Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano zaidi yazuka Iran huku kiongozi mkuu akishutumu umati kwa 'kumfurahisha Trump'
Maandamano dhidi ya serikali nchini Iran yameendelea kwa siku ya 13 mfululizo huku mtandao ukiminywa kote nchini.
Muhtasari
- Tunachokijua kufikia sasa kuhusu Iran
- Waandamanaji 'wanajaribu kumfurahisha Trump', asema kiongozi wa Iran
- Mtandao waminywa Iran 'kwa saa 12'
- Papa Leo ashutumu 'diplomasia inayotegemea nguvu' za kijeshi
- Israel inashambulia maeneo ya Hezbollah
- Mashambulizi ya Israel yaua watu 11 huko Gaza
- Trump afuta wimbi la pili la mashambulizi dhidi ya Venezuela
- Urusi yaishambulia Ukraine kwa kombora ambalo ni nadra sana kulitumia la Oreshnik
- Kuna "tishio halisi" la operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Colombia, rais aambia BBC
- Maandamano makubwa dhidi ya serikali yaendelea Tehran na miji mingine ya Iran
- FBI yazuwia maafisa wa Minnesota kushiriki uchunguzi wa mauaji ya mwanamke na afisa wa ICE
- Moto wa nyikani wateketeza eneo la makazi Australia
- Trump atishia kufanya mashambulizi mengine nchini Nigeria
- Baraza la Mawaziri Tanzania: Simbachewene atemwa Makonda apandishwa
- Venezuela yaanza kuwaachia wafungwa wa kisiasa
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Asha Juma
Tunachokijua kufikia sasa kuhusu Iran
Maandamano ya kupinga serikali nchini Iran yameendelea kwa siku ya 13 mfululizo huku kukatika kwa intaneti kote nchini kukiendelea kuzuia mawasiliano.
Tunachokijua kufikia sasa:
- Video zilizothibitishwa na BBC zinaonyesha waandamanaji wakikusanyika katika jiji la Zahedan, kusini-mashariki mwa Iran - pia tumetambua miji 16 zaidi ambayo imeshuhudia maandamano mapya.
- Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amewakemea waandamanaji, akionya kwamba utawala wake umejitolea kukabiliana na "wasumbufu"
- Maoni yake yanakuja huku mtandao wa intaneti ukiminywa - data inaonyesha kuwa nchi hiyo imekuwa bila mtandao kwa takriban saa 18
- Nchini Marekani, Rais Trump ameapa "kuishambulia [Iran] vikali" ikiwa utawala utaanza kuwaua waandamanaji
- Uingereza haijajipanga waziwazi msimamo wa Trump, lakini ilisihi mamlaka ya Iran "kujizuia"
- Shirika la ndege la Emirates flydubai limeiambia BBC kwamba limefuta safari za ndege kutokana na machafuko.
Soma zaidi:
Waandamanaji 'wanajaribu kumfurahisha Trump', asema kiongozi wa Iran
Akizungumza na wafuasi wake mapema asubuhi ya leo, Khamenei aliwapuuza waandamanaji na kuwaita "kundi la waharibifu" wanaotaka "kumfurahisha" Rais wa Marekani Donald Trump.
Katika hotuba ya video iliyotangazwa kwenye televisheni ya kitaifa, Khamenei alisema: "Kundi la waharibifu lilijitokeza Tehran na maeneo mengine na kuharibu majengo ya nchi yao ili kumfurahisha rais wa Marekani."
"Hiyo ni kwa sababu alitoa madai ya kipuuzi kwamba anawaunga mkono ninyi waandamanaji na watu ambao ni hatari kwa nchi. Kama ana uwezo, anapaswa kuendesha nchi yake mwenyewe."
Kiongozi huyo wa Iran, ambaye amekuwa madarakani tangu 1989, aliongeza kwamba mikono ya Trump "ina madoa ya damu ya zaidi ya Wairani elfu moja waliouawa wakati wa vita vya siku 12 [na Israeli]".
"Kundi la watu wasio na uzoefu na wasiojali wanamwamini na kutenda kulingana na matakwa yake. Wanachoma mapipa ya takataka ili kumfurahisha," anaongeza.
"Kila mtu ajue kwamba Jamhuri ya Kiislamu iliingia madarakani kupitia damu ya watu mia kadhaa wenye heshima na haitarudi nyuma mbele ya wale wanaokana hili."
Trump amekuwa mpinzani mkubwa wa utawala wa Iran kwa muda mrefu na aliahidi kuingilia kati ikiwa raia watauawa katika maandamano hayo.
Soma zaidi:
Mtandao waminywa Iran 'kwa saa 12'
Kukatika kwa intaneti kote nchini Iran kumeripotiwa tangu jana usiku.
Shirika la ufuatiliaji wa intaneti la NetBlocks liliripoti saa 04:30 GMT kwamba "Iran imekuwa bila mtandao kwa saa 12, huku muunganisho wa intaneti kitaifa ukiwa karibu 1% ya viwango vya kawaida".
Wairani wengi ambao hawaishi tena nchini humo wamesema kwenye mtandao wa X kwamba wamekuwa na wakati mgumu kuwasiliana na wanafamilia nchini Iran.
Baadhi walisema njia ya mawasiliano ya simu za nyumbani za familia zao pia zinaonekana kukatwa.
Mamlaka ya Iran imeweka vikwazo vya intaneti mara kwa mara wakati wa vipindi vya machafuko, ikitaja wasiwasi wa usalama na madai ya mashambulizi ya mtandaoni.
Kuminywa kwa intaneti hivi karibuni kulikuwa wakati wa vita vya siku 12 na Israeli katika msimu wa joto ambapo maafisa walitaja sababu hizo hizo.
Zaidi ya waandamanaji 100 waliaminika kuuawa wakati wa kuzimwa kwa umeme mwaka wa 2019, kulingana na mashirika ya haki za binadamu.
Maandamano hayo yalichochewa na ongezeko la bei ya mafuta lakini maelezo ya maandamano hayo yalijitokeza kikamilifu baada ya huduma za intaneti kurejeshwa.
Pia unaweza kusoma:
Papa Leo ashutumu 'diplomasia inayotegemea nguvu' za kijeshi
Papa Leo ameshuumu matumizi ya nguvu za kijeshi kama njia ya kufikia malengo ya kidiplomasia, katika hotuba kali ya kila mwaka ya sera za kigeni siku ya Ijumaa ambapo pia alitoa wito wa kulinda haki za binadamu nchini Venezuela.
Papa Leo alisema udhaifu wa mashirika ya kimataifa katika kukabiliana na migogoro ya kimataifa ulikuwa "sababu inayotia wasiwasi".
"Diplomasia inayokuza mazungumzo na kutafuta makubaliano miongoni mwa pande zote inabadilishwa na diplomasia inayotegemea nguvu," Leo aliwaambia mabalozi wapatao 184 walioidhinishwa na Vatican.
"Vita vimerudi kwa mtindo mwingine na ari ya vita inaenea," amesema Papa Leo.
Akizungumzia tukio la Rais Marekani Donald Trump kuagiza kukamatwa kwa rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Papa alitoa wito kwa serikali za dunia "kuheshimu matakwa" ya watu wa Venezuela katika siku zijazo.
Alisema mataifa lazima "yalinde haki za binadamu na za kiraia" za Wavenezuela.
Soma zaidi:
Israel inashambulia maeneo ya Hezbollah
Jeshi la Israeli limesema siku ya Ijumaa kuwa linashambulia maeneo lengwa ya Hezbollah nchini Lebanon.
Jeshi la Lebanon limesema siku ya Alhamisi kuwa limechukua udhibiti wa operesheni kusini mwa nchi, lakini Israel ikajibu kuwa juhudi za kuwapokonya silaha wapiganaji wa Hezbollah hazitoshi.
Lebanon imekuwa chini ya shinikizo kubwa la kimataifa, hasa kutoka Marekani kuipokonya silaha Hezbollah, tangu makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Novemba 2024 yalipomaliza vita vya mwaka mmoja kati ya Israel na Hezbollah.
Jeshi lilisema lengo lake limefikiwa kwa "njia yenye ufanisi na inayoonekana" lakini bado kuna kazi ya kufanywa kuondoa silaha na handaki ambazo hazijalipuka.
Akijibu taarifa ya jeshi la Lebanon, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema juhudi za kuipokonya silaha Hezbollah kikamilifu zilikuwa "mwanzo wa kutia moyo, lakini hazitoshi, kama inavyothibitishwa na juhudi za Hezbollah za kujihami tena na kujenga upya miundombinu yake ya ugaidi kwa usaidizi wa Iran".
Soma zaidi:
Mashambulizi ya Israel yaua watu 11 huko Gaza
Mashambulizi ya Israeli yamewaua Wapalestina wasiopungua 11 katika mashambulizi tofauti katika Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi, madaktari walisema, katika kile ambacho jeshi lilisema kilitokana na shambulio la roketi lililoshindwa la wanamgambo katika eneo hilo.
Madaktari walisema shambulio la anga la Israeli liliua watu wasiopungua wanne na kuwajeruhi wengine watatu, wakiwemo watoto, katika hema eneo la magharibi la Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Shambulio jingine liliua mtu mmoja mashariki mwa mji, karibu na mahali ambapo vikosi vya Israeli vinafanya kazi.
Baadaye Alhamisi, madaktari walisema mwanamume mmoja aliuawa katika shambulizi la Israeli dhidi ya shule iliyokuwa ikiwahifadhi familia zilizokimbia makazi yao huko Jabalia kaskazini mwa Gaza, huku shambulizi jingine likimuua mtu aliyekuwa kwenye hema karibu na Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Watu wengine wanne waliuawa katika shambulizi tofauti katika kitongoji cha Zeitoun cha Jiji la Gaza.
Jeshi la Israeli lilisema liliwashambulia wanamgambo kadhaa wa Hamas, maeneo ya kurusha roketi na kile kilichoelezwa kama "miundombinu ya magaidi," baada ya roketi kurushwa kutoka eneo la jiji la Gaza kuelekea Israeli.
Jeshi lilisema roketi hiyo haikufanikiwa kwenda mbali na kutua karibu na hospitali huko Gaza na kuishutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Chanzo kutoka kundi la wanamgambo wa Palestina kiliambia Reuters kuwa kinathibitisha madai hayo.
Soma zaidi:
Trump afuta wimbi la pili la mashambulizi dhidi ya Venezuela
Rais wa Marekani Donald Trump amesema siku ya Ijumaa kwamba amefuta wimbi la pili la mashambulizi dhidi ya Venezuela lililokuwa likitarajiwa hapo awali kufuatia ushirikiano kutoka kwa taifa hilo la Amerika Kusini.
Trump alisema Marekani na Venezuela zinashirikiana, akiongeza kuwa angalau dola bilioni 100 zitawekezwa na makampuni makubwa ya mafuta nchini Venezuela.
Hata hivyo, aliongeza kwamba meli zote za mafuta nchini Venezuela "zitasalia mahali pake kwa sababu za kiusalama".
Pia unaweza kusoma:
Urusi yaishambulia Ukraine kwa kombora ambalo ni nadra sana kulitumia la Oreshnik
Urusi imetumia kombora la balestiki la Oreshnik kama sehemu ya shambulio kubwa dhidi ya Ukraine usiku kucha.
Watu wanne wameuawa na wengine 25 kujeruhiwa mjini Kyiv Alhamisi usiku, ambapo milio mikubwa ilisikika kwa saa kadhaa, na kusababisha anga kuwaka kwa milipuko.
Ni mara ya pili tu kwa Moscow kutumia kombola la Oreshnik, ambalo lilitumiwa kwa mara ya kwanza kushambulia jiji kuu la Dnipro mnamo Novemba 2024.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema shambulio hilo lilikuwa jibu la shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine kwenye makazi ya Vladimir Putin mwishoni mwa Desemba, ambalo Kyiv inakanusha kulifanya.
Soma zaidi:
Kuna 'tishio halisi' la Marekani kuivamia Colombia, Rais aimbia BBC
Rais wa Colombia, Gustavo Petro, ameambia BBC anaamini kuwa sasa kuna “tishio halisi” la operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Colombia.
Haya yanajiri baada ya mazungumzo ya Trump kuhofia na kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya nchi hiyo.
Petro amesema Marekani inawatendea mataifa mengine hasa ya Amerika ya Latin kama sehemu ya “milki ya kifalme” ya Marekani, na hilo linapinga heshima ya nchi huru.
Petro ameeleza kuwa hatua kama hizi zinaweza kusababisha Marekani kutoka “kutawala dunia” na badala yake kuwa “imejitenga na dunia.Na hilo halijengi ufalme''.
Pia amekosoa vibaya mipango ya mashirika ya uhamiaji ya Marekani (kama ICE), akidai kuwa ''hawaangamizi wamarekani wa Latin pia raia wa Marekani ''.
Aliongeza kuwa Marekani haipaswi kutumia nguvu ya kijeshi badala yake ifanye mazungumzo ya diplomasia, na Colombia ili kutafuta ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo badala ya vita.
Kwa upande wao, baadhi ya vitisho vya utaratibu wa kijeshi kutoka Marekani vimetokana na kauli za Rais Donald Trump kuhusu uwezekano wa kuchukua hatua kama hizo dhidi ya Colombia kufuatia yale aliyofanya Venezuela hivi karibuni.
Pia unaweza Kusoma;
Maandamano makubwa dhidi ya serikali yaendelea Tehran na miji mingine ya Iran
Maelfu ya wananchi wa Iran wameandamana katika mji mkuu Tehran na miji mingine, katika kile kinachosemekana kuwa ni onyesho kubwa zaidi la upinzani dhidi ya mfumo wa kidini katika miaka mingi, video zilizothibitishwa na BBC Persian zinaonyesha.
Maandamano ya amani yaliyojitokeza jioni ya Alhamisi, katika Tehran na mji wa pili Mashhad, vikosi vya usalama havikuwatawanya wala kukabiliana na waandamanaji, na hali hiyo inathibitishwa na picha za video zilizopitiwa kwa uangalifu.
Baadaye, kikundi kinachofuatilia mtandao kiliripoti kuminywa kwa huduma ya intaneti katika taifa zima.
Waandamanaji wanaweza kusikika katika kanda za video za kutaka kupinduliwa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na kurejeshwa kwa Reza Pahlavi, mtoto aliyehamishwa wa marehemu shah wa zamani, ambaye aliwataka wafuasi wake kuingia mitaani.
Maandamano haya yalikuwa ni siku ya 12 mfululizo ya ghasia, yaliyosababishwa na hasira kwa kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Iran, na ambayo yameenea hadi miji na miji midogo zaidi ya 100 katika mikoa yote 31 ya Iran, kulingana na mashirika ya haki za binadamu.
Shirika la habari la mashirika ya haki za binadamu lililoko Marekani, Human Rights Activist News Agency (HRANA), limeripoti kuwa angalau waandamanaji 34 wameuawa, wakiwemo watoto watano, na askari wanane wa usalama wamepoteza maisha, huku waandamanaji wengine 2,270 wakikamatwa.
Shirika la haki za binadamu lililoko Norway, Iran Human Rights (IHR), limesema kuwa angalau waandamanaji 45, wakiwemo watoto 8, wameuawa na vikosi vya usalama.
BBC Persian imethibitisha vifo na utambulisho wa watu 22, huku mamlaka za Iran zikiripoti vifo vya askari sita wa usalama.
Maandamano hayo yalitokea muda mfupi baada ya Reza Pahlavi, ambaye baba yake aliondolewa madarakani na mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 na ambaye anaishi Washington DC, kuitaka jamii ya Iran kuandamana na kudai haki zao kwa umoja.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Pahlavi alisema: “Mamilioni ya Wairani walidai uhuru wao usiku huu,” akiwataja waandamanaji hao kama “wenzangu wajasiri.”
Alimshukuru Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa kushinikiza utawala uwajibike, na akawataka pia uongozi wa Ulaya wafanye vivyo hivyo.
Pahlavi pia ameitaka jamii ya Iran kuendeleza maandamano kuanzia saa 20:00 (saa za eneo) Ijumaa usiku.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimepunguza ukubwa wa maandamano ya Alhamisi.
Katika baadhi ya matukio, vimekanusha kabisa kuwa maandamano yalitokea, na badala yake kuonyesha mitaa tupu.
Hali kadhalika, shirika linalofuatilia intaneti, NetBlocks, limesema takwimu zake zinaonyesha kuwa Iran iko katikati ya kukatika kwa intaneti katika taifa zima.
“Tukio hili linakuja baada ya mlolongo wa hatua za kupunguza uhuru wa kidijitali zilizolengwa dhidi ya maandamano kote nchini, na kupunguza haki ya wananchi ya kuwasiliana katika wakati muhimu,” limesema NetBlocks, likirejelea kukosekana kwa mtandao katika miji kadhaa awali.
Soma zaidi:
FBI yazuwia maafisa wa Minnesota kushiriki uchunguzi wa mauaji ya mwanamke na afisa wa ICE
Maafisa wa Minnesota wanasema kuwa FBI imezuwia upatikanaji wao wa uchunguzi wa mauaji ya mwanamke na afisa wa Idara ya Uhamiaji (ICE).
Tukio hilo limezua ghasia mjini Minneapolis, ambapo wananchi wameandamana kulalamika juu ya kifo cha Renee Nicole Good, mwenye umri wa miaka 37, aliyefariki Jumatano baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya gari lake.
Gavana wa Minnesota, Tim Walz, amelaani kitendo cha utawala wa Trump kuzuia maafisa wa jimbo kushiriki katika uchunguzi, akisema kuwa ni haki ya jimbo kujihusisha na kesi hiyo.
Hata hivyo, Makamu wa Rais wa Marekani amesisitiza kuwa uchunguzi huo ni suala la serikali kuu.
Maafisa wametoa maelezo tofauti kuhusu tukio hilo.
Utawala wa Trump unasema afisa wa ICE alitenda hivyo kwa kujilinda, huku maafisa wa eneo hilo wakidai kuwa mwanamke huyo hakuwa tishio lolote.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem, amedai kuwa afisa wa ICE alimpiga Good mara kadhaa kwa sababu alikuwa anajaribu kumgonga afisa huyo na gari lake.
Bodi ya Ujasusi ya Shirikisho la Marekani (FBI) imesema itachunguza tukio hilo, huku Idara ya Kuzuia Uhalifu ya Minnesota (BCA) ikisema awali FBI ilikubali kufanya uchunguzi wa pamoja na jimbo, lakini baadaye ilibadilisha msimamo na kuzuia upatikanaji wa nyaraka na ushahidi muhimu.
Kutokana na hali hiyo, BCA imesema imejiondoa kutoka katika uchunguzi huo, kwa kusita, ikisema kuwa bila kupata nyaraka na ushahidi wote, haiwezekani kushiriki kikamilifu.
Soma pia:
Moto wa nyikani wateketeza eneo la makazi Australia
Raia wa Australia wamewekwa katika tahadhari kali kufuatia kuendelea kwa moto wa misituni unaoteketeza makazi na mali katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, huku wakionyeshwa haja ya kujiandaa na hasara kubwa ya mali au madhara makubwa zaidi.
Katika jimbo la Victoria, mamlaka zimeonya kuwa wimbi kali la joto linaloikumba Australia linaongeza hatari ya milipuko mikubwa ya moto wa misitu.
Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, siku za Ijumaa na Jumamosi zinatarajiwa kushuhudia viwango vya juu zaidi vya joto kuwahi kurekodiwa katika majimbo na maeneo mengi ya nchi hiyo.
Victoria na Australia Kusini zimetajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyo katika hatari kubwa zaidi, kutokana na mchanganyiko wa joto kali na upepo mkali.
Serikali ya jimbo la Victoria imetangaza marufuku kamili ya kuwasha moto, huku maeneo yote ya jimbo hilo yakiwekwa katika kiwango cha juu kabisa cha hatari ya moto, kinachojulikana kama “hatari kali” au “hatari mbaya sana”.
Akizungumza na ABC, Mkuu wa Mamlaka ya Zimamoto ya Victoria (CFA), Jason Heffernan, alisema kuwa wakazi wanapaswa kujiandaa kwa hali mbaya zaidi.
“Wakazi wa Victoria wanapaswa kujitayarisha kupoteza mali au hata madhara makubwa zaidi,” alisema.
Moto mkubwa wa misituni ulioripotiwa karibu na Longwood, katikati ya Victoria, umeunguza takribani hekta 36,000 za ardhi.
Katika mji mdogo wa Ruffy, angalau nyumba 20 zimeripotiwa kuharibiwa kabisa na moto huo.
Nahodha wa kikosi cha zimamoto cha Ruffy, George Noye, alisema mji huo umeathirika kwa kiwango kikubwa.
“Barabara kuu ya mji inaonekana kana kwamba bomu limelipuliwa; tumepoteza hata shule,” alisema.
Hata hivyo, alibainisha kuwa hadi sasa hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Wakati huohuo, Naibu Kamishna wa Polisi wa Victoria, Bob Hill, alisema watu watatu, watu wazima wawili na mtoto mmoja bado hawajulikani walipo katika eneo la Longwood.
Alisema maafisa wa usalama waliwahi kuzungumza na watu hao katika makazi yao siku iliyotangulia na kuwaonya watafute hifadhi, kwani ilikuwa imechelewa kuhamishwa. Hata hivyo, waliporejea baadaye, walikuta nyumba hiyo imeteketea kwa moto bila kuwapata watu hao watatu.
“Inawezekana wako salama na bado wako hai. Hatutaki kutoa hitimisho la haraka; tunaendelea kuchunguza kwa makini,” alisema Hill.
Katika eneo la Australian Capital Territory, linalojumuisha mji mkuu Canberra, marufuku kamili ya kuwasha moto imetangazwa kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka sita.
Kwa upande mwingine, jiji la Sydney linatarajiwa kushuhudia joto la hadi nyuzi joto 42 siku ya Jumamosi, kabla ya kushuka hadi takribani nyuzi joto 26 siku ya Jumapili.
Soma pia:
Trump atishia kufanya mashambulizi mengine nchini Nigeria
Rais Donald Trump ameonya kuwa Marekani inaweza kufanya mashambulizi mengine ya anga nchini Nigeria ikiwa mauaji ya Wakristo yataendelea.
Katika mahojiano na gazeti la New York Times, lililochapishwa siku ya Alhamisi, Bw Trump aliulizwa ikiwa mashambulizi ya hivi majuzi ya anga ya Marekani katika jimbo la Sokoto nchini Nigeria yakilenga wanamgambo wa wenye itikadi kali yalikuwa sehemu ya operesheni kubwa zaidi ya kijeshi.
Akijibu swali hilo, Trump alisema: “Ningependelea liwe shambulio la mara moja.” Hata hivyo, aliongeza kwa msisitizo: “Iwapo mauaji dhidi ya Wakristo yataendelea, basi yatakuwa mashambulizi ya mara kwa mara.”
Utawala wa Trump hapo awali umeikosoa vikali serikali ya Nigeria kwa kile ilichokitaja kuwa kushindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya mashambulizi ya wanamgambo wa jihadi.
Aidha, utawala huo umedai kuwa kinachoendelea nchini humo ni aina ya “mauaji ya kimbari”.
Shambulio la anga lililofanywa na Marekani lilitekelezwa usiku wa Krismasi, wiki chache baada ya Rais Trump kutoa onyo kuwa angechukua hatua dhidi ya Nigeria kufuatia madai hayo.
Hata hivyo, serikali ya Nigeria imekanusha madai hayo, ikieleza kuwa hali ya ukosefu wa usalama nchini humo inawaathiri wananchi wa dini zote, na kwamba vurugu hizo hazilengi Wakristo pekee.
Kufuatia hali hiyo, Nigeria imeendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kiusalama na Marekani. Akizungumza na BBC, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Yusuf Maitama Tuggar, alisema kuwa shambulio la usiku wa Krismasi lilikuwa ni “operesheni ya pamoja” na halikuhusishwa na dini yoyote maalum.
Kwa upande wao, maafisa wa serikali ya Nigeria walisema kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa “idhini kamili” ya Rais Bola Ahmed Tinubu, likishirikisha kikamilifu majeshi ya ulinzi na usalama ya Nigeria.
Baada ya mashambulizi hayo ya anga, Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth, aliandika ujumbe kwenye mtandao wa X akisema, “Mengine yanakuja,” huku akitoa shukrani kwa serikali ya Nigeria kwa msaada na ushirikiano wake.
Hata hivyo, bado haijabainika iwapo kauli hiyo inaashiria mipango ya mashambulizi zaidi katika siku zijazo.
Soma pia:
Baraza la Mawaziri Tanzania: Simbachewene atemwa Makonda apandishwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na uteuzi wa viongozi mbalimbali wa serikali.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Januari 8, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, Rais Samia amemtengua Mhe. George Simbachawene katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumteua Mhe. Patrobas Katambi kushika wadhifa huo.
Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Katambi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.
Ikumbukwe kuwa Mhe. Simbachawene aliteuliwa kuiongoza wizara hiyo mwezi Desemba 2025, kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika mabadiliko hayo, Rais Samia pia amemteua Katibu wa Rais Waziri, Mhe. Rajab Salum, kuwa Balozi.
Aidha, Mhandisi Zena Ahmed Said na Meja Jenerali Mbaraka Naziad Mkeremy nao wameteuliwa kuwa Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, Rais Samia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu (Kazi Maalum).
Kabla ya uteuzi huo, Prof. Kabudi alikuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Katika nafasi ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Rais amemteua Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Mhe. Dennis Lazaro Londo, akichukua nafasi ya Mhe. Katambi.
Awali, Mhe. Londo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Aidha, Rais Samia amemteua Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud (Mbunge wa Chaani) kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mhe. Ayoub ana uzoefu mkubwa wa kiuongozi, akiwa amewahi kuhudumu kama Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.
Mabadiliko haya yanafanyika miezi michache baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuapishwa kuendelea kuiongoza nchi, hatua inayotafsiriwa kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kasi ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa maslahi ya wananchi.
Maandamano ya siku ya Uchaguzi wa Oktoba 29,2025 yaliua vijana na mataifa ya kigdeni yalikemea vikosi vya usalama kwa kutumia nguvu kupita kiasi kudhibiti waandamanaji.
Haya yakijiri Jopo lilitwika jukumu la kuchunguza kilichotokea siku hiyo bado linaendelea na utathmini wake likitarajiwa kuwasilisha mapendekezo yao kwa umma.
Serikali ya Venezuela yaanza kuwaachia wafungwa wa kisiasa
Serikali ya mpito nchini Venezuela imeanza kuwaachilia watu wanaosadikiwa kuwa wafungwa wa kisiasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, katika kile maafisa walichoeleza kuwa ni ishara ya nia njema.
Wizara ya mambo ya nje ya Uhispania ilisema raia wake watano, akiwemo raia mmoja aliye na uraia pachai, wameachiliwa huru.
Mwanaharakati wa haki Rocio San Miguel anadhaniwa kuwa miongoni mwa wafungwa walioachiwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika msako mkali katika mji mkuu wa Caracas siku ya Jumamosi ili kukabiliana na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya mjini New York.
Kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa nchini Venezuela limekuwa hitaji la muda mrefu la Marekani, hasa wakati wa ukandamizaji mkubwa wakati wa uchaguzi au maandamano.
Jorge Rodriguez, mkuu wa Bunge la Venezuela na kaka yake rais wa mpito Delcy Rodriguez, alitangaza kwenye televisheni ya serikali kwamba "idadi kubwa" ya wafungwa wataachiliwa, bila kutaja idadi au utambulisho wao.
Mamia ya wafungwa wa kisiasa wanazuiliwa katika magereza ya Venezuela, lakini ni wachache tu wameachiliwa kufikia sasa .
Pia unaweza kusoma:
Natumai hujambo
Karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 09 Januari 2026.