Greenland: Trump aonywa kwamba kisiwa hicho hakiwezi kununuliwa kutoka kwa Denmark

Kisiwa cha Greenland kimesema kwamba hakiuzwi baada ya rais Donald Trump wa Marekani kusema kwamba angependa Marekani kukinunua kisiwa hicho kikubwa duniani.

Rais huyo alidaiwa kuzungumzia wazo hilo la kukinunua kisiwa hicho cha Greenland - eneo la Denmark linalojitawala katika chakula cha jioni na mikutano na washauri wake.

Lakini Serikali ya Greenland imepinga wazo lake ikisema kwamba wako tayari kwa biashara lakini sio kununuliwa.

Mipango ya rais Trump pia imepingwa na wanasiasa wa Denmark.

''Inaonekana ni mzaha wa siku ya wajinga ya Aprili mosi'', alituma ujumbe wa twitter waziri mkuu Lars Lokke Rasmussen.

Jarida la wall Street Journal lililochapisha habari hizo lilisema kwamba bwana Trump alizungumzia kuhusu ununuzi huo.

Duru zilizonukuliwa na vyombo vingine vya habari zilitofautiana kuhusu iwapo rais huyo alikuwa akifanya mzaha huku akiwa na wazo la kupanua himaya ya Marekani.

Maafisa katika kisiwa hicho cha Greenland wamesisitiza kwamba kisiwa hicho hakiko katika soko.

''Greenland ina utajiri wa madini, maji safi zaidi na barafu, samaki, chakula cha baharini kawi na ni kivutio kikuu cha utalii. Tuko wazi kwa biashara lakini sio kuuzwa'', ilisema wizara ya kigeni katika taarifa yake iliotumwa katika mitandao ya kijamii.

Waziri mkuu wa Greenland Kim Kielsen alirejelea matamshi yake katika taarifa nyengine tofauti .

''Greenland haiuzwi lakini iko wazi kibiashara na ushirikiano na mataifa mengine'', ilisema taarifa.

Mbunge wa Greenland Aaja Chemnitz Larsen pia alikuwa miongoni mwa wale waliopinga hamu hiyo ya rais wa Marekani.

''Hapana ahsante kwa bwana Trump kununua Greenland'' , aliandika katika mtandao wa Twitter, akiongezea ''ushirikiano wa usawa kati ya Marekani na Greenland ndio suluhu pekee''.

Poul Krarup muhariri mkuu wa gazeti la Sermitsiaq aliambia BBC hakuamini matamshi ya bwana Trump. ''Greenland ni sehemu ilio huru katika ufalme wa Denmark na inahitaji kuheshimiwa'', alisema.

Lakini alisema kwamba alidhani kwamba ndoto ya Bwana Trump haiwezi kuafikiwa.

''Tungependa kushirikiana na Marekani , bila shaka lakini sisi tuko huru na tunaamua marafiki zetu ni akina nani''.

Je Denmark imesema nini?

Wanasiasa nchini Denmark wamekejeli wazo hilo la Marekani.

''Iwapo anafikra finyu kama hizo basi ni wazi kwamba ameshikwa na wazimu'', msemaji wa maswala ya kigeni wa chama tawala cha Denmark Soren Espersen alisema.

Swala la Denmark kuuza raia 50,000 kwa Marekani ni swala lisilowezekana.

Katika vitu vyote ambavyo haviwezekani hili ni mojawapo. Waziri mkuu wa Denmark Mette Frederiksen ambaye alichukua mamlaka hivi karibuni hakutoa tamko lake.

Je Greenland iko wapi?

Greenland ndio kisiwa kikubwa zaidi duniani baada ya Australia ambayo inajulikana kama bara.

Kisiwa hicho kina takriban watu 56,000 walio na makaazi yao katika pwani yake. Takriban asilimia 90 ni raia wa Greenland . Ina serikali yake na bunge lake.

Asilimia 80 ya kisiwa hicho imefunikwa na barafu ambayo inahofiwa kuyeyuka kutokana na viwango vya joto duniani.

Kuyeyuka kwa barafu hiyo kumesaidia katika utafutaji wa madini katika ardhi ya kisiwa hicho.

Lakini inaaminika kwamba kuyeyuka kwa barafu hiyo kunaweza kusababisha madhara yanayotokana na mabaki ya kinyuklia yaliowachwa katika kambi kadhaa za jeshi la Marekani wakati wa vita baridi.

Kwa nini kisiwa hicho kinamvutia Trump?

Bwana Trump ameripotiwa kuvutiwa na kisiwa hicho kutokana na madini yake kama vile mkaa, Zinc, Shaba na Chuma.

Lakini huku Greenland ikiwa na utajiri wa mali asli, inategemea Denmark kwa thuluthi mbili za mapato yake .

Ina viwango vya juu vya watu kujitoa uhai, ulevi wa pombe na ukosefu wa ajira.

Marekani imekuwa ikikiona kisiwa hicho kama eneo muhimu la kimkakati na liliweka kambi ya wanahewa wake mbali na rada yake wakati wa vita baridi

Mbunge wa Republican Mike Gallagher alitaja wazo hilo la Trump kama la kisiasa.

''Marekani ina hamu ya kukimiliki kisiwa cha Greenland na hilo lazima lisemwe'', alituma ujumbe wake katika mtandao wa Twitter.

Je mataifa yanaweza kununua maeneo?

Kihistoria , mataifa yameyateka maeneo sio tu kijeshi lakini kupitia makubaliano ya kifedha.

Chini ya ununuzi wa Louisiana 1803 , Marekani ilichukua takriban maili 827,000 mraba ya ardhi ya Ufaransa kwa $15m (£12.3m).

Mwaka 1867, Marekani iliafikia mkataba na Urusi kuinunua Alaska kwa $7.2m.

Baadaye Marekani ililinunua eneo la West Indis la Denmark 1917 na kuvipatia jina visiwa vya Marekani vya Virgin Island.

Je Marekani imewahi kutaka kununua visiwa vya Greenland?

Wazo la kuinunua Greenland kwa mara ya kwanza liliwasilishwa 1860 chini ya urais wa Andrew Johnson.

Mwaka 1867 ripoti ya idara ya kigeni ilipendekeza kwamba eneo la kimkakati la Greenland pamoja na mali yake asli ni muhimu kulinunua.

Lakini hakuna hatua rasmi iliochukuliwa hadi 1946 , wakati Harry Truman aliipatia Denmark $100m kununua eneo hilo.

Alikuwa amewasilisha mpango wa kutaka kubadilishana ardhi ya Alaska na Greenland kulingana na AP.