Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano ya Iran hayajawahi kushuhudiwa katika historia
Maandamano dhidi ya serikali nchini Iran yamefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya miaka 47 ya Jamhuri ya Kiislamu, kulingana na wataalamu wengi na mashahidi wa macho.
Jiyar Gol, mwandishi wa BBC kwa Huduma ya Kiajemi, anasema idadi ya vifo huenda ikawa imefikia maelfu, akiongeza kuwa ingawa serikali imewahi kutumia nguvu hapo awali, safari hii hali ni ya kipekee na haijawahi kutokea.
Makadirio ya hivi karibuni ya idadi ya watu waliouawa katika maandamano ya kitaifa nchini Iran ni 2,571, kulingana na Shirika la Habari la Human Rights Activists (HRANA) lenye makao yake nchini Marekani.
Idadi hiyo inajumuisha waandamanaji 2,403, watu 147 waliokuwa wakihusishwa na serikali, watoto 12 walio chini ya umri wa miaka 18, na raia tisa wasio waandamanaji.
Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa afisa mmoja wa usalama wa Iran alisema idadi ya vifo huenda ikawa karibu watu 2,000.
Chanzo hicho kilisema makadirio hayo yanajumuisha wanajeshi wa usalama pamoja na raia, na kuwalaumu "magaidi" kwa vifo hivyo.
Wakati watu wakiendelea kujitokeza barabarani katika miji mbalimbali nchini humo, Rais wa Marekani Donald Trump ametishia "kupiga kwa nguvu mahali panapoumiza zaidi" iwapo mamlaka zitawadhibiti kwa nguvu waandamanaji, na kusema kuwa Marekani "iko tayari kusaidia."
Rais wa Marekani ameahidi kuchukua "hatua kali" endapo waandamanaji watanyongwa kama inavyotarajiwa.
Iwapo hatua hizo zitatekelezwa, maafisa wa Iran wameapa kujibu kwa kushambulia washirika wa Marekani na maslahi yake katika eneo hilo.
Lakini ni kwa namna gani maandamano haya na mwitikio wa serikali ya Iran dhidi ya ghasia hizi yanatofautiana na maandamano ya awali yaliyowahi kutokea nchini humo?
End of Unaweza kusoma
Wataalamu wanasema ukubwa na kuenea kwa maandamano ya mwaka huu hakujawahi kushuhudiwa hapo awali.
Mtafiti wa masuala ya kijamii, Eli Khorsandfar, anasema kuwa ingawa maandamano yamefanyika katika miji mikubwa ya Iran, pia yamesambaa hadi katika miji midogo, "ambayo majina yake huenda wengi hawajawahi kuyasikia."
Iran tayari imewahi kushuhudia maandamano hapo awali. Harakati zilizoitwa Green Movement za mwaka 2009 zilisababisha maandamano ya tabaka la kati kupinga madai ya udanganyifu wa uchaguzi.
Ingawa yalikuwa makubwa kwa kiwango chake, yalijikita zaidi katika miji mikubwa.
Maandamano mengine makubwa ya mwaka 2017 na 2019 yalikuwa yamejikita zaidi katika maeneo yenye umasikini.
Maandamano ya hivi karibuni yanayoweza kulinganishwa zaidi na yalitokea mwaka 2022, wakati maandamano yalipozuka kufuatia kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 akiwa kizuizini.
Mwanamke huyo alikuwa amekamatwa na polisi wa maadili wa Iran kwa sababu ya namna alivyovaa hijabu.
Maandamano hayo yaliongezeka kwa kasi baada ya kifo cha Amini, na kufikia kilele chake siku sita baadaye, kulingana na ripoti mbalimbali.
Hata hivyo, maandamano ya sasa yanaonekana kuwa makubwa zaidi, yameenea kwa upana zaidi, na yanaendelea kukua kwa uthabiti tangu yalipoanza tarehe 28 Desemba.
"Kifo kwa dikteta"
Kama ilivyokuwa kwenye maandamano ya mwaka 2022, uasi wa sasa una mizizi katika malalamiko maalum ambayo kwa haraka yalibadilika na kuwa madai ya mabadiliko makubwa ya mfumo mzima wa utawala.
"Harakati za mwaka 2022 zilianza na suala la wanawake. Lakini pia zilijumuisha madai mengine mengi… Maandamano ya Desemba 2025 yalianza na masuala yaliyoonekana kuwa ya kiuchumi, na kwa muda mfupi sana yakaanza kuwasilisha ujumbe wa pamoja," anasema Khorsandfar.
Mwishoni mwa Desemba, wafanyabiashara wa soko (bazaar) waligoma katikati ya Tehran, wakipinga mabadiliko makubwa ya thamani ya sarafu ya Iran (rial) dhidi ya dola ya Marekani.
Maandamano hayo yalisambaa hadi katika maeneo duni zaidi magharibi mwa nchi. Kama ilivyokuwa mwaka 2022, majimbo ya Ilam na Lorestan yalikuwa miongoni mwa vituo vikuu vya maandamano.
Kuelekea mwisho wa Desemba, maandamano makubwa yalifanyika yakihusisha maelfu ya watu, huku mamilioni ya Wairani, wakiwemo wa tabaka la kati, wakikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kupanda kwa kasi kwa bei za bidhaa.
Tangu wakati huo, waandamanaji wamekuwa wakipaza sauti mitaani wakisema: "Kifo kwa dikteta!"
Wanadai kuondolewa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na utawala anaouongoza.
Mchango wa Pahlavi
Maandamano ya mwaka 2022 yalionekana kukosa uongozi na hatimaye yalipungua kwa haraka.
Kwa upande mwingine, maandamano ya sasa yanahusisha watu mashuhuri, akiwemo Reza Pahlavi aliye uhamishoni, mwana wa Shah aliyeondolewa madarakani mwaka 1979, ambao wanajaribu kuyaelekeza au kuyaongoza maandamano hayo kwa mbali.
Hili linaweza kueleza kwa kiasi fulani kwa nini maandamano haya yamekuwa ya kudumu zaidi.
Katika maandamano ya sasa, kauli zinazodai kurejea kwa familia ya Pahlavi zimesikika mara nyingi zaidi kuliko wakati wowote uliopita.
Pahlavi alijitangaza kuwa Shah wa Iran akiwa uhamishoni nchini Marekani.
Wito wake wa kuhimiza watu kupaza sauti mitaani umesambazwa kwa kiwango kikubwa. Vijana wa Iran wamekuwa wakihamasishwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii kushiriki katika maandamano.
Ukubwa wa maandamano ya hivi karibuni katika miji kama Tehran unaonesha ufanisi wa wito wa Pahlavi.
Wachambuzi wanasema kuwa, kutokana na hilo, uwepo wa kiongozi wa upinzani anayejulikana umeimarisha kwa baadhi ya waandamanaji wazo kwamba kuna mbadala unaowezekana endapo serikali ya sasa itaanguka.
Hata hivyo, wengine wanasema kuwa dalili zozote za uungwaji mkono kwa Pahlavi hazimaanishi lazima kuwepo kwa nia ya kurejesha utawala wa kifalme.
Badala yake, ni ishara ya kukata tamaa na kutafuta mbadala wowote dhidi ya utawala wa kidini, hasa kutokana na ukosefu wa viongozi wa upinzani wanaoonekana wazi na wa kiraia ndani ya nchi.
Tishio la Trump la kuingilia kati
Sababu nyingine inayotofautisha maandamano ya mwaka 2025 na yale ya 2022, ni nafasi ya Marekani.
Maandamano ya mwaka huu, tofauti na yale ya awali, yanaonekana kuwa na uungwaji mkono wa Ikulu ya White House.
Trump ametishia kushambulia utawala wa Iran akiwaunga mkono waandamanaji, jambo ambalo halijawahi kutokea hapo awali.
Wakati wa harakati za maandamano ya mwaka 2009 dhidi ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa urais, waandamanaji walikuwa wakipiga kelele wakisema:
"Obama, Obama, ama uko nao au uko nasi!"
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, aliyeingia madarakani mwaka 2009, baadaye alijutia kutowaunga mkono waandamanaji mitaani kwa uwazi zaidi wakati huo.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema maandamano hayo yanachochewa na "maadui wa Iran."
Hata hivyo, changamoto kwake ni kwamba nchi yake ina marafiki wachache zaidi kuliko ilivyokuwa katika miaka ya hivi karibuni.
Mamlaka ya Iran imepoteza washirika muhimu: Bashar al-Assad ameondolewa madarakani kama rais wa Syria, na Hezbollah nchini Lebanon pia imedhoofishwa kwa kiasi kikubwa na mashambulizi ya kijeshi ya Israel.
Athari za vita
Tofauti na maandamano ya mwaka 2022, maandamano ya mwaka huu yalitokea miezi baada ya vita vya siku 12 na Israel na mashambulizi yaliyo kufuatia ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Mwandishi Abbas Abdi anaamini kuwa matukio haya yalimpa mamlaka ya Iran fursa ya kuunda umoja na mshikamano wa kijamii, lakini serikali haikuyatumia vizuri.
Baadhi ya wataalamu pia wanasema kuwa pigo kubwa lililowakumba jeshi la Iran mwaka jana limevunja heshima na sifa ya Islamic Revolutionary Guard Corps kama taasisi kuu ya kijeshi nchini kwa macho ya Wairani.
Akivutiwa na hamasa ya maandamano ya mwaka 2022, Khorsandfar anaona mabadiliko ya kudumu katika maandamano ya sasa: Katika mahojiano na wanawake waliokuwa mitaani miaka mitatu iliyopita, wengi walimwambia kuwa mafanikio yao makubwa ilikuwa kuondoa hofu ya kutokuwa huru kutokana na serikali ya ukandamizaji.