Maandamano Iran: Kwa nini Trump anasema Iran imevuka 'mstari mwekundu'?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani Donald Trump amerudia maonyo yake ya kutaka kuingilia masuala ya Iran, akisema anaweza kuchukua hatua kabla ya kukutana na maafisa wa Iran.

Amesema maafisa wa Iran wanataka mazungumzo. Hata hivyo, hajasema ni hatua gani anazokusudia kuchukua.

Kundi la Waangalizi lenye makao yake Marekani linasema zaidi ya watu 500 wamefariki katika maandamano Iran tangu Desemba 28.

Rais Donald Trump tayari ameonya kwamba Marekani itaingilia kati kuwalinda waandamanaji nchini Iran ikiwa watauawa.

Alipoulizwa ikiwa Iran imevuka mstari mwekundu, amesema, "Ndiyo, inaonekana imevuka mstari mwekundu."

"Tunaangalia hili kwa umakini mkubwa. Jeshi pia linaangalia hili kwa umakini sana. Tunafikiria hatua kadhaa. Tutafanya uamuzi," amesema Trump.

Video imeibuka ya chumba cha kuhifadhia maiti cha muda kilichowekwa nje kidogo ya mji mkuu wa Iran, Tehran. Wairani wengi wamekwenda huko kuwatafuta wapendwa wao. Timu ya BBC imeona miili 180 ikiwa imefungwa nguo nyeupe.

Huku kukiwa na machafuko yanayoendelea nchini Iran, serikali inaandaa mazishi. Kulingana na televisheni rasmi ya Iran, watu walibeba majeneza ya vikosi vya usalama na raia katika majimbo 10 kwa ajili ya mazishi.

Iran inailaumu Marekani na Israel kwa vifo hivi.

Wataalamu na mashuhuda wanasema maandamano ya kupinga serikali nchini Iran yamekuwa makali sana kiasi kwamba hayajawahi kuonekana hapo awali katika historia ya miaka 47 tangu mapinduzi ya kiislamu ya Iran.

Watu katika miji kote nchini wanajitokeza mitaani kuelezea hasira zao. Rais Donald Trump amesema Marekani iko tayari kuwasaidia wale wanaopinga utawala wa Iran.

Maafisa wa Iran wameonya kwamba ikiwa Marekani itashambulia, nayo itawashambulia washirika wa Marekani katika eneo hilo.

Maandamano kote nchini

Wataalamu wanaamini ukubwa na uzito wa machafuko ya sasa nchini Iran ni wa kihistoria.

Mtafiti wa sosholojia Eli Khorsandfar, anasema ni “maandamano yaliyoenea hadi miji ambayo hujawahi kuisikia.”

Kumewahi tokea maandamano nchini Iran hapo awali. "Harakati za Kijani" za 2009, yalikuwa ni maandamano ya watu wa tabaka la kati wakipinga udanganyifu katika uchaguzi. Ingawa yalikuwa mkubwa, lakini yalifanyika katika miji mikubwa pekee.

Maandamano ya sasa pia yanaonekana tofauti na maandamano ambayo yalifanywa katika maeneo maskini zaidi nchini mwaka 2017 na 2019.

Maandamano ya hivi sasa yanayofanana sana na yalitokea mwaka 2022. Machafuko hayo yalizuka baada ya kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22.

Mahsa Amini, mwanamke Mkurdi, alikamatwa na polisi wa maadili wa Iran kwa kutokuvaa hijabu yake vizuri. Alifariki akiwa chini ya ulinzi wao.

Ripoti kadhaa zilisema maandamano yaliyozuka baada ya kifo cha Amini yalifikia kilele siku sita baadaye. Kwa upande mwingine, maandamano ya sasa yameenea sana na yamekuwa yakiendelea kwa kasi tangu yalipoanza Desemba 28.

'Dikteta aondoke'

Kama maandamano ya 2022, waandamanaji sasa wanadai mabadiliko katika utawala.

"Maandamano ya 2022 yalianza na masuala ya wanawake. Lakini haya ya sasa yameleta masuala mengi zaidi. Desemba 2025, maandamano yalianza kuhusu masuala ya kiuchumi. Ndani ya kipindi kifupi, maandamano yanataka mabadiliko ya utawala," anasema Khorsandfar.

Mwishoni mwa Desemba, wafanyabiashara katika soko kuu la Tehran waligoma, wakitaja kiwango kikubwa cha ubadilishaji wa rial ya Iran dhidi ya dola ya Marekani.

Maandamano haya pia yameenea hadi maeneo maskini zaidi ya magharibi mwa nchi.

Tangu wakati huo, waandamanaji wamekuwa wakiandamana mitaani, wakiimba "Dikteta lazima aondoke!" Waandamanaji sasa wanadai mwisho wa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na mwisho wa utawala wa kidini.

Wanataka Pahlavi awe mtawala?

Hakuna kiongozi aliyeongoza maandamano ya mwaka 2022. Ndiyo maana yaliisha haraka sana. Lakini, kinyume chake, viongozi mashuhuri kama Reza Pahlavi wanashiriki kikamilifu katika maandamano ya sasa.

Baba yake, Reza Shah Pahlavi, aliondoka madarakani baada ya Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979. Reza Pahlavi, ambaye kwa sasa yuko uhamishoni, anajaribu kuongoza harakati hii kutokea mbali. Ndiyo maana maandamano haya yanaonekana kuendelea kwa muda mrefu.

Kauli mbiu za kutaka kurejea kwa utawala wa familia ya Pahlavi zinasikika zaidi kuliko hapo awali. Pahlavi, ambaye anaishi Marekani, amejitangaza kuwa Shah wa Iran.

"Najiandaa kurudi Iran, na ni hivi karibuni," Pahlavi amesema, akiwataka watu waingie mitaani.

Ujumbe wake, unaowataka watu kujitokeza mitaani, unasambazwa sana na wengi nchini Iran. Vijana wanahimizana kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii kujiunga na maandamano haya.

Ukali wa maandamano ya hivi karibuni katika miji kama Tehran unaonyesha jinsi ombi la Pahlavi lilivyokuwa na ufanisi.

Trump atishia kuingilia kati

Jambo lingine linalotofautisha maandamano ya 2022 na maandamano yanayoendelea sasa ni Marekani. Tofauti na maandamano ya awali, maandamano ya mwaka huu yanaonekana kupata uungwaji mkono kutoka Ikulu ya Marekani.

Trump anaonyesha uungaji mkono kwa waandamanaji na anatishia kushambulia maeneo ya serikali ikiwa atalazimika. Hili halijawahi kutokea hapo awali.

Mnamo 2009, wakati wa maandamano dhidi ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa rais wa Iran, waandamanaji waliimba, "Obama, Obama... uko pamoja nao au pamoja nasi?"

2009, Barack Obama alikuwa Rais wa Marekani. Baadaye alionyesha majuto makubwa kwa kutowaunga mkono hadharani waandamanaji wakati huo.

Rais wa Iran Massoud Pezeshkian anasema maadui wa Iran wanageuza na kudhibiti maandamano haya kwa faida yao.

Washirika wa Iran wamepungua katika siku za hivi karibuni, jambo ambalo ni tatizo jingine kwa nchi hiyo.

Tofauti na maandamano ya 2022, maandamano ya mwaka huu yalianza mara tu baada ya vita vya siku 12 na Israel, na mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran.

"Matukio haya, yangeipa serikali ya Iran fursa ya kukuza aina ya umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa Iran. Lakini serikali ilishindwa kufanya hivyo," anasema mwandishi wa habari Abbas Abdi.

Baadhi ya wataalamu wanasema mashambulizi makubwa dhidi ya Iran mwaka jana, yameharibu sifa na jina la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), machoni pa watu wa Iran, kikosi kikubwa cha jeshi nchini humo.

Kutokana na maandamano ya 2022, Khorsandfar anaona mabadiliko ya kudumu kutokana na ukandamizaji wa maandamano ya sasa.