Mzozo wa Sudan: Wanawake waiambia BBC visa vya kutisha vya ubakaji walivyopitia

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Kolthom alipokuwa akibakwa na wapiganaji wanne wa kijeshi katika eneo lililokumbwa na vita nchini Sudan la Darfur, pia alikuwa akinyanyaswa kutokana na rangi yake.
Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kufadhaishwa nayo.
"Walikuwa wanyama sana. Walinibaka kwa zamu chini ya mti ambapo nilikuwa nimeenda kukusanya kuni ili [kuwasha moto] kupata joto," alisema kwa sauti ya kutetemeka, ya chini kweli kupitia simu.
Tumebadilisha jina lake na la mtu mwingine aliyenusurika kubakwa aliyenukuliwa katika makala haya.
Kolthoum, ambaye yuko katika umri wa miaka 40, anatoka katika jamii ya Waafrika Weusi Wamasalit wa Darfur, wakati waliombaka walikuwa Waarabu kutoka Rapid Support Forces (RSF).
Kundi hili linashutumiwa kutekeleza maovu mengi katika mzozo ambao umezidi kuchukua sura ya kikabila huko Darfur.
Kolthoum aliishi El Geneina - kihistoria ikimaanisha ishara ya nguvu ya Waafrika weusi huko Darfur, na mji mkuu wa jadi wa ufalme wa Masalit.
Sasa ametoroka na mume wake mgonjwa na watoto.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kolthoum anasema wabakaji walimwambia aondoke katika jiji hilo kwa vile ni "mali ya Waarabu", na hivyo kuchochea hofu ya Waafrika wengi weusi kwamba RSF pamoja na wanamgambo washirika wanaojulikana kama Janjaweed, wanataka kubadilisha eneo hilo lenye mchanganyiko wa kikabila kuwa linalotawaliwa na Mwarabu.
Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katikati ya mwezi wa Aprili, baada ya majenerali wake wawili wenye nguvu, mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama "Hemedti" kutofautiana.
Ugomvi wao umezusha mzozo wa Darfur, ambao ulizuka kwa mara ya kwanza mwaka 2003, na kusababisha vifo vya takribani watu 300,000 katika eneo hilo.
Mzozo wa hivi karibuni umewalazimu zaidi ya watu 160,000, wengi wao kutoka jamii ya Massalit kukimbilia Chad.
Haijabainika ni watu wangapi wameuawa katika eneo hilo, huku makadirio ya chini kabisa ya vifo vya El Geneina ikifikia 5,000.
Wapiganaji wa RSF pia wameshutumiwa kwa kufanya ukatili katika jimbo lenye watu wengi zaidi nchini Sudan katika mji mkuu Khartoum.
Wanajeshi hao wanadhibiti sehemu kubwa ya jimbo hilo, huku jeshi likishindwa kuwarudisha nyuma.
Mapigano hayo yamesababisha kuhama kwa karibu watu milioni mbili tangu katikati ya Aprili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mjini Khartoum, ghasia hazijachukua mwelekeo wa rangi au kabila.
Waarabu na watu wa makabila mengine ni waathirika wa vita vinavyoendelea.
Ibtissam, 24, aliiambia BBC kwamba alikuwa njiani kumtembelea shangazi yake wakati wanajeshi watatu wa RSF walipomzuia.
"Walitoa bunduki zao na kuniuliza ninakwenda wapi. Nilipowaambia kuwa ninakwenda kwa shangazi yangu walinituhumu kuwa niko katika idara ya upelelezi ya jeshi," aliniambia huku sauti yake ikiwa inakatakata.
Kisha wanajeshi hao walimlazimisha kuandamana nao kwenye gari lao na kumpeleka katika nyumba iliyokuwa karibu.
"Nilimuona mwanaume mwingine ndani ya nyumba hiyo, akiwa amevuliwa nguo zake za ndani. Nilijaribu kukimbia. Lakini mwanajeshi mmoja alinipiga kofi, nikaanguka chini. Walitishia kuniua ikiwa ningesogea au kupiga kelele tena," alisema kwa njia ya simu huku akilia.
"Watatu hao walinibaka kwa zamu zaidi ya mara moja. Kisha wakanirudisha ndani ya gari lao na kunitupa kando ya barabara jua likiwa linazama," alisema.
Baada ya kunyamaza kwa muda mfupi, Ibtissam alielezea jinsi alivyohisi "kufedheheshwa na kukasirika".
"Nilitaka kujiua. Lakini nilijizuia. Nilirudi nyumbani na sikumwambia mtu yeyote kilichotokea."
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan ilisema mwanzoni mwa mwezi Julai kuwa imepokea ripoti za matukio 21 ya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana wasiopungua 57.
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk alibainisha kuwa "RSF imetambuliwa kama wahalifu" katika takriban kesi zote zilizoripotiwa ofisini mwake.
Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binadamu ya maeneo yanaamini kwamba idadi hii ni sehemu tu inayoonesha ukubwa halisi wa uhalifu huo.
Mwanaharakati wa haki za binadamu wa Sudan Ahlam Nasser alisema hana shaka kwamba ubakaji ulikuwa unatumiwa "kiutaratibu" kama silaha ya vita kuwatisha watu.
"[Ubakaji] umetumika huko Darfur hapo awali na unatumika katika vita hivi vya sasa vya Khartoum, hasa na wanajeshi wa RSF," alisema.
Mwanaharakati huyo sasa ametoroka nchi.
Alisema pia amesikia simulizi za kutisha kutoka kwa baadhi ya wanawake huko Khartoum.
"Katika visa vingine, akina mama walibakwa mbele ya watoto wao," Bi Nasser alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata hivyo, RSF imekanusha wapiganaji wake kuwa nyuma ya mashambulizi haya.
Katika rekodi ya sauti iliyotumwa kwa BBC, msemaji wake Mohammed al-Mukhtar alisema wapiganaji wao "wanajitolea kwa viwango vya juu vya maadili katika vita".
"Kuna kampeni za makusudi za kuharibu sifa ya wapiganaji wetu baada ya ushindi wa kijeshi ambao tumeupata," aliongeza.
Nilipomwambia kwamba nilizungumza na wanawake ambao wamewatambua wapiganaji wa RSF kuwa washambuliaji wao, Bw al-Mukhtar alisema kwamba watu wanaojifanya wanachama wa RSF walihusika na ukatili huo.
Mzozo huo umewaacha waathirika wa ubakaji na unyanyasaji wa kingono na usaidizi mdogo.
Hospitali nyingi hazifanyi kazi tena, na inaweza kuwa vigumu kufikia chache zilizopo.
Kolthoum na Ibtissam waliniambia maumivu wanayopitia yatawatesa milele.
"Sitasahau yaliyonipata. Aibu itanifuata milele, kama kivuli changu," Kolthoum alisema.















