Je, ni halali kwa Marekani kuwafukuza wahalifu kwenda barani Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Images
Utawala wa Marekani umegeukia bara la Afrika kama sehemu nyingine ya kuwafukuza wahamiaji ambao inasema ni wahalifu waliopatikana na hatia.
Wakati makumi ya watu wamesafirishwa kwa nchi za Amerika ya Kati na Kusini, wanaume 12 kutoka nchi zikiwemo Mexico, Myanmar na Yemen mwezi uliopita walipelekwa Eswatini na Sudan Kusini. Raia mmoja wa Sudan Kusini pia alirudishwa nyumbani.
Nchi nyingine za Kiafrika pia zinaripotiwa kushawishiwa na Marekani ili kuwakubali watu, ambao nchi zao hazitawarudisha, kulingana na mamlaka ya Marekani.
Ahadi ya Rais Donald Trump ya kufukuzwa nchini ilipata uungwaji mkono wakati wa kampeni yake mwaka jana. Lakini wataalam wa haki za Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yameshtushwa na kile kilichotokea na wanahoji kuwa kuondolewa huko na kupelekwa kwenye taifa ambalo si mahali pa asili ya wahamiaji hao, inayojulikana kama nchi za tatu, kunaweza kukiuka sheria za kimataifa.
Je, kuwapeleka nchi ya tatu ni halali katika sheria za kimataifa?
Uhamisho kuelekea nchi ya tatu unaweza kuwa halali, lakini tu chini ya hali fulani.
"Dhana nzima ya kuondolewa na kupelekwa nchi ya tatu inapaswa kuonekana kwa kuzingatia dhana pana ya hifadhi," anasema Prof Ray Brescia, kutoka Shule ya Sheria ya Albany nchini Marekani.
"Kuna kanuni katika sheria ya kimataifa, 'kutowarudisha kwa nguvu', ambayo ina maana kwamba hutakiwi kumrudisha mtu katika nchi yake kama si salama kwao, hivyo nchi ya tatu inaweza kutoa chaguo salama," anasema.
Kanuni hii haitumiki tu kwa nchi ya asili ya wahamiaji bali pia kwa nchi yoyote ya tatu ambayo wanaweza kupelekwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iwapo nchi hiyo haiko salama, kuhamishwa kunaweza kukiuka sheria za kimataifa, kama vile wakati Mahakama ya Juu ya Uingereza ilipozuia mpango wa serikali ya Uingereza kupeleka waomba hifadhi nchini Rwanda mwaka wa 2023.
Wahamiaji lazima wawe na nafasi ya kupinga uhamishwaji ikiwa ni hatari, kulingana na ushahidi kutoka vyanzo vya kuaminika kama vile ripoti za Umoja wa Mataifa au matokeo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Mahakama zinatarajiwa kutathmini hatari hii kwa makini.
"Mahakama inapaswa kuchunguza ni aina gani ya hadhi ya kisheria ambayo wahamiaji watakuwa nayo, ikiwa watazuiliwa, na ni aina gani ya makazi inatolewa," anasema Dk Alice Edwards, Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mateso na Unyanyasaji au Adhabu nyingine za Kikatili, Kinyama au Kushusha hadhi.
Lakini wahamiaji wengi wanatatizika kupata msaada wa kisheria kwa wakati.
"Inahitaji juhudi kubwa na kupata wakili ambaye anaweza kuchukua hatua haraka," anasema Prof Brescia.
"Njia hiyo ya kisheria inaweza isipatikane kwa kila mtu."
Je, kupelekwa Eswatini na Sudan Kusini kunakiuka sheria za kimataifa?
"Hakika kunakiuka katika mambo mawili," anasema Prof David Super, kutoka Kituo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Georgetown.
"Hakuna ushahidi kwamba Marekani inawapa watu nafasi ya kupinga kufukuzwa na hawaruhusiwi kutuma watu katika nchi ambako wanaweza kukabiliwa na ukandamizaji.
Kuna maswali mazito kuhusu "Sudan Kusini na Eswatini kuhusu rekodi zao za haki za binadamu," anaiambia BBC.
Wakati wahamiaji hao walipokuwa wakielekea Sudan Kusini kwa mara ya kwanza mwezi Mei, pingamizi la kisheria liliwasilishwa katika mahakama ya Marekani baada ya ndege kuwa tayari kupaa.
Jaji huyo aliamua kwamba majaribio ya kuwafukuza watu hao yamekiuka agizo lake kwamba wahamiaji lazima waruhusiwe kupinga kuondolewa hadi nchi za tatu.
Ndege hiyo ilirejeshwa hadi Djibouti, katika ufuo wa Afrika Mashariki, ambapo watu hao waliripotiwa kuzuiliwa kwenye kontena la meli kwenye kambi ya jeshi la Marekani huku kesi hiyo ikisikilizwa.
Kesi hiyo ilipelekwa katika Mahakama ya Juu ambayo iliruhusu uhamisho huo kuendelea lakini haikubainisha iwapo Sudan Kusini ilichukuliwa kuwa sehemu salama kwa wahamiaji hao.
"Tulichoona katika kesi zinazofanana ni kwamba watu mara nyingi wananyimwa msaada wa kisheria wanapohitaji, na kesi huanza kuchelewa sana," anasema Dk Edwards.
"Katika hali hii, tayari walikuwa wakielekea kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani na hilo ni tatizo kubwa."
Anaongeza kuwa mahakama lazima ziepuke siasa, haswa wakati haki za kimsingi ziko hatarini.
Je, Eswatini na Sudan Kusini ni salama?
Mbali na kunyimwa utaratibu unaostahili, wahamiaji wanapelekwa katika nchi ambazo huenda si salama, kunakiuka sheria za kimataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa sasa inashauri dhidi ya safari zote za kwenda Sudan Kusini, ikitaja vitisho vikiwemo uhalifu, migogoro ya silaha na utekaji nyara.
Mapema mwaka huu, nchi hiyo, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, ilisemekana kuwa kwenye ukingo wa kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Kuna wasiwasi wa kweli kuhusu sheria na utulivu nchini Sudan Kusini, kuhusu ghasia, ukosefu wa utulivu, na migogoro inayoendelea," anasema Dk Edwards.
Wale waliofukuzwa nchini Sudan Kusini wanaripotiwa kuzuiliwa katika kizuizi katika mji mkuu, Juba, unaojulikana kwa hali mbaya, kulingana na mwanaharakati wa kisiasa, Agel Rich Machar.
Serikali haijathibitisha eneo lao au muda gani watakaa kizuizini.
Huko Eswatini, ufalme mdogo, kusini mwa Afrika, maafisa wanasema wahamiaji hao wako katika kituo cha kurekebisha tabia na watarejeshwa makwao kwa usaidizi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema magereza ya Eswatini yanakabiliwa na matatizo ya msongamano, uingizaji hewa duni, na upungufu wa lishe bora na huduma za afya.
"Hatuoni kwamba watakaa kwa muda wa kutosha kujumuika na jamii," msemaji wa serikali ya Eswatini, Thabile Mdluli aliiambia BBC, bila kutoa dalili zozote za muda ambao watakaa nchini humo, au kama watatumikia vifungo vyao vilivyosalia kwanza.
Serikali ya Marekani inasema wale ambao wamepelekwa nchini Eswatini walifanya uhalifu wa "kinyama" ikiwa ni pamoja na ubakaji wa watoto, mauaji na unyanyasaji wa kijinsia.
Mzozo unaongezeka nchini Eswatini.
Chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini humo, People's United Democratic Movement (Pudemo) kinasema kwamba makubaliano kati ya nchi hizo mbili yalikuwa "usafirishaji haramu wa binadamu uliojificha kama mpango wa kuwafukuza".
Mwanaharakati anayeunga mkono demokrasia Lucky Lukhele anasema nchi lazima isiwe "mahali pa kutupia wahalifu".
Hata kama sheria za kimataifa zimekiukwa, Prof Super anasema huenda Marekani ikakabiliwa na madhara kwani haitambui mahakama nyingi za kimataifa.
"Hii inaonekana kuwa juu ya kuzuia, kutuma ujumbe kwamba ukifika Marekani utatendewa vibaya sana," anasema.
Bila kujali uhalali, uhamishaji wa nchi ya tatu mara nyingi huwaweka watu walio hatarini katika mazingira yasiyofahamika bila usaidizi mdogo au hadhi ya kisheria, anasema Dk Edwards.
"Ni wazo potofu sana."
Anasisitiza kuwa jumuiya ya haki za binadamu haizuii kila hatua ya kufukuzwa, isipokuwa pale tu watu wanakabiliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Je, kuna nini kwenye nchi mwenyeji?
Maelezo ya mikataba ya uhamisho yanasalia kuwa siri kwa kiasi kikubwa.
Bi Mdluli aliiambia BBC kwamba sababu za Eswatini kuwakubali waliofukuzwa "zimesalia kuwa habari za siri kwa sasa".
Hata hivyo, serikali zote mbili za Eswatini na Sudan Kusini zilitaja uhusiano wao mkubwa na Marekani kama motisha kuu.
Prof Brescia anasema baadhi ya nchi zinaweza kuogopa kulipiza kisasi kwa Marekani iwapo zitakataa, kama vile sheria kali za visa au ushuru wa juu zaidi.
Mwezi Aprili, Marekani ilisema kuwa itabatilisha viza zote zilizotolewa kwa raia wa Sudan Kusini baada ya kutowakubali raia aliyefukuzwa nchini.
Haijabainika ikiwa hilo limebadilika, kwa vile sasa limekubali watu waliofukuzwa kutoka Marekani.
Mwanaharakati wa kisiasa Machar anasema Sudan Kusini pia imekubali mkataba huu kwani inataka Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Makamu wa Rais Benjamin Bol Mel.
Serikali ya Marekani ilitoa vikwazo dhidi ya Bol Mel mwaka 2021 kutokana na madai ya ufisadi na kuviweka upya mwaka huu.
Hatahivyo, nchi nyingine, kama Nigeria, zinakataa.
"Tuna matatizo yetu ya kutosha," Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Tuggar alisema mwezi Julai, akikataa ombi la kuwachukua wafungwa wa Venezuela.
Dk Edwards anabainisha kuwa mikataba kama hiyo mara nyingi huja na motisha.
"Katika mipango ya zamani ya uhamishaji wa nchi ya tatu, kiasi kikubwa cha fedha, pamoja na ushirikiano wa kijeshi na usalama, ulikuwa sehemu ya mpango huo," anasema.
Mnamo Machi, ripoti zilisema kuwa utawala wa Trump ungeilipa El Salvador $6m (£4.5m) ili kuwakubali waliofukuzwa kutoka Venezuela.















