Vita vya Siri vya Korea Kaskazini na Kusini: Je, Kim Jong-un anakaribia kushinda?

c
    • Author, Jean Mackenzie
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mpaka kati ya Korea Kaskazini na Kusini una uzio mnene wa nyaya na mamia ya vituo vya walinzi. Jambo jingine la ajabu katika mpaka huo, ni uwepo wa spika kubwa za sauti.

Korea Kaskazini na Kusini bado ziko katika mvutano, ingawa imepita miaka mingi tangu pande hizo zirushiane makombora. Kwa sasa nchi hizo zinapigana kwa njia ya hila: vita vya taarifa.

Kusini inajaribu kupeleka taarifa Kaskazini, na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un anajaribu kuzuia hilo kwa nguvu zote, anawakinga watu wake kutokana na habari za nje.

Korea Kaskazini ndio nchi pekee duniani ambayo haina intaneti ya nje kwa watu wake wa kawaida. Vituo vyote vya televisheni, vituo vya redio na magazeti vinaendeshwa na serikali.

"Sababu ya udhibiti huu ni kwamba, mengi ya wanayowaambia watu ni uongo," anasema Martyn Williams, mtaalamu wa teknolojia na habari ya Korea Kaskazini, katika Kituo cha Stimson chenye makao yake mjini Washington.

Kufichua uwongo huo kwa watu, kunaweza kuiporomosha serikali, ndiyo mawazo ya Korea Kusini.

Vipaza sauti ni chombo kimoja kinachotumiwa na serikali ya Korea Kusini, lakini nyuma ya pazia harakati za kisasa za chinichini zimeshamiri.

Kuna idadi ndogo ya watangazaji na mashirika ambayo husambaza habari usiku wa manane kupitia mawimbi mafupi na ya kati ya redio, ili Wakorea Kaskazini waweze kusikiliza kwa siri.

Maelfu ya flashi (USB) na memori kadi husafirishwa kwa magendo kila mwezi zikiwa zimesheheni taarifa za kigeni - miongoni mwao ni, filamu za Korea Kusini, nyimbo na habari, zote zimeundwa ili kupinga propaganda za Korea Kaskazini.

Lakini wale wanaofanya kazi katika uwanja huo wanahofia kwamba Korea Kaskazini inapata ushindi.

Sio tu kwamba Kim anawakandamiza wale wanaopatikana na maudhui ya kigeni, lakini mustakabali wa kazi hii uko hatarini. Sehemu kubwa ya kazi hizo hufadhiliwa na serikali ya Marekani, na upunguzaji wa misaada kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump, umeathiri mipango hiyo.

Nyimbo na filamu

DC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Flashi zenye filamu na muziki husafirishwa hadi Korea Kaskazini kwa magendo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kila mwezi, timu ya shirika la Unification Media Group (UMG), la Korea Kusini, huchukua habari za hivi punde na taarifa za burudani na kuziweka pamoja. Kisha huziweka kwenye vifaa kama flashi.

Mauudhui hayo ni pamoja na "programu za elimu" - habari za kuwafundisha Wakorea Kaskazini kuhusu demokrasia na haki za binadamu, maudhui ambayo Kim anaaminika kuyaogopa zaidi.

Kisha vifaa hivyo hutumwa hadi kwenye mpaka wa China, ambapo washirika wanaoaminika wa UMG huzisafirisha kuvuka mto hadi Korea Kaskazini.

Tamthilia za Korea Kusini zinaweza kuonekana hazina tatizo, lakini zinafichua mengi kuhusu maisha ya kawaida ya kila siku. Na kuonyesha uhuru na jinsi Korea Kaskazini ilivyo nyuma kwa maendeleo.

Filamu hizi, huleta changamoto kwa uzushi wa Kim; kwamba wale wa Kusini ni maskini na wanaonewa.

"Baadhi ya [watu] wanatuambia walilia walipokuwa wakitazama filamu hizi," anasema Lee Kwang-baek, mkurugenzi wa UMG.

Ni vigumu kujua ni watu wangapi hasa wanaopata flashi hizo, lakini shuhuda aliyekimbia Kaskazini hivi karibuni, anasema taarifa zinaenea na zina athari chanya.

"Wakimbizi wa hivi karibuni zaidi kutoka Korea Kaskazini wanasema maudhui ya kigeni ndio ambayo yaliwachochea kuhatarisha maisha yao ili kutoroka", anasema Sokeel Park, ambaye shirika lake la Liberty linafanya kazi ya kusambaza maudhui haya.

Hakuna upinzani wa kisiasa au wapinzani wanaojulikana nchini Korea Kaskazini, na kukusanyika kwa maandamano ni hatari sana - lakini Park anatumai baadhi yao watahamasishika kutekeleza vitendo vya upinzani.

Kutoroka Korea Kaskazini

FC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mpaka huo una uzio mnene na walinzi wanaoshika doria katika eneo hilo

Kang Gyuri, ambaye ana umri wa miaka 24, alikulia Korea Kaskazini, ambako aliendesha biashara ya uvuvi. Kisha mwishoni mwa 2023, alikimbilia Korea Kusini kwa mashua.

Tulipokutana katika bustani majira mchana huko Seoul mwezi uliopita, alikumbuka kusikiliza matangazo ya redio na mama yake akiwa mtoto. Na kisha kutazama maudhui kwenye falshi.

Kadiri alivyozidi kutazama ndivyo alivyogundua kuwa serikali inamdanganya. "Nilikuwa nikifikiri ilikuwa kawaida serikali kuweka vikwazo. Nilidhani nchi nyingine zinaishi chini ya udhibiti kama huu," anaelezea. "Lakini niligundua ilikuwa ni Korea Kaskazini pekee."

Kim Jong Un, anajua sana hatari hii kwa serikali yake, na anapinga.

Wakati wa janga Uviko 19, alijenga uzio mpya wa umeme kando ya mpaka na China, na kufanya kuwa vigumu zaidi kwa habari kusafirishwa. Na sheria mpya zilizoanzishwa 2020 zimeongeza adhabu kwa watu wanaokamatwa wakisikiliza na kusambaza habari za vyombo vya habari vya kigeni.

Kang anasema wale wanaosambaza maudhui wanaweza kufungwa au kuuawa. Baada ya msako kuanza Bi Kang na marafiki zake wakawa waangalifu.

Anasema anafahamu kuhusu vijana wengi walionyongwa kwa kukamatwa na maudhui ya Korea Kusini.

Tabia za Korea Kusini

FV
Maelezo ya picha, Kang Gyuri alikimbilia Korea Kusini kwa boti mwishoni mwa 2023

Hivi karibuni Kim pia alipiga marufuku tabia zinazohusishwa na kutazama tamthilia za Kusini. 2023, alifanya kuwa kosa kwa watu kutumia misemo ya Kikorea Kusini au kuzungumza kwa lafudhi ya Kikorea Kusini.

Maafisa wa 'vikosi vya vijana', wanashika doria mitaani, wamepewa jukumu la kufuatilia mienendo ya vijana.

Bi Kang anakumbuka kusimamishwa mara nyingi, kabla ya kutoroka, na kukaripiwa kwa kuvaa na kutengeneza nywele zake kama Mkorea Kusini.

Kikosi hicho kingemnyang'anya simu na kusoma jumbe zake, anaongeza, ili kuhakikisha hajatumia maneno yoyote ya Kikorea Kusini.

Mwishoni mwa 2024, simu ya rununu ya Korea Kaskazini ilitoroshwa nje ya Korea Kaskazini na Daily NK, (shrika la habari la UMG huko Seoul).

Simu hiyo imeundwa ili lahaja ya neno la Kikorea Kusini inapoingizwa, itatoweka, na nafasi yake kuchukuliwa na neno sawa la Kikorea Kaskazini.

"Simu ni sehemu ya jinsi Korea Kaskazini inavyojaribu kuwajaza watu nadharia za Kaskazini," anasema Williams.

Kufuatia hatua hizi zote za ukandamizaji, anaamini kwamba Korea Kaskazini sasa "inaanza kushinda” katika vita hivi vya taarifa.

Ufadhili wa Trump

Kufuatia kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House mapema mwaka huu, fedha zilikatwa kwa mashirika kadhaa, ikiwa ni pamoja na yale ya kupenyeza habari Korea Kaskaini.

Pia alisitisha fedha kwa vyombo viwili vya habari, vinavyofadhiliwa na serikali, Radio Free Asia na Sauti ya Amerika (VOA), ambavyo hupeperusha matangazo usiku kwenda Korea Kaskazini.

Steve Herman, mkuu wa zamani wa ofisi ya VOA iliyoko Seoul, anasema: "Hii ilikuwa mojawapo ya njia chache, ambayo watu wa Korea Kaskazini walikuwa nayo kupata habari, na imefungwa bila maelezo."

UMG bado inasubiri kujua kama ufadhili wao utakatwa moja kwa moja au la.

Park kutoka Liberty anasema, "Trump amempa Kim mkono wa usaidizi, na kuita hatua hiyo ni ya "kutoona mbali."

Anasema Korea Kaskazini, pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wake wa silaha za nyuklia, kuna tishio kubwa la usalama - huku vikwazo, diplomasia na shinikizo la kijeshi vimeshindwa kumshawishi Kim kuondoa silaha za nyuklia, habari ndiyo silaha bora zaidi iliyobaki.

"Hatujaribu tu kupambana na tishio la Korea Kaskazini, tunajaribu kusuluhisha," anasema. "Ili kufanya hivyo unahitaji kubadilisha namna nchi ilivyo."

Nani atatoa ufadhili?

FC

Chanzo cha picha, AFP/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Athari za baadhi ya sera za Rais Trump zinaweza kuwa zimeipa Korea Kaskazini ushindi katika vita vya taarifa

Swali lililobaki: Nani atafadhili kazi hii? Suluhisho mojawapo linaweza kuwa ni Korea Kusini. Lakini Chama cha upinzani cha kiliberali kinaelekea kujaribu kuboresha uhusiano na Pyongyang, kumaanisha kufadhili wa vita vya taairfa utasita.

Mgombea mkuu wa chama hicho katika uchaguzi wa rais wa wiki ijayo tayari ameashiria kuwa atazima vipaza sauti iwapo atachaguliwa.

Hata hivyo Park bado ana matumaini. "Jambo zuri ni kwamba serikali ya Korea Kaskazini haiwezi kuingia katika vichwa vya watu na kuzitoa habari ambazo zimeshaingia kwa miaka mingi," anadokeza.

Na jinsi teknolojia zinavyokua, ana uhakika kueneza habari kutakuwa rahisi. "Kwa muda mrefu ninaamini hilo ndilo litakaloibadilisha Korea Kaskazini."