Ni utajiri gani unaomvutia Trump katika kisiwa cha Greenland?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Rais Donald Trump anaamini kwamba Greenland inapaswa kuwa sehemu ya Marekani.

Trump alisema maneno hayo muda mfupi baada ya kushinda uchaguzi wa Novemba 2024, na mara tu alipoingia madarakani, akaelezea mara kwa mara nia yake ya kunyakua kisiwa hicho cha Aktiki.

Wiki hii alimteua mjumbe maalum kwenda kisiwa cha Greenland, eneo linalojitegemea la Ufalme wa Denmark ambalo lina ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba milioni 2 lakini lina wakazi wapatao 56,000 pekee.

Mjumbe maalum wa Trump ni Jeff Landry, gavana wa Republican wa Louisiana na mmoja wa watu waaminifu zaidi katika kampeni ya MAGA yaani (Make America Great Again).

Akijibu swali kutoka BBC, rais alisisitiza wiki hii kwamba anahitaji kisiwa hicho kwa sababu za "ulinzi wa kitaifa".

"Tunahitaji kisiwa hicho," Trump alisema.

Tangazo hilo jipya liliikasirisha serikali ya Denmark, ambayo tena ilidai kupitia njia za kidiplomasia kwamba Rais wa Marekani aheshimu uhuru wa eneo la Greenland.

Pia unaweza kusoma:

Tamaa ya tangu zama za kale

Mipango ya Trump kwa Greenland si mipya. "Ingekuwa mpango mzuri wa mali isiyohamishika," alisema mwaka wa 2019, wakati wa muhula wake wa kwanza, alipotangaza nia yake katika kisiwa hicho.

Hata hivyo, wakati huo alisema kwamba kuchukua eneo hilo haikuwa kipaumbele chake.

Mshauri wa uchumi wa Ikulu ya White House wakati huo, Larry Kudlow, alielezea katika mahojiano kwenye Fox News Sunday kile ambacho utawala wa Trump ulikuwa unakimezea mate kisiwani humo.

Ni "eneo la kimkakati" lenye "madini mengi yenye thamani," Kudlow alisema.

Wawakilishi wa serikali ya Marekani hata waliwaendea Wadenmark kujaribu kufikia makubaliano, lakini hilo halikuwezekana.

Umuhimu wa eneo la Greenland umeongezeka katika mipango ya baadaye ya Republican, kama inavyosisitiziwa katika muhula wa pili wa utawala wa Trump.

Wataalamu wanadhania kwamba hii inahusiana na uchoraji ramani wa hivi karibuni wa utajiri wa madini wa eneo la Greenland na mabadiliko ya kiuchumi yenye kuizunguka.

Madini adimu

Kihistoria, eneo hilo linalofuatiliwa kwa umakini na mamlaka za Marekani kulitokana na msimamo wake wa kimkakati.

Kwanza, kama njia ya kudhibiti maendeleo ya kimataifa ya Wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kisha, wakati wa Vita Baridi, kudhibiti njia za baharini kati ya Ulaya na Amerika Kaskazini, na kwa sababu ya ukaribu wake na Aktiki.

Jeshi la Marekani limekuwa likiendesha Kituo cha Anga cha Pituffik, ambacho hapo awali kilijulikana kama Kituo cha Anga cha Thule, kwa miongo kadhaa kati ya Bahari ya Atlantiki na Aktiki. Kituo hicho kinatumika kama kituo cha uchunguzi wa makombora ya balestiki.

Lakini ripoti iliyochapishwa katikati ya mwaka wa 2023 na utafiti wa jiolojia wa Denmark na Greenland ilikadiria kwamba kilomita za mraba 400,000 za eneo la kisiwa hicho ambazo kwa sasa hazijafunikwa na barafu zina amana za madini 38 kwenye orodha iliyoandaliwa na Tume ya Ulaya.

Mbali na idadi kubwa ya madini ya shaba, grafiti, niobamu, titani, na rhodium, pia kuna amana kubwa za kile kinachoitwa 'madini adimu duniani' kama vile neodymium na praseodymium, ambazo sifa zake za kipekee za sumaku huzifanya kuwa za msingi katika utengenezaji wa mota za magari ya umeme na magurudumu yaendeshwayo na upepo.

"Greenland inaweza kuwa na hadi 25% ya rasilimali zote za madini adimu duniani," mwanajiolojia Adam Simon, profesa katika Chuo Kikuu cha Michigan, aliambia BBC News Brazil miezi michache iliyopita.

Hii itakuwa sawa na takriban tani milioni 1.5 za madini.

Mzozo na China

Madini adimu yamekuwa yakitafutwa kwa hamu na gamu kwa misingi ya kutafuta vyanzo vya nishati safi na mbadala - ili kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa.

"Kufikia mwaka wa 2024, tutakuwa tunatumia takriban asilimia 4,500 ya madini adimu duniani kote kuliko mwaka wa 1960," Simon alisema.

"Hata kama uchimbaji madini huko Greenland utafikiwa kwa muda mfupi, bado tutahitaji akiba zaidi ya madini adimu ili kukidhi mahitaji ya sasa ya soko."

Kwa sasa, China inaongoza soko la uchimbaji na usindikaji wa madini adimu. Wachina wanasimamia takriban theluthi moja ya madini, 60% ya uchimbaji, na 85% ya usindikaji wa nyenzo hizi.

Lakini utawala wa China katika soko hili ulikuwa tayari umefikia 95% kufikia mwaka wa 2010, na kuipa Beijing nguvu kubwa ya kisiasa na kiuchumi juu ya uzalishaji barani Ulaya na Marekani.

Kwa sasa, kampuni mbili za uchimbaji madini zinazotafuta madini adimu huko Greenland ni za Australia, lakini moja wapo inamilikiwa na serikali ya China, kama mwekezaji.

China imekuwa ikijaribu kuimarisha uwepo wake huko Greenland kwa miaka mingi.

Xi Jinping aliielezea nchi yake kama iliyo "karibu na Aktiki," ingawa iko karibu kilomita 1,500 kutoka eneo hilo.

Kama sehemu ya mpango huu, kampuni ya ujenzi ya China ilijaribu kujenga angalau viwanja viwili vya ndege huko Greenland, lakini ikapuuzwa na makampuni ya Denmark, katika mzozo ambapo Washington iliripotiwa kutoa shinikizo kuunga mkono Denmark.

Harakati hizi zote za Wachina katika eneo hilo ziliishtua Marekani, ambayo inaiona Beijing kuwa mpinzani wake mkuu wa kimataifa.

Katika muhula wake wa kwanza, utawala wa Trump ulijumuisha vipengele vya madini adimu duniani miongoni mwa nyenzo muhimu kwa usalama wa taifa wa Marekani na kusaini makubaliano ya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya kiteknolojia na kisayansi kati ya Greenland na Marekani.

Ushawishi wa Elon Musk

Ingawa nia ya kupata madini adimu huko Greenland ilikuwa tayari wazi wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, ushawishi wa bilionea Elon Musk, Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla, mmoja wa watengenezaji wakubwa wa magari ya umeme duniani, haupaswi kupuuzwa.

"Hakika, Tesla inavutiwa na madini adimu duniani pamoja na lithiamu, shaba, nikeli, na grafiti. Hivyo basi, ni jambo la busara kuzingatia mgongano unaowezekana kutokea wa maslahi ikiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayotegemea upatikanaji wa madini adimu yuko katika nafasi ya kisiasa yenye mamlaka ya kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuathiri upatikanaji wa madini haya duniani kote," Simon aliiambia BBC Januari iliyopita.

Kwa tahadhari hiyo hiyo, hata hivyo, pia alipendekeza Musk kujizuia juu ya ukomo wa faida unaoweza kupatikana, na kwa Trump mwenyewe, akazungumzia shambulio dhidi ya Greenland.

"Katika hatua ya sasa ya utafutaji wa madini, kuna uwezekano mkubwa kwamba tutakuwa na wachimbaji wenye uwezo wa kufikia uzalishaji thabiti wa kibiashara huko Greenland katika kipindi cha chini ya miaka 10," Simon alisema.

"Ingawa serikali zinafanya kazi kwa matarajio ya miaka 4, makampuni haya makubwa ya uchimbaji madini hupanga biashara zao kwa matarajio ya miaka 40," mwanajiolojia huyo aliongeza.

Ni jambo linalowezekana kuharakisha uchimbaji madini katika maeneo ya kisiwa hicho, lakini changamoto ya pili itakuwa usafirishaji kwa kutumia meli kubwa katika eneo la mbali lenye vilima vya barafu na changamoto zingine za baharini.

Hivyo basi, itakuwa vigumu kwa Trump kujivunia uchimbaji madini adimu wa kiwango cha juu huko Greenland, hata kama atashinda changamoto kubwa za kijiografia zenye kuhusiana na suala hilo.

Soma zaidi:

Imefasiriwa na Asha Juma