Kwa nini timu za England zinatawala Ulaya?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sam Drury
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Author, Gary Rose
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Ligi Kuu ya England (EPL) inaendelea kuonyesha nguvu yake barani Ulaya baada ya timu tano za England kumaliza ndani ya nafasi nane bora katika hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kufuzu moja kwa moja kwa hatua ya mtoano.
Idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia timu sita iwapo Newcastle United watafanikiwa kushinda hatua ya mchujo wa nyumbani na ugenini, baada ya kumaliza nafasi ya 12 kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi Paris St-Germain mjini Paris.
Arsenal walimaliza kileleni mwa msimamo, Liverpool nafasi ya tatu, Tottenham ya nne, Chelsea ya sita, huku Manchester City wakimaliza nafasi ya nane.
Iwapo Newcastle watafanikiwa kuvuka mchujo, historia mpya itaandikwa kwa kuwa hakujawahi kuwa na timu sita za EPL kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.
Kocha wa Tottenham, Thomas Frank, amesema: "Hii ni ishara ya wazi ya ubabe. Tumeisema kwa miaka kadhaa kuwa EPL ndiyo ligi bora duniani, na huu ni uthibitisho."

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Je, ni nguvu ya fedha au ushindani?
Sababu kubwa inayotajwa ni nguvu ya kifedha ya EPL, ambayo ipo juu zaidi kuliko ligi nyingine barani Ulaya.
Timu sita za England zipo ndani ya 10 bora duniani kwa mapato, kulingana na Deloitte Football Money League, huku nusu ya timu 30 bora zikitoka England. Mapato makubwa ya haki za matangazo ya televisheni yamezipa klabu hizo uwezo mkubwa wa kifedha.
Majira ya joto yaliyopita, klabu za ligi kuu England (EPL) zilitumia zaidi ya pauni bilioni tatu (£3bn) kwenye usajili kiasi ambacho ni kikubwa kuliko matumizi ya klabu za ligi za Ujerumani (Bundesliga), Hispani (La Liga), Italia (Serie A) na Ufaransa (Ligue 1) kwa pamoja.
Mlinzi wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock, ameiambia BBC Sport: "Sababu kubwa zaidi ni nguvu ya kifedha. Lakini pia ushindani mkali ndani ya EPL umeifanya kila timu kuimarika zaidi."
Mshambuliaji wa Newcastle, Anthony Gordon, anaamini pia kuwa mtindo wa kucheza wa Ligi ya Mabingwa umesaidia timu za England.
"EPL inahitaji nguvu sana, mbio, mapambano hasa mipira ya juu. Ulaya timu zinajaribu kucheza soka la wazi zaidi."
Je, timu za England zilikuwa na michezo rahisi?

Chanzo cha picha, Opta
Takwimu za Opta zinaonyesha kuwa baadhi ya timu za England zilipata ratiba nyepesi na michezo rahisi. Ratiba ya Arsenal ilikuwa ya tatu kwa urahisi, Tottenham ya nne, Liverpool ya saba na Chelsea ya nane.
Manchester City walikuwa nafasi ya 14 kwa ugumu wa ratiba, huku Newcastle waliokutana na PSG wakiorodheshwa nafasi ya 32, miongoni mwa timu zilizokuwa na ratiba ngumu zaidi.
Rekodi zinaweza kuvunjwa, na vipi mataifa mengine?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mara ya mwisho timu tano za England kufuzu mtoano ilikuwa mwaka 2017. Msimu huu, kwa kuwa timu tano zimemaliza ndani ya nane bora, zinaepuka kukutana zenyewe katika hatua ya 16 bora, jambo linaloongeza uwezekano wa idadi kubwa kufika robo fainali.
Hata hivyo, Warnock anaonya: "Ratiba ya EPL ni ngumu sana kila wiki. Hilo linaweza kuathiri uwezo wa timu za England kushinda taji lenyewe."
Mataifa mengine hali ikoje? Mbali na England, mataifa mengine yaliyofanikiwa kutoa timu zilizofuzu moja kwa moja ni Ujerumani (Bayern Munich), Hispania (Barcelona) na Ureno (Sporting CP).
Hata hivyo, vigogo kadhaa wamelazimika kupitia mchujo, akiwemo Paris St-Germain, Real Madrid, Juventus, Inter Milan, Borussia Dortmund na Atletico Madrid.
Real Madrid walipata kipigo cha kutikisa cha 4-2 dhidi ya Benfica, huku kipa Anatoliy Trubin akifunga bao la ushindi dakika za mwisho.
Mshangao mkubwa umetoka kwa Bodo/Glimt ya Norway, ambao waliifunga Atletico Madrid siku chache baada ya kuifunga Manchester City. Ushindi huo umeifanya Bodo/Glimt kuwa timu ya kwanza ya Norway kufuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa tangu Rosenborg mwaka 1997.












