Serikali ya Tanzania yakanusha madai ya kupanga kumpa sumu Tundu Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Serikali ya Tanzania imekanusha vikali tuhuma zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kudai kuwa zinaihusisha yenyewe na kiongozi wa upinzani, Tundu Antipas Lissu, katika mpango wa kumuwekea sumu mshtakiwa huyo.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Julai 3, 2025, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Serikali imetoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa hizo, ikisisitiza kuwa "hazina ukweli wowote."
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amefafanua kuwa Tundu Antipas Lissu, ambaye anatajwa na wanaharakati hao nje ya nchi na pia katika taarifa ya chama chake cha siasa, anakabiliwa na mashtaka Mahakamani. Mbali na mashataka ya uchochezi, Lissu anakabiliwa na shitaka la uhaini, ambalo halina dhamana na kama akikutwa na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Taarifa ya msigwa inasema kuwa Lissu anashikiliwa gerezani mpaka hapo shauri lake litakapohitimishwa Mahakamani. Serikali imesisitiza kuwa "haijawahi kuwa na mpango wa kumwekea sumu mtu yeyote aliyepo gerezani wala haina mpango wa kufanya hivyo kwa mtu yeyote."
Imetaja taarifa hizo kuwa "nia ovu ya kuchafua sifa na heshima kubwa ya Tanzania" na kwamba mamlaka zimeanza kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika na kuchapisha na kusambaza "uongo huo."
Kauli hii ya Serikali inakuja kufuatia taarifa iliyotolewa na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA ikidai kupokea "kwa mshtuko mkubwa taarifa zinazodai kuwa kiongozi wao Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho, ana mpango wa kuwekewa sumu akiwa kizuizini."

Chanzo cha picha, Msigwa
Taarifa hiyo ya CHADEMA, iliyotiwa saini na Brenda Rupia, mMkurugenzi wa mawasiliano na uenezi, ilitaja vyanzo mbalimbali, ikiwemo ujumbe wa David McAllister, mmoja wa viongozi waandamizi wa Bunge la Ulaya, aliyedai kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) kwamba: "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kutisha za jaribio la kumtilia sumu kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu akiwa kizuizini."
CHADEMA imedai kuwa tukio hili ni "jambo la kupuuza, hasa tukikumbuka kuwa si mara ya kwanza viongozi wa Chadema kulengwa na vitisho, mashambulizi au uonevu wa aina mbalimbali," na kuonya kuwa "taaria nyinyi tuliwazolishwa kwa mamlaka husika zikipuuzwa au kutochukuliwa hatua yoyote."
Kufuatia madai hayo, CHADEMA ilizitaka mamlaka husika, ikiwemo Vyombo vya ulinzi na usalama na ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, kuchukua hatua za haraka, huru na za kina kuchunguza madai hayo.
Waliitaka Serikali pia kutoa kauli ya wazi na kuhakikisha usalama wa kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Lissu akiwa kizuizini. Pia, walitoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa, mashirika ya haki za binadamu, mabalozi na wadau wengine kufuatia ukweli wa jambo hilo na kushinikiza uwajibikaji, ulinzi wa haki za binadamu, na kuheshimiwa kwa misingi ya demokrasia nchini Tanzania.















