Mfanyakazi wa shambani wa Afrika Kusini asema alilazimishwa kuwalisha nguruwe wanawake
Mfanyikazi wa shambani mzungu kutoka Afrika Kusini anayetuhumiwa kuwaua wanawake wawili weusi anasema alilazimishwa kuwalisha nguruwe miili yao, kulingana na wanasheria.
Muhtasari
- Mahakama yaamuru raia wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya Tundu Lissu walindwe
- Burundi na M23 wabadilishana wafungwa wa kivita
- Mfanyakazi wa shambani wa Afrika Kusini asema alilazimishwa kuwalisha nguruwe wanawake
- Urusi yapuuza agizo kuhusu manowari ya Trump, na kuhimiza tahadhari juu ya matamshi ya nyuklia
- Moja ya kesi kubwa zaidi za ugaidi nchini Urusi yaanza Moscow huku watu 19 wafikishwa Mahakamani
- Msichana wa miaka miwili apatikana kwenye sanduku la mwanamke New Zealand
- Iran na Pakistan zatia saini mikataba 12
- Mkulima Mzungu anayetuhumiwa kuwalisha nguruwe miili ya wanawake kufika mahakamani
- Trump athibitisha mjumbe wa Marekani Witkoff kuzuru Urusi wiki ijayo
- Mamia ya maafisa wa zamani wa Israel wamtaka Trump kumshinikiza Netanyahu kumaliza vita
- Wanafunzi kutoka China huambiwa wawapeleleze wenzao Uingereza - ripoti
- Wachimba madini wapatikana wamekufa baada ya saa 70 za kunasa
- Korea Kusini yaondoa vipaza sauti vya propaganda dhidi ya Korea Kaskazini kwenye mpaka
- Viongozi wa Magharibi walaani video za mateka waliodhoofika huko Gaza
- Zaidi ya wahamiaji 60 kutoka Afrika wafariki baada ya boti kupinduka
Moja kwa moja
Rashid Abdallah & Dinah Gahamanyi
Mahakama yaamuru raia wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya Tundu Lissu walindwe

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama Kuu imeamuru mashahidi ambao ni raia wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, walindwe.
Hii inamaanisha kuwa watatakiwa kutoa ushahidi wao kwa kificho (bila kuonekana), majina yao kutokutajwa mahakamani wala taarifa zao zinazoweza kuwafanya watambulike, wao, familia zao, marafiki zao na watu wengine wa karibu yao, kulingana na taarifa ya gazeti la mtandaoni la Mwananchi Tanzania.
Kulingana na taarifa hiyo uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Agosti 4, 2025 na Jaji Hussein Mtembwa kufuatilia maombi yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mshitaka (DPP), imezuia pia taarifa zao kusambazwa, kuchapishwa na kutangazwa na chombo chochote cha habari, bila ridhaa ya Mahakama.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 akiwa kwenye mkutano wa CHADEMA huko Mbinga kusini mwa Tanzania kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam na baadaye kupandishwa kizimbani Aprili 10, 2025.
Lissu aliyekamatwa kwa tuhuma za kufanya uchochezi wa kutofanyika Uchaguzi Mkuu 2025, baada ya kumaliza mkutano wa hadhara alipokuwa akiendelea kunadi msimamo wa chama hicho wa 'No Reforms, No Election, ikimaanisha bila mabadiliko hakuna uchaguzi.
Pia Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini ambalo halina dhamana kisheria na adhabu kwa mshtakiwa anayekutwa na hatia ni kifo.
Unaweza pia kusoma:
Burundi na M23 wabadilishana wafungwa wa kivita

Chanzo cha picha, Rwanda Gov
Burundi ilikabidhiwa wanajeshi 20 ambao walikuwa wamekamatwa katika mapigano na vuguvugu la DRC la M23 tangu 2023, huku M23 ikirudishiwa idadi sawa na hiyo.
Habari za kubadilishana wafungwa kati ya Burundi na M23 ziliripotiwa kwa mara ya kwanza kwenye tovuti mbalimbali za habari wiki iliyopita, lakini BBC Idhaa ya Maziwa Makuu baadaye ilipata vyanzo ambavyo vilikuwa vinafahamu habari za mazungumzo hayo.
Vyanzo hivi viliiambia BBC kuwa mabadilishano ya wafungwa wa kivita yalifanyika kwenye mpaka wa Nemba kati ya Rwanda na Burundi mnamo siku ya Ijumaa, Julai 25, 2025.
Kwa upande wa M23, msemaji wa jeshi la kundi hilo, alipoulizwa kuhusu habari hizo na BBC alijibu kuwa ''hakuna maoni'', akimaanisha ''hatuna la kusema kuhusu hilo''.
Upande wa Burundi haujakanusha wala kuthibitisha kuwa hatua hii ilifanyika. Hata hivyo, msemaji wa jeshi la nchi hiyo, Jenerali Gaspard Baratuza, alisema kuwa "Ikiwa walifanya hivyo, ni vizuri, ni ndani ya vifungu vya sheria za kimataifa zinazohusu vita."
Unaweza pia kusoma:
Mfanyakazi wa shambani wa Afrika Kusini asema alilazimishwa kuwalisha nguruwe wanawake

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
Maelezo ya picha, Adrian de Wet (kushoto) akiwa amesimama na bosi wake Zachariah Johannes Olivier (kulia) Mfanyikazi wa shambani mzungu kutoka Afrika Kusini anayetuhumiwa kuwaua wanawake wawili weusi anasema alilazimishwa kuwalisha nguruwe miili yao, kulingana na wanasheria.
Adrian de Wet ni mmoja wa wanaume watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji baada ya Maria Makgato, 45, na Lucia Ndlovu, 34, kuuawa wakidaiwa kutafuta chakula kwenye shamba karibu na Polokwane katika jimbo la Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini mwaka jana.
Miili yao ilidaiwa kutolewa na kulishwa nguruwe katika jaribio dhahiri la kufuta ushahidi.
Bw De Wet, 20, aligeuka kuwa shahidi wa serikali kesi ilipoanza siku ya Jumatatu na anasema mmiliki wa shamba hilo Zachariah Johannes Olivier aliwapiga risasi na kuwaua wanawake hao wawili.
Bi Makgato na Bi Ndlovu walikuwa wakitafuta bidhaa za maziwa zilizokwisha muda mfupi uliopita ambazo zilikuwa zimeachwa kwa nguruwe walipouawa.
Bw De Wet, msimamizi katika shamba hilo, alitoa ushahidi kwamba alilazimishwa kutupa miili yao ndani ya boma la nguruwe, kulingana na mwendesha mashtaka na wakili wake.
Ikiwa mahakama itakubali ushahidi wake, mashtaka yote dhidi yake yatafutwa.
Kesi hiyo imezua ghadhabu kote Afrika Kusini, na hivyo kuzidisha mivutano kuhusu ubaguzi wa rangi nchini humo.
Mvutano huo umeenea hasa katika maeneo ya vijijini, licha ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi zaidi ya miaka 30 iliyopita. Mashamba mengi ya kibinafsi yanasalia mikononi mwa wazungu wachache, wakati wafanyakazi wengi wa mashambani ni weusi na wanalipwa vibaya, jambo linalochochea chuki miongoni mwa watu weusi, huku wakulima wengi weupe wakilalamikia viwango vya juu vya uhalifu.
Soma zaidi:
Urusi yapuuza agizo kuhusu manowari ya Trump, na kuhimiza tahadhari juu ya matamshi ya nyuklia

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi ilisema Jumatatu kwamba kila mtu anapaswa kuwa "muangalifu sana" kuhusu matamshi ya nyuklia, ikijibu taarifa ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba alikuwa ameamuru kuwekwa upya kwa manowari za nyuklia za Marekani.
Katika majibu yake ya kwanza ya umma kuhusu maoni ya Trump, Kremlin ilipuuza umuhimu wake na kusema haikutazami kuingia kwenye mabishano ya umma na Trump.
Trump alisema Ijumaa kuwa ameamuru manowari mbili za nyuklia kuhamishwa hadi "maeneo yanayofaa" kujibu matamshi kutoka kwa rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev kuhusu hatari ya vita kati ya wapinzani hao wenye silaha za nyuklia.
"Katika suala hili, ni dhahiri kwamba manowari za Amerika tayari ziko kwenye jukumu la kupigana. Huu ni mchakato unaoendelea, hilo ndilo jambo la kwanza," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari.
"Lakini kwa ujumla, kwa kweli, hatungependa kujihusisha na mzozo kama huo na hatungependa kutoa maoni juu yake kwa njia yoyote," aliongeza. "Kwa kweli, tunaamini kwamba kila mtu anapaswa kuwa muangalifu sana na matamshi ya nyuklia."
Kipindi hiki kinakuja wakati mgumu, huku Trump akitishia kuweka vikwazo vipya kwa Urusi na wanunuzi wa mafuta yake, ikiwa ni pamoja na India na Uchina, isipokuwa pale Rais Vladimir Putin atakubali ifikapo Ijumaa kumaliza vita vya miaka mitatu na nusu nchini Ukraine.
Unaweza pia kusoma:
Moja ya kesi kubwa zaidi za Ugaidi nchini Urusi yaanza Moscow huku watu 19 wafikishwa Mahakamani

Chanzo cha picha, Mikhail Sinitsyn/TASS
Mahakama ya Moscow imeanza kusikiliza kesi ya wale wanaotuhumiwa kwa ugaidi kufuatia shambulio la mwaka jana kwenye Jumba la Jiji la Crocus katika mkoa wa Moscow, ambapo watu 147 waliuawa. Kesi hiyo inafanyika nyuma ya milango iliyofungwa.
Watu kumi na tisa wanashtakiwa: wahusika wanne wana daiwa kuwa "washirika"
Wahusika wa shambulio hilo bado hawajapatikana.
Washtakiwa wakuu wanne wanatoka Tajikistan: Dalerdzhon Mirzoyev, Saidakram Rachabalizoda, Shamsiddin Fariduni na Muhammadsobir Faizov. Mkubwa ana umri wa zaidi ya miaka 30, huku mdogo akiwa na umri wa zaidi ya miaka 20.
Washtakiwa watatu wakuu wanatoka katika familia moja. Walikuw ani wafanyakazi za kibarua - kama madereva wa teksi, kwenye kiwanda na kwenye teneo la ujenzi. Mdogo kati ya wanne, hao ni Muhammadsobir Faizov mwenye umri wa miaka 20, alifanya kazi kama kinyozi katika mkoa wa Ivanovo, akituma pesa kwa familia yake huko Tajikistan.
Vyanzo vya jeshi katika kesi hiyo vinasema kwamba kaka yake mkubwa alikuwa mpatanishi kati ya wahalifu na waandaaji, lakini hayuko kizimbani - anatafutwa, wakili wa waathiriwa anaamini kuwa mshukiwa huyo Faizov Sr. amejificha Uturuki.
Watu wengine wapatao 24, ambao vyombo vya kisheria vinawaita washirika, walihusika katika kesi hiyo. Baadhi yao bado wanatafutwa, na wengine kadhaa wamekamatwa nje ya nchi.
Unaweza pia kusoma:
Msichana wa miaka miwili apatikana kwenye sanduku la mwanamke New Zealand

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi nchini New Zealand wamemkamata mwanamke mmoja baada ya msichana wa miaka miwili kupatikana akiwa hai ndani ya sanduku lake.
Kisa hicho kilitokea kaskazini mwa New Zealand siku ya Jumapili wakati basi lililokuwa likisafiri kutoka Whangarei kwenda Auckland liliposimama kwenye kituo cha basi katika mji mdogo.
Polisi walisema dereva wa basi alimtilia shaka mwanamke huyo alipoomba kupata eneo la kuhifadhia mzigo wake chini ya basi wakati wa mapumziko wakati wa safari.
"Dereva aliingiwa na wasiwasi alipoona begi la mwanamke likisogea. Alipofungua sanduku hilo, alimuona msichana wa miaka miwili ndani," polisi wa New Zealand walisema katika taarifa.
Kulingana na mamlaka, msichana huyo alikuwa amevaa nepi pekee na alikuwa amejifungiwa ndani ya sanduku kwa takriban saa moja.
Bado haijulikani iwapo kuna uhusiano wowote kati ya msichana huyo na mwanamke aliyemfungia kwenye sandugu. Mshtakiwa atafikishwa katika mahakama ya eneo hilo siku ya Jumatatu.
Kwa mujibu wa polisi, "Mwili wa msichana huyo ulikuwa wa joto sana lakini hakuwa amejeruhiwa kimwili."
Polisi wanasema baada ya tukio hilo, msichana huyo alipelekwa hospitalini ambako alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.
"Tungependa kumpongeza dereva wa basi, ambaye aliona kuna kitu kibaya na kuchukua hatua mara moja, vinginevyo matokeo yangekuwa mabaya zaidi," polisi.
Unaweza pia kusoma:
Iran na Pakistan zatia saini mikataba 12

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kutoka kulia, Waziri Mkuu wa Pakistani Shahbaz Sharif na Rais wa Iran Massoud Pezhikian Katika ziara ya Rais wa Iran Masoud Pezzeghian mjini Islamabad, Iran na Pakistan zimetia saini hati na makubaliano 12 ya ushirikiano.
Mikataba hii inahusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kisayansi na kiufundi, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya matumizi ya pamoja ya lango la mpaka la Mirjava (Taftan).
Baada ya kukutana na Shahbaz Sharif, Bw. Pezhikian aliita Pakistan "nyumba yake ya pili" katika mkutano na waandishi wa habari na kwa mara nyingine tena aliishukuru Iran kwa msaada wake wakati wa vita vya siku 12 na Israel.
Wakati wa safari yake kutoka Tehran hadi Pakistan, Bw. Pezzekiyan pia aliishukuru Pakistan kwa msaada wake kwa Iran wakati wa mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran.
Waziri Mkuu wa Pakistani Shahbaz Sharif pia ameishukuru Iran kwa juhudi zake za kuhakikisha haki za watu wa Gaza zinaheshimiwa na kusema: "Watu wa Pakistan sawa na watu wa Iran wanatetea haki za watu wa Gaza."
Unaweza pia kusoma:
Mkulima Mzungu anayetuhumiwa kuwalisha nguruwe miili ya wanawake wawili kufika mahakamani

Maelezo ya picha, Mauaji ya wanawake wawili weusi yaliyofanywa na mkulima na wafanyakazi wake wawili yalizua ghadhabu nchini Afrika Kusini Mkulima mzungu wa Afrika Kusini na wafanyakazi wake wawili wanaotuhumiwa kuwapiga risasi wanawake wawili weusi na kuwalisha nguruwe miili yao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mauaji yao.
Maria Makgato, 45, na Lucia Ndlovu, 34, inadaiwa walikuwa wanatafuta chakula katika shamba hilo karibu na Polokwane katika jimbo la Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini mwaka jana walipouawa.
Miili yao inaelezwa walipewa nguruwe katika jaribio dhahiri la kuondoa ushahidi.
Mmiliki wa shamba Zachariah Johannes Olivier, 60, na wafanyikazi wake Adrian de Wet, 19, na William Musora, 50, bado hawajawasilisha ombi la dhamana na wanasalia gerezani.
Kesi hiyo imezua ghadhabu kote Afrika Kusini, na hivyo kuzidisha mivutano ya rangi nchini humo.
Mvutano huo umeenea hasa katika maeneo ya vijijini, licha ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Wanaume hao watatu pia wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua kwa kumpiga risasi mume wa Bi Ndlovu, ambaye alikuwa na wanawake hao katika shamba hilo - pamoja na kumiliki bunduki isiyo na kibali.
Bw Musora, raia wa Zimbabwe, anakabiliwa na mashtaka ya ziada chini ya Sheria ya Uhamiaji ya Afrika Kusini kuhusu hadhi yake kama mhamiaji haramu.
Trump athibitisha mjumbe wa Marekani Witkoff kuzuru Urusi wiki ijayo

Chanzo cha picha, AFP
Donald Trump amethibitisha Jumapili kuwa mjumbe wake maalum Steve Witkoff atazuru Urusi katika wiki ijayo, kabla ya muda wa mwisho ambao rais wa Marekani ameuweka wa kuiwekea vikwazo vipya kwa Moscow.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump pia alisema nyambizi mbili za nyuklia alizoziweka kufuatia mzozo wa mtandaoni na rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev sasa "ziko katika eneo hilo."
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Trump hajasema kama alimaanisha nyambizi zinazotumia nguvu za nyuklia au za nyuklia. Pia hakueleza kwa kina kuhusu maeneo halisi zilikotumwa, ambayo yanafichwa na jeshi la Marekani.
Ziara hiyo inakuja huku muda uliowekwa na Trump mwishoni mwa wiki ijayo kwa Urusi kuchukua hatua za kumaliza vita vya Ukraine la sivyo itakabiliwa na vikwazo vipya.
Kiongozi huyo wa Republican alisema Witkoff atazuru "nadhani wiki ijayo, Jumatano au Alhamisi."
Rais wa Urusi Vladimir Putin tayari amekutana na Witkoff mara kadhaa huko Moscow, kabla ya juhudi za Trump za kurekebisha uhusiano na Ikulu ya Kremlin kukwama.
Trump hapo awali alitishia kwamba hatua mpya zinaweza kumaanisha "ushuru wa pili" unaolenga washirika waliobaki wa biashara wa Urusi, kama vile China na India. Hilo litaumiza zaidi Urusi, lakini litaleta usumbufu mkubwa kimataifa.
Licha ya shinikizo kutoka Washington, Urusi imeendelea na mashambulizi yake dhidi ya jirani yake inayoungwa mkono Magharibi.
Pia unaweza kusoma:
Mamia ya maafisa wa zamani wa Israel wamtaka Trump kumshinikiza Netanyahu kumaliza vita

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamia ya maafisa wa usalama wa Israel waliostaafu wakiwemo wakuu wa zamani wa mashirika ya kijasusi wamemtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuishinikiza serikali yao kukomesha vita huko Gaza.
"Ni uamuzi wetu wa kitaalamu kwamba Hamas haileti tishio tena la kimkakati kwa Israel," maafisa hao wa zamani waliandika katika barua ya wazi iliyosambazwa na vyombo vya habari siku ya Jumatatu.
"Mwanzoni vita hivi vilikuwa vita vya haki, vita vya kujihami, lakini tulipofikia malengo yote ya kijeshi, vita hivi vilikoma kuwa vita vya haki," anasema Ami Ayalon, mkurugenzi wa zamani wa shirika la ujasusi wa ndani Shin Bet.
Vita hivyo vinavyokaribia mwezi wa 23, "vinapelekea Taifa la Israel kupoteza usalama na utambulisho wake," Ayalon alionya katika video iliyotolewa kuandamana na barua hiyo.
Barua hiyo ikiwa imetiwa saini na watu 550, wakiwemo wakuu wa zamani wa Shin Bet na shirika la kijasusi la Mossad, inamtaka Trump "kumuelekeza" Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusitisha mapigano.
Israel ilianzisha operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza kujibu shambulio baya la Oktoba 7, 2023 lililofanywa na kundi la Hamas la Palestina. Katika wiki za hivi karibuni, Israel imekuwa chini ya shinikizo la kimataifa la kukubali kusitishwa kwa mapigano ambayo huenda mateka wa Israel walioachiliwa kutoka Gaza na mashirika ya Umoja wa Mataifa kusambaza misaada ya kibinadamu.
Lakini baadhi ya Israel, wakiwemo mawaziri katika serikali ya muungano ya Netanyahu, badala yake wanashinikiza majeshi ya Israel kusukuma mbele vita na Gaza kukaliwa kwa mabavu yote au kwa sehemu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, barua hiyo ilitiwa saini na wakuu watatu wa zamani wa Mossad: Tamir Pardo, Efraim Halevy na Danny Yatom. Wengine waliotia saini ni pamoja na wakuu watano wa zamani wa Shin Bet -- Αyalon pamoja na Nadav Argaman, Yoram Cohen, Yaakov Peri na Carmi Gilon -- na wakuu watatu wa zamani wa jeshi, akiwemo waziri mkuu wa zamani Ehud Barak, waziri wa zamani wa ulinzi Moshe Yaalon na Dan Halutz.
Barua hiyo inasema jeshi la Israel "limetimiza kwa muda mrefu malengo mawili ambayo yanaweza kufikiwa kwa nguvu: kuisambaratisha miundo ya kijeshi ya Hamas na utawala. Lakini, la tatu, na muhimu zaidi, linaweza kupatikana tu kupitia makubaliano: kuwaleta mateka wote nyumbani," iliongeza.
"Kuwafukuza wapiganaji wakuu waliosalia wa Hamas kunaweza kufanywa baadaye," barua hiyo ilisema. Katika barua hiyo, maafisa hao wa zamani wanamwambia Trump kwamba anaaminika na Waisraeli walio wengi na anaweza kuweka shinikizo kwa Netanyahu kumaliza vita na kuwarudisha mateka.
Baada ya kusitishwa kwa mapigano, waliotia saini wanasema, Trump anaweza kuutaka muungano wa kikanda kuunga mkono Mamlaka ya Palestina iliyofanyiwa mageuzi kuchukua mamlaka ya Gaza kama njia mbadala ya utawala wa Hamas.
Wanafunzi kutoka China huambiwa wawapeleleze wenzao Uingereza - ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanafunzi kutoka China katika vyuo vikuu vya Uingereza wanashinikizwa kuwapeleleza wanafunzi wenzao ili kujaribu kuzuia mjadala wa masuala ambayo ni nyeti kwa serikali ya China, ripoti mpya inafichua.
Taasisi ya fikra tunduizi ya UK-China Transparency (UKCT) inasema uchunguzi wake pia uliangazia ripoti za maafisa wa serikali ya China kuwaonya wahadhiri kuepuka kujadili mada fulani katika madarasa yao.
Inakuja siku chache baada ya sheria mpya kuanza kutekelezwa ya kuweka wajibu zaidi kwa vyuo vikuu kudumisha uhuru wa kitaaluma na uhuru wa kujieleza.
Ubalozi wa China mjini London uliita ripoti hiyo "isiyo na msingi na ya kipuuzi", na kuongeza kuwa China inaheshimu uhuru wa kujieleza nchini Uingereza na kwingineko.
Mdhibiti, Ofisi ya Wanafunzi (OfS), anasema uhuru wa kujieleza na uhuru wa kitaaluma ni "msingi" kwa elimu ya juu.
Sheria mpya, iliyoanza kutumika wiki iliyopita, inasema vyuo vikuu vinapaswa kufanya zaidi ili kukuza uhuru wa kitaaluma na uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na katika kesi ambapo taasisi zina makubaliano na nchi nyingine.
Vyuo vikuu vinaweza kutozwa faini ya mamilioni ikiwa vitashindwa kufanya hivyo, OfS imesema.
Hata hivyo, ripoti ya UKCT inasema baadhi ya vyuo vikuu vinasita kushughulikia suala la kuingiliwa na China kwa sababu ya kutegemea kwao fedha za ada za wanafunzi wa China.
Ripoti hiyo inadai kuwa baadhi ya wasomi wa China waliohusika katika tafiti nyeti wamenyimwa viza na serikali ya China, huku wengine wakisema wanafamilia waliorudi China walinyanyaswa au kutishiwa kwa sababu ya kazi zao nchini Uingereza.
Mada hizo nyeti zinaweza kuanzia sayansi na teknolojia hadi siasa na ubinadamu, ripoti hiyo inasema, kama vile ripoti hiyo inasema mfano wa mada hizo ni kama dhulma katika mkoa wa Xinjiang wa China, kuzuka kwa Covid au kuongezeka kwa kampuni za teknolojia za China.
Baadhi ya wanafunzi waliripoti vitisho kutoka kwa wanafunzi wengine au maafisa wengine wa China, na vile vile kutoka kwa wafanyakazi katika Taasisi za Confucius.
Hizi ni taasisi za ubia zinazofanya kazi katika vyuo vikuu kadhaa vya Uingereza, ili kuzileta pamoja taasisi za Uingereza na China, pamoja na wakala wa serikali ya China ambao hutoa ufadhili.
Hufundisha utamaduni na lugha ya Kichina kwenye vyuo vikuu vya Uingereza, lakini wamekosolewa kwa madai ya uhusiano na Chama cha Kikomunisti cha China.
Wachimba madini wapatikana wamekufa baada ya saa 70 za kunasa

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mtu ameshikilia picha ya Jean Miranda Ibaceta, mchimba madini aliyekufa Wafanyakazi wote watano katika mgodi wa shaba wa El Teniente nchini Chile ambao walikuwa wamenasa katika ajali ya kuporomoka kwa udongo wiki iliyopita wamepatikana wakiwa wamekufa, imesema kampuni ya serikali ya uchimbaji shaba ya Codelco siku ya Jumapili, huku ikiahidi uchunguzi na kuboresha usalama.
Idadi ya waliofariki imefikia sita, ikiwa ni pamoja na mtu mmoja aliyefariki wakati ajali hiyo ilipotokea Alhamisi jioni, saa 70 kabla ya mfanyakazi wa mwisho aliyenaswa kupatikana.
Kuporomoka huko kulichochewa na mojawapo ya tetemeko kubwa la ardhi kuwahi kurekodiwa huko El Teniente, la kipimo cha 4.2.
Rais Gabriel Boric alitoa wito wa siku tatu za maombolezo kwa wachimba migodi hao. Wanaume walionaswa walikuwa na umri wa miaka 29 hadi 34 na walikuwa wameajiriwa na kampuni ya uchimbaji ya Gardilcic, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Kampuni ya Codelco ndiye mchimbaji mkuu zaidi wa madini ya shaba duniani na Chile ndio mzalishaji mkubwa zaidi duniani ambayo hutoa takriban robo ya shaba inayotumika katika viwanda kuanzia ujenzi hadi vifaa vya elektroniki.
Juhudi za uokoaji zilianza kwa kasi Ijumaa jioni, mara tu tetemeko la Alhamisi ilipopungua.
Codelco iligundua mfanyakazi wa kwanza aliyenaswa siku ya Jumamosi na wengine wanne waliosalia siku ya Jumapili, chini ya timu ya uokoaji ya watu wapatao 100.
Waziri wa Madini, Aurora Williams alisema Wizara ya Kazi na mdhibiti wa madini Sernageomin watafanya tathmini itakapokuwa salama kwa shughuli kuanza tena El Teniente, mgodi wa Codelco mwaka jana ulizalisha tani 356,000 za shaba.
Pia unaweza kusoma:
Korea Kusini yaondoa vipaza sauti vya propaganda dhidi ya Korea Kaskazini kwenye mpaka

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Korea Kusini wakiondoa kipaza sauti ambacho kimeundwa kwa ajili ya matangazo ya propaganda katika mpaka na Korea Kaskazini Serikali ya Korea Kusini imeanza kuondoa vipaza sauti Jumatatu vilivyokuwa vikirusha matangazo ya kuipinga Korea Kaskazini kwenye mpaka na nchi hiyo, imesema wizara ya ulinzi ya Seoul, huku serikali mpya ya Rais Lee Jae Myung ikijaribu kupunguza mvutano kati yake na Pyongyang.
Muda mfupi baada ya kuchukua madaraka mwezi Juni, utawala wa Lee ulizima matangazo ya propaganda ya kukosoa utawala wa Korea Kaskazini huku ukitarajia kufufua mazungumzo yaliyokwama na jirani yake.
Lakini hivi karibuni Korea Kaskazini ilipinga hatua za mapatano na kusema haina nia ya kuzungumza na Korea Kusini.
Nchi hizo zimesalia katika vita baridi baada ya vita vya Korea vya 1950-53 kumalizika kwa suluhu na uhusiano umezorota katika miaka michache iliyopita.
Hatua ya Korea Kusini ya kuondoa vipaza sauti kuanzia Jumatatu ni "hatua ya kivitendo ya kusaidia kupunguza mvutano kati ya Kusini na Kaskazini," wizara hiyo ilisema katika taarifa yake Jumatatu.
Pia unaweza kusoma:
Viongozi wa Magharibi walaani video za mateka waliodhoofika huko Gaza

Chanzo cha picha, HAMAS
Maelezo ya picha, Mateka wa Israel Evyatar David akiwa amezuiliwa kwenye handaki huko Gaza Viongozi wa nchi za Magharibi wamelaani video za mateka wa Israel waliodhoofika zilizotolewa na watekaji wao huko Gaza, huku Shirika la Msalaba Mwekundu likitoa wito wa kutaka kuonana na wateka wote waliosalia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy alisema "picha za mateka zilizotolewa kwa ajili ya propaganda ni za kuudhi" na lazima waachiliwe "bila masharti."
Wito huo unakuja baada ya Kundi la Kiislamu ya Kijihadi la Palestina kuchapisha video ya Rom Braslavski, akiwa amekonda na akilia, siku ya Alhamisi, na Hamas kutoa video ya Evyatar David aliyedhoofika siku ya Jumamosi.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema "amechukizwa" na picha hizo, na kuongeza kuwa kuachiliwa kwa mateka wote ni jambo la lazima ili kupata usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema Ufaransa inaendelea kufanya kazi bila kuchoka ili kuachiliwa kwa mateka, kurejesha usitishaji mapigano, na kuwezesha misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.
Viongozi wa Israel wanaishhutumu Hamas kwa kuwaweka mateka na njaa.
Kundi la wapiganaji la Hamas limekanusha kuwaweka mateka na njaa makusudi, na kusema mateka wanakula kile ambacho wapiganaji hao na watu wengine wanchokula wakati wa mzozo wa njaa huko Gaza.
Wote Braslavski, 21, na David, 24, walichukuliwa mateka kutoka tamasha la muziki la Nova tarehe 7 Oktoba 2023 wakati wa shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel.
Ni miongoni mwa mateka 49, kati ya 251 waliotekwa awali, ambao Israel inasema bado wanazuiliwa huko Gaza. Idadi hiyo ni pamoja na mateka 27 ambao wanaaminika kuwa wamekufa.
Baada ya video hizo kutolewa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alizungumza na familia mbili za mateka, akielezea "mshtuko mkubwa" na kuwaambia juhudi za kuwarudisha mateka wote "zitaendelea daima na bila kuchoka."
Siku ya Jumapili, Netanyahu alizungumza na mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo hilo, akiomba kuhusika kwao mara moja katika kutoa chakula na matibabu kwa mateka.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema "imeshtushwa" na video ambazo zinatoa "ushahidi wa hali ya kutishia maisha ambayo mateka wanakumbana nayo."
Shirika hilo la kutoa misaada limerudia wito wake wa kupewa nafasi ya kuwaona mateka ili kutathmini hali zao, kuwapa usaidizi wa kimatibabu na kuwezesha mawasiliano na familia zao.
Kikosi cha Hamas cha Al-Qassam Brigedi kimesema kitajibu vyema ombi lolote la Msalaba Mwekundu la kupeleka chakula na dawa kwa wafungwa ikiwa njia za kupeleka misaada ya kibinadamu zitafunguliwa Gaza mara kwa mara na kudumu, na mashambulizi ya anga yatasitishwa wakati wa kupokea msaada.
Pia kumekuwa na ukosoaji kutoka kwa Wapalestina, kwani shirika hilo halijaruhusiwa kuwatembelea wafungwa wa Kipalestina wanaozuiliwa katika jela za Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023.
Kwa upande mwingine, ripoti kutoka Gaza zinasema Wapalestina waliokuwa wakitafuta chakula karibu na maeneo ya usambazaji walishambuliwa na wanajeshi wa Israel katika maeneo mawili tofauti siku ya Jumapili. Takriban Wapalestina 27 waliuawa, hospitali za Gaza zinasema.
Pia unaweza kusoma:
Zaidi ya wahamiaji 60 kutoka Afrika wafariki baada ya boti kupinduka

Chanzo cha picha, AFP
Zaidi ya wahamiaji 60 wamefariki dunia baada ya boti iliyokuwa imebeba takriban watu 150 kuzama katika pwani ya Yemen kufuatia hali mbaya ya hewa siku ya Jumapili.
Chombo hicho kilizama katika jimbo la kusini mwa Yemen la Abyan, na miili 68 imepatikana, mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Yemen (IOM) aliiambia BBC.
Alisema watu 12 wameokolewa na makumi ya wengine bado hawajapatikana.
Wengi wa waathiiriwa wanaaminika kuwa raia wa Ethiopia, ilisema IOM, ambayo imelitaja tukio hilo kuwa la kuhuzunisha.
Yemen inasalia kuwa njia kuu ya wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika wanaosafiri kwenda mataifa ya Ghuba ya Kiarabu kutafuta kazi, huku IOM ikikadiria kuwa mamia wamekufa au kupotea katika ajali kam hizo katika miezi ya hivi karibuni.
Mkuu wa IOM Yemen Abdusattor Esoev amesema boti hiyo ilikuwa imebeba wahamiaji karibu 157.
Yemen ni nchi maarufu ambapo wahamiaji wengi waliokata tamaa wanaoelekea kaskazini mwa Saudi Arabia hupita ili kwenda kutafuta fursa bora zaidi za maisha.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu
Nikukaribishe katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumatatu ya tarehe 4 Agosti, 2025
