Ndege mwenye haya lakini hatari zaidi duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Si vigumu kufikiria kwamba ndege aina ya cassowaries wanatoka katika familia ya mababu ya dinosari.
Ndege hawa wana haya na kwa kawaida ni vigumu kuwaona katika makazi yao ya asili ya misitu ya mvua.
Cassowari mkubwa zaidi ana urefu wa futi sita na uzito wa hadi pauni 160. Cha kushangaza ni kwamba ndege hao wakubwa hawawezi kuruka, lakini miguu yao yenye nguvu huwasaidia kukimbia kwa kasi kubwa sana.
Kulingana na mtandao wa Wikipedia wao ni waogeleaji hodari na wanaweza kukimbia kwa kasi kwenye ardhi na majini.
Ndege hao wenye asili ya misitu ya kitropiki ya New Guinea na kaskazini mwa Australia, Wanaweza kukimbia kwa maili 31 kwa saa wakiwa msituni.
Miguu yao yenye nguvu pia huwasaidia kuruka juu, hadi futi 7 angani. Vilevile Miguu hiyo pia hutumika na ndege huyo kujilinda dhidi ya adui kwani anaweza kurusha mateke makali mbali na kutumia kucha zao zenye nchi kumi kumshambulia mnyama yoyote ambaye ni tishio.
Kwa kawaida ni ndege wasio na fujo kupita kiasi, lakini wanaweza kufanya uharibifu mkubwa ikiwa wamekasirishwa au kukasirika.
Kulingana na BBC kumekuwa na kesi zilizorekodiwa za watu kuuawa na cassowaries, na moja ya hivi karibuni zaidi ni ile ya mwaka 2019, wakati Marvin Hajos, 75, alikufa baada ya kushambuliwa na moja ya cassowaries wake aliokuwa akiwafuga.
Bw Hajos alikuwa amefuga wanyama wa kigeni, ikiwa ni pamoja na llamas, kwa miongo kadhaa, ripoti kutoka kwa magazeti ya ndani zinasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Aina ya Cassowary
Kuna aina tatu za ndege huyo hatari. Lakini ndege wa aina hii anayejulikana zaidi ni Cassowary wa kusini.
Yeye ndiye ndege wa tatu kwa urefu na wa pili kwa uzito zaidi duniani, akiwa mdogo tu kuliko mbuni na emu.
Aina nyingine mbili ni zile za Cassowary wa kaskazini na Cassowary dwarf.
Cassowary wa kaskazini ndiyo aliyegunduliwa hivi majuzi zaidi na ndiye aliye hatari zaidi kuangamia. Spishi ya nne na ambayo imeangamia ni ile ya Cassowary mfupi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, ndege hawa wanakula chakula gani?
Asilimia 90 ya chakula cha Cassowary huwa ni matunda, ingawa spishi zote hula mimea na nyama, ikiwa ni pamoja na mimea inayochipuka, mbegu za nyasi, fangasi, mayai, wanyama wasio na uti wa mgongo, wanyama wadogo wenye uti wa mgongo kama vile samaki, panya, ndege wadogo, vyura, mijusi, na nyoka.
Kifaranga wa Cassowary aanguliwa

Chanzo cha picha, Birdland
Hivi karibuni kifaranga wa cassowary, alianguliwa kwa mafanikio kwa mara ya kwanza katika mbuga ya ndege huko Cotswolds.
Wafugaji katika Birdland huko Bourton-on-the-Water, Gloucestershire, wamekuwa wakijaribu kufuga ndege hao, wasioweza kuruka kwa zaidi ya miaka 25.
Kifaranga huyo ni wa nne pekee kuanguliwa barani Ulaya mwaka huu na wa kwanza nchini Uingereza tangu 2021.
"Tulipomwona kifaranga huyo kwa mara ya kwanza ilikuwa ni wakati wa kipekee sana," mlinzi Alistair Keen alisema.















