto kwenda kulia) Mustapha Hadji, Serge Aurier, Samson Adamu, Aliou Cisse na Joseph Yobo.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Morocco, ambao pia watakuwa wenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) mwaka huu, waliingia kama wenyeji wa Afcon 2025 baada ya Guinea kupokonywa michuano hiyo kwa sababu ya wasiwasi wa miundombinu na vifaa.

Saa chache kabla ya droo ya Jumatatu kuanza, kamati ya maandalizi ya eneo hilo ilitangaza kwamba Rabat, Casablanca, Agadir, Marrakech, Fes na Tangier zitaandaa mechi wakati wa Afcon 2025 katika viwanja tisa.

Viwanja vinne vitakuwa katika mji mkuu Rabat, ambapo fainali itachezwa kwenye Uwanja wa Complexe Sportif Prince Moulay Abdellah.

Morocco ni waandaji-wenza wa Kombe la Dunia mwaka wa 2030, pamoja na Uhispania na Ureno, na wanapanga kujenga uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 115,000 viungani mwa Casablanca ifikapo 2027, ambao wanatumai kuwa unaweza kuandaa fainali ya kimataifa.

Droo kamili ya makundi ya Afcon 2025

Kundi A: Morocco, Mali, Zambia, Comoro

Kundi B: Misri, Afrika Kusini, Angola, Zimbabwe

Kundi C: Nigeria, Tunisia, Uganda, Tanzania

Kundi D: Senegal, DR Congo, Benin, Botswana

Kundi E: Algeria, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Sudan

Kundi F: Ivory Coast, Cameroon, Gabon, Msumbiji

Imetafsiriwa na Seif Abdalla