Maoni: Utawala wa kimabavu huporomoka polepole, lakini wa Iran haujafikia huko

Muda wa kusoma: Dakika 5

Utawala wa kimabavu huporomokaje? Ernest Hemingway anasema - huporomoka polepole kisha ghafla.

Waandamanaji nchini Iran na wafuasi wao nje ya nchi wana matumaini kwamba utawala wa Kiislamu jijini Tehran uko katika hatua ya kuporomoka.

Wiki mbili za machafuko zimeongeza mgogoro mkubwa kwa utawala. Ingawa hii si mara ya kwanza kwa Wairan kuandamana, lakini maandamano haya yanakuja baada ya Iran kupigwa vibaya na Marekani na Israel.

Katika pigo la hivi karibuni kwa uchumi wa Iran, vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa na Umoja wa Mataifa chini ya makubaliano ya nyuklia ya 2015 ambayo sasa yamekufa, vimerudishwa tena na Uingereza, Ujerumani na Ufaransa mwezi Septemba.

Mwaka 2025, mfumuko wa bei ya chakula ulikuwa zaidi ya 70%. Sarafu, rial, ilifikia kiwango cha chini kabisa mwezi Desemba. Watu wa Wairan wanaohangaika kulisha kulisha familia zao ni kutoka na vikwazo hivi.

Ingawa utawala wa Iran uko chini ya shinikizo kubwa, ushahidi unaonesha, hauko hauko karibu na kuporomoka.

Nani anailinda Iran?

Vikosi vya usalama bado ni tiifu. Tangu mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, serikali ya Iran imetumia muda na pesa kuunda mtandao wa kikatili wa ukandamizaji.

Katika wiki mbili zilizopita, vikosi vya serikali vilitii amri ya kuwapiga risasi raia wenzao mitaani. Matokeo yake ni kwamba maandamano ya wiki chache zilizopita yameisha - kwa kadiri tunavyoweza kujua katika nchi ambayo watawala wanaendelea kuzima mawasiliano.

Mkandamizaji mkubwa wa maandamano ni Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Irai (IRGC), kikosi muhimu zaidi.

Kina jukumu mahususi la kutetea itikadi na mfumo wa serikali ya mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, kinasimamiwa moja kwa moja na kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei.

IRGC inakadiriwa kuwa na watu kama 150,000 walio na silaha, wanaofanya kazi sambamba na jeshi la kawaida la Iran.

Mchanganyiko wa madaraka, pesa, ufisadi na itikadi, inamaanisha kuwa IRGC ina kila sababu ya kutetea mfumo huo

IRGC ina kikosi cha usaidizi, wanamgambo wa Basij, wa kujitolea. Kuna mamilioni ya wanachama wa Basij. Makadirio mengine kutoka magharibi yanasema wanachama wake wako kwenye maelfu, bado ni idadi kubwa sana. Basij wako mstari wa mbele katika ukandamizaji dhidi ya waandamanaji kwa niaba ya utawala.

Niliwaona IRGC na Basij katika shughuli zao hatua huko Tehran mwaka 2009, walipokuwa wakijaribu kuvunja maandamano makubwa baada ya uchaguzi wa rais uliokuwa na utata. Basij walijipanga mitaani wakiwa na marungu.

Nyuma yao kulikuwa na wanaume waliovaa sare wakiwa na silaha za moto. Vikosi vya pikipiki vikizunguka Tehran, kuvishughulikia vikundi vilivyokuwa vikijaribu kuandamana.

Katika kipindi cha chini ya wiki mbili, maandamano ambayo yaliziba mitaa yalipunguzwa hadi vikundi vidogo vya wanafunzi wakiimba na kuchoma moto vishungu vya takataka.

Tehran itasalimu amri?

Uwezo wa ikosi vya usalama kudhiti maandamano, haimaanishi kwamba kiongozi mkuu au maluteni wake watapumzika. Rais wa Marekani Donald Trump bado anatishia kuchukua hatua. Mamilioni ya Wairani wanaotaka kuanguka kwa utawala wamejawa na chuki na hasira.

Huko Tehran, serikali na kiongozi mkuu wanaonekana kutafuta njia za kupambana na shinikizo wanalokabiliana nalo. Kauli kali za utawala zimechanganywa na ofa ya kutaka kuanza tena mazungumzo na Marekani.

Ni vigumu kuona jinsi pande hizo mbili zinavyoweza kufikia makubaliano kuhusu mipango ya nyuklia ya Iran na mpango wa makombora ya masafa marefu baada ya kushindwa katika raundi za awali za mazungumzo.

Lakini mazungumzo yanaweza kuipa muda Iran, hasa ikiwa Trump anaweza kushawishika kwamba makubaliano yanawezekana.

Kama sehemu ya kampeni yake ya shinikizo, Trump anasema ataweka ushuru wa 25% kwa bidhaa za nchi yoyote inayofanya biashara na Iran. Ingawa ni vigumu kuona ushuru huo unavyoweza kufanya kazi. China hununua mafuta mengi ya Iran.

Trump na Rais wa China Xi Jinping walikubaliana kusitisha vita vyao vya kibiashara msimu uliopita wa vuli, huku mkutano wa kilele ukitarajiwa kufanyika Beijing mwezi Aprili.

Mkutano huo utashughulikia masuala makubwa zaidi yanayokabili mataifa mawili makubwa duniani. Je, Trump atahatarisha au kuvuruga mkutano huo ili tu kuendelea na shinikizo dhidi ya Iran?

Huko Tehran, kipaumbele kikubwa kwa Kiongozi Mkuu anayezeeka Ayatollah Khamenei ni kulinda mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu. Maandamano yatajibiwa vikali.

Faida kwa utawala huo ni ukosefu wa uongozi thabiti miongoni mwa waandamanaji. Mwana mkubwa wa Shah aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi karibu nusu karne iliyopita amekuwa akijaribu kuwa kiongozi. Mvuto wake unaonekana kufifishwa na historia ya familia yake na uhusiano wake wa karibu na Israel.

Jambo moja ambalo linaweza kuwatia wasiwasi viongozi wa kidini na wanajeshi huko Tehran linatoka kwa mshirika wao wa zamani, Rais wa zamani Bashar al-Assad wa Syria.

Alionekana kama ameshinda vita, na polepole na Saudi Arabia na Umoja wa Kiarabu walikuwa wakijaribu kumrudisha katika jukwaa la kimataifa, pale alipokabiliwa na shambulio la waasi lililopangwa vizuri mwishoni mwa 2024.

Urusi na Iran, washirika wake wawili muhimu zaidi hawakuwa tayari au labda hawakuweza kumwokoa. Ndani ya siku chache, Assad na familia yake walisafiri kwa ndege kwenda uhamishoni Moscow.

Utawala wa kimabavu huporomoka polepole, kisha ghafla. Utawala wa Assad ulipoanguka, ulianguka kwa kasi sana. Mfano mwingine ambao Tehran inaweza kuutazama, ni anguko la Rais Ben Ali wa Tunisia mwaka 2011, wakati jeshi lilipoamua kuwalinda waandamanaji dhidi ya vikosi vya usalama vya ndani.

Kuanguka kwa Ben Ali kulisababisha kujiuzulu kwa Hosni Mubarak wa Misri. Huenda angenusurika na maandamano makubwa kama jeshi lisingeamua kwamba ili kuokoa nafasi zao inabidi yeye aondoke.

Je, hilo linaweza kutokea nchini Iran?

Wapinzani wa utawala wa Kiislamu wana matumaini kwamba shinikizo zaidi ndani na nje ya nchi na kuibuka kwa uongozi, utawezesha kuporomoka polepole kisha ghafla.