Wakimbizi waliotumwa Rwanda kutoka kisiwa cha mbali cha Uingereza wazungumza na BBC
Alice Cuddy na Swaminathan Natarajan ,
BBC News

Kundi la wahamiaji walisafirishwa hadi Rwanda kutoka eneo la mbali la Uingereza na serikali ya Uingereza zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Wanasema wanahisi kutengwa na kutokuwa salama - huku mmoja akielezea nchi hiyo ya Kiafrika kama "gereza la wazi".
Huku vyama vya kisiasa vikiwa vimegawanyika kuhusu mpango tata wa serikali wa kutuma waomba hifadhi kutoka Uingereza hadi Rwanda, BBC imesafiri hadi katika taifa hilo la Afrika kuzungumza na wahamiaji wanne ambao tayari wako huko - ingawa chini ya makubaliano tofauti - kuhusu maisha yao nchini humo.
Kikundi hicho kidogo kiliwasili kutoka Diego Garcia, kisiwa kilicho katika Bahari ya Hindi. Wanasema mahitaji yao magumu ya kimatibabu, katika baadhi ya matukio kama matokeo ya ubakaji na mateso ya hapo awali, hayatimizwi nchini Rwanda.
Kila mmoja wao anapokea sawa na $50 (£39) kwa wiki kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine muhimu, lakini chini ya masharti ya kukaa kwao - yaliyokubaliwa na Uingereza na serikali za Rwanda - hawaruhusiwi kufanya kazi.
Wote wanne wanasema wamekabiliwa na unyanyasaji na ushawishi wa ngono usiohitajika mitaani. Wanasema, kwa kweli, "wamejifunga" - wanaogopa sana kutoka - wakati wanangojea Uingereza kupata mahali pa kudumu pa kuishi.
Kundi hilo - wote Watamil wa Sri Lanka - walihamishiwa Rwanda kwa matibabu ya haraka baada ya majaribio ya kujiua. Kwa sasa wako nje ya hospitali ya kijeshi na wanaishi katika orofa mbili nje kidogo ya mji mkuu, Kigali, zinazolipiwa na mamlaka ya Uingereza.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hadhi yao ya kisheria nchini Rwanda si sawa na ilivyo kwa waomba hifadhi waliosafirishwa kwenda huko kutoka Uingereza - lakini wakili anayewakilisha wawili kati ya hao wanne anasema "uzoefu wao mbaya unazua wasiwasi mkubwa" kuhusu uwezo wa Rwanda kutoa mahali salama kwa " wakimbizi walio katika mazingira magumu sana”.
Afisa mkuu wa Rwanda aliiambia BBC kuwa "ana imani kamili" na mfumo wa matibabu wa nchi yake na wasiwasi wa wahamiaji kuhusu usalama wa kibinafsi haukushirikiwa na wengine. "Tuna watu wa kigeni wanaostawi hapa," aliongeza.
Ili kulinda utambulisho wao, majina ya wahamiaji yamebadilishwa
Hakuna hata mmoja kati ya hao wanne aliyejaribu kuingia Uingereza - badala yake waliwasilisha madai ya hifadhi kwa Diego Garcia, ambayo inatumika kama kambi ya siri ya kijeshi ya Uingereza na Marekani.
Walikuwa miongoni mwa makumi ya watu waliofika kisiwani hapo Oktoba 2021 - iliripotiwa hapo awali na BBC . Walisema wamekuwa wakikimbia mateso na kujaribu kusafiri kwa meli hadi Canada kudai hifadhi.
Wanne tuliokutana nao nchini Rwanda walisema walikuwa waathiriwa wa mateso na unyanyasaji wa kijinsia katika nchi zao - baadhi kwa sababu ya uhusiano wa zamani na waasi wa Tamil Tiger, ambao walishindwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sri Lanka miaka 15 iliyopita.

Katika barabara tulivu, katika ghorofa ya vyumba viwili vya kulala, Azhagu anasema amegunduliwa kuwa na ugonjwa mkali wa mfadhaikobaada ya kupatwa na kiwewe au mshtuko, na kutokuwa na uhakika juu ya maisha yake ya baadaye na kutengwa kunafanya mambo kuwa mabaya zaidi.
“Hatupati matibabu ifaavyo. Tuna maswala ya afya ya akili, "anasema kijana huyo wa miaka 23. "Kila tunapoenda kuwaambia madaktari kuhusu matatizo yetu hawawezi kutusaidia."
Wahudumu wa afya wa Rwanda wamemzomea, anadai, na wakati mmoja baada ya kujidhuru, anasema alitishiwa kukamatwa na kuambiwa arudi Diego Garcia.
Mayur, 26, ambaye anaishi katika nyumba hiyo, anasema amekata tamaa ya kupata ushauri nasaha. Anasema hapati dawa zinazofaa na hapati kuwa na “mazungumzo mazuri”. "Ndiyo maana sitaki kwenda hospitali," anaongeza.
Wakili Tom Short, kutoka kampuni ya Uingereza ya Leigh Day, anasema tathmini huru ya kitaalamu iligundua "kila mteja wetu ana mahitaji magumu ya matibabu ambayo hayatimizwi nchini Rwanda".
Tuliwasiliana na hospitali ya kijeshi ambako Watamil wote wamekuwa wakipokea matibabu, lakini tulitumwa kwa serikali ya Rwanda.
Afisa mkuu wa Rwanda aliyehusika na mpango wa kuhamisha waomba hifadhi kutoka Uingereza, Doris Uwiceza Picard, alitetea mfumo wa matibabu wa nchi yake - akiongeza wahamiaji walikuwa wakishughulikiwa "kadiri tuwezavyo".

Watatu kati ya wahamiaji hao - vijana wawili na mwanamke, Lakshani - wamedai madai yao ya ulinzi wa kimataifa yameidhinishwa na utawala wa British Indian Ocean Territory (Biot), unaosimamia Diego Garcia. Umoja wa Mataifa na wanasheria wanaowakilisha kundi hilo wanasema hili, kwa kweli, linawapa hadhi ya ukimbizi. Wa nne katika kundi hilo - babake Lakshani, Khartik - ameruhusiwa kuandamana na binti yake.
Ina maana kundi hilo haliwezi kurejeshwa Sri Lanka, lakini Uingereza imesema haitawakaribisha. Serikali ya Conservative iliiambia BBC mwaka jana kwamba Biot "haiwezi kuwa mlango wa nyuma kuingia Uingereza".
Wakati Biot iko chini ya uhuru wa Uingereza, inaelezewa kama "tofauti kikatiba".
Kundi hilo nchini Rwanda lilituonyesha nyaraka za kisheria, jumbe za WhatsApp, barua pepe na barua walizoandika kwa mwaka uliopita kwa maafisa wa Uingereza, akiwemo Waziri Mkuu Rishi Sunak, wakiomba kuhamishwa.
"Sijui ni miaka mingapi zaidi tutalazimika kuishi kama wafungwa wasio na utaifa wa serikali ya Uingereza bila uhuru," ujumbe mmoja ulisema.
Wanne hao pia walituambia kwamba kunyanyaswa kumewafanya waogope kuondoka katika nyumba zao.

Katika ghorofa ya Lakshani, pazia la rangi kijivu linavutwa kwenye madirisha yenye vizuizi - kukifunga chumba kutoka kwa ulimwengu wa nje.
“Hatutoki nje. Daima tunaogopa,” kijana huyo wa miaka 23 alituambia tulipomtembelea yeye na Khartik, 47. “Siwaleti wanawake hapa. Hakuna marafiki."
Wote wawili wanasema kumekuwa majaribio kadhaa ya kuvunja nyumba zao. Wanatuonyesha video zinazoonyesha wavamizi wakinaswa na majirani.
Pia walikumbuka tukio moja kwenye mtaa wa karibu, wakati, wanasema, kundi la wanaume lilikuwa limewatenganisha na kujaribu kumgusa Lakshani huku wakitumia "maneno yasiyofaa sana".
Tukio hilo na mengine kama hayo, yamekuwa yakiwahofisha wawili hao, walisema. Lakshani anasema awali alishambuliwa kingono nchini Sri Lanka na kwa Diego Garcia.
Azhagu alituambia yeye na Mayur pia walikuwa wamesumbuliwa mitaani. "Wageni walikuja na kuuliza 'naweza kufanya mapenzi na wewe?' Watu walikuwa wakicheka. Tulikimbia hospitali.”
Wote wawili waliripoti wasiwasi wao kwa Crown Agents, kampuni isiyo ya kuunda faida ya maendeleo ya kimataifa ambayo inafanya kazi na serikali ya Uingereza na inatumika kama sehemu kuu ya mawasiliano ya wahamiaji nchini Rwanda.
Wote wanne walituambia Crown Agents hawakuchukulia malalamiko yao kwa uzito.
“Waliniuliza: ‘Kwa nini unaenda nje huku unajua kwamba utapata matatizo?’” Azhagu asema, akikumbuka mojawapo ya mazungumzo na kampuni hiyo. “Niliwauliza: 'Kwa nini mnatuweka hapa ilhali mnajua kuna matatizo?' Hawakujibu.”
Crown Agentsi hawakujibu walipotafutwa ili kutoa maoni yao na BBC.
Mawakili wanaowakilisha kundi hilo walisema wameibua visa vingi vya unyanyasaji wa mitaani na majaribio ya kuvunja nyumba zao na maafisa wa Biot, ambao "hawajajibu kwa kiasi kikubwa".
Utawala wa Biot haukujibu maombi ya kutoa maoni.

Wanne hao walituambia hawakuwa wamefika kwa polisi wa Rwanda ili kupata usaidizi. Wote walisema hawakuamini utekelezaji wa sheriawa polisi waliovalia sare kulingana na masaibu yao ya zamani zamani ya unyanyasaji.
Afisa mkuu wa Rwanda, Bi Picard, alisema "hakuwa na uhakika jinsi gani tunaweza kusaidia ikiwa mamlaka ya kitaifa haijafikiwa".
"Wasiwasi wa "[wahamiaji] kuhusu usalama wao haushirikiwi na mtu yeyote. Si kwa Wanyarwanda, si wakazi,” aliambia BBC. "Inavunja moyo wangu kusikia kwamba mtu anaweza kuhisi hayupo salama katika nchi hii, haswa wakati tumefanya kazi kwa bidii kuifanya nchi hii kuwa salama kwa kila mtu."
Ushauri wa serikali ya Uingereza kuhusu safari za nje unasema viwango vya uhalifu viko chini sana nchini Rwanda, lakini kuna visa vya wizi, uporaji wa mifuko na wizi wa majumbani mjini Kigali.

Watamil walikubali kuwa kuna utangamano mzuri na Rwanda lakini wanasema matukio mabaya yamewazidishia kiwewe cha zamani na kuwaacha wakiwa na hofu.
Lakshani na Khartik walisema hali yao ya maisha nchini Rwanda ni bora kuliko katika kambi ya Diego Garcia, ambapo walikuwa wamelala kwenye mahema katika kambi iliyojaa panya, walikuwa na uwezo mdogo wa kupata simu, na hawakuweza kupika chakula chao wenyewe.
Kuna Mtamil wa tano ambaye amesalia nchini Rwanda baada ya kusafirishwa pia kutoka kwa Diego Garcia kufuatia jaribio la kujiua. Bado anafuatilia madai ya ulinzi wa kimataifa. BBC imezungumza naye kwa njia ya simu, kwani kwa sasa yuko katika hospitali ya kijeshi na haruhusiwi kuondoka.
BBC imeona barua ya kumruhusu kutoka hospitalini rasmi - ikisema anapaswa kutibiwa kama mgonjwa wa nje. Anasema anazuiliwa kinyume na mapenzi yake baada ya kukataa kurejea Diego Garcia. Wakili wake ametoa wito kwa Biot kumtafutia suluhu.
Wahamiaji wanne tuliokutana nao wameambiwa kwamba, ikiwa hawataki kubaki Rwanda, wanaweza kurejea katika kambi ya Diego Garcia hadi wapate makazi mapya katika "nchi ya tatu salama".
Ofisi ya Mambo ya Nje haikujibu maswali ya BBC kuhusu iwapo Rwanda ilikuwa ikizingatiwa kama "nchi ya tatu salama" ya kulipatia kundi hilo tena makazi ya kudumu.
Tulipowauliza wahamiaji kuhusu mpango wa serikali ya Uingereza kutumia Rwanda kushughulikia na kuwahifadhi baadhi ya waomba hifadhi kutoka Uingereza, wote walisema walikuwa na wasiwasi. "Wakimbizi hao watavumilia magumu yale yale tunayokabili," mmoja alisema.
Wakili wa Leigh Day Tom Short alisema wateja wake wawili nchini Rwanda wameachwa na serikali ya Uingereza bila ya uhakika na katika "hali ya mateso ya kudumu". Nyaraka za mahakama, zilizowasilishwa London, zinahoji jinsi wahamiaji wanavyoshughulikiwa nchini Rwanda, na Diego Garcia, "ni sawa na ukatili, unyama au udhalilishaji kinyume na sheria za kimataifa".
Afisa wa Rwanda Bi Picard alisema "hali haifanani " kati ya kundi la Watamil na wale ambao wanaweza kuhama kutoka Uingereza - ambao, alisema, "watashughulikiwa na kujumuishwa katika jamii yetu".
Bi Picard alisema nchi yake "siku zote iko wazi" kwa mazungumzo juu ya kusuluhisha kundi la Diego Garcia kabisa, na kwamba ikiwa hilo litatokea, "watapewa ulinzi na dhamana zote na mahitaji ya ujumuishaji ambayo wangekuwa nayo".
Lakini "hivi sasa wanachukuliwa kama wahamiaji wa kimatibabu wanaohitaji matibabu", alisema.
Hakuna pesa iliyotolewa kwa Rwanda kuchukua na kuwahifadhi wahamiaji kutoka Diego Garcia, alisema Bi Picard, na "kiungo pekee" na mpango wa ukimbizi wa Uingereza-Rwanda ni kwamba nchi hizo mbili "zilikuwa washirika wa karibu sana".
Ofisi ya Mambo ya Nje imekataa maombi ya BBC kutoa maelezo ya mpango wa Diego Garcia. Makubaliano hayo yalikubaliwa kwa kutumia hati za kidiplomasia ambazo hazijasainiwa zilizoandikwa kwa mtu wa tatu - zinazojulikana kama "arifa za maneno" - zilizotumwa kati ya Ubalozi wa Uingereza mjini Kigali na serikali ya Rwanda. Ofisi ya Mambo ya Nje ilituambia kwamba kutoa taarifa chini ya ombi la Uhuru wa Habari "kungeathiri uhusiano" kati ya nchi hizo mbili.

Sio Conservatives wala Labour wangeweza kutoa maoni yao kuhusu hatima ya wahamiaji wa Diego Garcia nchini Rwanda au watakachofanya nao ikiwa watashinda uchaguzi.
Pande zote mbili zimeahidi kupunguza uhamiaji, lakini chama cha Labour kimesema kitafutilia mbali mpango wa Conservatives kuwasafirisha baadhi ya waomba hifadhi kutoka Uingereza hadi Rwanda.
Bw Sunak amefanya kuwasilisha mpango wa Rwanda kuwa kipaumbele kikuu cha uwaziri mkuu wake, akisema kuwa kutawazuia watu kuvuka Mfereji wa kuingia Uingereza kwa boti ndogo.
Chama cha Labour kimeelezea mpango huo - ambao tayari umewagharimu walipa kodi £310m - kama "utapeli kuanzia mwanzo hadi mwisho".
Katika taarifa yake, chama cha Liberal Democrats kilielezea kesi za Watamil nchini Rwanda kuwa "zinazozua wasiwasi " na kusema zinahitaji "kuchunguzwa ipasavyo".
Sera ya Conservatives kutuma waomba hifadhi kutoka Uingereza hadi Rwanda, waliongeza, ilikuwa "isiyo na maadili, haiwezi kutekelezeka na ya gharama kubwa [kwa] walipa kodi".
Kiongozi mwenza wa chama cha Green Party Carla Denyer ameuelezea mpango wa Rwanda kama "wa kuadhibu" na "usio wa kibinadamu" - akiongeza kuwa njia ya kuwazuia watu kuhatarisha maisha yao katika boti ndogo ni kutoa "njia salama na za kisheria" kwa ajili yao kuomba hifadhi kutoka nje ya nchi.
Reform UK hakikujibu maombi ya kutoa maoni. Katika rasimu ya waraka wake wa sera, chama hicho kinasema kitatumia Maeneo ya Ng'ambo ya Uingereza kushughulikia kwa haraka madai ya waomba hifadhi wanaowasili kupitia nchi salama.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi limetoa wito kwa Uingereza "kutoa suluhu" kwa ajili ya kundi hilo nchini Rwanda, na waomba hifadhi wapatao 60 bado wapo kwa Diego Garcia, sambamba na "majukumu yake ya kimataifa".
Wakati wanasubiri, wahamiaji wanaendelea kuwa na ndoto ya siku zijazo kwenda mahali pengine.
"Tunashangaa iwapo tunapaswa kushukuru Uingereza kwa kuokoa maisha yetu tulipofika Diego Garcia, au iwapo tunapaswa kuwakasirikia kwa kuweka maisha yetu katika hali ya kutatanisha," Mayur anasema.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












