Kwa nini jina la balozi huyu wa Iran nchini Pakistan liko kwenye orodha ya wanaosakwa zaidi na FBI?

Reza Amiri Moghadam aliteuliwa kuwa balozi wa Iran nchini Pakistan mnamo 2023

Chanzo cha picha, X/@IraninIslamabad

Muda wa kusoma: Dakika 4

Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) limemweka Reza Amiri-Moghaddam, balozi wa Iran nchini Pakistan, pamoja na raia wengine wawili wa Iran, kwenye orodha yake ya "Watu wanaotafutwa".

Taarifa iliyotolewa na FBI inadai kuwa Reza Amiri Moghadam na watu wengine wawili, Taghi Daneshvar na Gholam Hossein Mohammadnia, wanaweza kuwa walihusika katika utekaji nyara wa Robert A. "Bob" Levinson, wakala maalum aliyestaafu wa FBI, mnamo Machi 2007.

FBI imetangaza kwamba Bob Levinson alitoweka kutoka kisiwa cha Iran cha Kish mnamo Machi 9, 2007.

Maafisa wa Iran hawajazungumzia suala hilo. BBC idhaa ya Urdu imewasiliana na ubalozi wa Iran nchini Pakistani kwa jibu rasmi, lakini bado haijapata jibu.

Katika kujibu gazeti la Dawn la nchi hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Shafqat Ali Khan amesema: "Kwa upande wa Pakistan, inamheshimu balozi wa Iran kwa nafasi yake katika kukuza uhusiano kati ya nchi hizo mbili."

Shafqat alisisitiza: "Balozi, hasa kutoka nchi jirani yenye urafiki, anafurahia mapendeleo, kinga na heshima zote."

Taarifa ya FBI inasema nini?

FBI imetoa matangazo dhidi ya hawa watu watatu, na kutangaza kwamba shirika hilo linawachunguza maafisa wa Iran kwa jukumu lao katika utekaji nyara wa afisa huyo mstaafu na jaribio la serikali ya Iran kuhusisha kitendo hiki na watu wengine au vyombo vingine.

FBI imedai kuwa Reza Amiri Moghadam, Taghi Daneshvar, na Gholam Hossein Mohammadnia ni mawakala wa kijasusi wa Iran.

"Watu hawa watatu ni miongoni mwa maajenti wa kijasusi ambao walihusika katika utekaji nyara wa Bob Levinson wa 2007 na katika kusaidia serikali ya Iran kuficha kitendo hicho," alisema Steven Jens, naibu mkurugenzi wa ofisi ya FBI Washington.

Pia aliongeza: "Bob Levinson huenda alikufa mahali mbali na familia yake, marafiki na wafanyakazi wenzake."

Wakala maalum wa FBI alitoweka nchini Iran

Chanzo cha picha, FBI/YOUTUBE

Alisisitiza kuwa FBI itaendelea kuwasaka waliohusika katika kesi hii.

Kulingana na FBI, zawadi ya serikali ya Marekani ya dola milioni 50 kwa taarifa zitakazowezesha kupatikana na kuachiliwa kwa Bob Levinson bado zinaendelea kutumika.

Taarifa hiyo pia inasema kuwa shirika hilo linadai kuhojiwa kwa Reza Amiri Moghadam, Taghi Daneshvar, na Gholam Hossein Mohammadnia kuhusiana na kesi hii.

Je! FBI walisema nini kuhusu Reza Amiri Moghadam?

Reza Amiri Moghadam alianza rasmi kazi yake kama balozi wa Iran nchini Pakistan mnamo Julai 2023.

Hakuna habari nyingi zinazopatikana kumhusu kwenye tovuti rasmi ya Ubalozi wa Iran nchini Pakistan.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, balozi wa Iran nchini Pakistan alizaliwa mwaka 1961 na ana Shahada ya Uzamivu ya Uhusiano wa Kimataifa.

Kwa mujibu wa tovuti hiyo hiyo, pamoja na kuhudumu kama balozi wa Islamabad, pia aliwahi kuwa naibu wa mambo ya nje na sera za kimataifa katika Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran.

Hata hivyo FBI inadai kuwa Reza Amiri Moghadam hapo awali aliongoza idara ya operesheni ya Wizara ya Ujasusi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Taarifa hiyo ilisema: "Wakati wa uongozi wa awali wa Moghadam katika nafasi hii, maafisa wa ujasusi barani Ulaya waliripoti kwake moja kwa moja."

Reza Amiri Moghadam, Balozi wa Iran, na Shahbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan

Chanzo cha picha, X/@GovtofPakistan

Je, ni watu gani wengine kwenye orodha ya "Wanaotafutwa"?

Kwa mujibu wa taarifa ya FBI, Taghi Daneshvar, anayejulikana pia kama Seyed Taghi, ni afisa mkuu katika Wizara ya Ujasusi ya Iran na ameshiriki katika operesheni za "kukabiliana na ugaidi".

Madai ya taasisi hii ya Marekani yanaonesha kwamba wakati wa kutoweka kwa Bob Levinson, mtu aliyeitwa Mohammad Sinai (pia anajulikana kama Mohammad Basiri) alikuwa akifanya kazi chini ya usimamizi wa Taqi Daneshvar.

Mtu wa tatu kwenye orodha ya FBI inayosakwa zaidi ni Gholam Hossein Mohammadnia.

Gholam Hossein Mohammadnia, aliyekuwa balozi wa Iran nchini Albania, na mwanadiplomasia mwingine wa Iran walifukuzwa nchini humo na serikali ya Albania kwa "kutishia usalama wa taifa."

Wakati huo, Iran ilidai kuwa hatua hii ilichukuliwa kwa shinikizo kutoka kwa Marekani na Israel.

FBI inatoa zawadi kwa taarifa kuhusu wakala maalum aliyestaafu

Chanzo cha picha, FBI

Je, wakala aliyestaafu wa FBI alikuwa akifanya nini nchini Iran?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya FBI, Robert A. "Bob" Levinson, mfanyakazi mstaafu wa serikali ya Marekani, alifanya kazi katika Wizara ya sheria ya Marekani kwa miaka 28, wakati huo pia alishirikiana na FBI na Utawala wa Kupambana na Dawa za Kulevya.

Alistaafu kutoka FBI mnamo 1998 na kisha akafanya kazi kama mpelelezi wa binafsi.

Kulingana na FBI, alisafiri hadi kisiwa cha Kish mnamo Machi 8, 2007, akiwakilisha kampuni kadhaa kubwa, na hakuna habari kuhusu aliko baada ya hapo.

Hata hivyo, serikali ya Marekani na FBI hawajawahi kueleza hasa kile Levinson alikuwa akifanya akiwa Iran.

Hata hivyo, David Levinson, mtoto wa Bob, ametangaza kuwa familia yake imepokea video ya baba yake ikimuonesha akiwa kifungoni.

David na mama yake wametoa video wakihimiza serikali kufanyia kazi kuachiliwa kwa Bob, ambayo pia inajumuisha kipande cha picha cha Bob akiomba msaada.

Katika ujumbe huu wa video, Bob Levinson anasema: "Nimekuwa kifungoni kwa miaka mitatu na nusu."

Aliongeza: "Serikali ya Marekani lazima ijibu madai ya kundi linalonishikilia mateka."