Kwanini korongo maarufu wa Uganda wako hatarini kutoweka?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Wycliffe Muia
- Nafasi, BBC News, Mbarara
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Korongo maarufu wa Uganda, anayetambuliwa kwa muonekano wake haswa shungi lake la rangi ya dhahabu, mabako mekundu chini ya shingo na miguu myembamba nyeusi amekuwa fahari nchini Uganda.
Ndege huyu amechorwa kwenye bendera na nembo ya taifa, na timu zote za michezo za Uganda pia zimepewa jina lake.
Hata hivyo, idadi ya ndege hawa imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, na wataalamu wa uhifadhi wanaonya kuwa huenda wakatoweka kabisa ikiwa hatua za kuwalinda hazitachukuliwa.
Ndege huyo analindwa na sheria- inaainisha kifungo cha maisha au ulipe faini ya bilioni 20 za Uganda sawa na dola milioni tano za kimarekani kwa wale wataopatikana na hatia ya kuwaua.
Tukirejelea desturi za jadi, tamaduni za Buganda zilikataza kuua ndege huyo zikimchukulia koorongo kama ishara ya utajiri, bahati nzuri na maisha marefu.
Imani hii ilisema kuwa mtu yeyote akimuua korongo, familia yake ingeathiriwa na msiba na watajikusanya nyumbani kwa mwathiriwa, wakilia kwa sauti hadi mtu huyo apoteze akili au kufa.
''Hadithi kama hizo zilizua uoga, na korongo hao waliendelea kuheshimwa, kuenziwa na sio kuuawa,'' Jimmy Muheebwa, mkuu wa hifadhi katika mbuga ya Uganda, kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali liliambia BBC.
Hata hivyo, kwa wakulima kutoka magharibi ya Uganda, ambapo Korongo wengi hupatikana, hofu hii ya kihistoria imeanza kupotea, na sasa ni wachache tu kama wahifadhi wa mazingira wanaojua sheria inayolinda ndege hawa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
'' Sioni haja ya kuwaenzi ndege hawa kwasababu wanavamia mashamba yetu na kuharibu mazao yetu.Tunahofia usalama wa chakula katika eneo hili,'' Tom Muunguzi, mkulima wa mahindi kutoka kijiji kilichokaribu na mji wa Mbarara mkoa wa MagharubI, aiambia BBC.
Mkulima mwingine anayeishi karibu na mji wa Mbarara, Fausita Aritua, anakubaliana na mwenzake akisema hutumia muda mwingi akiwafurusha Korongo kwenye shamba lake la mahindi.
''Huwa hatuvuni mazao mengi kama hapo awali kwasababu ndege hawa wanavamia kila kitu,'' anaiambia BBC.
Ndege hawa hupatikana zaidi nchini Uganda lakini pia ni maarufu katika nchi za Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji, Afrika Kusini na Zimbabwe.
Wao si wahamaji, lakini uhamia maeneo mengine kwa msimu kulingana na chakula na hali ya hewa.
Kwa urefu wa mita moja, Korongo hawa hupendelea kuishi maeneo oevu kama vile ufuo wa mito, kandokando ya bwawa ambapo huzaana na kula mbegu za nyasi , vyura, wadudu na wadudu wengine wa majini.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, na shinikizo kubwa la chakula, wakulima wamelazimika kulima katika maeneo ya mwamba, na hivyo kupunguza maeneo ya makazi ya Korongo.
Idadi yao imepungua kwa zaidi ya asilimia 80% katika miaka 25 iliyopita, na kutoka zaidi ya 100,000 katika miaka ya 1970, leo ni chini ya 10,000. Taasisi ya kimataifa ya kuhifadhi mazingira (IUCN) iliweka Korongo kwenye orodha ya ndege walio hatarini kupotea mwaka 2012.

''Licha ya muonekano wake mzuri na umaarufu wake, ndege hawa wanakabiliwa na changamoto si haba.Ina maana kuwa iwapo mikakati kabambe haitachukuliwa kukabiliana na hali hii, tunaweza kushuhudia Korongo hawa wakipotea,'' Dan Sseruge, mtaalamu wa ndege nchini Uganda aiambia BBC.
Katika maeneo ya Mbarara, wahifadhi walisema kuwa ilikuwa vigumu kupata ndege hawa, na waliona mara ya kwanza tu asubuhi mapema.
Ndege wengi walikuwa wakikufa baada ya kupewa sumu na wakulima wa mahindi na mchele kutoka wilaya ya Lwengo.
Gilbert Tayebwa, Afisa wa Uhifadhi wa Taasisi ya kimataifa ya Korongo (ICF), alisema kuwa sumu kutoka kwa wakulima ni tishio kubwa kwa ndege hawa, kwani wanaharibu mazao yao.
Hata hivyo, wahifadhi wanajaribu kuwahamasisha wakulima kutumia mbinu mbadala kama vile kutengeneza vinyago vya kutishia ndege.
Wakati mwingine, wakulima huwaua Korongo wakiwapata wamevamia mazao yao yaliyonyunyiziwa na kemikali za kilimo.
''Huwa nawafukuza tu kwasababu nililelewa nikijua hupaswi kuwauwa. Lakini serikali inapaswa kufidia wakulima walioharibiwa mazao yao na ndege hawa'' anaiambia BBC.
Hata hivyo, John Makombo mkurugenzi wa hifadhi katika mamlaka ya wanyamapori nchini Uganda alisema hilo haliwezekani.
''Ni miongoni mwa spishi ambazo zinahuru wa kwenda mahali popote na cha kutamausha nikuwa serikali haina uwezo wa kufidia uharibifu unaofanywa na ndege hawa.'' anaiambia BBC.
Mtaalam wa mazingira katika taasisi ya ICF, Sarah Kugonza anasema Korongo pia wanakabiliwa na changamoto zingine sio tu wakulima.Kama hakuna uhifadhi murua wa maeneo oevu , vinda wao huenda wakaliwa na tai.
Korongo kila uchao wanajipata wanahisi mazingira sio salama.
''Wakati mwingi maeneo oevu huwa yamefurika na siku hizi Korongo huuawa na kamba za umeme wanaporuka angani,'' Kugonza anasema.
Pia muonekano wao mzuri umevutia wengi kuamua kuwakamata na kuishi nao nyumbani, kulingana na Ainomucunguzi.
Lakini Korongo ambao huishi kwa zaidi ya miongo miwili hawawezi kuzaa wakiwa wamefungiwa kwani wanaaminika kuwa waaminifu.
''Ndege hawa huwa na mwenza mmoja maishani mwao. Ikiwa na maana kuwa iwapo mwenza wake ameuawa ama kufariki inakuwa vigumu kupata wenza wapya,'' anasema bwana Muheebwa.
Huvutia wapendwa wao kwa kusakata densi,kuruka na kutembea huku wamejipinda na mara nyingi hutembea kwa makundi kulingana na familia zao au kama wenza.
Ndege hawa hulinda viota vyao kwa udi na uvumba,'

Chanzo cha picha, International Crane Foundation
Kwa jina la sayansi Balearica regulorum gibbericeps, Korongo huwa na aina ya kipekee ya kupumzika kwani hurejea kwa viota vyao kila mwaka, wakitaga mayai kati ya 2 hadi 5 ambayo huagua mayai yao ndani ya siku 28 au 31.
Uharibifu wowote kwa viota huathiri majira ya uzazi.
Ndoa yao ya mke mmoja pia imevutia hisia zisizofaa za waganga wa kienyeji, ambao wanadai kuwa sehemu za korongo zinaweza kuleta uaminifu kutoka kwa mshirika - au bahati nzuri.
"Baadhi ya watu wamenaswa wakiwinda Korongo ili kupeleka baadhi ya viungo vyao vya mwili kwa waganga wakiamini kuwa watapata utajiri. Au ikiwa wewe ni mwanamke, mumeo hatakuacha kamwe," Bwana Tayebwa kutoka ICF alisema.
Hili pia ni jambo ambalo wahifadhi wanajaribu kukabiliana nalo - pamoja na kuwatahadharisha watu kuhusu sheria inayolinda Korongo.

Katika juhudi za kukabiliana na upungufu wa idadi, serikali ya Uganda na vikundi vya wahifadhi sasa wanahamasisha jamii kulinda maeneo oevu.
Rais Yoweri Museveni, ambaye chimbuko lake ni mkoa wa magharibi, ameanza kusihi wanaojaribu kusogea maeneo oevu waondoke mara moja, kulingana na chombo cha habari nchini humo .
Rais pia ametangaza 2025 ni mwaka wa kuhifadhi maeneo oevu.
Taasisi ya ICF imeajiri watunzaji kuangalia na kuhakikisha maeneo wanayoishi Korongo yamelindwa kikamilifu,
Bwana Muhebwa amesema kuwa juhudi hizi japo zinajikokota zinasaidia kuokoa hali lakini idadi ya Korongo bado inapungua.
Mustakabali wa taasisi ya UWA ya hifadhi ni kuwa kielelezo katikamasuala yakutekeleza sheria.
''Tuwatia nguvuni na kuwashitaki watakaopatikana wakiwapa sumu Korongo,'' anasema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi












