Misheni ya siri ya kuusafirisha mwili wa Rais nyumbani - rubani aifichulia BBC

    • Author, Bushra Mohamed
    • Nafasi, BBC World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Takriban miaka 31 iliyopita, marubani wawili wa Kenya, Hussein Mohamed Anshuur na Mohamed Adan, walitembelewa na mgeni ambaye hawakumtarajia katika ofisi yao katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, nje kidogo ya jiji la Nairobi.

Ni mwanadiplomasia wa Nigeria, ambaye aliwaomba kumfanyia kazi nyeti na ya kisiri ya kuusafirisha mwili wa mtawala wa zamani wa Somalia Siad Barre hadi nyumbani kwao baada ya kiongozi huyo kufariki dunia akiwa uhamishoni nchini Nigeria akiwa na umri wa miaka 80.

Anshuur, ambaye awali alikuwa rubani katika Jeshi la Angani la Kenya, na Adan ni washirika katika Bluebird Aviation, mojawapo ya mashirika makubwa ya ndege ya kibinafsi nchini Kenya ambayo walikuwa wameanzisha miaka michache iliyopita.

Akizungumza na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza kuhusu ujumbe huo, Anshuur aliiambia BBC kwamba mwanadiplomasia huyo wa Nigeria alifika "moja kwa moja", akimtaka yeye na Hussein "kodi ndege na kusafirisha mwili kwa siri" kutoka mji mkuu wa Nigeria wa Lagos wakati hu, hadi mji wa Garbaharey alikozaliwa Barre wa kusini mwa Somalia kwa mazishi, umbali wa kilomita 4,300.

Anshuur alisema walishangazwa na ombi hilo: "Tulijua mara moja kuwa huu haukuwa mkataba wa kawaida."

Barre alitoroka Somalia tarehe 28 Januari 1991 baada ya kupinduliwa na wanamgambo, hivyo kuurejesha mwili wake Somaliabila shaka kungepandisha joto la kisiasa, ambalo lingehusisha serikali nyingi, uhusiano dhaifu wa kikanda na hatari ya kuanguka kwa kidiplomasia.

Anshuur anasema walihofia madhara yanayoweza kutokea kwani mwanadiplomasia huyo aliomba ndege iandaliwe nje ya taratibu za kawaida.

"Ikiwa mamlaka ya Kenya ingegundua, inaweza kusababisha matatizo makubwa," Anshuur alisema.

Marubani walijadili suala hilo siku nzima ili kutathmini ombi hilo, hasa ikiwa serikali ya Kenya, wakati huo ikiongozwa na Rais Daniel arap Moi, iligundua walichopanga kufanya.

Barre alinyakua mamlaka katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu mwaka 1969. Wafuasi wake walimwona kama mfuasi wa Afrika Kusini, ambaye aliunga mkono sababu kama vile kampeni dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Kwa wakosoaji wake, alikuwa dikteta ambaye alisimamia ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu hadi alipoondolewa madarakani.

Barre awali alikimbilia Kenya, lakini serikali ya Moi ilikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa bunge na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kumkaribisha. Barre baadaye alipewa hifadhi ya kisiasa na Nigeria, wakati huo ikiwa chini ya uwala wa kijeshi Jenerali Ibrahim Babangida, na aliishi Lagos hadi alipofariki kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Kwa kuzingatia unyeti wa misheni hiyo, marubani walimuomba mwanadiplomasia wa Nigeria kuwapa siku moja zaidi ya kabla hawajatoa jibu la ombi lake. Ofa waliopewa ya kifedha ilikuwa ya faida kubwa - japo hawakufichua kiasi halisi - lakini hatari ilikuwa kubwa.

"Tulimshauri kwanza kutumia ndege ya Jeshi la Wanahewa la Nigeria, lakini alikataa," Anshuur alikumbuka. "Alisema kuwa operesheni hiyo ilikuwa nyeti sana na kwamba serikali ya Kenya lazima isifahamishwe."

Pia akizungumza na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza kuhusu ujumbe huo, mtoto wa kiume wa mtawala wa zamani wa Somalia, Ayaanle Mohamed Siad Barre, aliiambia BBC kwamba "usiri haukuwa kuhusu kuficha chochote kinyume cha sheria".

Alieleza kuwa kulingana na desturi ya Kiislamu maziko yanatakiwa kufanyike haraka iwezekanavyo, na hivyo taratibu za kawaida zilikiukwa, ingawa baadhi ya serikali zilifahamu mpango huo.

"Wakati ulikuwa unayoyoma," alisema. "Kama tungelipitia utaratibu wote, tungelichelewesha mazishi."

Alisema aliambiwa na maafisa wa Nigeria kwamba njia ya kurukia ndege ya Garbaharey ilikuwa "ndogo sana" kwa ndege ya kijeshi.

"Ndio maana uamuzi wa kutumia shirika la ndege la Bluebird Aviation ilikuwa chagua bora," mtoto wa Barre aliambia BBC.

Marubani wakati huo hawakuwa na mawasiliano na familia ya Barre, kwa hiiyo walitegemea uamuzi wa mwanadiplomasia wa Nigeria, Anshuur alisema, mnamo tarehe 10 Januari 1995.

"Haikuwa rahisi," Anshuur anakumbuka. "Lakini tulihisi tuna wajibu wa kufanikisha safari hiyo."

Hii haikuwa mara yao ya kwanza kumhudumia na marehemu rais huyo wa zamani.

Wakati Barre na familia yake walipoukimbia mji mkuu wa Somalia Mogadishu, alitua Burdubo, katika eneo la Garbaharey.

Kipindi hicho, marubani walikuwa wakisafirisha vifaa muhimu - ikiwa ni pamoja na chakula, dawa na mahitaji mengine ya kimsingi - hadi kwa familia ya Barre.

Lakini kabla ya kuanza safari, marubani walitaka kuhakikisho kutoka kwa serikali ya Nigeria.

"Kwamba mambo yakienda mrama, Nigeria lazima iwajibike," Anshuur alisema. "Na tulitaka kuandamana na maafisa wawili wa ubalozi."

Nigeria ilikubali. Ndipo marubani wakajiandaa kwa safari yao kisiri - na walifanikiwa.

Marubani waliwasilisha orodha ya safari ikionyesha kuwa walikuwa wakielekea Kisumu, mji wa ufukweni mwa Ziwa Victoria, magharibi mwa Kenya.

"Hiyo ilikuwa kwenye karatasi tu," Anshuur alisema.

"Tulipokaribia Kisumu, tulizima rada na kugeuza mwelekeo kwenda Entebbe, Uganda."

Wakati huo, mifumo ya ufuatiliaji wa anga katika eneo kubwa la Afrika Mashariki ilikuwa bado hafifu, pengo ambalo marubani walijua lingeweza kutumiwa kimkakati.

Walipotua Entebbe, waliwaarifu maafisa wa uwanja wa ndege kuwa walikuwa wametokea Kisumu. Maafisa wawili wa Nigeria waliokuwa ndani ya ndege waliagizwa kubaki kimya na kutoshuka.

Baada ya kujaza mafuta, Yaoundé nchini Cameroon ilitangazwa kuwa kituo kinachofuata, ambako wanadiplomasia wa Nigeria waliokuwa wakiratibu operesheni hiyo walikuwa wanasubiri.

Baada ya kusimama kwa muda mfupi, ndege iliendelea hadi Lagos. Kabla ya kuingia anga la Nigeria, serikali ya nchi hiyo iliwapa marubani alama maalum ya Jeshi la Anga la Nigeria – "WT 001" ili kuepusha mashaka.

"Maelezo hayo yalikuwa muhimu," Anshuur alisema. "Bila hivyo, huenda tungezuiwa na kuhojiwa."

Safari ya mwisho na hatari Zaidi

Walitua Lagos majira ya saa 7:00 mchana tarehe 11 Januari, ambako familia ya Barre ilikuwa tayari inasubiri.

Baada ya mapumziko ya siku nzima, marubani walijiandaa kwa hatua ya mwisho ya safari kuusafirisha mwili wa Barre hadi Garbaharey.

Tarehe 12 Januari 1995, jeneza la mbao lilipakiwa ndani ya ndege. Safari hii iliandamana na maafisa wawili wa Nigeria pamoja na wanafamilia sita, akiwemo mwana wa marehemu, Ayaanle Mohamed Siad Barre.

Kwa mtazamo wa marubani, usalama wa siri uliendelea kuwa kipaumbele cha juu.

"Hatukuwahi kuwaambia maafisa wa viwanja vya ndege Cameroon, Uganda au Kenya kwamba tulikuwa tumesafirisha mwili," Hussein alisema.

"Hilo lilifanywa makusudi."

Ndege ilirudia njia ile ile, ikisimama kwa muda mfupi Yaoundé kabla ya kuelekea Entebbe kwa ajili ya mafuta. Maafisa wa Uganda waliambiwa kuwa safari ya mwisho ilikuwa Kisumu.

Walipokaribia Kisumu, marubani waligeuza mwelekeo tena, safari hii wakielekea moja kwa moja Garbaharey.

Baada ya jeneza kushushwa, Anshuur na rubani mwenzake walihudhuria mazishi, kisha wakarudi Uwanja wa Ndege wa Wilson, wakiwa na maafisa wawili wa Nigeria.

"Ni baadaye tu ndipo ilizama akilini katika kile tulichokuwa tumefanya," Anshuur aliiambia BBC.

Alipoulizwa iwapo angefanya hivyo tena, alijibu: "Nina umri wa miaka 65 sasa na hapana, singefanya kazi kama hiyo leo kwa sababu teknolojia ya usafiri wa anga imeimarika sana hivi kwamba sasa kuna ufikiaji wa kutosha wa rada ya trafiki ya anga ndani ya bara la Afrika.

"Kwa kweli haiwezekani kutumia mapungufu katika udhibiti wa trafiki ya anga ambayo ilikuwepo nyuma mnamo 1995."