Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Cilia Flores ni nani, na sababu za kukamatwa kwake akiwa na Maduro ni zipi?
- Author, Tom Bennett
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakati majeshi ya Marekani yalipofanya uvamizi wa usiku katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas, hawakumtoa tu Rais Nicolás Maduro kutoka makazi yake na kumsafirisha hadi New York, bali walimkamata pia mke wake.
Cilia Flores, mwenye umri wa miaka 69, kwa muda mrefu ametambulika kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Venezuela.
Akiwa mwanasiasa mahiri kwa haki yake mwenyewe, amekuwa na mchango mkubwa katika kuunda mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo kwa miongo kadhaa.
Baada ya kuliongoza Bunge la Taifa la Venezuela kwa miaka kadhaa, Flores alisaidia kuimarisha mamlaka ya mume wake kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2013.
Akiwa Mke wa kiongozi wa ngazi ya juu Venezuela , Rais Maduro alimpa jina la heshima la "Mpiganaji wa Kwanza." Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa alichagua kubaki nyuma ya pazia, akijenga taswira ya kifamilia zaidi ya utawala ambao wakosoaji wake wamekuwa wakiutaja kuwa wa kiimla na wenye ukandamizaji.
Aliendesha kipindi cha televisheni kilichoitwa Con Cilia en Familia, na mara chache alionekana kwenye televisheni ya taifa akicheza muziki wa salsa pamoja na mume wake.
Hata hivyo, nyuma ya pazia, aliaminika kuwa mmoja wa washauri muhimu zaidi wa Rais Maduro na mbunifu wa mikakati iliyosaidia kudumisha utawala wake.
Katika maisha yake ya kisiasa, Flores amekabiliwa na tuhuma nyingi za rushwa na upendeleo wa kifamilia.
Katika miaka ya karibuni, baadhi ya wanafamilia wake wamepatikana na hatia katika mahakama za Marekani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.
Kwa sasa, anatarajiwa kukabiliana na mashtaka ya biashara ya dawa za kulevya na silaha katika mahakama ya New York, pamoja na mume wake.
Flores alikutana na Nicolás Maduro mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakati akiwa wakili mchanga aliyekuwa akijijengea jina . Katika kipindi hicho, alijihusisha na utetezi wa washukiwa wa jaribio la mapinduzi lililoshindikana mwaka 1992.
Miongoni mwa washukiwa hao alikuwa Hugo Chávez, ambaye baadaye angekuwa rais wa Venezuela.
Ni katika mazingira hayo ndipo alipokutana na Maduro, ambaye wakati huo alikuwa akimfanyia kazi Chávez kama mlinzi wa usalama.
"Nilikutana na Cilia wakati wa harakati hizo," Maduro aliwahi kusimulia. "Alikuwa wakili wa maafisa wa kijeshi waliokuwa wamefungwa, na pia wakili wa Kamanda Chávez. Kuwa wakili wa Chávez akiwa gerezani haikuwa kazi nyepesi."
"Katika miaka ile ya mapambano, nilimfahamu zaidi, na baadaye akanivutia."
Kuanzia hapo, maisha yao yaliunganishwa kwa karibu na Chávez na harakati zake za kisiasa zilizojulikana kama Chavismo.
Baada ya Chávez kushinda urais mwaka 1998, Flores alipanda kwa kasi katika ulingo wa siasa.
Aliingia Bunge la Taifa mwaka 2000 na kufikia mwaka 2006 alikuwa tayari amechaguliwa kuwa kiongozi wake.
Kwa kipindi cha miaka sita, aliongoza bunge lililotawaliwa kwa kiasi kikubwa na chama kimoja, baada ya vyama vikuu vya upinzani kususia uchaguzi wakidai haukuwa huru wala wa haki.
Chávez alipofariki dunia mwaka 2013, Flores alisimama imara kumuunga mkono Maduro, ambaye alishinda kwa ushindi uliokuwa na ushindani mkali katika uchaguzi wa urais uliofuata.
Miezi michache baadaye, wawili hao walifunga ndoa, wakihalalisha uhusiano wa muda mrefu waliokuwa nao. Walikuwa wakiishi pamoja na kulea watoto kutoka mahusiano ya awali watatu wa Flores na mmoja wa Maduro.
"Alikuwa nguzo muhimu sana katika utawala wa Maduro," alisema José Enrique Arrioja, mwandishi wa habari wa Venezuela na mhariri mkuu wa Americas Quarterly.
"Hakuwa tu mshauri wa karibu kihisia, bali pia mshauri wa kisiasa. Alikuwa mtu mwenye dhamira kubwa ya mamlaka."
Mwaka 2012, Flores alituhumiwa na vyama vya wafanyakazi kwa kuingilia mchakato wa ajira, akidaiwa kushawishi kuajiriwa kwa hadi watu 40, wakiwemo wanafamilia wake.
"Familia yangu iko hapa, na ninajivunia kuwa ni familia yangu. Nitawatetea," alijibu wakati huo.
Mnamo Novemba 2015, jina lake liliibuka tena katika kesi maarufu ya "wapwa wa dawa za kulevya," baada ya wapwa wake wawili Francisco Flores de Freitas na Efrain Antonio Campo Flores, kukamatwa nchini Haiti katika operesheni ya siri iliyoendeshwa na Shirika la Kudhibiti Dawa za Kulevya la Marekani (DEA).
Walinaswa wakijaribu kusafirisha kilo 800 za kokeini kwenda Marekani.
Ingawa Flores aliwashutumu maafisa wa Marekani kwa kuwateka nyara wapwa wake, mahakama ya Marekani iliwahukumu kifungo cha miaka 18 jela kwa makosa ya biashara ya dawa za kulevya.
Walirejeshwa Venezuela mwaka 2022 kupitia makubaliano ya kubadilishana wafungwa chini ya utawala wa Rais Joe Biden.
Hata hivyo, mwezi uliopita, utawala wa Donald Trump ulitangaza vikwazo vipya dhidi ya wapwa hao wawili pamoja na mpwa wa tatu, Carlos Erik Malpica Flores.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, alisema kuwa Nicolás Maduro na washirika wake wanahusika katika kusambaza dawa za kulevya zinazoathiri jamii ya Marekani.
Hati ya mashtaka iliyofunguliwa hivi karibuni dhidi ya Flores inamtuhumu, miongoni mwa mashtaka mengine, kwa kupokea mamia ya maelfu ya dola kama rushwa mwaka 2007 ili kupanga mkutano kati ya mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya na mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Venezuela.
Kwa mujibu wa Christopher Sabatini, mtaalamu wa masuala ya Amerika ya Kusini katika taasisi ya Chatham House, Flores anaonekana na wakosoaji wake kama sehemu ya serikali iliyojaa rushwa, inayokiuka haki za binadamu na kutumia nguvu kupita kiasi.
"Alikuwa nguvu iliyokuwa nyuma ya kiti cha enzi," anasema Sabatini. "Lakini kama ilivyo kwa nguvu nyingi zilizo nyuma ya pazia, mchango wake haukuwa wazi, na wengi hawakutambua ukubwa wa ushawishi wake."
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu Ya tarehe 5 Januari 2025.
Ripoti ya ziada kutoka BBC Mundo
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid