Trump: 'Tutashambulia ikiwa kuna shughuli za nyuklia'; Araqchi: 'Tutatoa jibu ambalo hutaweza kujificha'

Chanzo cha picha, Reuters
Abbas Araqchi, akimjibu Donald Trump, alisema, "Ikiwa uchokozi huo utarudiwa, bila shaka tutajibu kwa uamuzi zaidi. Jibu ambalo halitawezekana tena kufichwa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Mashambulizi haramu ya hivi majuzi ya vituo vya nyuklia vya Iran yalithibitisha kwamba hakuna suluhu la kijeshi. Lakini suluhisho la mazungumzo linaweza kufanya kazi."
Saa kadhaa zilizopita, Rais wa Marekani alisema siku ya , Jumatatu, Julai 28, akiwa Scotland pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer: "Wanatuma ishara mbaya sana, ishara mbaya sana. Na hawapaswi kufanya hivi... Tuliharibu uwezo wao wa nyuklia. Wanaweza kuanza tena. Wakifanya hivyo, tutawafuta haraka zaidi ."
Bw. Trump alisema atafanya shambulio kama hilo "kwa furaha" na "hadharani".
Akizungumzia mahojiano ya hivi majuzi ya televisheni ya Abbas Araqchi, alisema: "Waziri wa Mambo ya Nje [wa Iran] anazungumza kuhusu mambo ambayo hapaswi kuyazungumzia."
Rais wa Marekani pia alisema: "Nadhani wanahusika katika mazungumzo na wanawaambia Hamas na kutoa amri, na hilo si jambo zuri.

Chanzo cha picha, PA
Abbas Araqchi alizungumza na Fox News wiki jana, na Bw. Trump alijibu baada ya matangazo hayo, akamwandikia kwenye mtandao wake wa Kijamii kwamba vifaa vya nyuklia vya Iran vimeharibiwa na kwamba angefanya hivyo tena ikiwa ni lazima.
Baada ya shambulio la Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Fordow, Natanz na Isfahan, Bw. Trump amerudia kusema kwamba angeshambulia tena vituo hivyo ikibidi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mfano, mwezi mmoja uliopita, akijibu swali la mwandishi wa BBC Noumiya Iqbal, alisema katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba ikiwa mashirika ya kijasusi yatahitimisha kwamba Iran inaweza kurutubisha madini ya uranium kwa kiwango cha kutia wasiwasi, atashambulia tena "bila kusita."
Rais wa Marekani ambaye yuko Scotland alisema siku ya ya Jumatatu baada ya mazungumzo na Ursula von der Leyen, rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya: "Iran ilipigwa vibaya na ipasavyo. Lakini bado wanazungumza kuhusu kurutubisha. Ni nani angesema hivyo baada ya mkanganyiko huo? Je, ni upumbavu kiasi gani kusema hivyo? Kwa hivyo, hatutaruhusu hilo litokee."
Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema leo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran: "Kuendelea na mpango wa nyuklia wa Iran, ikiwa ni pamoja na kurutubisha, ni wazi kabisa."
"Tunasubiri ripoti muhimu kutoka kwa Shirika la Nishati ya Atomiki kuhusu hali ya vifaa vya nyuklia baada ya shambulio la Marekani na Wazayuni.
Kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, sisi bado ni sehemu ya mikataba ya ulinzi na tutafafanua mwongozo mpya na wakala, kwa kuzingatia azimio la Baraza la Ushauri la Kiislamu, ambalo linatulazimisha kuona jinsi ya kuendeleza ushirikiano.
Kuhusiana na matamshi ya Steve Whittaker, mwakilishi wa Donald Trump katika mazungumzo na Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa haina mpango wa kufanya mazungumzo na Marekani, na wakati wowote maslahi na wasiwasi wa taifa yanapohitaji, uamuzi unaohitajika utatolewa na kutangazwa."
Vikwazo vya nchi za Ulaya

Bwana Baghaei pia alisema: "Ndani ya wiki mbili zijazo, afisa wa IAEA atasafiri kwenda Iran, na tutajadili masuala ya kiufundi katika safari hiyo."
Ebrahim Rezaei, Msemaji wa Kamisheni ya Usalama wa Kitaifa na Sera za Kigeni ya Bunge hilo jana alisema kuwa, kikao cha hivi karibuni cha kamisheni hiyo kilichunguza madhara yanayoweza kutokea ya nchi ya Ulaya iliyosalia katika mapatano ya JCPOA kuamsha utaratibu wa kichochezi.
Amesema: "Wajumbe wengi wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa walipendekeza kwamba iwapo utaratibu huu utaamrishwa na nchi za Magharibi, basi serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatakiwa kujiondoa katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT).
Bw. Rezaei alisema kuwa "hatua za kuandika na kuhakiki" za mpango huu zinaendelea.
Esmail Baghaei amesema leo kuhusu mazungumzo na nchi tatu za Ulaya yaliyofanyika mjini Istanbul siku ya Ijumaa: "Mazungumzo ya Iran na pande za Ulaya yana mada iliyo wazi na yenye mipaka: kuondolewa vikwazo na masuala yanayohusiana na mpango wa nyuklia.
Kila mazungumzo kwa kawaida yana pande mbili, lakini kuibua masuala yasiyohusiana na baadhi ya nchi za Magharibi kunaonyesha tu mkanganyiko na ukosefu wa mshikamano katika misimamo yao."
Kuhusu kuamrisha utaratibu wa kufyatua risasi, Bw. Baghaei alisema: "Vyama vya Ulaya vimejaribu kwa muda mrefu kutumia hoja au suala katika Azimio nambari 2231 kama njia ya mazungumzo ya kutumia shinikizo. Tumesisitiza kuwa chombo hiki hakika hakifai."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje pia alisema: "Ukiacha suala hili la kisheria, vyama vya Ulaya kimsingi havina mamlaka ya kutumia chombo hiki kurejesha vikwazo."
"Tumeliweka wazi hili, katika mazungumzo ya Ijumaa na kabla. Pia wanafahamu vyema kwamba iwapo watalitumia vibaya gari hili, bila shaka watakabiliwa na jibu linalofaa kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa Bw. Baghaei, suala kuu ni "ikiwa vyama vya Ulaya vinaweza kujiona kuwa vyama vilivyojitolea kwa JCPOA au la."
Pia alisema kwamba "pengine ndani ya wiki mbili zijazo," afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki atazuru Iran, na kwamba mkutano unatarajiwa kujadili "mambo ya kiufundi."
Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama lilipitishwa miaka 10 iliyopita, wakati huo huo na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kufuta maazimio ya awali ya Baraza la Usalama kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Azimio hilo linatarajia utaratibu wa kufufua maazimio yaliyokatishwa hapo awali ikiwa mataifa yenye nguvu duniani hayaridhishwi na ushirikiano wa nyuklia wa Iran. Muda wa mwisho wa kutumia utaratibu huu utaisha Oktoba mwaka huu.
Nchi tatu za Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zimetangaza kuwa iwapo Iran haitaingia katika makubaliano mapya ya nyuklia ndani ya takribani wiki nne, zitatayarisha njia ya kufufuliwa maazimio ya awali na kurejesha vikwazo vya awali vya Baraza la Usalama.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












