Klabu bingwa Afrika: Yanga kuvunja mwiko wa miaka 24?
Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Chanzo cha picha, Yanga twitter
'Yanga afrika yanga umoja wa mataifa, mabingwa wa afrika mashariki na kati eeeeh', ni kibwagiza kilichowahi kutamba sana katika miaka ya 1990s kilichoimbwa na msanii maarufu Pepe Kalle na bendi yake ya Empire Bakuba.
Ilikuwa miaka yenye mafanikio na sifa kubwa kwa Klabu ya Yanga ya Tanzania. Pamoja na ubingwa wa Afrika Mashariki na kati, kufika hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka 1998, yalikuwa mafanikio makubwa zaidi ya kukumbukwa kwa klabu hiyo ya mitaa ya jangwani.
Ukubwa wa mafanikio hayo unatokana na ukubwa mashindano hayo kwa ngazi ya klabu. Mchuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, ndio mashindano makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu. Kushinda kombe lake au kutinga hatua ya makundi,robo au nusu fainali ni jambo la kusifika.
Yanga haikufanya hivyo kwa miaka 24 iliyopita baada ya mfumo wa michuano hiyo kubadilishwa kuwa ulivyo sasa. Mwishoni mwa wiki hii, mabingwa hao wa Tanzania mara 28 wanakutana na mabingwa wa Sudan, Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mchezo wa pili wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika. Je inaweza kuuvunja mwiko huo mwaka huu?
Inawezekana au haiwezekani?

Chanzo cha picha, Yanga Twitter
Wakiwa kwenye moja ya nyakati nzuri zaidi kifedha na kimipango katika miaka ya hivi karibuni, wenyeji Yanga walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al Hilal katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Yanga walitangulia kwa bao la mshambuliaji wake tegemeo, Fiston Kalala Mayele dakika ya 50, kabla ya Al Hilal kusawazisha kupitia kwa Mohamed Yousif dakika ya 67.
Bao la Yousif limeiweka Yanga njia panda, ikihitaji ushindi wowote au sare ya kuanzia 2-2 kwenda mbele katika uwanja 'mgumu' huko Sudan.
'Ni mchezo mgumu, lakini katika soka maajabu hutokea, Simba iliwahi kupindua meza, na hata Ulaya tunaonea meza zikipinduliwa, inawezekana ingawa wanahitaji kuwa juu ya kiwango chao cha kawaida', anasema Omari Mkambala, mwandishi wa michezo, BBC.
Mashabiki wengi, baada ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, wameonyesha kuvunjika moyo na matokeo ya 1-1, wengi wana imani ya mguu ndani mguu nje ya kufuzu makundi, kutokana na uwezo wa wapinzani wao na uimara wao wawapo katika uwanja wao wa nyumbani.
'Ni ama kusuka au kunyoa'

Chanzo cha picha, Yanga twitter
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iliposhiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo mwaka 1969 ilifanikiwa kutinga hadi hatua ya robo fainali. Mwaka uliofuata,1970 walifika tena hatua ya robo fainali.
Ukiacha kombe la shirikisho ilipofuzu hatua ya makundi mara mbili, mwaka 2016 na 2018 na Kombe la washindi la Afrika walipofika hatua ya robo fainali mwaka 1995, mwaka 1998 ndio mwaka wa mwisho wa klabu hiyo kufanikiwa kwenye michuano ya Afrika.
Watani wao wa jadi Simba, imekuwa ikifanya vyema kufika makundi na robo fainali katika miaka ya hivi karibuni, jambo linalowatesa wenzao wa Yanga, waliowahi kujiita 'wa kimataifa'.
' Yanga wana kikosi cha kupigana, inaundwa na wachezaji wengi wa kimataifa, ila kiwango walichokionyesha Dar es Salaam, kiliwakera mashabiki. Huko Sudan ni ama waamue kusuka ama kunyoa, washambulie mwanzo mwisho, wakiachia nafasi, au walinde na kushambulia kwa kushtukiza', anasema Dixon Busagaga, mchambuzi wa soka Tanzania.
Yanga chini ya Nabi Mohammed ilitinga hatua ya 32 bora baada ya kuiondosha katika hatua ya kwanza timu ya Zalan Rumbek ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, Mayele akifunga 6 kati ya hao, 'hat trick' ugenini na nyumbani.
Wanakutana na Hilal, inayonolewa na Florent Ibenge, aliyewaongoza RS Berkane ya Morocco kutwaa Kombe la Shirikisho msimu uliopita. Hilal imetinga raundi ya pili baada ya kuitoa St. George ya Ethiopia kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya 2-2
Mshindi wa jumla atakwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu itakayotolewa itakwenda kumenyana na timu ya Kombe la Shirikisho kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo dada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mbali na Yanga, Jumapili hii wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, Simba wanawakaribisha Primiero de Agosto katika uwanja wa Benjamin Mkapa. Chini ya kocha Juma Mgunda katika mchezo wa awali ugenini Simba iliibuka na shindi wa mabao 3-1 na kutanguliza mguu mmoja kwenye hatua ya makundi.
Kwenye kombe la Shirikisho, matajiri wa lambalamba, Azam iliyoanza mzunguko wa kwanza vibaya kwa kuchapwa 3-0 ugenini wanarejeana na Al Akhdar ya Libya.












