Jinsi historia ya uchafuzi wa wanadamu inavyoandikwa kwenye uso wa dunia

edfc

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Chris Baraniuk
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Watafiti wanakusanya ushahidi wa athari ya shughuli za binadamu kwenye sayari hii. Mwaka 2012 hadi 2017, Raffaele Siano alichota mabaki ya mchanga yaliyo chini kabisa ya bahari kwenye bandari ya Brest. Vijidudu vinavyoishi katika bandari hii ya Ufaransa havijapona kutoka Vita vya Pili vya Dunia.

Yeye na wenzake kutoka Taasisi ya Sayansi ya Bahari (Ifremer), iliopo Ufaransa, walipochambua vipande vya DNA vilivyo katika mchanga huo - waligundua kitu cha ajabu.

Tabaka la mchanga wa zamani wa kabla ya mwaka 1941 - ulikuwa na vijidudu vinavyoitwa dinoflagellate, ambavyo vilikuwa tofauti sana kijeni na vijidudu vilivyokuwa kwenye tabaka za kina kifupi na za hivi karibuni.

Siano anaeleza kuwa bandari ya Brest ililipuliwa wakati wa vita. Na mwaka 1947, meli ya mizigo ya Norway ililipuka katika Ghuba ya Brest. Maafa hayo yalisababisha vifo vya watu 22 na kueneza ammonium nitrate katika bahari, kemikali yenye sumu inayotumika kutengenezea mbolea na vilipuzi.

"Kulikuwa la kundi la vijidudu, ambao walikuwa wengi sana kabla ya Vita vya Pili ya Dunia - na baada ya Vita vya Pili vya Dunia karibu wote wametoweka," anasema Siano.

Walichapisha utafiti huo mwaka 2021.

Pia unaweza kusoma

Mazingira hukumbuka

fdc

Chanzo cha picha, Ifremer

Maelezo ya picha, Wanasayansi katika bandari ya Etang de Thau, Kusini mwa Ufaransa

Asili ina namna yake ya kukumbuka matukio - hasa shughuli za binadamu zinazochafua mazingira, wakati mwingine huonekana kwenye pete za miti, mchanga w pwani na mifumo ya ikolojia.

Siano na wenzake ni wanaikolojia lakini pia wanafanya kazi na wanahistoria. "Ardhi ilibadilika kwa sababu ya athari za shughuli za binadamu na pia matukio ya kihistoria," anasema Siano.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Timu hiyo ilipochanganua chembe za mchanga kutoka Brest, pia iligundua ongezeko la polepole la metali nzito kadiri muda unavyosonga. Tabaka mpya za mchanga zina kiasi kikubwa cha zebaki, shaba, risasi na zinki.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa kuna kiwango kama hicho cha baadhi ya kemikali za metali – hasa risasi na kromiamu - katika Bandari ya Pearl, kambi kuu ya wanamaji ya Marekani huko Hawaii ambayo ilishambuliwa na ndege za kivita za Japan mwaka 1941.

Hata hivyo, Siano anasema hawezi kuwa na uhakika ikiwa metali hizi zilitoka moja kwa moja katika mabomu hayo. Lakini vyovyote vile iwavyo, kuna dalili katika bandari ya Brest na Pearl ya uchafuzi wa mazingira uliofanyika katika historia ya mwanadamu.

Watafiti wengine pia wameizunguka dunia kutafuta rekodi za kijiolojia za uchafuzi wa mazingira. Huko China, mchanga unaonyesha ongezeko kubwa la kemikali za chuma tangu 1950 - hilo linahusishwa na kuongezeka kwa uchafuzi wa hewa katika ya nusu ya pili ya Karne ya 20.

Utafiti mwingine unaeleza kuwa viwanda vya ujenzi wa meli, vinaweza kuchangia kuongezeka kwa metali nzito katika pete za miti katika maeneo fulani ya China.

Hata ufuaji vya vyuma huko Roma, karne nyingi zilizopita, umeacha alama yake. Utafiti mmoja wa 2022, uligundua ongezeko kubwa la kemikali za chuma katika barafu na mchanga katika maeneo ya Ulaya, na inahusishwa na maendeleo ya viwanda wakati wa utawala wa Kirumi.

Jean-Luc Loizeau kutoka Chuo Kikuu cha Geneva amechunguza mchanga wa Ziwa Geneva, karibu na mtambo wa kusafisha maji machafu. Anasema mabaki ya hapo yana athari ya shughuli za binadamu.

Katika utafiti wa 2017, yeye na wenzake wanaelezea juu ya uwepo wa uchafu wa metali nzito ambao ulionekana katika tabaka za mchanga kutoka miaka ya 1930. Miongoni mwa mifano anayotoa ni ongezeko la kemikali za zebaki katika miaka ya 1970.

"Tunajua kulikuwa na ajali. Zebaki ilimwagika baada ya kupasuka kwa tanki na athari ya kemikali hizo inaonekana kwenye mchanga," anasema.

Kando na metali, vifaa vyenye mionzi pia vimepatikana katika maeneo mbalimbali duniani. Nchini Switzerland, kwa mfano, kemikali ya radiamu ilitumika kwa muda mrefu kutengeneza saa zinazowaka. Mabaki ya radiamu kutoka katika viwanda vya kutengeneza saa yamepatikana katika maeneo ya kutupia taka na majengo katika nchi hiyo.

Silaha za Nyukilia

gv

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Chembe za uchafu zilitokea wakati Marekani ilipodondosha bomu la atomiki huko Hiroshima, Japani

Silaha za nyuklia za wakati wa karne ya 20 zimeacha athari pia. Kuna mashimo makubwa katika jangwa la Nevada kutokana na majaribio makubwa ya silaha hizo. Na uchafuzi uliosababishwa na kulipuliwa kwa nyuklia uko wazi.

Mwaka 2019, watafiti walieleza kwamba baadhi ya chembe za mchanga kwenye fukwe karibu na jiji la Japani la Hiroshima, ni chembe za uchafu kutokana na bomu la atomiki la Marekani katika eneo hilo, lililodondoshwa tarehe 6 Agosti 1945, kuelekea mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia.

Bomu liligeuza majengo kuwa vumbi, moto kutoka katika mlipuko ulikutana na vumbi hilo, na mlipuko huo ukaenea katika mazingira ya karibu.

Mabaki ya milipuko ya nyuklia hayabaki nje tu. Yanaweza kuwa katika dari yako. Vumbi hilo mara nyingi hukaa kwa miongo kadhaa - hivyo athari ya uchafu huo inaweza kubaki.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2003 uliripoti juu uchunguzi katika nyumba 201 katika jimbo la New Jersey la Marekani. Miongoni mwa athari ambazo watafiti walizigundua kulikuwa na kiwango cha kemikali ya risasi, iliyohusiana na uchafuzi wa hewa wakati wa Karne ya 20. Lakini pia walipata kiasi kidogo cha mionzi aina ya Caesium-137.

Uchafu huo ulikuwa unapatikana zaidi kwenye nyumba za zamani. Watafiti walipendekeza kuwa, marudio ya majaribio ya silaha za nyuklia nchini Marekani ndio yamechangia, hasa katika miaka ya 1950 na 1960.

Siano na wenzake sasa wamekusanya zaidi ya mashungu 120 ya michanga kutoka nchi tisa tofauti barani Ulaya, kwa matumaini ya kupata uhusiano zaidi kati ya matukio ya kihistoria na uharibifu wa DNA au uchafu wa chuma ulioachwa kwenye chembe hizo.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah