Nyoka hutoa ishara gani anapokaribia kuuma?

7 Septemba 2023 Vipul mwenye umri wa miaka 17, alikuwa amelala katika nyumba yao huko Surendranagar, India na ghafla alihisi kitu kinagusa mkono wake.

Alipoamka kutoka usingizini, Vipul alihisi ndoano iligonga mkononi mwake. Lakini akarudi kulala. Lakini ghafla mama yake alimuona nyoka kitandani kwake na kuita kila mtu. Ilichukua muda wa saa mbili na nusu hadi tatu kumfikisha Vipul hospitalini kwa matibabu. Na muda mfupi baadaye Vipul alifariki.

Matukio ya watu kuumwa na nyoka huongezeka wakati wa pepo za mvua, hasa katika maeneo ya vijijini. Ukiumwa na nyoka kuna uwezekano mkubwa wa kufa ikiwa hutatibiwa haraka.

Je, nyoka huuma wakati gani?

Karmsheel Dharmendra Trivedi, mfanyakazi wa kuokoa nyoka katika makazi ya binadamu na kujenga ufahamu kwa umma kuwahusu kwa miaka 38, anasema:

"Hupaswi kumwogopa nyoka, kwa sababu nyoka wanatuogopa sisi binadamu. Kuchukua tahadhari na kukuza uelewa wa tabia ya nyoka kunaweza pia kuzuia kuumwa na nyoka.”

"Sumu ni silaha ya kuwinda ya nyoka, ambayo huitumia kwenye mawindo yake kwa ajili ya chakula. Kwa hivyo sumu ya nyoka ni muhimu kwa nyoka na wanaitumia kwa uangalifu sana. Humuuma binadamu kama njia ya mwisho ikiwa hana njia nyingine ya kutoroka. Usimtanie nyoka na ikiwa huogopi uwepo wake, atapita kimya kimya kwenye miguu yako."

Dharmendra Trivedi anafafanua zaidi, "tunajua kwamba majira ya baridi ni kipindi cha kujificha kwa nyoka. Kisha hutoka wakati wa kiangazi na hapo ndipo huzaliana na kutaga mayai."

“Mayai huanguliwa. Katika majira ya monsuni, vyura, panya, mijusi, wadudu na wanyama ambao ni chakula cha nyoka hupatikana kwa urahisi, hivyo nyoka huwapata ndani au karibu na nyumba za watu."

Akizungumzia kuhusu tabia ya nyoka, mtaalamu wa magonjwa ya wanyama kutoka Jabalpur, Vivek Sharma anasema, “kuumwa na nyoka hutokea katika sehemu za nyumba ambapo kuna giza au mwanga mdogo kama vile jikoni, ama stoo.

Pia, mahali ambapo nyoka hula, kama vile dampo za takataka – huko kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na mijusi, vyura, au panya, kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kuumwa na nyoka mahali kama hapo."

Anasema, “ni mara chache sana utamwona nyoka akivuka chumba kimoja kwenda kingine. Nyoka hupendelea maeneo yenye giza na yenye mwanga hafifu. Wanakuja kutafuta kimbilio katika maeneo kama hayo.”

Nyoka huonya kabla ya kuuma

Dharmendra Trivedi anasema, “wapo aina ya nyoka ambao hutoa onyo kabla ya kuuma. Anapoonesha meno yake, hutoa sauti ya psii na anapojizungusha na mwili wake kugusana. Ikiwa unaelewa ishara hizi tatu za tabia ya nyoka, unaweza kujiokoa. Lakini nyoka mweusi hatoi onyo na anakuuma moja kwa moja.”

“Nyoka wa kawaida wanaweza kuonekana na kuuma wakati wowote wa mchana au usiku. Lakini nyoka weusi mara nyingi hutoka nje usiku na kuuma.”

Dhamendra anazidi kueleza, “meno ya nyoka ni kama sindano. Sumu ya nyoka huingia mwilini kwa njia hizi tatu - ndani ya misuli, ndani ya mshipa na kati ya tabaka mbili za ngozi.”

“Wakati wowote nyoka anapouma, bila hata kuchelewa kwa dakika moja, nenda hospitali au kwa daktari mzoefu kwa matibabu. Usikimbilie kwenda kwenye hekalu au kwenye sherehe ya kuondoa sumu ya nyoka. Huo ni upuuzi.”

Sumu yake huathirije mwili?

Dkt. Hemang Doshi - amekuwa akitibu watu wanaoumwa na nyoka kwa miaka mingi, anasema, "sumu ya kobra na nyoka mweusi ni sumu inayoathiri mishipa ya fahamu na aina nyingine ya nyoka huathiri damu.

Sumu inayoathiri mfumo wa fahamu huleta dalili kama vile kupooza, ugumu wa kupumua. Sumu inapoathiri mfumo wa mzunguko wa damu, hiyo inamaanisha kuwa sumu huchanganyika kwenye damu na kusababisha kuvuja kwa damu (kupasuka kwa mishipa ya damu) katika sehemu za ndani ya mwili."

“Nyoka anapouma, athari ya sumu yake huanza kuonekana kwenye mwili ndani ya dakika 10-15. Dakika 30-45 athari ya nguvu ya sumu inakuwa ya juu. Ikiwa umeumwa na nyoka mweusi, sumu yake huchukua saa moja na nusu hadi saa mbili - sumu yake kuanza kuathiri na athari huwa ya juu ndani ya masaa manne hadi sita.”

Kaka yake Vipul Sagar Koli, ambaye alikufa kwa kuumwa na nyoka anasema, "ndugu yangu aliumwa na nyoka mwendo wa 12 au 12:30. Tulijua baada ya saa moja. Alipoanza kukosa pumzi tulimpeleka kwa daktari.

Ilituchukua saa mbili na nusu hadi saa tatu na nusu kufika hospitali, kutokana na hilo daktari alishindwa kumuokoa kwani muda ulikuwa umeyoyoma.”

Chukua tahadhari

Badala ya kutibu kuumwa na nyoka, watu wanaoishi katika maeneo yenye hatari - wanapaswa kufuata tabia rahisi ili kuepuka kuumwa na nyoka.

Watu wanaolala nje au katika nyumba za vijijini wanapaswa kulala na vyandarua. Vyandarua hulinda sio tu kutoka kwa mbu bali pia kutokana na kuumwa na nyoka. Hili ni suluhisho rahisi na lenye ufanisi.

Kabla ya kwenda kwenye nyumba yenye giza au yenye mwanga hafifu au sehemu za nje, chukua tochi mkononi mwako na uiwashe na uangalie vizuri. Tikisa, piga hodi, na uangalie vizuri kabla ya kuweka mkono wako mahali patupu ambapo macho yako hayaoni.

Makati wa kwenda mashambani au bustanini, vaa buti na ikiwa kitu kimeangukia kichakani, usipeleke mkono bila kuangalia. Kuumwa na nyoka kunaweza kuepukika kwa tahadhari chache tu.