SADC, EAC zataka M23 na wahusika wengine kuwa sehemu ya mazungumzo

Mkutano wa pamoja wa EAC-SADC kuhusu mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeitaka M23 na makundi mengine yasiyo ya kiserikali kujumuishwa katika mazungumzo.

Muhtasari

  • Wafungwa wa Kipalestina waachiliwa huru na Israel baada ya Hamas kuwaachia huru mateka wa Israel
  • Mzozo wa DRC Vita haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro DRC-Rais Ruto
  • Tanzania yakanusha kuhusu uhaba wa ARV
  • Gaza Hamas imewaachilia huru mateka watatu wa Kiyahudi chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
  • Rais Samia awataka viongozi wa kikanda kupata suluhu,vinginevyo historia itawahukumu
  • TanzaniaMkutano wa kikanda kutatua mzozo wa DRC waanza Tanzania
  • Trump atia saini amri ya kufungia msaada kwa Afrika Kusini kwasababu ya sheria ya ardhi
  • Mzozo wa DRC: Mkutano wa kikanda kutatua mzozo wa DRC waanza Tanzania
  • Tanzania : Rais Samia awataka viongozi wa kikanda kupata suluhu,vinginevyo historia itawahukumu

Moja kwa moja

Lizzy Masinga na Martha Saranga

  1. SADC-EAC yataka M23 na wahusika wengine kuwa sehemu ya mazungumzo,

    M23

    Chanzo cha picha, AFP

    Mkutano wa pamoja wa EAC-SADC kuhusu mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeitaka M23 na makundi mengine yasiyo ya kiserikali kujumuishwa katika mazungumzo na majadiliano yanayoendelea kwa lengo la kutatua mgogoro wa mashariki mwa Congo.

    Mkutano huo pia umesisitiza umuhimu wa kuondolewa kwa vikundi vya kigeni, kutokomeza kundi la waasi wa Kihutu, Forces Démocratiques pour la Libération du Congo (FDLR), linaloendesha shughuli zake mashariki mwa DRC, pamoja na kuondolewa kwa hatua za ulinzi za Rwanda na vikosi vya Rwanda kujiondoa DRC.

    Wakuu wa majeshi kutoka nchi wanachama wameagizwa kukutana ndani ya siku tano ili kuandaa mpango wa usalama wa Goma na maeneo jirani, pamoja na kujadili ufunguzi wa Uwanja wa Ndege wa Goma na njia kuu za usafirishaji, ikiwa ni pamoja na kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu mashariki mwa DRC.

    Viongozi wa nchi wametaka kusitishwa mara moja kwa mapigano, kutangazwa kwa usitishaji wa mapigano rasmi, na kurejeshwa kwa huduma muhimu kama vile maji, chakula, na bidhaa nyingine za msingi.

    Wamesisitiza kuwa suluhisho la kisiasa na kidiplomasia ndilo njia endelevu zaidi ya kutatua mgogoro wa mashariki mwa DRC.

    Mkutano huo umeagiza mchakato wa mazungumzo yanayoendelea (Luanda na Nairobi) kuunganishwa kuwa mchakato mmoja wa Nairobi-Luanda ili kuimarisha ushirikiano.

    Unaweza kusoma;

  2. Watu 30 hawajulikani walipo baada ya maporomoko ya ardhi China

    xyz

    Takribani watu 30 wametangazwa kuwa hawajulikani walipo baada ya maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Jinping kilichopo kusini-magharibi mwa China, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China.

    Maporomoko hayo ya ardhi yalitokea katika kijiji cha Jinping kilichopo mkoa wa Sichuan saa 11:50 kwa saa za hauko (03:50 GMT), yakifukia nyumba 10 na kuwazuia baadhi ya wakazi. Watu wawili walinusurika.

    Kituo cha dharura kimeanzishwa kwenye eneo la tukio, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye ofisi ya usimamizi wa dharura ya wilaya hiyo.

    Rais wa China Xi Jinping ameagiza "msako mkali kufanyika ili kuwanusuru watu wote wasiojulikana walipo" na hatua kuchukuliwa kwa wale waliokolewa.

    Maelfu ya wafanyakazi wa dharura wanatafuta manusura, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya China.

  3. Hakimu azuia mpango wa Rais Trump kuwapeleka wafanyakazi wa USAID likizo ya malipo

    XYZ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Hakimu Carl Nichols amezuia kwa muda mpango wa Rais Donald Trump wa kuwapa likizo ya malipo wafanyakazi 2,200 wa Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID), saa chache kabla ya mpango huo kutekelezwa.

    Hakimu alitoa amri ya "zuio la muda mfupi" akijibu kesi ya dharura iliyofunguliwa na vyama viwili vya wafanyakazi vyenye nia ya kunusuru shirika hilo.

    Amri hiyo itadumu kwa wiki moja, hadi tarehe 14 Februari saa sita usiku.

    Uamuzi wa Trump ni kufuatia kile anachodai kuwa USAID, shirika la misaada la kimataifa ,halipaswi kutumia pesa za walipa kodi na kutaka kulifuta – na mipango ya kuwapa likizo karibu wafanyakazi 10,000 wa shirika hilo, isipokuwa wafanyakazi 611.

    Takriban wafanyakazi 500 walikuwa tayari wamepelekwa likizo ya kiutawala na wengine 2,200 walikuwa wanatarajiwa kujiunga nao kuanzia saa sita usiku wa Ijumaa (05:00 GMT).

    Lakini kesi ya dharura iliyofunguliwa Ijumaa ilidai kwamba serikali ilikuwa inakiuka Katiba ya Marekani, na pia kwamba wafanyakazi hao walikuwa wakiteseka.

    Hakimu Nichols aliunga mkono vyama vya wafanyakazi, akisema wangeathirika "kwa namna ambayo isingeweza kushughulikiwa" kama mahakama isingeingilia kati, huku akisema kusingekuwa na "athari yoyote kwa serikali".

    Amri hiyo pia inawarudisha kazini wafanyakazi 500 waliokuwa tayari wamepewa likizo ya kiutawala.

    Soma;

  4. Wafungwa wa Kipalestina waachiliwa huru na Israel baada ya Hamas kuwaachia huru mateka wa Israel

    XYZ

    Kwa mara ya tano hii leo kumeshuhudiwa kubadilishana kwa mateka na wafungwa wa Kipalestina tangu Israel na Hamas walipokubaliana kusitisha mapigano. Hamas imeachilia wanaume watatu - Or Levy, Ohad Ben Ami, na Eliyahu Sharabi - na kuwakabidhi kwa maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu huko Deir al-Balah, Gaza.

    Sasa wako Israel wakiungana tena na familia zao.

    Shirika la Msalaba Mwekundu la Palestina (PRCS) limesema kuwa wafungwa saba walioachiliwa walikimbizwa hospitali baada ya kufika Ramallah mapema leo. "Wote walioachiliwa leo wanahitaji huduma ya matibabu na uchunguzi kutokana na ukatili waliokutana nao katika kipindi cha miezi iliyopita.

    Wapo saba waliopelekwa hospitali," amesema Abdullah al-Zaghari, mkuu wa shirika hilo, akizungumza na shirika la habari la AFP.

    Idara ya Habari ya gereza linalosimamiwa na Hamas imesema kuwa kati ya wafungwa 183 waliotarajiwa kuachiliwa leo, 18 walihukumiwa kifungo cha maisha, 54 walihukumiwa kifungo cha muda mrefu, na 111 walikamatwa Gaza baada ya tarehe 7 Oktoba 2023.

    "Uachiliwaji huu unawakilisha hatua mpya katika mapambano ya kudumu ya kuachilia wafungwa wote," inasema taarifa hiyo.

    Kabla ya leo, takribani wafungwa 383 waliachiliwa kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas, ambayo yalianza kutekelezwa mwezi uliopita.

    Soma;

  5. Vita haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro DRC-Rais Ruto

    xyz

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Maelezo ya picha, Rais wa Kenya William Ruto

    Rais wa Kenya, William Ruto – ambaye pia ni Mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika Mashariki EAC – amesema kuwa vita haviwezi kuwa suluhisho kwa mgogoro wa kihistoria katika Jamhuri ya Kidemokrasa ya Congo (DRC).

    Ruto ametoa wito kwa M23 kusitisha hatua za kusonga mbele na Kinshasa kusitisha hatua za kulipiza kisasi.

    ‘’Kwa Pamoja tunawasihi pande zote kutekeleza mapatano ya kusitisha mapigano, na hasa M23 kusitisha hatua yoyote ya kusonga mbele na jeshi la DRC kusitisha hatua zote za kulipiza kisasi.

    Kusitisha mapigano mara moja ndio njia pekee ya kutengeneza mazingira yanayohitajika kwa ajili ya mazungumzo ya kimkakati na utekelezaji wa mkataba kamili wa amani."

    "Inaonekana wazi kuwa mgogoro nchini DRC ni nyeti, na wa muda mrefu, na unahusisha wahusika wengi wanaotafuta maslahi tofauti.

    Masuala yanayohusika ni ya kihistoria na kiuchumi, yanaanzia miongo mingi iliyopita na kuvuka mipaka ya kitaifa na kikanda.

    Kwa sababu hii, pia ni wazi kuwa mgogoro wa aina hii hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi.

    ‘Tunapaswa kupinga shinikizo la kufikiria kuwa tunaweza kwa namna fulani kupigana au kulipiza kisasi ili kupata suluhisho katika hali ya mgogoro mgumu kama huu."

    Ruto alikuwa akizungumza katika mkutano wa kikanda unaofanyika Dar es Salaam, Tanzania, ili kujadili mgogoro unaozidi kuongezeka nchini DRC.

    Mkutano huu unafanyika kwa siri, na taarifa rasmi itatolewa baadaye kuhusu masuala yaliyojadiliwa na yaliyoafikiwa.

    Soma;

  6. Tanzania yakanusha kuhusu uhaba wa ARV

    XYZ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya afya nchini Tanzania imesema kuwa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI haziuzwi na kwamba zipo za kutosha.

    Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo ripoti kwenye vyombo vya habari na mitandaoni zikielezea uhaba wa dawa na kuwalazimu watumiaji kununua dawa hizo.

    ‘Watumiaji wa dawa hizi hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa hizi’ imeeleza taarifa ya wizara ya afya

    Wizara hiyo imewataka wananchi kupuuza taarifa hizo na kuendelea kutumia kwa usahihi.

    Hivi karibuni rais wa Marekani Donald Trump alitoa agizo la kusitisha usambazaji wa dawa za HIV ,TB na Malaria,hatua iliyozua siutafahamu barani Afrika.

    Siku ya Jumanne, wakandarasi na washirika wanaofanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) nchini Tanzania na Kenya walianza kupokea barua hizo ili kusitisha ufadhili huo mara moja, kulingana na vyanzo.

    Soma;

  7. Hamas imewaachilia huru mateka watatu wa Kiyahudi chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.

    xyz

    Hamas imewaachilia huru mateka watatu wa Kiyahudi kutoka Israeli huko Gaza kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina waliokamatwa Israeli.

    Eli Sharabi, Ohad ben Ami na Or Levy wamekabidhiwa kwa jeshi la Israeli.

    Wanafamilia wa mateka hao wamesema kwamba wanaume hawa wanaonekana kuwa katika hali mbaya kiafya.

    Waisraeli walikusanyika kwenye uwanja uliofahamika kama Hostages Square huko Tel Aviv ili kushuhudia kuachiliwa kwa wanaume hao.

    Zaidi ya wafungwa 180 wa Kipalestina wanaachiliwa katika magereza ya Israeli chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas ambayo yalianza tarehe 19 Januari.

    Katika hatua ya kwanza ya makubaliano, mateka 33 wa Kiyahudi wanatarajiwa kuachiliwa huru.

    Soma;

  8. Rais Samia awataka viongozi wa kikanda kupata suluhu,vinginevyo historia itawahukumu

    Rais Samia

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, mwenyeji wa mkutano wa kilele wa kikanda wa kutatua mzozo wa DRC, amezitaka pande zinazohusika katika mzozo huo kushiriki kikamilifu katika mazungumzo.

    "Tunatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo wa DRC kushiriki vyema katika mazungumzo, kuweka kipaumbele kwa ustawi wa watu wake na kujitolea kuishi pamoja kwa amani."

    Wakuu wa nchi

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Aliwataka viongozi wa ukanda huo kutafuta suluhu la mzozo huo, huku akionya kuwa iwapo watashindwa, historia itawahukumu vikali.

    “Kama viongozi wa kanda, historia itatuhukumu vikali ikiwa tutanyamaza na kutazama hali inavyozidi kuwa mbaya siku hadi siku.

    Na kulingana na falsafa ya suluhisho la Kiafrika kwa shida za Kiafrika, nchi zetu zina jukumu la pamoja la kuhakikisha tunashughulikia kwa haraka changamoto zilizopo za ukosefu wa usalama ambazo zimeathiri sana ustawi wa raia wasio na hatia.

    Unaweza kusoma

  9. Mkutano wa kikanda kutatua mzozo wa DRC waanza Tanzania

    Kagame

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Mkutano wa kikanda umeanza katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam unaolenga kutatua mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Mkutano huo wa pamoja umehudhuriwa na viongozi wa nchi wanachama kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

    Rais wa DRC Felix Tshisekedi anahudhuria mkutano huo, akiwa amemtuma Waziri Mkuu wake Judith Suminwa badala yake.

    Rais wa Burundi Evariste Ndiyishimiye, ambaye amekuwa akiunga mkono Kinshasa pia amemtuma waziri mkuu wa nchi hiyo.

    Rais wa Rwanda Paul Kagame anahudhuria. Kumekuwa na kutoaminiana kwa kiasi kikubwa kati ya Kigali na Kinshasa, huku Rais Tshisekedi akiishutumu Kigali kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo limeteka maeneo muhimu, likiwemo Goma mashariki mwa nchi hiyo.

    Kwa upande mwingine, Kigali imekikosoa kikosi cha SADC nchini Congo akikitaja kama "kikosi cha kijeshi" kinachohusika katika "operesheni za kivita" kusaidia serikali ya Congo "kupambana na watu wake".

    Wakuu wa nchi

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Tshisekedi amekataa mara kwa mara kufanya mazungumzo na M23, badala yake akitaka Rwanda kujiondoa katika ardhi ya Congo na vikwazo dhidi ya Kigali.

    Mkutano huo unajaribu kusuluhisha usitishaji mapigano na kuzuia mzozo huo kukumba eneo kubwa zaidi.

    Machafuko hayo hadi sasa yamesababisha mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kuacha huduma muhimu mjini Goma kutatizwa kwa kiasi kikubwa. Wakati EAC inatetea mazungumzo ya moja kwa moja na M23, SADC inalingana na matakwa ya Kinshasa ya kujiondoa kwa Rwanda.

  10. Trump atia saini amri ya kufungia msaada kwa Afrika Kusini kwasababu ya sheria ya ardhi

    Mashamba

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya kufungia msaada wa kifedha kwa Afrika Kusini, baada ya kutishia kufanya hivyo mapema wiki hii.

    Trump alisema anaweka amri hiyo kwa sababu ya sheria mpya ya ardhi ya Afrika Kusini, ambayo anasema inakiuka haki za watu, na pia kwa sababu ya kesi yake ya mahakama ya kimataifa inayoishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki.

    Inazidisha mzozo kati ya nchi hizo mbili karibu wiki moja baada ya Trump kutishia kupunguza ufadhili bila kutaja ushahidi, kwamba "Afrika Kusini inanyakua ardhi" na "matabaka fulani ya watu" yalikuwa yakitendewa "vibaya sana".

    Mshauri wa karibu wa Trump Elon Musk, ambaye alizaliwa nchini Afrika Kusini, pia alijiunga na ukosoaji huo akiuliza X kwa nini Ramaphosa alikuwa na "sheria za umiliki za kibaguzi".

    Rais Cyril Ramaphosa bado hajatoa kauli yake lakini hapo awali alitetea sera ya ardhi ya Afrika Kusini baada ya tishio la Trump siku ya Jumapili.

    Alisema serikali haijanyakua ardhi yoyote na sera hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata ardhi kwa usawa.

    Sheria ya Rais Ramaphosa ilitiwa saini mwezi uliopita, na inaruhusu unyakuzi wa ardhi bila kulipwa fidia katika mazingira fulani.

    Umiliki wa ardhi kwa muda mrefu umekuwa suala la kutatanisha nchini Afrika Kusini huku mashamba mengi ya binafsi yakimilikiwa na watu weupe, miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa kibaguzi wa ubaguzi wa rangi.

    Kumekuwa na wito wa mara kwa mara kwa serikali kushughulikia mageuzi ya ardhi na kukabiliana na dhuluma za zamani za ubaguzi wa rangi.

    Unaweza pia kusoma;

  11. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu