Akina mama wanaoomboleza walalama dhidi ya wasafirishaji haramu wa wahamiaji

Senait Mebrehtu alimpoteza bintiye kwenye Ziwa Turkana mwaka jana
Maelezo ya picha, Senait Mebrehtu alimpoteza bintiye kwenye Ziwa Turkana mwaka jana
    • Author, Ashley Lime & Netsanet Debessai
    • Nafasi, BBC News & BBC Tigrinya, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati jua linapozama katika ufuo wa Ziwa Turkana, mama mmoja aliyejawa na simanzi aliketi kandokando ya ziwa hilo, akilia kwa uchungu huku akirusha maua ndani ya maji hayo yaliyobadilika rangi kutokana na magugu.

Kisa? anaomboleza kifo cha binti yake wa miaka 14, aliyekufa maji alipokuwa akijaribu kufika Kenya kupitia njia mpya inayotumiwa na wasafirishaji haramu wa watu.

Senait Mebrehtu, Mkristo wa Kipentekoste kutoka Eritrea, ambaye alikuwa ameomba hifadhi nchini Kenya miaka mitatu iliyopita, alizuru kaskazini-magharibi mwa Kenya kupaona eneo ambalo maisha ya binti yake wa miaka 14 Hiyab yalikoishia mwaka jana.

Hiyab alikuwa akisafiri na dada yake wakati walipovuka ziwa hilo kubwa usiku wa manane safari hatari iliyochochewa na upepo mkali na mashua hafifu.

Dada yake alinusurika, lakini Hiyab hakufika mwisho wa safari.

"Kama wasafirishaji wangeniambia kuwa kuna ziwa kubwa na la hatari kama hili hapa Kenya, nisingewaruhusu mabinti zangu kufika huku," alisema Bi Senait kwa huzuni, alipokuwa ameketi katika ufukwe wa magharibi wa ziwa hilo.

Bi Senait alifika mji mkuu wa Nairobi, Kenya kwa ndege akiwa na watoto wake wawili wa umri mdogo kwa kutumia visa ya utalii, akikimbia mateso ya kidini.

Awali, hakuweza kusafiri na mabinti zake wawili wakubwa kwa sababu walikuwa karibu na umri wa kuandikishwa jeshini jukumu ambalo kwa kawaida huchukua muda mrefu na mara nyingi huambatana na ajira ya lazima.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Eritrea ni taifa lenye utawala wa chama kimoja, lenye mfumo wa kijeshi uliokithiri.

Vijana wengi hujikuta wakitumikishwa kwa miaka mingi katika huduma ya taifa, hali inayowasukuma wengi kutoroka.

Mabinti zake walimlilia mama yao kujiunga naye nchini Kenya.

Kwa msaada wa jamaa, walikubaliana kuwalipia wasafirishaji haramu waliowatoa Eritrea na kuwapeleka kwa njia ya hatari ilimradi wafike Kenya.

Maisha ya mabinti hao wawili yalikabidhiwa wasafirishaji hao haramu ambao waliwapitisha kwa njia iliyochukua wiki kadhaa kwa gari na kwa miguu kutoka Eritrea, wakapitia kaskazini mwa Ethiopia, kisha kusafirishwa hadi ukanda wa kaskazini-mashariki mwa Kenya kwenye fukwe za Ziwa Turkana, ziwa kubwa zaidi duniani lenye maji ya kudumu lililo katika eneo la jangwa.

Msafirishaji mmoja wa kike nchini Kenya alithibitisha kwa BBC kuwa Ziwa Turkana sasa linazidi kutumika na wahamiaji kama njia ya kuvukia kuingia Kenya bila vibali.

"Tunaiita 'njia ya kidijitali' kwa sababu ni mpya sana," alisema msafirishaji huyo wa watu.

Msafirishaji huyo, ambaye hupata takriban dola 1,500 kwa kila mhamiaji anayemuingiza au kumpitisha Kenya kiasi ambacho ni mara nne ya mshahara wa kawaida wa mfanyakazi wa kawaida nchini humo alizungumza na waandishi wa BBC katika eneo la siri, kwa masharti ya kutotajwa jina.

Kwa zaidi ya miaka 15, amekuwa sehemu ya kikosi kikubwa cha usafirishaji haramu wa binadamu unaofanya kazi katika Kenya, Uganda, Rwanda, na Afrika Kusini.

Pia unaweza kusoma:

Wahamiaji wanaosafirishwa ni hasa wale wanaotoroka kutoka Eritrea, Ethiopia, na Somalia.

Kutokana na Kenya kuimarisha doria kwenye barabara zake, wasafirishaji sasa wanategemea njia ya Ziwa Turkana kuingiza wahamiaji nchini humo.

Kulingana naye, maajenti walioko katika kijiji cha wavuvi cha Lomekwi huwapokea wahamiaji na kupanga usafiri wa barabarani kuwapeleka Nairobi safari ya saa 15.

Akiwaonya wazazi kuhusu hatari za mashua dhaifu zinazotumika kuvusha watu, alisisitiza kuwa watoto hawapaswi kuruhusiwa kuvuka peke yao.

"Siwezi kusema napenda pesa ninazopata kwa sababu kama mama, siwezi kufurahia ninapoona maafa yanayowakumba watoto wa wanawake wengine," aliiambia BBC.

"Ningependa kuwashauri wahamiaji, iwapo watanisikia. Ningependa kuwaomba wabaki katika nchi zao," aliongeza, akitoa onyo kuhusu ukatili na ujeuri wa baadhi ya wasafirishaji haramu.

Ziwa Turkana ni ziwa kubwa zaidi la jangwa la kudumu duniani
Maelezo ya picha, Ziwa Turkana ni ziwa kubwa zaidi la jangwa la kudumu duniani

Osman, mhamiaji wa Eritrea ambaye hakutaka kutaja jina lake halisi kwa sababu za kiusalama, alivuka kwa wakati mmoja na Hiyab na dada yake.

Alikumbuka jinsi mashua ya Hiyab ilivyopinduka mbele ya macho yake muda mfupi baada ya kuondoka katika kijiji cha wavuvi cha Ileret kusini-magharibi kuelekea Lomekwi.

"Hiyab alikuwa kwenye mashua mbele yetu injini ya mashua aliyoabiri haikuwa ikifanya kazi na ilikuwa ikisukumwa na upepo mkali," alisema.

"Walikuwa takriban mita 300 [futi 984] ndani ya maji wakati boti yao ilipopinduka, na kusababisha vifo vya watu saba."

Dadake Hiyab alinusurika kwa kung'ang'ania boti iliyokuwa ikizama hadi chombo kingine ambacho pia kilikuwa kikiendeshwa na wasafirishaji haramu kikaja kuwaokoa.

Bi Senait aliwalaumu wasafirishaji haramu kwa vifo hivyo akisema walijaza zaidi ya wahamiaji 20 kwenye boti hiyo.

"Sababu ya vifo ilikuwa uzembe wa kawaida. Waliweka watu wengi kwenye mashua ndogo ambayo haikuweza hata kubeba watu watano," alisema.

Wakati wa ziara ya BBC mjini Lomewki, wavuvi wawili walisema waliona miili ya wahamiaji wanaoaminika kuwa Waeritrea ikielea katika ziwa hilo, ambalo lina urefu wa kilomita 300 (maili 186) na upana wa 50, mnamo Julai 2024.

"Kulikuwa na takriban miili minne kwenye ufuo. Kisha, siku chache baadaye miili mingine ilionekana," Brighton Lokaala alisema.

Mvuvi mwingine, Joseph Lomuria, alisema aliona miili ya wanaume wawili na wanawake wawili - mmoja wao akionekana kuwa kijana.

Mnamo Juni 2024, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, lilirekodi wakimbizi 345,000 wa Eritrea na wanaotafuta hifadhi katika Afrika Mashariki, kati ya 580,000 duniani kote.

Kama familia ya Bi Senait, wengi hutoroka ili kukwepa kujiandikisha kijeshi katika nchi ambayo imekumbwa na vita vingi katika eneo hilo, na ambapo shughuli huria za kisiasa na kidini hazikubaliwi huku serikali ikijaribu kushikilia mamlaka.

Wakili wa Eritrea mwenye makao yake nchini Uganda, Mula Berhan, aliiambia BBC kuwa Kenya na Uganda zinazidi kuwa mahali pazuri pa wahamiaji hao kwa sababu ya vita vya Ethiopia na Sudan, ambazo zote ni jirani na Eritrea.

Ramani inayoonyesha njia ambayo baadhi ya Waeritrea wanapitia sasa kusafiri hadi Kenya na Uganda
Maelezo ya picha, Ramani inayoonyesha njia ambayo baadhi ya Waeritrea wanapitia sasa kusafiri hadi Kenya na Uganda

Mlanguzi huyo wa kike alisema kwa uzoefu wake baadhi ya wahamiaji hao waliishi Kenya, lakini wengine walitumia kama nchi ya kupita kuelekea Uganda, Rwanda na Afrika Kusini, wakiamini ni rahisi kupata hadhi ya ukimbizi huko.

Mtandao wa magendo unafanya kazi katika nchi hizi zote, ukiwakabidhi wahamiaji kwa "mawakala" tofauti hadi wafike mahali pa mwisho, ambayo wakati mwingine inaweza pia kuwa Ulaya au Amerika Kaskazini.

Kazi yake ni kuwakabidhi wahamiaji hao ambao wako kwenye usafiri wa Nairobi kwa mawakala wanaowaweka katika "nyumba za muda" hadi sehemu inayofuata ya safari yao itakapopangwa na kulipiwa.

Kufikia hatua hii kila mhamiaji pengine amelipa karibu dola $5,000 kwa safari hadi kufikia hapo.

BBC iliona chumba katika jengo la ghorofa ambalo lilikuwa likitumika kama nyumba ya muda ya kuishi.

Wanaume watano wa Eritrea walikuwa wamefungiwa ndani ya chumba hicho, ambacho kilikuwa na godoro moja.

Katika nyumba hizo, wahamiaji wanatarajiwa kulipa kodi na pia kulipia chakula chao na mfanyabiashara huyo alisema anafahamu wanaume watatu na mwanamke kijana ambao walikufa kwa njaa kwani walikuwa wamekosa pesa.

Alisema maajenti hao walitupa miili hiyo na kutaja vifo vyao kuwa ni bahati mbaya.

"Wasafirishaji haramu wanaendelea kudanganya familia wakisema watu wao wako hai, na wanaendelea kutuma pesa," alikiri.

Wanawake wahamiaji, alisema, mara nyingi walinyanyaswa kingono au kulazimishwa kuolewa na wasafirishaji wa wanaume.

Alisema yeye mwenyewe hakuwa na nia ya kuacha biashara hiyo yenye faida kubwa lakini alihisi wengine wanapaswa kufahamu kile kinachoweza kuwa mbele yao.

Ni faraja kidogo kwa Bi Senait, ambaye angali anaomboleza kifo cha mtoto wake wa miaka 14 huku akieleza kufarijika kwamba binti yake mkubwa alinusurika na hakudhuriwa na wasafirishaji haramu.

"Tumepitia yale ambayo kila familia ya Eritrea inapitia," alisema.

"Mungu aiponye nchi yetu na atukomboe na haya yote."

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid