Mfanya magendo afichua namna anavyowasaidia watu kufika Ulaya

    • Author, Andrew Harding, Khue Luu and Patrick Clahane
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya miezi kadhaa ya simu na mkutano mmoja mfupi, mahojiano yetu na yeye yanafanyika katika chumba cha hoteli, katika mji wa kaskazini mwa Uingereza ambao hatutoutaja kwa jina.

Katika miezi ya kwanza ya mwaka huu - Vietnam imeibuka ghafla bila kutarajiwa - kama chanzo cha wahamiaji wanaotaka kuingia Uingereza kinyume cha sheria kwa boti ndogo.

Wahamiaji wengi wa Vietnam wanasema kushindwa kwa biashara na madeni nyumbani kwao, ndio sababu ya kutafuta kazi nchini Uingereza.

Wataalamu wa uhamiaji wanasema mara nyingi wahamiaji hutafuta viza halali za kazi katika nchi za Ulaya, kama Hungary.

Hapa ndipo operesheni ya kughushi ya Thanh inapokuja. Anasaidia kuunda nyaraka bandia zinazohitajika ili kupata viza halali ya kazi.

“Siwezi kuhalalisha uvunjifu wa sheria. Lakini ni biashara yenye faida kubwa,” anasema Thanh, akisisitiza kwamba hatoi nyaraka za kughushi kwa watu wanaotafuta viza za Uingereza.

Kupitia mahojiano yetu na walanguzi wa Kivietinamu na wateja wao - watu hulipa kati ya dola za kimarekani 15,000 na 20,000 kusafiri kutoka Vietnam hadi Ulaya na kisha kuvuka bahari kuingia Uingereza.

Ni biashara hatari. Zaidi ya watu 50 wamekufa wakivuka maji kwa boti mwaka huu akiwemo Mvietnam mmoja, na kuufanya mwaka 2024 kuwa mbaya hadi sasa.

Thanh alituambia, alisafiri kwa ndege kwa mara ya kwanza kutoka Vietnam hadi Hungary kwa viza halali - ingawa aliipata kwa kutumia hati ghushi.

Kisha alisafiri kwa ndege hadi Paris na kukaa siku chache katika nyumba iliyoandaliwa na genge la magendo la Kivietinamu nje kidogo ya jiji.

Kisha alichukuliwa akiwa na watu wengine katika basi dogo hadi ufuoni, na kukabidhiwa mikononi mwa genge moja la Kikurdi linalodhibiti mashua hizo. Malipo ya kuvuka kwa mafanikio hufanywa baada ya kuwasili nchini Uingereza.

Na Thanh alikuwa na bahati, kuwakwepa polisi wa Ufaransa waliokuwa wakishika doria kwenye ufuo wa Calais, na alivuka kwa mashua ya upepo.

Pia unaweza kusoma

Madai ya Uongo

Thanh aliomba hifadhi alipohojiwa na afisa wa uhamiaji wa Uingereza - akielezea kuwa aliondoka Vietnam kwa sababu alikuwa na deni kwa majambazi baada ya biashara kufeli. Alisema maisha yake yalikuwa hatarini. Alimwambia afisa huyo alisafirishwa kwa nguvu hadi Uingereza ili kufanya kazi katika genge ili kulipa deni lake.

Tumesikia hadithi kama hizo kutoka kwa Wavietnamu wengine tuliokutana nao kaskazini mwa Ufaransa.

Azungumza ukweli!

Akiwa ameketi mbele yangu kwenye sofa, Thanh alikiri kwamba hakuwa amesafirishwa kwa nguvu kuja Uingereza. Alikuwa ametunga hadithi hiyo kama sehemu ya dai lake la kupata hifadhi. Na alikwenda mbali zaidi, akidai wahamiaji wote wa Kivietinamu aliowajua waliambiwa watoe simulizi za uwongo kama hiyo.

“Ndiyo. Ni uongo. Sikusafirishwa kwa nguvu kupitia magendo,” anasema.

“Hivyo ndivyo inavyofanyika. [Watu hudanganya kuhusu kusafirishwa] ili wafanikiwe katika mchakato wa kupata hifadhi ya usalama,” anasema.

Kazi ya Genge

Safari ya Thanh kuja Ulaya, inaanza huko Vietnam kwa mara ya kwanza mwaka 2007. Alikuwa na umri wa miaka 20. Aliacha shule na kufanya kazi katika kiwanda cha nguo kusini mwa nchi. Lakini familia yake ilimtaka aende nje ya nchi, Ulaya, kutafuta mishahara mazuri.

“Nilikopa dola za kimarekani 6,000 kutoka kwa jamaa na majirani [ili kulipia safari].”

Safari hiyo ilimpeleka kwanza kwenye kazi ya shambani nje ya Prague, katika Jamhuri ya Cheki. Alitumia zaidi ya mwaka mmoja kuchuma vitunguu na mboga kabla ya kuamua kufanya kazi nchini Ujerumani. Alivuka mpaka kinyume cha sheria kwa basi dogo, Thanh anasema aliitupa pasi yake ya kusafiria na nyaraka zingine, na kuchagua jina jipya.

Alipofika Ujerumani aliiambia mamlaka kwamba ana umri wa miaka 14. Wasafirishaji haramu ambao walimtoza dola 1,000 (£771) ili kumpeleka Ujerumani walimshauri itakuwa rahisi akisema yuko chini ya miaka 16.

“Nilionekana kijana siku hizo. Hakuna aliyenipinga kwa hilo.”

Thanh anasema alikaa Ujerumani kwa takribani miaka miwili. Akapata rafiki wa kike, na akawa baba. Lakini msako mkali wa polisi ulianza kuathiri biashara yake ya kuuza sigara. Mwaka 2010, aliamua kwenda Uingereza.

Alivuka hadi Ufaransa bila familia yake mpya, alitupa hati zake za Ujerumani na kubuni utambulisho mwingine wa uwongo.

Nyakati hizo, maelfu ya wahamiaji walikuwa wakijaribu kuvuka bahari kwenda Uingereza kwa kujificha kwenye malori na vyombo vya usafiri. Thanh anasema alifanya majaribio kadhaa lakini hakufanikiwa.

Akiwa amekwama nchini Ufaransa, akipiga kambi katika msitu karibu na Dunkirk, Thanh alipewa kazi na wasafirishaji wa watu wa Vietnam.

Miaka michache baadaye, genge hilo - la Thanh lilihusika katika vifo vya wahamiaji 39 wa Kivietinamu ambao walikosa hewa, ndani ya lori huko Essex.

Aliinuka ndani ya genge na kuwa mmoja wa washiriki wakuu. Lakini baadaye alikamatwa, na kuhukumiwa, na kufungwa kwa miaka kadhaa, baada ya kuachiwa alirudi Vietnam. Anasema aliachana na ulimwengu wa magendo. Lakini, kama anavyosema, sifa yake ilimrudisha.

"Watu wa Ulaya waliwasiliana nami wakiomba msaada," alituambia.

"Nilisaidia watu wapatao 1,000 kufika Uingereza kwa mafanikio, kwa hivyo nilijulikana sana kwa mafanikio hayo."

Kughushi nyaraka

Mwaka 2017, anasema aliingia tena kwenye biashara ya magendo - wakati huu, Thanh hasafirishi watu, bali anaghushi hati kwa ajili yao.

Taarifa za benki, hati za malipo, ankara za kodi, chochote ambacho balozi za Ulaya zinahitaji kwa watu wanaoomba viza ya wanafunzi, kazi, au biashara.

“Tulifanya kazi na wafanyakazi katika benki fulani, wafanyakazi wa benki huonyesha maelezo [ya uongo] kwa wafanyakazi wa ubalozi. Tumefanya kazi na benki nyingi za Vietnam.”

Wakati huo akiwa Vietnam, Thanh alikuwa na familia mpya huko. Lakini mapema mwaka huu, aliamua kuondoka.

Thanh anajionyesha kama mtu aliyetubu ambaye sasa anajutia maisha yake ya uhalifu na anataka kuzuia watu wengine wa Vietnam kufanya makosa kama yake. Zaidi ya yote, anataka kuwaonya dhidi ya kuja Uingereza kinyume cha sheria, akisema haifai.

"Nataka tu watu nchini Vietnam waelewe kwamba haifai kukopa pesa nyingi kusafiri hapa. Si rahisi sana kwa wanaofika kinyume cha sheria kupata kazi au kupata pesa.

Thanh anahimiza Uingereza na serikali za Ulaya kufanya juhudi kubwa zaidi kutangaza ukweli kwamba hakuna kazi hapa kwa wahamiaji haramu. Pia analaumu magenge ya magendo kwa kuwadanganya wateja wao kuhusu hali halisi na fursa.

Tunapomuuliza Thanh, kuhusu unafiki wake na kuendelea kwake kujihusisha na mambo ya magendo, anashtuka.

“Hatumlazimishi mtu yeyote kufanya anachofanya. Wanatuomba msaada, kama katika biashara yoyote. Hakuna biashara haramu. Ikiwa una sifa nzuri, wateja wanakuja kwako, bila vitisho au vurugu."

“Kama ningeweza kuanza tena, nisingeondoka Vietnam. Nadhani maisha yangu yangekuwa bora zaidi ikiwa ningebaki nyumbani. Nimekumbana na misukosuko mingi sana. Sina mustakabali mzuri.”

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah