Jinsi uchafuzi wa mazingira unavyosababisha ugumba kwa wanaume

Chanzo cha picha, Getty Images
Ubora wa manii unaonekana kupungua kote ulimwenguni lakini ni suala linalojadiliwa kidogo sana kama sababu ya utasa. Sasa wanasayansi wanafikiria kidogo juu ya kile kinachoweza kuwa nyuma ya tatizo hilo.
"Tunaweza kukusuluhisha. Hakuna shida. Tunaweza kukusaidia," daktari alimwambia Jennifer Hannington. Kisha akamgeukia mumewe, Ciaran Hannington, na kusema: "Lakini hakuna mengi tunayoweza kukufanyia."
Wanandoa hao wanaoishi Yorkshire, Uingereza, walikuwa wamejaribu kutafuta mtoto kwa miaka miwili. Walijua inaweza kuwa vigumu kwao kushika mimba kwani Jennifer ana ugonjwa wa ovari ya polycystic, hali ambayo inaweza kuathiri uwezo wake wa kuzaa. Jambo ambalo hawakutarajia ni kwamba kulikuwa na matatizo kwa upande wa Ciaran pia.
Uchunguzi uliweka bayana masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na idadi ndogo ya manii na kasi ndogo ya manii. Mbaya zaidi, masuala haya yalifikiriwa kuwa magumu kutibu kuliko ya Jennifer - labda hata hayawezekani.
Hannington bado anakumbuka majibu yake: "Nilishtuka. Nilihuzunika. Nilikataa kabisa. Nilifikiri madaktari walikuwa wamekosea." Alifahamu fika wakati wote anataka kuwa baba. "Nilihisi kama ningemwacha mke wangu."
Kwa miaka mingi, afya yake ya akili ilidhoofika. Alianza kutumia muda mwingi peke yake, kukaa kitandani na kugeukia pombe kwa ajili ya kujifariji. Kisha hofu ikaanza.
"Nilikuwa kwenye matatizo," anasema. "Ilikuwa mahali penye kina, giza."
Ugumba kwa mwaume huchangia takriban nusu ya visa vyote vya ugumba na huathiri 7% ya idadi ya wanaume. Walakini, haijajadiliwa sana kuliko utasa au ugumba kwa mwanamke, kwa sehemu kutokana na miiko ya kijamii na kitamaduni inayoizunguka.
Kwa wanaume wengi walio na matatizo ya uzazi, sababu bado haijafafanuliwa - na suala la unyanyapaa kwao inamaanisha wengi wanateseka kimya kimya.
Utafiti unaonyesha kuwa tatizo linaweza kuongezeka. Mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa mazingira yameonyeshwa kuathiri uwezo wa kuzaa wa wanaume, na hasa, ubora wa manii - na uwezekano wa kupata madhara makubwa zaidi kwa watu binafsi, na jamii nzima.
Tatizo la uzazi lililofichwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Idadi ya watu ulimwenguni imeongezeka sana katika karne iliyopita. Miaka 70 tu iliyopita - ndani ya maisha ya mwanadamu - kulikuwa na watu bilioni 2.5 tu duniani. Mnamo 2022, idadi ya watu ulimwenguni ilifikia bilioni nane. Hata hivyo, kasi ya ongezeko la watu imepungua, hasa kutokana na mambo ya kijamii na kiuchumi.
Viwango vya kuzaliwa duniani kote viko chini ya rekodi. Zaidi ya 50% ya idadi ya watu duniani wanaishi katika nchi zilizo na kiwango cha uzazi chini ya watoto wawili kwa kila mwanamke - na kusababisha idadi ya watu ambayo bila suala la uhamiaji itapungua polepole.
Sababu za kushuka huku kwa viwango vya uzazi ni pamoja na maendeleo chanya, kama vile uhuru mkubwa wa kifedha wa wanawake na udhibiti wa afya zao za uzazi.
Kwa upande mwingine, katika nchi zilizo na viwango vya chini vya uzazi, wanandoa wengi wangependa kupata watoto wengi kuliko wao, utafiti unaonyesha, lakini wanaweza kusita kwa sababu za kijamii na kiuchumi, kama vile ukosefu wa msaada kwa familia.
Wakati huo huo, kunaweza pia kupungua kwa aina tofauti ya uzazi, inayojulikana kama fecundity - maana yake ni uwezo wa kimwili wa mtu wa kuzalisha watoto.
Hasa, utafiti unapendekeza kwamba wigo mzima wa matatizo ya uzazi kwa wanaume unaongezeka, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya manii, kupungua kwa viwango vya testosterone, na kuongezeka kwa viwango vya upungufu wa nguvu za kiume na saratani ya tezi dume.
Seli zinazoogelea

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mbegu za kiume ni seli za kupendeza," anasema Sarah Martins Da Silva, msomi wa matibabu katika dawa za uzazi katika Chuo Kikuu cha Dundee na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake. "Ni ndogo, zinaelea, zinaweza kuishi nje ya mwili. Hakuna chembechembe nyingine zinazoweza kufanya hivyo. Ni jambo la kipekee."
Mabadiliko yanayoonekana madogo yanaweza kuwa na athari kubwa kwa seli hizi maalum, na haswa, uwezo wake wa kurutubisha yai. Vitu muhimu vya uzazi ni uwezo wake wa kusonga mbele kwa ufanisi (motility), umbo na saizi yao (mofolojia), na ni ngapi katika idadi fulani ya manii (sperm count). Ni mambo ambayo huchunguzwa wakati mwanamume anapoenda kuangalia uzazi.
"Kwa ujumla, unapopata mbegu chini ya milioni 40 kwa mililita moja ya shahawa au manii, unaanza kuona matatizo ya uzazi," anasema Hagai Levine, profesa wa magonjwa katika Chuo Kikuu cha Hebrew cha Jerusalem.
Idadi ya manii, anaelezea Levine, inahusishwa kwa karibu na nafasi za uzazi. Ingawa idadi kubwa ya manii haimaanishi uwezekano mkubwa zaidi wa kutunga mimba, chini ya ya idadi ya milioni 40/ml uwezekano wa kushika mimba hushuka haraka.
Mnamo 2022, Levine na washirika wake walichapisha mapitio ya mienendo ya kimataifa ya hesabu ya manii. Ilionyesha kuwa hesabu za manii zilishuka kwa wastani kwa 1.2% kwa mwaka kati ya 1973 hadi 2018, kutoka 104 hadi 49 milioni / ml. Kuanzia mwaka wa 2000, kiwango hiki cha kushuka kiliongezeka hadi zaidi ya 2.6% kwa mwaka.
Mabadiliko ya mtindo wa maisha ya mtu binafsi yanaweza yasitoshe kukomesha kushuka kwa ubora wa manii. Ushahidi unaoongezeka unaonyesha kuwa kuna tishio pana zaidi la kimazingira: vichafuzi vyenye sumu.
Dunia iliyojaa sumu
Rebecca Blanchard, mshiriki wa ufundishaji wa mifugo na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza, anachunguza athari za kemikali za mazingira zinazopatikana ndani ya nyumba kwenye afya ya uzazi wa kiume.
Anatumia mbwa kama mfano wa mlinzi - aina ya mfumo wa tahadhari ya mapema kwa afya ya binadamu.
"Mbwa anashiriki mazingira yetu," anasema. "Anaishi katika kaya moja na anaathiriwa na vichafuzi vya kemikali sawa na sisi. Tukimtazama mbwa, tunaweza kuona kinachoendelea kwa binadamu."
Utafiti wake ulijikita zaidi kwenye kemikali zinazopatikana katika plastiki, vizuia moto na vitu vya kawaida vya nyumbani. Baadhi ya kemikali hizi zimepigwa marufuku, lakini bado ziko kwenye mazingira au vitu vya zamani. Uchunguzi wake umebaini kuwa kemikali hizi zinaweza kuvuruga mifumo yetu ya homoni, na kudhuru uzazi wa mbwa na wanaume.
"Tuligundua kupungua kwa unyumbulikaji wa mbegu za kiume zikiwa kwenye uke kwa binadamu na mbwa," anasema Blanchard. "Pia kulikuwa na ongezeko la kiasi cha kugawanyika kwa DNA."

Chanzo cha picha, Alamy
Matokeo hayo yanafanana na utafiti mwingine unaoonyesha tatizo la uzazi linalosababishwa na kemikali zinazopatikana kwenye plastiki, dawa za nyumbani, kwenye mnyororo wa chakula na angani. Inathiri wanaume na wanawake na hata watoto wachanga. Kaboni nyeusi, kemikali na phthalates zote zimepatikana kufikia watoto kwenye mji wa mimba.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza pia kuathiri vibaya uwezo wa kuzaa kwa mwanaume, huku tafiti kadhaa za wanyama zikionyesha kuwa manii huathirika zaidi na athari za kuongezeka kwa joto.
Mawimbi ya joto yameonyeshwa kuharibu manii katika wadudu, na athari sawa imeonekana kwa wanadamu. Utafiti wa 2022 uligundua kuwa halijoto ya juu iliyoko - kutokana na ongezeko la joto duniani, au kufanya kazi katika mazingira ya joto - huathiri vibaya ubora wa manii.
Lishe duni, mkazo na pombe

Chanzo cha picha, Getty Images
Kando na mambo haya ya kimazingira, matatizo ya mtu binafsi yanaweza pia kudhuru uzazi wa kiume, kama vile lishe duni, maisha ya kukaa tu, msongo wa mawazo, na matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
Katika miongo ya hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko kuhusu wazazi wa baadae - na wakati wanawake mara nyingi wanakumbushwa kuhusu ukomo wao wa uzazi kibaolojia, suala la umri ulifikiriwa kuwa sio jambo la kuzingatiwa kwa uzazi wa mwanaume.
Sasa, jambo hilo linabadilika. Umri mkubwa kwa uzazi umehusishwa na kupungua kwa ubora wa manii na kupungua kwa uwezo wa uzazi.
Kuna wito unaokua wa uelewa zaidi wa masuala ya utasa na ugumba kwa mwanaume na mbinu mpya za kuzuia, utambuzi na matibabu - pamoja na kuongezeka kwa ufahamu wa haja ya haraka ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.
Wakati huo huo, kuna chochote ambacho mtu anaweza kufanya ili kulinda au kuongeza ubora wao wa manii?
Mazoezi na lishe bora inaweza kuwa mwanzo mzuri, kwani yamehusishwa na uboreshaji wa ubora wa manii. Blanchard anapendekeza kuchagua vyakula vya kikaboni na bidhaa za plastiki zisizo na BPA (Bisphenol A), kemikali inayohusishwa na matatizo ya uzazi kwa wanaume na wanawake. "Kuna mambo madogo ambayo unaweza kufanya," anasema.
Na, anasema Hannington, usiteseke kimya kimya.
Baada ya miaka mitano ya matibabu na raundi tatu za ICSI (Intracytoplasmic Sperm Injection), mbinu ya IVF ambayo manii huingizwa katikati ya yai la mwanamke, yeye na mke wake walifanikiwa kupata watoto wawili.
Kwa watu ambao wanapaswa kulipia matibabu ya uzazi wenyewe, utaratibu kama huo hata hivyo hauwezi kumudu. Nchini Marekani, awamu moja ya IVF inaweza kugharimu zaidi ya $30,000 na bima ya IVF inaweza kuwa ngumu kutegemea na mkataba wa mwajiri wako. Na Hannington anasema bado anahisi hajakaa sawa kiakili kutokana na aliypitia.
"Ninashukuru kila siku kwa kupata watoto wangu, lakini huwezi kusahau," anasema. "Itabaki kuwa sehemu yangu ya maisha."














