Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni nchi zipi zinaweza kulengwa na Trump baada ya Venezuela?
- Author, Tom Bennett
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Muhula wa pili wa Rais wa Marekani, Donald Trump, unaendelea kuundwa kwa misingi ya malengo yake ya sera za kigeni.
Hatua zake za hivi karibuni zinaonyesha mwelekeo wa matumizi ya nguvu katika kulinda maslahi ya Marekani katika maeneo yanayoonekana kuwa ndani ya ushawishi wake.
Akiwa ametekeleza vitisho vyake dhidi ya Venezuela, Trump alisimamia operesheni ya kushtukiza iliyofanyika usiku katika mji mkuu Caracas, ambapo rais wa nchi hiyo pamoja na mke wake walikamatwa kutoka katika makazi yao yaliyoimarishwa kwa ulinzi mkali.
Akielezea operesheni hiyo, Trump alirejea Azimio la Monroe la mwaka 1823, lililoweka msingi wa ukuu wa Marekani katika ulimwengu wa Magharibi, na kulipa tafsiri mpya kwa kulitaja kama "Donroe Doctrine".
Haya ni baadhi ya mataifa ambayo Trump ameyapa onyo au kauli kali dhidi yao katika siku za hivi karibuni.
Greenland
Marekani tayari ina kambi ya kijeshi nchini Greenland, inayojulikana kama Kituo cha Anga cha Pituffik. Hata hivyo, Trump ameonyesha nia ya kutaka udhibiti wa kisiwa chote.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa Greenland ni muhimu kwa usalama wa taifa la Marekani, akidai kuwa eneo hilo limejaa meli za Urusi na China.
Greenland, kisiwa kikubwa cha Aktiki kilicho sehemu ya Ufalme wa Denmark, kiko takribani kilomita 3,200 kaskazini-mashariki mwa Marekani. Kina utajiri mkubwa wa madini adimu yanayotumika katika teknolojia za kisasa, zikiwemo simu janja, magari ya umeme na vifaa vya kijeshi. Kwa sasa, uzalishaji wa madini hayo nchini China unazidi kwa mbali ule wa Marekani.
Zaidi ya hilo, Greenland ina nafasi muhimu ya kimkakati katika Bahari ya Atlantiki ya Kaskazini, ikitoa njia ya kuelekea eneo la Aktiki. Kadri barafu za ncha ya dunia zinavyoendelea kuyeyuka, njia mpya za usafirishaji wa baharini zinatarajiwa kufunguliwa.
Waziri Mkuu wa Greenland, Jens Frederik Nielsen, alitupilia mbali wazo la udhibiti wa Marekani, akilielezea kama dhana isiyo na uhalisia.
"Hakuna shinikizo tena. Hakuna minong'ono zaidi. Hakuna dhana zaidi ya kuhusishwa. Tuko wazi kwa mazungumzo. Tuko wazi kwa majadiliano. Lakini hii lazima ifanyike kupitia njia zinazofaa na kwa kuheshimu sheria za kimataifa," alisema.
Colombia
Saa chache baada ya operesheni nchini Venezuela, Trump alimkosoa vikali Rais wa Colombia, Gustavo Petro, kwa kauli ya tahadhari kali.
Colombia, jirani wa magharibi wa Venezuela, ina akiba kubwa ya mafuta na ni mzalishaji muhimu wa dhahabu, fedha, zumaridi, platinamu na makaa ya mawe. Pia ni kitovu kikuu cha biashara ya dawa za kulevya katika eneo la Amerika ya Kusini, hususan kokeini.
Tangu Marekani ilipoanza kushambulia boti katika Bahari ya Karibiani na Pasifiki ya mashariki mwezi Septemba mwaka 2025, ikidai kuwa zilikuwa zikisafirisha dawa za kulevya, mvutano kati ya Trump na rais huyo wa mrengo wa kushoto umeongezeka.
Mwezi Oktoba, Marekani iliweka vikwazo dhidi ya Petro, ikimtuhumu kwa kuruhusu magenge ya dawa za kulevya kustawi.
Akizungumza ndani ya ndege ya Air Force One, Trump alisema Colombia inaendeshwa na kiongozi "asiye na afya ya akili" anayehusika na uzalishaji na uuzaji wa kokeini kwa Marekani.
Aliongeza kuwa hali hiyo haitadumu kwa muda mrefu. Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa operesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia, alijibu kuwa wazo hilo "lina mvuto kwake".
Kwa muda mrefu, Colombia imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika vita dhidi ya dawa za kulevya, ikipokea msaada mkubwa wa kijeshi kila mwaka.
Iran
Iran kwa sasa inashuhudia maandamano makubwa ya kupinga serikali. Trump ameonya kwamba iwapo waandamanaji zaidi watauawa, mamlaka ya Iran itakabiliwa na 'mashambulizi makali' kutoka Marekani.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema Marekani inafuatilia hali hiyo kwa karibu na haitasita kuchukua hatua ikiwa historia ya ukandamizaji itajirudia.
Ingawa Iran iko nje ya wigo wa kijiografia wa "Donroe Doctrine", Trump ameendelea kuitaja kama tishio, hasa baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran mwaka uliopita.
Mashambulizi hayo yalifuatia operesheni ya Israel iliyolenga kudhoofisha uwezo wa Iran kutengeneza silaha za nyuklia, hali iliyoishia katika mgogoro wa siku 12 kati ya Iran na Israel.
Katika mkutano wa hivi karibuni huko Mar- Alago kati ya Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, suala la Iran lilitajwa kuwa kipaumbele, huku kukiwa na taarifa za uwezekano wa mashambulizi mapya mwaka 2026.
Mexico
Kupanda kwa Trump madarakani mwaka 2016 kulihusishwa kwa kiasi kikubwa na sera zake kali kuhusu uhamiaji, hususan wito wa kujengwa kwa ukuta mpakani mwa Mexico.
Aliporejea madarakani mwaka 2025, siku yake ya kwanza ofisini alisaini amri ya kubadili jina la Ghuba ya Mexico na kuiita "Ghuba ya Amerika".
Trump mara kwa mara amedai kuwa Mamlaka za Mexico hazifanyi vya kutosha kuzuia uingizaji wa dawa za kulevya na wahamiaji haramu nchini Marekani. Akizungumza Jumapili, alisema dawa za kulevya zinaingia kwa wingi kupitia Mexico na kwamba 'Marekani italazimika kuchukua hatua.'
Hata hivyo, Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, amepinga waziwazi uwezekano wa operesheni ya kijeshi ya Marekani ndani ya ardhi ya Mexico.
Cuba
Cuba, taifa la kisiwa lililo umbali mfupi kusini mwa Florida, limekuwa chini ya vikwazo vya Marekani tangu miaka ya 1960. Limekuwa na uhusiano wa karibu wa kisiasa na kiuchumi na Venezuela chini ya utawala wa Nicolás Maduro.
Trump alisema Jumapili ya tarehe 4 Januari 2026 kuwa uingiliaji wa kijeshi hauonekani kuwa wa lazima, akidai kuwa 'Cuba iko tayari kuanguka'.
"Sidhani tunahitaji hatua yoyote dhidi yao", alisema. "Inaonekana inadhoofika."
"Sijui kama watamudu hali, lakini Cuba sasa haina mapato," aliongeza.
"Walipata mapato yao yote kutoka Venezuela, kutoka kwa mafuta ya Venezuela."
Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 30 ya mafuta ya Cuba hutoka Venezuela, hali inayoiweka nchi hiyo katika hatari endapo usambazaji huo utasitishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye asili yake ni ya wahamiaji wa Cuba, kwa muda mrefu amekuwa akiunga mkono mabadiliko ya utawala nchini humo, akiwaambia wanahabari Jumamosi: "Kama ningeishi Havana, na ningekuwa serikalini, ningekuwa na wasiwasi - angalau kidogo".
"Rais Trump anapozungumza mnapaswa kumchukulia kwa uzito," alisema.