Ana Montes: Jinsi jasusi wa Cuba alivyoisaliti Marekani

Montes

Chanzo cha picha, cbs

Ana Belén Montes alionekana kukata tamaa alipokuwa akipigwa picha mara baada ya kuachiliwa kutoka kifungo cha miaka 20 jela. Sasa ana umri wa karibu miaka 66, nywele zake za kahawia zina mistari ya kijivu.

Kulikuwa na machache ya kuonesha kwamba Montes alikuwa ametumia miaka kama jasusi wa Cuba aliyepenya ndani kabisa ya serikali ya Marekani. Au kwamba aliwahi kuchukuliwa na Marekani kuwa mmoja majasusi hatari zaidi wanaolenga taifa.

Na hiyo, wataalamu wanasema, ndiyo hasa iliyomfanya kuwa jasusi kamili.

Sindano kwenye jaa la nyasi

Ana Montes alikamatwa Septemba 21, 2001, na hatimaye kupatikana na hatia ya kula njama ya kufanya ujasusi dhidi ya Marekani.

Kufikia wakati huo, maafisa wa ujasusi wa Marekani walikuwa wakimtafuta jasusi wa Cuba ndani ya serikali kwa karibu muongo mmoja lakini kugundua ni nani alikuwa akipitisha habari ya siri kwa Wacuba imeonekana kuwa kazi kubwa.

"Kweli ni sawa na kutafuta sindano kwenye nyasi," alisema Pete Lapp, jasusi mstaafu wa FBI ambaye pamoja na mshirika wake, Steve McCoy, walikuwa sehemu ya timu ambayo ilikuwa muhimu katika kuthibitisha Montes alikuwa jasusi wa Cuba.

Lapp na timu yake walipewa jukumu la kutafuta jasusi. Ili kufanya mambo kuwa magumu zaidi, Bw Lapp alisema Wacuba pia walifanya kazi ya kuficha jinsia ya Montes kwa kupendekeza kwamba jasusi huyo alikuwa mwanaume mwenye kibali cha hali ya juu, jambo ambalo lilipanua orodha ya walengwa.

"Ingekuwa kazi rahisi zaidi ikiwa tungejua tunatafuta mwanamke," alisema.

Ilibainika kuwa FBI haikuwa tu inamtafuta mwanamke, lakini afisa wa juu wa ujasusi wa Marekani kuhusu Cuba na Amerika ya Kati.

Malkia wa Cuba

Montes

Chanzo cha picha, FBI

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Na Montes, Alipewa jukumu la kupeleleza kwa niaba ya serikali yao kabla hata hajamaliza shule na kwa sababu hiyo, Bw Lapp alisema, alijiunga na Shirika la Ujasusi la Marekani kama "wakala aliyeajiriwa kikamilifu wa idara ya ujasusi ya Cuba."

"Alifanya kazi nzuri ya kuwa karibu-mkamilifu, kila kitu alichotimiza kama mchambuzi alijenga tu ukuta wa usalama karibu naye," alisema.

Ana Montes alipitia safu ya huduma za kijasusi za Marekani, kwanza kwenye jalada la El Salvador na Nikaragua, kabla ya kuhamia kuwa mfanyakazi mkuu wa ujasusi anayeichunguza Cuba. Ndani ya mashirika, utaalamu wake ulimpatia jina la utani Malkia wa Cuba.

Lakini kwa takriban miaka 17 pia alipitisha baadhi ya taarifa za siri za juu zaidi za taifa kwa serikali adui ya kigeni.

"Mojawapo ya sababu nadhani ilichangia asikamatwe ni kwamba alikariri habari ambayo aliichukua," alisema Jim Popkin, ambaye kitabu chake, Code Name Blue Wren, kinaorodhesha kupanda kwa Montes kupitia safu hadi kukamatwa kwake.

"Alikuwa na kazi yake ya siku ambapo alikaa tu kimya, kwa bidii na kukariri kadiri alivyoweza hati hizi za siri. Na kisha kazi yake ya usiku ilikuwa kwenda nyumbani, akiandika kwenye kompyuta ndogo ya Toshiba, kuificha na kumpa mtu mwingine."

Badala ya kufanya kazi kwa ajili ya pesa, Montes baadaye aliwaambia maafisa kwamba aliipeleleza Marekani kwa sababu hakukubaliana na sera za kuingilia kati serikali yake katika Amerika ya Kati na Cuba.

"Alikuwa hatari sana kwa sababu alitoa utambulisho wa kweli wa wafanyikazi wa Marekani wanaofanya kazi Cuba," Bw Popkin alisema.

Taarifa hizo pekee zingeweza kuhatarisha maisha, lakini Montes pia alifichua kuwepo kwa satelaiti ya siri ya mabilioni ya dola ambayo Marekani iliitumia kupeleleza Urusi, China na Iran.

"Ndio maana maafisa wa ujasusi wanamwita mmoja wa majasusi waharibifu zaidi katika historia ya Marekani, yaani jasusi wa kike aliyeharibu zaidi kuwahi kuwepo," Bw Popkin alisema.

Mtandao wa udanganyifu

Kufikia mwaka wa 2000, maafisa wa ujasusi walishuku Montes huenda alikuwa jasusi ana Bw Lapp na timu yake wakaanza kumchunguza.

"Nilikuwa na msimamo, tusizingatie kumnasa katika kitendo cha ujasusi. Tuhakikishe tumepata mtu sahihi kwanza," Bw Lapp alisema.

Baada ya miaka mingi ya kumtafuta jasusi, mafanikio yalikuja wikendi ya Siku ya Ukumbusho mwaka wa 2001, wakati Lapp na timu yake walipotafuta nyumba ya Montes na kugundua zaidi ya muongo mmoja wa habari za siri kwenye kompyuta ndogo chini ya kitanda chake.

"Nilipigwa na butwa," alisema Bw Lapp, ambaye ataeleza kwa kina uchunguzi wake katika kitabu kijacho kiitwacho Malkia wa Cuba.

Montes anapokea Cheti cha Kitaifa cha Ujasusi cha tofauti kutoka kwa George Tenet wa CIA

Chanzo cha picha, Image source, US Department of Defense

Kwa Montes, kuishi maisha ya ujasusi katika sehemu mbalimbali hakumaanisha tu kusema uwongo kwa mashirika ya juu zaidi ya kijasusi ya nchi, lakini pia kulimaanisha kusema uwongo kwa watu wa karibu zaidi - ikiwa ni pamoja na familia yake.

Wanne wa wanafamilia wake wa karibu walifanya kazi katika Ofisi ya Shirikisho ya Uchunguzi akiwemo dada yake, Lucy. Kama watu wengine ulimwenguni, waligundua Montes alikuwa jasusi wa serikali ya Cuba siku ambayo alikamatwa.

Bw Popkin, ambaye ametumia muda kuhoji familia kwa ajili ya kitabu chake, alisema wakati wa kukamatwa kwake hasira ya familia kwa usaliti ilikuwa ahueni.

"Ilimpa [Lucy] ahueni kiasi cha kuweza kuelewa zaidi kidogo kuhusu dada yake na kwa nini uhusiano wao, ambao ulikuwa wa karibu sana, ulikuwa umezorota kwa miaka mingi," alisema.

Ana Montes alitumikia zaidi ya kifungo chake cha miaka 25 gerezani na aliachiliwa tarehe 6 Januari.

Kwa kuwa sasa ametoka gerezani na kurudi nyumbani kwake Puerto Rico, Montes alisema anatumai kuishi "maisha tulivu na ya siri."

Lakini ndani ya saa chache baada ya kuachiliwa, Montes pia alionyesha kwamba bado alikuwa akifikiria Cuba.

"Ninawahimiza wale wanaotaka kuniangazia badala yake kuzingatia masuala muhimu, kama vile matatizo makubwa yanayowakabili watu wa Puerto Rico au vikwazo vya kiuchumi vya Marekani kwa Cuba," alisema katika taarifa iliyosambazwa na BBC News kupitia wakili wake, Linda Backiel.

"Ni nani katika kipindi cha miaka 60 iliyopita amewauliza watu wa Cuba ikiwa wanataka Marekani iweke kizuizi kinachowafanya wateseke?"

Lakini kwa Bw Lapp, na wanaume na wanawake ambao walipambana kumfikisha mahakamani kwa miaka mingi, uhuru wa Montes ulikuja kama pigo.

"Nilijua siku hii inakuja, lakini haimaanishi kuwa bado haijauma," alisema.