Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran yafikiria njia ya mazungumzo ya nyuklia na Marekani kuzuia vita
Iran imesema iko katika hatua ya kutathmini masharti ya kurejea kwenye mazungumzo ya nyuklia na Marekani, huku pande zote zikionyesha utayari wa kufufua mazungumzo ya kidiplomasia katika mzozo uliodumu kwa miaka mingi.
Muhtasari
- China yakosoa Dalai Lama kupewa tuzo ya Grammy
- Mvulana 13, aogelea kilomita 4 ili kuiokoa familia yake iliyokwama baharini
- Iran yafikiria njia ya mazungumzo ya nyuklia na Marekani kuzuia vita
- Mbunge akamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono
- Bei ya dhahabu na fedha yashuka
- Watu 80 waliotekwa nyara Nigeria warejea nyumbani baada ya kutoroka
- Mzozo juu ya ufadhili wasababisha baadhi ya shughuli za serikali kufungwa Marekani
- Mwanamuziki wa Nigeria afariki baada ya kuumwa na nyoka
- Familia yatafuta majibu baada ya Mkenya aliyepigana upande wa Urusi kuuawa Ukraine
- Kivuko cha Rafah kilichoko kati ya Gaza na Misri chafunguliwa
- Tuzo za Grammy: Trump atishia kumshtaki mchekeshaji Trevor Noah
- Mkanganyiko juu ya mgomo wa magari ya umma washuhudiwa Nairobi
- China yawanyonga watu 4 zaidi wa genge la kimafia la Myanmar
- Mzozo wa Marekani na Iran: Trump ajibu onyo la Khamenei
- Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza ażuru Ethiopia kujadili uhamiaji haramu
- M23 yaitaka Congo kutoingiza siasa katika vifo vya wachimba madini Rubaya
- Watu 12 wafariki katika shambulio la basi Ukraine
- Jeshi la Nigeria lamuua kamanda mmoja wa Boko Haram
Moja kwa moja
Asha Juma, Beldeen Waliaula & Rashid Abdallah
China yakosoa Dalai Lama kupewa tuzo ya Grammy
China imejibu kwa hasira tuzo ya Grammy kwa Dalai Lama - ikisema inapinga tuzo za sanaa kutumika "kisiasa dhidi ya China."
Kiongozi huyo wa kiroho wa Kibuddha alitajwa katika kipengele cha vitabu vya sauti kwa kitabu chake cha Meditations: The Reflections of His Holiness the Dalai Lama.
Dalai Lama alisema amekubali tuzo hiyo kwa "shukrani na unyenyekevu".
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 90 ameishi uhamishoni kutoka nchi yake ya Tibet tangu 1959 na analaumiwa kwa kuwa muasi na anayetaka kujitenga na Beijing.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Lin Jian aliuambia mkutano wa waandishi wa habari: "Tunapinga vikali pande husika kutumia tuzo za sanaa kama chombo cha udanganyifu wa kisiasa dhidi ya China."
Kiongozi huyo wa kiroho, anayeishi Dharamshala nchini India, aliondoka China akihofia maisha yake baada ya wanajeshi wa China kuzuia uasi.
Anataka uhuru zaidi kwa Tibet, lakini Beijing Tibet kuwa ni sehemu muhimu ya China.
Tuzo hiyo ya Dalai Lama, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, ilichukuliwa kwa niaba yake na mwanamuziki Rufus Wainwright, ambaye alikuwa miongoni mwa wasanii waliotajwa kwenye kitabu hicho.
Pia unaweza kusoma:
Mvulana 13, aogelea kilomita 4 ili kuiokoa familia yake iliyokwama baharini
Mvulana wa miaka 13 amesifiwa baada ya kuogelea katika maji yenye mawimbi na mwanga hafifu ili kumwokoa mama yake na ndugu zake wawili waliokuwa wamebebwa na maji baharini karibu na pwani ya Australia.
Familia hiyo ilikuwa ikiendesha ubao wa kuteleza kwenye maji huko Geographe Bay, karibu na Quindalup Magharibi mwa Australia, siku ya Ijumaa wakati upepo mkali ulipowapeleka mbali, wanasema polisi.
Kijana huyo alianza kupiga makasi ili kurudi ufukweni ili kutoa taarifa lakini mtumbwi wake aina ya kayaki uliingia maji - kwa hivyo aliogelea kilomita 4 zilizobaki hadi ufukweni.
"Ushujaa, nguvu na ujasiri ulioonyeshwa na familia hii ulikuwa wa ajabu, hasa kijana aliyeogelea kilomita 4 ili kutoa taarifa," kimesema Kikundi cha Uokoaji Majini cha Naturaliste.
Kamanda wa kikundi hicho Paul Bresland amesema, aliogelea kwa saa mbili za kwanza akiwa amevaa koti la kuokoa maisha.
"Kijana huyo alifikiri hatafanikiwa akiwa amevaa koti la kuokoa maisha, kwa hivyo aliliacha, na akaogelea saa mbili zilizofuata bila koti la kuokoa maisha."
Mvulana huyo aliweza kutoa taarifa Ijumaa jioni, na kusababisha msako kutoka kwa mashirika mbalimbali, Polisi wa Australia Magharibi walisema katika taarifa siku ya Jumatatu.
Mama huyo mwenye umri wa miaka 47, mwanawe mwingine wa kiume, 12, na binti yake mwenye umri wa miaka nane, walipatikana na helikopta ya uokoaji wakiwa wameshikilia ubao wa kuogelea kama kilomita 14 kutoka ufukweni.
"Meli ya uokoaji ya kujitolea ilielekezwa mahali walipo na wote watatu waliokolewa na kurudishwa ufukweni," kikosi hicho kimesema.
Inspekta James Bradley amesema, “kwa bahati nzuri, watu wote watatu walikuwa wamevaa jaketi za kuokoa maisha, jambo ambalo lilichangia kuwa hai," aliviambia vyombo vya habari vya ndani.
Polisi walisema familia hiyo ilichunguzwa na wahudumu wa afya kabla ya kupelekwa hospitali iliyo karibu.
Familia hiyo baadaye iliruhusiwa kuondoka na kuwatembelea wafanyakazi wa uokoaji wa baharini ili kuwashukuru, kulingana na ABC.
Iran yafikiria njia ya mazungumzo ya nyuklia na Marekani kuzuia vita
Iran imesema iko katika hatua ya kutathmini masharti ya kurejea kwenye mazungumzo ya nyuklia na Marekani, huku pande zote zikionyesha utayari wa kufufua mazungumzo ya kidiplomasia katika mzozo uliodumu kwa miaka mingi.
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mazungumzo hayo yanaangaliwa kwa kina, akisisitiza kuwa Tehran inataka kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi “haraka iwezekanavyo”.
Vyanzo vya Iran vimeeleza kuwa mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi huenda wakakutana nchini Uturuki siku chache zijazo.
Haya yanajiri wakati mvutano ukiwa mkubwa, kufuatia kuongezeka kwa uwepo wa kijeshi wa Jeshi la Marekani karibu na Iran, baada ya maandamano makubwa ya wananchi dhidi ya serikali ya Iran mwezi uliopita.
Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Iran kufanya makubaliano mapya ya nyuklia, akidai Tehran isitishe kabisa urutubishaji wa uranium, ipunguze mpango wake wa makombora ya masafa marefu na iache kuunga mkono makundi washirika katika eneo hilo.
Iran imekataa masharti hayo, ikisema yanakiuka uhuru wake, ingawa maafisa wawili wa Iran wamesema mpango wa makombora ndio kikwazo kikubwa zaidi katika mazungumzo kuliko suala la nyuklia.
Pia unaweza kusoma:
Mbunge akamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono
Mbunge wa kujitegemea amekamatwa kwa mara ya pili akituhumiwa kwa makosa ya kingono.
Mbunge wa zamani wa chama cha Labour Dan Norris, mwenye umri wa miaka 66, anachunguzwa kwa ubakaji wa mwanamke na amekamatwa tena kwa tuhuma za kumbaka mwanamke wa pili, kumnyanyasa kingono mwanamke wa tatu, unyanyasaji wa kimapenzi, na kuwachungulia wanawake kadhaa.
Meya huyo wa zamani wa Magharibi mwa Uingereza alikamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 2025 kwa tuhuma za makosa ya kingono dhidi ya msichana, utekaji nyara wa mtoto, na ubakaji wa mwanamke.
Makosa yote yanadaiwa kutokea kati ya miaka ya 2000 na 2020.
Norris pia anachunguzwa kwa utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma. Yuko nje kwa dhamana.
Alichaguliwa kuwa mbunge wa chama cha Labour katika jimbo la North East Somerset na Hanham mwezi Julai 2024, akimshinda mbunge wa chama cha Conservative Jacob Rees-Mogg.
Chama cha Labour kilimsimamisha kazi Norris mara moja kilipofahamishwa kuhusu kukamatwa kwake mwezi Aprili.
Licha ya kusimamishwa kwake, Norris amekataa kujiuzulu kutoka nafasi yake kama mbunge.
Ombi linalomtaka ajiuzulu limepata zaidi ya sahihi 2,000.
Norris kwa sasa ni mbunge huru lakini hajahudhuria Bunge la Commons tangu alipokamatwa.
Atapoteza nafasi yake kama mbunge ikiwa atashtakiwa, kuhukumiwa na kufungwa jela.
Norris pia alikuwa meya wa Magharibi mwa Uingereza alipokamatwa kwa mara ya kwanza. Muhula wake uliisha Mei 2025.
Polisi walisema uchunguzi wao kuhusu Norris ulianza Desemba 2024.
Pia unaweza kusoma:
Bei ya dhahabu na fedha yashuka
Bei ya dhahabu imeendelea kushuka kwa karibu 10% huku fedha nayo ikishuka kwa 15%.
Bei ya madini hayo zilipanda mwezi Januari baada ya wawekezaji kuwekeza kwa wingi katika madini hayo katika kile kinachoitwa mali "salama" kutokana misukosuko ya kisiasa na kiuchumi.
Lakini bei hiyo imeshuka siku ya Ijumaa baada ya Rais Donald Trump kumteua Kevin Warsh, gavana wa zamani wa benki kuu, kuwa mwenyekiti wake mpya.
Baada ya kushuka katika biashara ya Asia siku ya Jumatatu, dhahabu iliimarika na kufikia thamani ya dola za kimarekani 4,750 kwa wakia (gramu 28), ikishuka karibu 3% siku hiyo. Fedha pia iliimarika hadi dola $82 kwa wakia, ikishuka kwa 3.4%.
Kuteuliwa kwa Warsh siku ya Ijumaa kulipokelewa vyema kwa ujumla na masoko ya fedha na kusababisha ongezeko la 1% la thamani ya dola ya Marekani.
Sababu nyingine iliyotajwa ya kushuka thamani ya madini ni mabadiliko ya vigezo vya biashara ya madini kwenye soko kubwa, jambo lililofanya iwe tabu kwa wacheza kamari wa madini kufanya biashara.
Dhahabu ilipanda thamani na kufikia zaidi ya dola 5,500 kwa gramu 28 mwishoni mwa Januari mwaka huu, huku fedha pia ikifikia zaidi ya dola 120 kwa gramu 28.
Licha ya kushuka kwa kasi kwa bei ya dhahabu, bei hiyo imeshuka tu pale ilipokuwa wiki chache zilizopita na bado iko juu kwa takriban 70% kuliko ilivyokuwa wakati kama huu mwaka jana.
Pia unaweza kusoma:
Watu 80 waliotekwa nyara Nigeria warejea nyumbani baada ya kutoroka
Polisi wamethibitisha kuwa waumini kadhaa waliotekwa nyara na watu wenye silaha katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria wamerejea nyumbani wiki kadhaa baada ya kutekwa kwao.
Walikuwa miongoni mwa watu 177 waliotekwa mwezi uliopita kutoka makanisa matatu katika kijiji cha mbali cha Kurmin Wali.
Polisi wanasema watu hao 80 walitoroka siku hiyo hiyo waliyochukuliwa lakini wakajificha katika vijiji vya jirani kwa wiki mbili "kutokana na hofu ya kukamatwa tena," msemaji wa polisi wa jimbo hilo Mansur Hassan ameiambia BBC.
Serikali inasema juhudi zinaendelea kuhakikisha watu 86 waliobaki, wanaachiliwa. Shambulio hilo lilikuwa sehemu ya wimbi la utekaji nyara kwa ajili ya fidia, lakini hakuna kundi lililosema lilihusika na utekaji nyara huo.
Polisi awali walikanusha watu hao kutekwa nyara, hatimaye walithibitisha utekaji nyara huo Januari 21 baada ya wakazi wa eneo hilo kuripoti kwa BBC kwamba waumini 177 walitekwa nyara, huku 11 wakitoroka muda mfupi baadaye.
Mwezi Novemba, zaidi ya wanafunzi na waalimu 300 walichukuliwa kutoka shule ya Kikatoliki katika jimbo la Niger, ambalo ni jirani na Kaduna, kabla ya kuachiliwa katika makundi mawili.
Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama, ikiwa ni pamoja na uasi wa makundi ya Kiislamu kaskazini-mashariki, vurugu za wanaotaka kujitenga kusini-mashariki, na mapigano ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima katika maeneo ya kati kuhusu ardhi na maji.
Wataalamu wa usalama wanasema juhudi za kukabiliana na migogoro hii zinatatizwa na ufisadi, uhaba wa taarifa za kijasusi, na mafunzo duni ya vikosi vya polisi vya eneo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Mzozo juu ya ufadhili wasababisha baadhi ya shughuli za serikali kufungwa Marekani
Shughuli za serikali ya Marekani zimefungwa kwa siku ya tatu leo Jumatatu huku kukikosekana suluhisho baada ya chama cha Democratic kuweka mageuzi juu ya sera za uhamiaji kama takwa kwa makubaliano yoyote ya ufadhili wa shughuli za serikali.
Maseneta wa Democratic na Warepublican walikubaliana kuhusu miswada mitano ya matumizi siku ya Alhamisi, lakini wakaondoa muswada wa sita kuhusu ufadhili wa mwaka mzima kwa Wizara ya Usalama wa Nchi (DHS).
Badala yake, Seneti iliidhinisha ufadhili wa wiki mbili kwa DHS ambao unawapa wabunge muda zaidi wa kutatua mizozo kuhusu bajeti ya muda mrefu.
Chama cha Democratic kinataka mabadiliko katika operesheni za kuwasaka wahamiaji, ikiwa ni pamoja na kuwataka maafisa kuvaa kamera za kurikodi na kutovaa barakoa.
Ufadhili ulioidhinishwa na Seneti lazima upitishwe na Baraza la Wawakilishi kabla ya kwenda kwa Rais Donald Trump kwa ajili ya kutiwa saini.
Kifurushi cha Seneti kinajumuisha ufadhili kwa wizara ya ulinzi, wizara ya afya, hazina, mfumo wa mahakama ya shirikisho na mashirika mengine hadi mwisho wa mwaka wa fedha wa 2026 tarehe 30 Septemba.
Lakini ufadhili wa mashirika haya ya shirikisho uliisha saa sita usiku Jumamosi, na kusababisha kufungwa kwa sehemu ya shughuli zake, kwani Baraza la Wawakilishi bado halijaidhinisha.
Hata hivyo, athari zitakuwa ndogo, kwani huduma nyingi za serikali hazifanyi kazi mwishoni mwa wiki.
Kamati ya Kanuni za Bunge inatarajiwa kukutana Jumatatu alasiri ili kujadili mpango wa ufadhili.
Akizungumza na NBC News siku ya Jumapili, Mwakilishi wa Chama cha Democratic, California, Ro Khanna amesema anaunga mkono wenzake kupiga kura ya hapana kuhusu ufadhili wa DHS.
"Sioni sababu ya chama cha Democratic kupiga kura ya kuendelea na ufadhili wa ICE wakati wanawaua raia wa Marekani," alisema.
Mgogoro huo unakuja huku maelfu ya watu wakiandamana mitaani huko Minneapolis, kupinga operesheni dhidi ya wahamiaji ambazo zimesababisha hasira kubwa baada ya maafisa wa shirikisho kuwapiga risasi na kuwaua raia wawili wa Marekani.
DHS ni idara kubwa inayojumuisha mashirika mengi, ikiwa ni pamoja na Uhamiaji na Forodha (ICE), Forodha na Ulinzi wa Mipaka (CBP), Walinzi wa Pwani na Timu ya Ulinzi wa Viongozi (Secret Service).
Pia unaweza kusoma:
Mwanamuziki wa Nigeria afariki baada ya kuumwa na nyoka
Mwanamuziki chipukizi nchini Nigeria amefariki siku ya Jumamosi baada ya kuumwa na nyoka katika mji mkuu, Abuja.
Ifunanya Nwangene, mwenye umri wa miaka 26, alipata umaarufu baada ya kuonekana kwenye The Voice Nigeria 2021, shindano la kimataifa la uimbaji kwenye televisheni. Alijulikana kwa uhodari wake, kuchanganya jazz, opera, muziki wa kitamaduni na soul.
Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mhudumu wa Wanyama pori akimtoa nyoka kwenye nyumba yake, huku watu walio karibu wakisikika wakipiga kelele: "Ni nyoka aina ya cobra!"
Rafiki wa karibu, Sam Ezugwu, mwanzilishi mwenza na mkurugenzi wa Kwaya ya Amemuso ameiambia BBC, Nwangene alikuwa akipanga kuandaa tamasha lake la kwanza baadaye mwaka huu.”
Hillary Obinna, rafiki mwingine aliyeimba pamoja naye, ameiambia BBC kwamba aliambiwa alikuwa amelala wakati "aliposhtuka baada ya kuumwa na nyoka.”
Amesema nyoka wawili walipatikana ndani ya nyumba hiyo.
Kwanza alitafuta matibabu katika kliniki iliyo karibu lakini hawakuwa na dawa yoyote ya kuzuia sumu kwa hivyo alienda hospitalini.
Ezugwu anasema alikimbilia hospitalini Jumamosi baada ya kujua alikuwa amepelekwa huko. Alisema hospitali ilikuwa na aina moja tu ya dawa ya kuzuia sumu.
"Walipokuwa wakijaribu kumtuliza, hakuweza kuongea lakini aliweza kufanya ishara za mikono. Alikuwa akipata shida kupumua," aliongeza.
Ezugwu alisema aliendesha gari kwenda kutafuta dawa nyingine ya kuzuia sumu lakini akarudi na kugundua kuwa amefariki.
Alisema kwaya nzima ilienda hospitalini jioni hiyo, "ikitumaini muujiza ungetokea."
Katika taarifa, hospitali ilikana kwamba dawa ya kuzuia sumu haikuwepo na kusema madai hayo "hayana msingi na hayaonyeshi uhalisia wa hali ilivyokuwa."
Kituo cha Matibabu cha Shirikisho, Jabi kilisema Jumapili: "Wafanyakazi wetu wa matibabu walitoa matibabu ya haraka na yanayofaa, ikiwa ni pamoja na juhudi za kufufua mwili, dripu, oksijeni ndani ya pua, na dawa mchanganyiko ya kuzuia sumu ya nyoka."
Kituo hicho kinasema tathmini yao inaonyesha Nwangene amepata matatizo makubwa kutokana na kuumwa na nyoka. Hali yake ilizorota ghafla kabla ya kuhamishiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, na madaktari "hawakuweza kumfufua.”
Kifo cha Nwangene kimekuja huku kukiwa na mjadala mpya nchini Nigeria kuhusu ubora wa huduma za afya na usalama wa mgonjwa, kufuatia mfululizo wa madai ya uzembe katika kimatibabu.
Hizi ni pamoja na kifo cha hivi karibuni cha mwana wa mwandishi wa riwaya Chimamanda Ngozi Adichie mwenye umri wa miezi 21. Katika kesi hiyo, hospitali imekana kufanya makosa yoyote.
Kujibu kilio cha umma, waziri wa afya wa Nigeria amekiri "changamoto za kimfumo" katika mfumo wa afya na kutangaza kuundwa kwa kikosi kazi cha kitaifa kuchunguza "matibabu na usalama wa wagonjwa".
Waathiriwa wengi wa kuumwa na nyoka nchini Nigeria wanaaminika kuishi vijijini na Wanigeria wengi wameshtushwa na kifo cha Nwangene katika sehemu ya mji mkuu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema barani Afrika, watu 435,000 na 580,000 huumwa na nyoka kila mwaka.
Kuumwa na nyoka husababisha vifo 30,000 kila mwaka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ingawa baadhi ya makadirio yanaonyesha idadi halisi ni kubwa zaidi.
Pia unaweza kusoma:
Familia yatafuta majibu baada ya Mkenya aliyepigana upande wa Urusi kuuawa Ukraine
Familia moja nchini Kenya inatafuta majibu na usaidizi ili kuurudisha mwili wa ndugu yao mwenye umri wa miaka 29, ambaye aliuawa nchini Ukraine alipokuwa akipigana upande wa Urusi.
Clinton Nyapara Mogesa, mwenye umri wa miaka 29, aliondoka Kenya kwenda kufanya kazi Qatar mwaka 2024, na baadaye familia yake ikagundua kwamba alisafiri kwenda Urusi.
Siku ya Jumamosi, serikali ya Ukraine iliripoti kwamba alifariki huko Donetsk, mashariki mwa Ukraine, baada ya kuajiriwa nchini Qatar. Ukraine imesema Urusi haikuuchukua mwili wake, na alikuwa amebeba pasipoti za Wakenya wengine wawili.
Kifo chake kimekuja huku kukiwa na wasiwasi kuhusu Wakenya kuandikishwa kupigana vitani Ukraine.
Familia ya Mogesa iliiambia Citizen TV ya Kenya kwamba waliuza ardhi ili kumsaidia kupata pesa za kusafiri hadi Qatar kutafuta ajira.
"Kifo chake kimetushtua," kaka yake Joel Mogere aliambia kituo hicho. Amesema, Mogesa alikuwa mtoto wa mwisho na "mtoa matunzo kwa famili na tumaini la familia hii."
Mama yake, Mellen Moraa, amesema anaugua kisukari na mwanawe alikuwa akimlipia dawa na kumtunza, na anasema hajui la kufanya.
"Ninaomba serikali itusaidie," aliongeza.
Mwezi uliopita Serikali ya Kenya ilisema Wakenya 18 waliokuwa wakipigana nchini Urusi wameokolewa na kurejeshwa makwao.
Novemba iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Kenya alisema takriban Wakenya 200 wanapigania Urusi na mitandao ya kuajiri bado inaendelea.
Nchi zingine za Kiafrika zimeripoti visa vya vijana kupewa ofa za kazi zenye malipo makubwa nchini Urusi ambazo baadaye zilisababisha kuajiriwa jeshini.
Tathmini ya ujasusi ya Ukraine inakadiria kwamba zaidi ya watu 1,400 kutoka nchi 36 barani Afrika wameajiriwa kupigana upande wa Urusi.
Ukraine imeonya mara kwa mara kwamba mtu yeyote anayepigana upande wa Urusi atachukuliwa kama mpiganaji adui, huku njia salama ikiwa ni kujisalimisha.
Shirika la ujasusi la Ukraine siku ya Jumamosi liliwaonya raia wa kigeni dhidi ya kusafiri kwenda Urusi au kukubali ajira huko, hasa kazi zisizo rasmi au haramu.
Pia unaweza kusoma:
Kivuko cha Rafah kilichoko kati ya Gaza na Misri chafunguliwa
Wapalestina wameanza kutumia tena kivuko cha Rafah kilichoko kati ya Gaza na Misri.
Kivuko hicho kilikuwa kimefungwa kuanzia mwezi Mei 2024, baada ya eneo la Gaza kudhibitiwa na majeshi ya Israel.
Kufunguliwa kwa kivuko hicho ni mojawapo ya hatua za kutekeleza mkataba wa amani uliopendekezwa na Marekani na kuanza kutekelezwa mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita.
Ni watu wachache tu wameweza kuvuka pande zote mbili. Msaada wa kibinadamu na bidhaa za kuuzwa bado hazitaruhusiwa kuingia eneo hilo.
Takriban wapalestina 20,000 ambao wanaugua na waliojeruhiwa, wanasuburia kuondoka Gaza kutafuta matibabu.
Israel inasema wagonjwa 50 pekee ambão watakuwa wameambtana na jamaa wao wawili ndiyo watakuwa wakiruhusiwa kutoka Gaza kila siku, huku watu 50 kati ya maelfu waliotoroka Gaza ndiyo wataruhusiwa kurejea kila siku.
Shirika la afya duniani (WHO) ndilo litakuwa linasimamia mchakato wa kuwahamisha wagonjwa kutoka eneo linalodhibitiwa na Hamas hadi kuwavukisha eneo la pili linalodhibitiwa na wanajeshi wa Israel.
Waziri wa ulinzi wa Israeli Israel Katz, ameonya kuwa yeyote atakayevuka ‘mstari wa manjano’ ambao unaashiria eneo linalodhibitiwa na Israel, watakabiliwa vikali.
Kivuko cha Rafah kinasimamiwa na maafisa wa Umoja wa Ulaya na Wapalestina huku Israel ikifanya uchunguzi wa kiusalama.
Siku ya Jumapili, mamlaka za Israel zilisema jaribio la kufungua kivuko hicho lilikamilika vizuri.
Katika mpango wa vipengee 20 wa kumaliza vita eneo la Gaza uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani, unasema kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah utafuata utaratibu ule ule uliotekelezwa chini ya makubaliano ya awali yaliyoafikiwa mwaka uliopita.
Kabla ya uvamizi wa Israel, kivuko hicho kilikuwa njia ya pekee ya Wapalestina kukimbia eneo la Gaza, na njia muhimu ya kuingiza misaada ya kibinadamu.
Soma zaidi:
Tuzo za Grammy: Trump atishia kumshtaki mchekeshaji Trevor Noah
Rais Donald Trump amezomea hafla ya Jumapili usiku ya utoaji wa tuzo za Grammy, ambayo ilishuhudia wasanii kadhaa wakizungumza dhidi ya sera za wahamiaji katika utawala wake, na kutishia kumshtaki mchekeshaji Trevor Noah, ambaye alikuwa mshereheshaji ya tuzo za Grammy mwaka huu kutokana na mzaha alioufanya kuhusu madai ya uhusiano wa rais Trump na Jeffrey Epstein.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social, Trump aliandika: "Tuzo za Grammy ndiyo MBAYA ZAIDI, ambazo haziwezi hata kutazamwa."
"CBS ina bahati ya kutokuwa na takataka kama hii tena," alisema hivyo akirejelea Disney kuchukua haki za utangazaji wa sherehe ya tuzo hiyo kuanzia mwaka ujao.
Rais kisha akasema mzaha wa Noah, uliomaanisha alitumia muda wake katika kisiwa cha Epstein: "Noah alisema, Uwongo kunihusu, kwamba Donald Trump na Bill Clinton walitumia muda wao katika Kisiwa cha Epstein. SI KWELI!!!"
"Siwezi kumzungumzia Bill, lakini sijawahi kwenda Kisiwa cha Epstein, wala mahali popote karibu na hapo, na hadi taarifa ya uwongo na ya kuniharibia sifa usiku wa leo, sijawahi kushtumiwa kuwa huko, siyo hata na Vyombo vya Habari Bandia," ujumbe huo uliongeza.
Kisha Trump akamwonya Noah, akisema "ni bora aeleze ukweli wake kwa usahihi, na kuueleza ipasavyo na haraka," aliongeza: "Inaonekana kama nitawatuma wanasheria wangu kumshtaki mshereheshaji huyu maskini, mwenye kusikitisha, asiye na kipaji, na mlaghai"
Rais alisema atamshtaki mchekeshaji huyo amlipe pesa "nyingi", huku akinukuu makubaliano ya kifedha aliyopata kutoka ABC na CBS na kuandika: "Jiandae Noah, tutapambana!".
Pia unaweza kusoma:
Mkanganyiko juu ya mgomo wa magari ya umma washuhudiwa Nairobi
Abiria wamekwama leo asubuhi Jumatatu huku mkanganyiko kuhusu mgomo wa Magari ya Huduma za Umma (PSV) ukisababisha msongamano mkubwa wa magari jijini Nairobi.
Baadhi ya matatu zimezuiwa katika barabara kadhaa kama vile ya Outering huko Kariobangi na pia Jogoo road.
Usumbufu huo umesababisha msongamano na abiria kuchelewa kupata usafiri huku madereva na abiria waliokata tamaa wakijitahidi kutafuta njia mbadala.
"Kuna watu wa matatu ambao wanabeba abiria lakini ukiingia mjini kuna hali ya wasiwasi kidogo," abiria mmoja aliyezungumza na BBC amesema.
Polisi wameshuhudiwa katika barabara mbalimbali za mjini wakishika doria.
Ilani ya mgomo huo imetolewa huku kukiwa na mvutano unaoendelea kati ya waendeshaji wa matatu na mamlaka za uchukuzi kuhusu wasiwasi wa usalama na kuongezeka kwa matukio ya unyanyasaji kutoka kwa waendeshaji boda boda.
China yawanyonga watu 4 zaidi wa genge la kimafia la Myanmar
China imewanyonga watu 4 wa familia ya kimafia ya Bai, moja ya zinazojulikana kumiliki vituo vya kuwalaghai watu nchini Myanmar, kulingana na chombo cha habari cha eneo.
Wanne hao walikuwa miongoni mwa wanafamilia 21 na washirika wao wa karibu, walipatikana na hatia ya kuwalaghai watu, mauaji, kuwajeruhi watu miongoni mwa uhalifu mwingine na mahakama ya wilaya ya Guangdong.
Mwezi Novemba mwaka uliopita, mahakama iliwapa hukumu ya kifo watu watano wa familia hiyo ikiwemo kiongozi wa ukoo huo Suocheng, ambaye alifariki baada ya hukumu hiyo.
Wiki iliyopita China iliwanyonga jamaa 11 wa familia ya kimafia ya Ming, ambao wamekuwa wakiwalaghai watu na operesheni zao zakihalifu Kusini mashariki mwa bara Asia.
Kwa miaka kadhaa, familia za Bais, Ming, na zinginezo za kimafya zimekuwa zikiendesha mji wa Laukkaing, ambapo wanamiliki vituo vya kuchezea kamari, biashara ya ngono na ulaghai wa mitandao.
Maafisa walisema kwamba kundi la Bais, ambalo linadhibiti wanamgambo wao, lilianzisha vituo 41 vya kuendesha shughuli za ulaghai wa mtandaoni na kasino, mamlaka ilisema.
Ndani ya vituo hivyo kulikuwa na utamaduni wa vurugu, ambapo vipigo na mateso yalikuwa jambo la kawaida.
Mahakama ilisema shughuli za uhalifu za familia ya Bai zilisababisha vifo vya raia sita wa China, mtu mmoja kujiua na majeruhi kadhaa.
Familia ya Bai ilipata umaarufu eneo la Laukkaing mwaka wa 2000, baada ya kiongozi wa genge lililokuwa eneo hilo kuondolewa baada ya oparesheni ya kijeshi iliyoongozwa na Min Aung Hlaing, ambaye ndiye kiongozi wa kijeshi wa serikali ya Myanmar kwa sasa.
Soma zaidi:
Mzozo wa Marekani na Iran: Trump ajibu onyo la Khamenei
Akijibu onyo la Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei kwamba shambulio lolote la Marekani dhidi ya Iran litasababisha mzozo wa kikanda,
Rais wa Marekani Donald Trump amejibu onyo la kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei kwamba shambulio lolote la Marekani dhidi ya Iran litasababisha mzozo wa kikanda, na kusema kuwa "Unatarajia aseme nini? Ni kawaida kabisa kwamba angesema hivyo. Tuna meli kubwa na zenye nguvu zaidi duniani huko, karibu sana; siku mbili hadi tatu na tunatumaini tutafikia makubaliano. Na ikiwa hatutafikia makubaliano, basi tutaona kama yuko sahihi au la".
Khamenei alikuwa ameonya leo kwamba shambulio lolote dhidi ya Iran litasababisha mzozo wa kikanda, akisisitiza kwamba Iran "sio mwanzilishi wa vita" na haina nia ya kushambulia nchi yoyote, lakini alisisitiza kuwa "watu wa Iran watajibu vikali kwa yeyote anayeshambulia au kusumbua nchi yao".
Bunge la Iran pia lilitangaza Jumapili kwamba Iran inayaona majeshi ya nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimeorodhesha Kikosi cha Iran cha Islamic Revolutionary Guard Corps kwenye orodha ya mashirika ya kigaidi ya kambi hiyo kuwa "makundi ya kigaidi".
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump alizungumzia mawasiliano kati ya Iran na Washington, huku kukiwa na vitisho vya Marekani vya kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
Soma zaidi:
Hali ya hofu Tanzania: BBC Africa Eye yachunguza matukio ya watu kutekwa
#BBCAfricaEye inachunguza wimbi la watu kutoweka linaloeneza hofu kote Tanzania.
Samia Suluhu alipokuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania mwaka 2021, baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake akiwa madarakani, kulikuwa na matumaini kwamba urais wake ungesaidia kuvunja kwa utawala wa kiimla.
Aliondoa marufuku ya mikutano ya vyama vya upinzani, akaruhusu vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru zaidi, na akatoa wito wa ushirikiano na ujumuishaji mpana wa kisiasa.
Hata hivyo, matumaini ya mabadiliko ya kudumu yalififia haraka.
Kuanzia viongozi wa upinzani na watetezi wa haki za binadamu, hadi wasanii na hata wanachama wa chama tawala chenyewe, msako mkali usio na kifani dhidi ya wakosoaji wa serikali umeitikisa Tanzania.
Kupitia ushuhuda mzito wa manusura wa utekaji nyara na mateso, Wakisimulia tena kwa undani mambo ya kutisha waliyopitia filamu hii inafichua kampeni ya vitisho na hofu ambayo wakosoaji wa serikali wanavumilia nchini.
Serikali ya Tanzania iliambia BBC kuwa haijawahi kujihusisha na utekaji nyara na haijawahi kumtafuta mtu yeyote ambaye ni mkosoaji wa serikali.
Bonyeza link hiyo chini ili utazame filamu hiyo ya uchunguzi kupitia ukurasa wetu wa YouTube.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza ażuru Ethiopia kujadili uhamiaji haramu
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Yvette Cooper, yuko ziarani nchini Ethiopia, katika juhudi za kutaka kupunguza wahamiaji haramu wanaotoka pembe ya Afrika wakijaribu kuingia Uingereza.
Cooper amesema, kutengeneza nafasi za ajira nchini humo kutasaidia kupunguza watu kuhama taifa hilo na pia kuwekwa kwa sheria ambazo zitadhibiti magenge yanayoendeleza biashara haramu ya ulanguzi wa watu.
Waziri huyo aidha aliahidi kuwa wahamiaji ambao hawana vibali vya kuishi Uingereza, watarejeshwa Ethiopia.
"Tunashirikiana pamoja kukabiliana na changamoto za kiuchumi, ambazo zinachangia watu kuhama taifa hilo, na pia magenge yanayofaidika na biashara hiyo haramu." amesema Cooper.
"Hii inakuja na ushirikiano mpya wa kuimarisha biashara, na kutengeneza nafasi za ajira nchini Ethiopia, ili watu waweze kupata maisha bora bila kuhatarisha yao."
Serikali tofauti za Uingereza zimejaribu kukabiliana na uhamiaji haramu bila mafanikio.
Takriban 30% ya wanaotumia kivuko cha Uingereza kuingia nchini humo kwa boti ndogo, wengi wao ni raia wa Ethiopia, Eritrea, Somalia na Sudan.
Soma zaidi:
M23 yaitaka Congo kutoingiza siasa katika vifo vya wachimba migodi Rubaya
Waasi wa kundi la M23, wameishtumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa kugeuza vifo vya wachimba migodi kuwa suala la kisiasa.
Mwisho wa wiki iliyopita, watu mia mbili walifariki eneo la Rubaya nchini DRC baada ya kuporomoka kwa mgodi mmoja eneo hilo.
Katika taarifa yao, kundi la waasi la M23, limesema kuwa serikali ya Kinshasa inakwepa majukumu ya kuwajibikia vifo hivyo kutokana na utepetevu wao.
Msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka, alisema kumekuwa na vifo vingi ambavyo vimetokana na migodi kuporomoka hapo awali, ila idadi kamili ya waliofariki bado haijulikani, na bado serikali haijashughulikia suala la usalama wa migodi.
“Badala ya kufanya swala hili kuwa la kisiasa, serikali inafaa kushughulikia mapungufu yake.” alisema Kanyuka.
Kundi hilo linasema vifo katika migodi ya Rubaya, vilitokana na maporomoko ya ardhi, baada ya mvua kubwa kunyesha na kusema kuwa watasimamia matibabu ya waliojeruhiwa.
Kundi la waasi wa M23, liliuteka mji wa Rubaya mwaka wa 2024 na wamekuwa wakisimamia shughuli za kuchimba madini eneo hilo, licha ya serikali kupiga marufuku.
Juhudi za kudumisha amani mashariki mwa DRC bado hazijafua dafu, kutokana na mivutano kati ya makundi yaliyojihami na serikali ya taifa hilo.
Soma zaidi:
Watu 12 wafariki katika shambulio la basi Ukraine
Ndege isiyo na rubani inayomilikiwa na Urusi, ilishambulia basi moja ambalo lilikuwa limewabeba wafanyikazi wa migodini mashariki ya kati ya eneo la Dnipropetrovsk.
Shambulio hilo la hapo jana liliwauwa watu 12 waliokuwa kwenye basi hilo lililokuwa karibu na maeneo ya Ternivka, mji ulioko kilomita 65, kutoka enela vita, kulingana na polisi wa eneo hilo.
Kampuni ya nishati ya DTEK nchini Ukraine, imesema wale waliouawa walikuwa wafanyikazi wa kampuni hiyo, ambao walikuwa wamemaliza zamu yao ya kazi.
Shambulio hilo lilitokea wakati ambapo kumekuwa na makubaliano ya kupunguza mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine.
Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametangaza kuwa vita hivyo viko karibu kumalizika, na kuongezea kuwa Rais Putin wa Urusi alikuwa amekubali kusitisha mashambulizi kutokana na hali ya baridi inayoshuhudiwa kwa sasa.
Mapema Jumapili, ndege isiyo na rubani ilishambulia hospitali moja ya kujifungua kina mama eneo la Zaporizhzhia, na kuwajeruhi wanawake saba waliokuwa wakipokea matibabu.
Soma zaidi:
Jeshi la Nigeria lamuua kamanda mmoja wa Boko Haram
Wanajeshi wa Nigeria wamefanya operesheni ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram, kaskazini mwa taifa hilo na kumuua kamanda mmoja na wapiganaji wengine kumi wa kundi hilo.
Operesheni hiyo ilifanyika katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Jeshi la Nigeria lilimuwinda kamanda wa kundi hilo la Boko Haram, Abu Khalid, ambaye alikuwa amejificha katika msitu wa Sambisa na kumuangamiza pamoja na wapiganaji wake.
Khalid alikuwa anashikilia nafasi ya pili katika uongozi wa kundi la Boko Haram, na alikuwa anaongoza oparesheni nyingi za kundi hilo.
Katika jimbo la Zamfara, wanajeshi wa Nigeria waliweza kuzuia shambulio dhidi ya raia kutoka kwa makundi yaliyojihami.
Soma zaidi: