Maandamano Iran: Jeshi linasimama wapi na serikali inataka nini?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika siku ya kumi na nne ya maandamano ya kitaifa nchini Iran, jeshi la Jamhuri ya Kiislamu limetoa taarifa kali likionya kuhusu "njama" ya Israel na "makundi ya kigaidi" ya "kuvuruga usalama wa umma."

Jeshi kwa kushirikiana na vikosi vingine vya usalama - limetangaza kwamba litalinda "maslahi ya kitaifa, miundombinu ya kimkakati ya nchi, na mali ya umma.”

Lakini taarifa hiyo haielezi ni jinsi gani jeshi litashirikiana na "vikosi vingine" kudhibiti hali ya usalama. Kwa hivyo, ni muhimu kupitia uingiliaji kati wa kijeshi wakati wa maandamano ili kuelewa njia ambazo ushirikiano huu unaweza kufanyika.

Wakati wa maandamano ya Novemba 2019, ambayo yalisababisha vifo vya watu wengi, taarifa maalum zilitolewa kuhusu jinsi jeshi lilivyoingilia kati katika kukabiliana na waandamanaji.

Wiki moja baada ya maandamano kumalizika, Abdolreza Rahmani Fazli, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa, alifichua jukumu la jeshi katika "usafirishaji, upangaji, na usaidizi" kwa vyombo vya usalama.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya Hassan Rouhani alisema, "katika wakati ambapo tulikuwa na uhaba wa polisi, tulileta jeshi kulinda maeneo nyeti ili jeshi la polisi liwe huru na liweze kwenda sehemu tofauti."

Katika taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu, msisitizo wa kusaidia "vikosi vingine vya usalama" kulinda "miundombinu ya kimkakati na mali ya umma" unaonyesha dhamira kama hiyo: Wanajeshi watachukua jukumu la kulinda vituo nyeti na majengo ya serikali na polisi wataingia mitaani.

Jeshi hushughulikia maandamano?

Kwa serikali ya Iran sio jambo la kawaida kutumia wanajeshi kukabiliana na maandamano.

Kwa mfano, mwishoni mwa maandamano ya Januari 2017, ambayo yalifanyika kwa mara ya kwanza katika miji zaidi ya 100, jeshi lilionyesha utayari wake wa kuwasaidia polisi, lakini usaidizi huu hautekelezwa kivitendo.

Wakati huo, Abdolrahim Mousavi, kamanda wa jeshi, alisema katika ujumbe kwa Hossein Ashtari, kamanda wa jeshi la polisi wakati huo: "Ikihitajika, wenzako katika jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran watasimama pamoja na mashujaa katika polisi mbele ya wale waliodanganywa na shetani mkuu."

Ujumbe huo ulisisitiza "utayari wa jeshi" kutekeleza maagizo ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu "katika misheni yoyote."

Ujumbe kutoka kwa kamanda mkuu wa jeshi ulitafsiriwa kwamba jeshi liko tayari kuingilia kati katika kuzuia waandamanaji, lakini Ali Khamenei hakuona uingiliaji kati huo kuwa muhimu.

Uchunguzi kuhusu maandamano ya mwaka 2009 hauonyeshi dalili zozote za matumizi ya vikosi vya kijeshi katika kukabiliana na waandamanaji, hata katika hali ngumu katika mji mkuu.

Hassan Abbasi, mwanaharakati wa vyombo vya habari vya kihafidhina ambaye wakati huo alikuwa karibu na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, alielezea Julai 2010 kuwa jeshi "liko kimya katika kambi zake, na ikiwa litachukua hatua, halitapiga kelele."

Matamshi hayo yenye utata, ambayo yalitolewa kwa hadhira ndogo, yaliripotiwa katika vyombo vya habari miaka kadhaa baadaye Agosti 2016, na kusababisha majibu kutoka kwa makamanda wa kijeshi.

Katika moja ya majibu, Ahmad Reza Pourdastan, kamanda wa Vikosi vya Ardhini wakati huo, alisema kauli za Hassan Abbasi zilitolewa "bila ufahamu wa misheni za vikosi vya jeshi," kauli ambayo ilionyesha wazi kwamba huo, jeshi halikuingia mitaani."

Sheria zinaruhusu matumizi ya jeshi?

Kifungu cha 143 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu kinasema wajibu wa jeshi ni "kulinda uhuru wa eneo na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu."

Kwa msingi huu, inaonekana katiba iliandikwa kwa njia ambayo, ikiwa ni lazima, kuna uwezekano wa kutumia jeshi kukabiliana na vitisho dhidi ya "mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu."

Kwa kuzingatia ukweli kwamba serikali ya Iran inasema waandamanaji wa mitaani ni maadui wa mfumo huo, bila shaka inaamini vikosi vya jeshi vinawajibika kukabiliana nao wakati wa uhitaji.

Kifungu cha 150 cha Katiba pia kinasema wajibu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ni “kulinda mapinduzi na mafanikio yake,” hilo halitofautiani sana, na wajibu wa “kulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu”.

Kwa maneno mengine, ikiwa watawala wa Jamhuri ya Kiislamu watataka jeshi lijihusishe katika masuala ya kisiasa na usalama, wanaweza kuhalalisha uingiliaji kati kwa urahisi kwa kutaja Kifungu cha 143 na jukumu la jeshi la kulinda "mfumo."

Hata hivyo, hamu kama hiyo haijawahi kuwepo miongoni mwa watawala.

Serikali ina wasiwasi kutumia jeshi?

Maafisa wakuu wa serikali ya Iran, katika taarifa rasmi, wamekuwa wakielezea jeshi kama kikosi kinachoaminika. Jeshi la sasa haliwezi kulinganishwa, na jeshi la wakati wa vita vya Iran-Iraq, ambapo maafisa wake wengi walipewa mafunzo wakati wa utawala wa Pahlavi.

Haiwezi kusahaulika kwamba miaka 47 baada ya mapinduzi ya 1979, idadi kubwa ya wale waliojiunga na jeshi kabla ya mapinduzi hawapo tena jeshini na wamestaafu.

Kwa maneno mengine, isipokuwa watu wachache, maafisa wote katika jeshi wamefunzwa kwa itikadi kali wakati wa enzi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Licha ya haya yote, inaonekana kwamba serikali ya Iran bado haiwaamini wanajeshi wake kama vile inavyoziamini "taasisi zake za mapinduzi."

Machoni mwa watawala wa Iran, kutuma vikosi vya jeshi kukabiliana na waandamanaji ni hatua hatarishi, hasa kwa kuwa vikosi hivi havijafunzwa kwa ajili ya kuzuia maandamano mijini.

Kutokana na hali hii, inaonekana kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mwelekeo wa kutumia jeshi kukabiliana na waandamanaji wa mitaani, isipokuwa katika hali mbaya ya "uhaba wa polisi" na ikifika hatua taasisi za usalama zikiwa na wasiwasi kuhusu kuanguka kwa "maeneo nyeti."

Wasiwasi ambao umekuwa mkubwa sana katika maandamano ya hivi karibuni, kutokana na idadi kubwa ya mashambulizi dhidi ya majengo ya serikali.