Lookman na Banda watuzwa wachezaji bora wa soka barani Afrika

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Lookman na Banda
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mchezaji kutoka Nigeria Ademola Lookman ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika 2024 kwenye tuzo za shirikisho la kandanda la Afrika (CAF) zilizofanyika usiku wa kuamkia leo Marrakech, Morocco.

Mshambuliaji huyo wa Atalanta aliwashinda wachezaji wa Ivory Coast Simon Adingra, Mshambuliaji wa Guinea Serhou Guirassy, Achraf Hakimi wa Morocco na mlinda lango wa Afrika Kusini Ronwen Williams.

Lookman ni mchezaji wa pili wa Nigeria kushinda taji hilo mfululizo baada ya Victor Osimhen mwaka 2023.

Mshambulizi wa Orlando Pride Barbra Banda naye aliandikisha historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Zambia kushinda tuzo hiyo upande wa wanawake, akiwashinda Sanaa Mssoudy wa Morocco na Chiamaka Nnadozie kutoka Nigeria.

Washindi walipigiwa kura na jopo la wataalamu wakiwemo wanachama wa kamati kuu ya CAF, wanahabari Barani Afrika, Wachezaji na Makocha.

Mwaka wa kufana kwa Lookman

Lookman aliye na miaka 27 alikuwa amepigiwa upatu kushinda tuzo hiyo kufuatia kushamiri kwake msimu wa 2023-24.

Alikuwa nguzo muhimu katika kuisaidia timu yake ya Atalanta kushinda kombe Lao la kwanza Barani Ulaya katika historia akifunga mabao matatu kwa mpigo kwenye fainali dhidi ya Bayer Leverkusen - na kuwa Mchezaji wa sita kufunga mabao matatu katika Fainali Barani Ulaya na wa kwanza tangu mwaka 1975.

Katika Soka ya Kimataifa, Lookman alitajwa katika timu bora ya Mashindano ya Soka Barani Afrika Nchini Ivory Coast, akifunga mabao matatu huku timu yake ya Taifa Super Eagles ikimaliza ya pili nyuma ya wenyeji Ivory Coast mwezi Februari.

Mchezaji huyo wa zamani wa Everton, Fulham na Leicester pia alikuwa Mwafrika pekee katika orodha ya wachezaji waliowania tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu ambapo alimaliza katika nafasi ya 14.

Lookman kwa mara nyengine amekuwa kiungo muhimu kwa Atalanta msimu huu akifunga mabao manane na kuisaidia timu hiyo kusalia kileleni mwa jedwali la Serie A.

Tuzo za kufuatana kwa Banda

Barbra Banda (kushoto) alifunga bao la kuipatia ushindi Orlando Pride mwezi Novemba katika mashindano ya NWSL huku Washington Spirit wakiambulia patupu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Barbra Banda (kushoto) alifunga bao la kuipatia ushindi Orlando Pride mwezi Novemba katika mashindano ya NWSL huku Washington Spirit wakiambulia patupu

Ufanisi wa Banda umewadia chini ya mwezi baada ya kupokea tuzo ya BBC ya Mchezaji Bora wa kike wa mwaka.

Mchezaji huyo aliye na umri wa miaka 24 pia alitajwa Mchezaji Bora katika ligi kuu ya kandanda ya wanawake nchini Marekani baada ya kuisaidia Orlando Pride kushinda taji lake la kwanza.

Alifunga mabao 17 na kuwa wa pili katika orodha ya wafungaji bora - Nyuma ya Temwa Chawinga wa Malawi - Bao lake Muhimu akifunga kwenye fainali ambapo Pride iliishinda Washington Spirit 1-0.

Banda aidha alikuwa bora kwa taifa lake kwenye Mashindano ya Olimpiki kule Paris, akiifungia Copper Queens ya Zambia mabao manne, yakiwemo mabao matatu ya kipindi cha kwanza dhidi ya Australia. Mabao kumi aliyofunga ndani ya mechi mbili yamemfanya kuwa mfungaji bora kutoka Afrika katika historia ya michezo ya Olimpiki.

Kikosi kinachong'aa

Kusherehekea kushamiri kwa wachezaji bora barani mwaka huu, CAF iliandaa hafla ya aina yake kukiwa na wasanii bora wa Afrika Jukwaani.

Mwanamuziki Maarufu wa Tanzania Diamond Platinumz pamoja na msanii wa Morocco Dystinct waliongoza burudani katika usiku ambao Rais wa Cameroon Paul Biya alituzwa tuzo maalum kufuatia mchango wake katika soka barani.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa na rais wa FIFA Gianni Infantino, ambaye alipongeza Taifa la Morocco baada ya kuthibitishwa kuwa waandalizi wenza wa Mashindano ya Kombe la Dunia 2030 wiki iliyopita.

Ulikuwa Usiku mzuri wa nahodha wa Afrika kusini Williams, ambaye - licha ya kukosa tuzo kuu - alipata tuzo mbili. Mlinda lango huyo wa Mamelodi Sundowns alitajwa Kipa Bora Barani Afrika mwaka huu na mchezaji Bora wa Vilabu Barani Afrika.

Katika Usiku Uliojaa wasanii wa haiba kubwa Jijini Marrakesh Morocco, ilitangazwa pia timu bora ya Caf/Fifpro ya wanaume na wanawake.

Washindi wa CAF 2024

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mchezaji Bora wa Mwaka upande wa Wanaume: Ademola Lookman (Nigeria & Atalanta)

Mchezaji Bora wa Mwaka upande wa Wanawake: Barbra Banda (Zambia & Orlando Pride)

Kocha Bora wa Wanaume wa Mwaka: Emerse Fae (Ivory Coast)

Kocha Bora wa Wanawake wa Mwaka: Lamia Boumehdi (TP Mazembe)

Mlinda Lango Bora wa Wanaume wa Mwaka: Ronwen Williams (Afrika Kusini & Mamelodi Sundowns)

Mlinda Lango Bora wa Wanawake wa Mwaka: Chiamaka Nnadozie (Nigeria & Paris FC)

Klabu Bora ya Mwaka ya Wanaume: Al Ahly (Misri)

Klabu Bora ya Mwaka ya Wanawake: TP Mazembe (Jamhuri ya Kongo)

Mchezaji Bora wa Mwaka wa Interclub wa Wanaume: Ronwen Williams (Afrika Kusini & Mamelodi Sundowns)

Mchezaji Bora wa Mwaka wa Interclub wa Wanawake: Sanaa Mssoudy (Morocco & AS Far)

Mchezaji mchanga Bora wa Mwaka upande wa Wanaume: Lamine Camara (Senegal & Monaco)

Mchezaji Mchanga Bora wa Mwaka upande wa Wanawake: Doha El Madani (Morocco & AS Far)

Timu Bora ya Mwaka ya Wanaume: Ivory Coast

Timu Bora ya Mwaka ya Wanawake: Nigeria

Goli Bora la Mwaka (lililochaguliwa na mashabiki): Cristovao Mabululu (Angola) – Angola v Namibia (Afcon 2023)

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla