Chile yatangaza “hali ya janga” baada ya moto wa misituni kuua takribani watu 18
Rais wa Chile, Gabriel Boric, ametangaza hali ya janga katika mikoa miwili ambako moto mkubwa wa misituni umesababisha vifo vya takribani watu 18.
Zaidi ya watu 50,000 wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao katika mikoa ya Ñuble na Biobío, iliyopo takribani kilomita 500 kusini mwa mji mkuu, Santiago.
Rais Boric alisema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kadiri shughuli za uokoaji na tathmini zinavyoendelea.
Moto hatari zaidi umeteketeza misitu mikavu iliyo karibu na jiji la pwani la Concepción, na kwa mujibu wa maafisa wa kushughulikia maafa, takribani nyumba 250 zimeharibiwa.
Vyombo vya habari vya ndani vimeonesha picha za magari yaliyoungua na kubaki mabaki barabarani.
Shirika la misitu la Chile, Conaf, lilisema kuwa zima moto walikuwa wakipambana na moto kote nchini siku ya Jumapili. Moto hatari zaidi, liliongeza, upo katika mikoa ya Ñuble na Biobío.
Moto umeteketeza ekari 21,000 katika mikoa hiyo miwili hadi sasa.
“Kwa kuzingatia uzito wa moto unaoendelea wa misituni, nimeamua kutangaza hali ya janga katika mikoa hiyo miwili,” Rais Gabriel Boric alisema katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa X.
Chini ya hali ya janga, majeshi ya Chile yanaweza kupelekwa kusaidia katika kudhibiti hali hiyo.
Sehemu kubwa ya uhamishaji wa wakazi ilifanyika katika miji ya Penco na Lirquén, kaskazini mwa Concepción, miji ambayo kwa pamoja ina wakazi wapatao 60,000.
Upepo mkali umechochea kuenea kwa moto huo, hali iliyochangiwa na joto kali la majira ya kiangazi, na hivyo kuhatarisha jamii na kuvuruga juhudi za kuzima moto.
Sehemu kubwa ya Chile iko chini ya tahadhari ya joto kali, huku halijoto zikitarajiwa kufikia nyuzi joto 38 za Selsiasi kati ya Santiago na Biobío katika siku chache zijazo.
Chile imekumbwa na msururu wa matukio ya moto mkubwa na mbaya katika miaka ya hivi karibuni, hali iliyochochewa zaidi na ukame wa muda mrefu.
Miaka miwili iliyopita, moto wa misituni uliua takribani watu 120 katika mkoa wa Valparaíso, karibu na mji wa Santiago.
Unaweza kusoma;