Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jeremy Bowen: Mgawanyiko ndani ya Israeli juu ya vita huko Gaza
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, International Editor
- Muda wa kusoma: Dakika 12
Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi na kwa mbali ndiye mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika siasa za nchi hiyo, hajabadilika kuhusu kile anachoamini kuwa ukweli wa msingi kuhusu vita vya Gaza.
Ameipa Israel na dunia ya nje ujumbe thabiti tangu Hamas iliposhambulia Israel karibu miaka miwili iliyopita.
Alieleza wazi msimamo wake alipotoa amri ya mashambulizi makubwa ya ardhini katika Ukanda wa Gaza tarehe 28 Oktoba 2023, wiki tatu baada ya mashambulizi hayo, na tangu wakati huo amekuwa akirudia ujumbe huo mara nyingi.
"Tutapigana kuilinda nchi yetu. Tutapigana bila kurudi nyuma. Tutapigana kwa nchi kavu, baharini na angani. Tutamwangamiza adui juu ya ardhi na chini ya ardhi. Tutapigana na tutashinda.
Hii itakuwa ushindi wa mema dhidi ya mabaya, wa mwanga dhidi ya giza, wa maisha dhidi ya kifo. Katika vita hivi tutasimama imara, tukiwa na mshikamano zaidi kuliko wakati wowote, tukiwa na uhakika juu ya haki ya sababu yetu."
Hotuba yake ilifuata misururu ya mwito wa kuhamasisha wa Winston Churchill mnamo Juni 1940 wa "tutapigana kwenye fukwe," baada ya kushindwa kwa Uingereza na Ujerumani kaskazini mwa Ufaransa na uokoaji wa wanajeshi zaidi ya 338,000 kutoka Dunkirk.
Kabla ya Churchill kuwaambia Waingereza katika hotuba yake maarufu kwamba "hatutawahi kujisalimisha," hakuwa amewaepusha na ukweli kwamba walikuwa wamepata "janga kubwa la kijeshi".
Hamas ilisababisha Israel kushindwa vibaya zaidi tarehe 7 Oktoba, na hofu kwamba waliweza kuvunja mipaka, kuua na kuchukua mateka wengi bado ni halisi sana kwa Waisraeli.
Ni jambo kubwa linalounda mitazamo ya vita hivyo, jinsi vinavyopiganwa, na jinsi vinavyoweza kuisha.
Waisraeli wachache sana wamewahi kutilia shaka kuwa sababu yao ni ya haki, lakini kauli ya Netanyahu kwamba "watakuwa na mshikamano zaidi kuliko wakati wowote" iko mbali kabisa na hali ya Israel karibu miaka miwili baadaye.
Israel kwa sasa imegawanyika zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake, na Netanyahu, ambaye tayari alikuwa kiongozi wa mgawanyiko mkubwa wakati Hamas iliposhambulia, anaongoza taifa lililogawanyika kwa mpasuko ambao sasa umegeuka mapengo.
Mitazamo ya Waisraeli kuhusu mateso ya Gaza
Kilele cha maandamano dhidi ya Netanyahu huko Tel Aviv, mamia ya Waisraeli walisimama kimya, kila mmoja akiwa ameshika bango lenye jina la mtoto wa Kipalestina aliyeuawa na Israel huko Gaza.
Mabango mengi yalikuwa na picha za wasichana au wavulana waliotabasamu, kando na tarehe ya kuzaliwa na tarehe ya kuuawa kwao.
Watoto wasio na picha waliwakilishwa na mchoro wa ua.
Maandamano ya kimya yenye lengo la kusitisha mauaji yanazidi kukua, mengine hufanyika nje ya vituo vya anga, ambako waandamanaji hujaribu kuvuta macho ya marubani wanaokwenda kushambulia Gaza lakini waandamanaji bado wanawakilisha mtazamo wa wachache.
Timina Peretz, mmoja wa waandaaji wa maandamano, anasema walianza baada ya Israel kuvunja usitishaji wa mapigano na Hamas tarehe 18 Machi na kurejea vitani.
"Tuligundua ni watoto wangapi walifariki ndani ya wiki hiyo hiyo. Nakataa kukaa kimya wakati haya yanatokea, mauaji ya kimbari na njaa ya watu…
Mtaani, tunapata mrejesho mzuri kutoka kwa watu, wengine wakisema 'asante'. Lakini pia tuna watu wengi wanaotutukana na kuchukizwa sana na picha hizi."
Nilimuuliza ikiwa wanaitwa wasaliti.
"Bila shaka, wengi sana. Wanasema kwamba tukifikiri namna hii au tukitenda hivi, basi tunapaswa kuhamia Gaza.
Hawawezi kuelewa kuwa wazo la msingi la kuukosoa serikali ni sehemu ya demokrasia."
Takwimu za maoni zilizokusanywa tangu Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) liliporejea vitani Gaza mwezi Machi, zikivunja usitishaji wa mwisho wa mapigano, zinaonyesha kuwa wengi wa Wayahudi wa Israel hawaguswi na mateso ya Wapalestina Gaza.
Utafiti wa siku tatu za mwisho wa Julai uliofanywa na Taasisi ya Demokrasia ya Israel ulionyesha kwamba asilimia 78 ya WaIsrael, ambao ni takriban asilimia 80 ya idadi ya watu, wanaamini kuwa Israel "inajitahidi kuepusha mateso yasiyo ya lazima kwa Wapalestina Gaza."
Watafiti walichagua swali la binafsi zaidi, wakiuliza iwapo mtu "anaguswa au haguswi na ripoti za njaa na mateso ya Wapalestina Gaza?"
Asilimia 79 ya WaIsrael waliosema hawaguswi, huku asilimia 86 ya Waarabu wa Palestina waliopo Israel waliosema wanaguswa sana au kiasi.
Netanyahu, mawaziri wake na wasemaji wake wanasisitiza kuwa Hamas, Umoja wa Mataifa, mashahidi, wafanyakazi wa misaada na serikali za kigeni wanatoa uongo kuhusu mgogoro wa kibinadamu Gaza.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwa Kiingereza kwa vyombo vya habari vya kimataifa tarehe 10 Agosti, Netanyahu alilaani ripoti za njaa Gaza. Alitaka "kuvunja uongo… wanaonyimwa chakula Gaza ni mateka wetu tu."
Kwa miaka mingi amelinganisha ukosoaji dhidi ya Israel na chuki dhidi ya Wayahudi.
Akaunti kuhusu njaa, na wanajeshi wa IDF kuwaua Wapalestina waliokuwa wakisaka chakula ambazo zimeaminiwa na kulaaniwa na washirika wa Israel kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, alisema, zinapaswa kuangaliwa kwa muktadha wa historia ndefu ya mateso ya Wayahudi barani Ulaya.
''Tuliambiwa tunaeneza uchochezi katika jamii ya Kikristo, tuliambiwa tunatia sumu visima, tuliambiwa tunaua watoto wa Kikristo kwa ajili ya damu yao.
Na kadri uongo huu ulivyoenea duniani, ulifuatiwa na mauaji ya kutisha, programu, na hatimaye mauaji ya watu kwa bomu ya nyuklia.
Leo, taifa la Kiyahudi linasingiziwa kwa njia ileile."
'Tuko katika kipindi cha mshtuko,mateka wanakufa'
Bi Peretz anailaumu vyombo vya habari vya Israel kwa kutoripoti mateso na vifo vya Wapalestina.
Mada hiyo ilifikia karibu na mazungumzo ya kitaifa ilipogusiwa kwenye kipindi maarufu cha mazungumzo cha Jumamosi usiku kilichoandaliwa na Eyal Berkovic, aliyekuwa mchezaji wa West Ham United.
Mmoja wa wageni wa kawaida alikuwa mwandishi wa habari wa Kiyahudi aitwaye Emmanuelle Elbaz-Phelps.
Walikuwa wakijadili, kama kawaida, mateso ya mateka na familia zao, na wanajeshi wa Israel waliouawa vitani Gaza.
Kisha, aliniambia, alihisi ni wajibu wake kama mwandishi wa habari kusema jambo ambalo halisemwi mara kwa mara kwenye TV ya Israel:
"Nilisema tu kwamba vita hivi pia vinaua Wapalestina wengi Gaza, ambalo ni kauli rahisi tu, bila mtazamo wa kisiasa. Hakukuwa na uvumilivu wa kulisikiliza."
Sauti zilipanda. Berkovic, anayejulikana kwa kutosema kwa upole, alijibu:
"Haitupasi kuwasikitikia watu wa Gaza, wao ni maadui zetu."
Bi Elbaz-Phelpsambaye ni mwandishi wa runinga ya Ufaransa alimjibu: "Lakini acha niseme kuwa nahuzunishwa na picha za kutisha zinazotoka huko."
Na yeye akamwambia: "Sawa, unaweza kumaliza hoja yako."
Alisema: "Hii ni picha halisi ya maoni ya Waisraeli."
"Maumivu ya Waisraeli kuhusu tarehe 7 Oktoba hayaeleweki kikamilifu nje ya Israel," asema mwandishi.
Bi Emmanuelle Elbaz-Phelps anaamini kwamba raia wa Israel bado wako ndani ya hali ya mshtuko mkubwa kutokana na mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba, jambo ambalo halijatambuliwa vya kutosha na jumuiya ya kimataifa.
"Dunia ya nje inazungumzia mateso ya watu wa Gaza jambo ambalo ni la haki lakini hakuna utambuzi wa kina juu ya kiasi ambacho watu wa Israel bado wanaishi katika hali ya mshtuko.
Hatujafikia hatua ya baada ya mshtuko.
Tuko bado ndani ya mshtuko.
Mateka wanakufa ndani ya mahandaki ya Hamas.
Raia wanaisihi serikali kupata suluhisho, wafanye makubaliano ya kuwaokoa mateka.
Ni hadi mateka watakaporudi nyumbani ndipo, labda, mchakato wa uponyaji utaweza kuanza. Maumivu ya raia wa Israeli, na jinsi wanavyoendelea kuishi kwenye kumbukumbu ya tarehe 7 Oktoba, ni jambo ambalo halieleweki kikamilifu nje ya Israel."
Mateso magumu kuvumilika
Inakadiriwa kuwa kuna takriban mateka 20 wa Kiyahudi ambao bado wako hai ndani ya Gaza.
Waisraeli kutoka mirengo yote ya kisiasa wameshtushwa sana na video za hivi karibuni zilizochapishwa na watekaji, zikionesha vijana wawili waliodhoofika sana wakiwa ndani ya mitaro ya ardhini.
Hatima ya mateka hao imekuwa msingi mkuu wa mitazamo ya Waisraeli wengi kuhusu vita.
Dahlia Scheindlin, mtaalamu wa kura za maoni ambaye amekuwa mkosoaji wa wazi wa namna Netanyahu anavyoendesha vita, anakutana nami katika "Mraba wa Mateka" karibu na makao makuu ya jeshi la Israel jijini Tel Aviv.
Tangu Oktoba 2023, eneo hilo limekuwa kitovu cha harakati za familia za mateka wanaotaka wapendwa wao waachiliwe kutoka Gaza.
"Sababu kuu inayofanya Waisraeli wengi kuendelea kuunga mkono vita ni matumaini kwamba mateka watarudishwa salama," anasema.
Akizungumzia ukosefu wa hisia kwa watu wa Gaza, anabainisha:
"Sehemu kubwa ya Waisraeli wanaamini kuwa mateso ya Wapalestina yamezidishwa au hata kutungwa na Hamas."
Anaongeza kuwa Waisraeli wengi huona kuwa tatizo ni katika namna taarifa zinavyowasilishwa:
"Kwa muda mrefu Waisraeli wamekuwa na mazoea ya kutegemea mkakati wa kuwasilisha simulizi yao kwa ulimwengu wanauita Hasbara.
Hali hii ya kulaumu ukosoaji wa Israel kwa mawasiliano duni ya kimataifa imechukua mkondo mkali wakati wa vita, hasa kuhusu shutuma za njaa Gaza.
Mrengo wa kulia kabisa unaiita hali hii kampeni ya uongo. Wanaamini hata vyombo vya habari vya Israel vinavyoanza kuonesha mateso hayo vinasaidia kueneza simulizi ya Hamas.
Lakini kwa Waisraeli wengi wa kawaida, hili ni jambo gumu sana kulikabili.
Wanalifumbia macho kwa sababu haliwastahimili kihisia.
Wako ndani ya maumivu yao ama kwa sababu ya mateka au kwa kuwa ndugu zao wapo vitani Gaza na hawawezi kukabiliana na uwezekano kwamba Israel huenda inafanya makosa makubwa."
'Ni rahisi sana kuhukumu…"
Nje ya maeneo ya wasomi na Waisraeli wasio wa kidini kama Tel Aviv na miji ya pwani ya Mediterania, mashaka kuhusu uhalali wa mwenendo wa Israel katika vita hayaonekani kwa wingi.
Katika eneo la mbali ndani ya Ukingo wa mto Jordan ama West bank, kwenye barabara ya vumbi, kuna makazi ya walowezi wa Kiyahudi yanayoitwa Esh Kodesh, sehemu ya mtandao wa walowezi wadogo waliokuwa hapo awali mabanda kwenye vilima, lakini sasa wamejenga makazi.
Aaron Katzoff, mzaliwa wa Los Angeles, Marekani na baba wa watoto saba, ameanzisha kiwanda cha kutengeneza divai na baa iitwayo Settlers inayovutia kwa mtindo wa "Magharibi ya Kale ya Marekani".
Divai yake hupewa jina la kiibada: "Unabii wa Kioevu" (liquid prophecy).
Baa ya walowezi si tu mahali pa starehe, bali pia ni kitovu cha kijamii kwa wateja wengi wa mrengo wa kulia, wanaoshikilia imani za kidini kwa dhati.
Wengi hufika kutoka maeneo ya mbali mahsusi kwa ajili ya mahali hapo.
Nilipowasili, baadhi ya wateja walikuwa wamejihami kwa silaha.
Askari mmoja, akiwa na sare zenye vumbi, alikula mkate wa nyama na kunywa divai nyekundu huku bunduki ya M-16 ikiwa mapajani mwake.
Silaha nyingine ziliwekwa nyuma ya baa.
Mwanamke mmoja alivaa bastola kiunoni juu ya gauni la maua, na vijana mezani walikuwa "wanapumzika baada ya operesheni Gaza," Aaron alieleza.
Aaron Katzoff, ambaye bado anahudumu kama afisa wa akiba wa IDF na tayari amepigana Gaza, hana mashaka kuhusu uhalali wa vita:
"Shuka kwenye mitaro Gaza. Ukae bila oksijeni, kwenye joto na unyevunyevu, ukipambana na magaidi wanaojificha nyuma ya wanawake na watoto huku wakikushambulia…
Ni rahisi sana kuketi katika chumba chenye kiyoyozi na kuwahukumu. Vita si rahisi."
Nilimuuliza kuhusu kusitisha vita, kama Waisraeli wengi wanavyotaka. Alijibu kwa utulivu:
"Wakati mwingine huwezi kufika hapo sasa hivi. Unataka kila kitu kiwe kama pepo… lakini dunia si hivyo.
Mambo huchukua muda, na ndiyo, ni jambo la kusikitisha lakini huo ndiyo uhalisia."
Kuporomoka kwa uungwaji mkono kabla ya 7 Oktoba
Kabla ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, maelfu ya Waisraeli walikuwa wakiandamana kupinga mabadiliko ya mfumo wa mahakama, wakiona kama tishio kwa demokrasia.
"Serikali hii imekuwa haipendwi hata kabla ya vita," anasema mchambuzi wa siasa Dahlia Scheindlin.
"Tofauti na nchi nyingine ambako vita huimarisha serikali, hapa kulikuwa na kuporomoka kabisa kwa uungwaji mkono."
Licha ya kuporomoka huko, Netanyahu ameweza kupata uungwaji mkono wa baadhi ya wafuasi wa mrengo wa kulia kwa kusisitiza kwamba vita haviwezi kuisha hadi Hamas ishindwe kabisa.
Hata hivyo, bado anaachwa nyuma kwenye kura za maoni, huku wapinzani wakidai anaendeleza vita ili asiondoke madarakani na kukabiliwa na uchunguzi wa kiusalama au kesi ya ufisadi inayomsubiri.
Washirika wake wenye misimamo mikali, Bezalel Smotrich na Itamar Ben-Gvir, wametishia kuivunja serikali iwapo Netanyahu atafanya makubaliano yoyote na Hamas.
Wao hawataki tu Hamas ishindwe, bali pia Gaza iunganishwe rasmi na Israel, Wapalestina wafukuzwe, na walowezi wa Kiyahudi wachukue nafasi zao.
Wakati huo huo, familia za mateka walioko Gaza wamemwomba Netanyahu afanye makubaliano ya kuwaachilia kabla hawajafariki.
Lakini waziri mkuu ameendelea kushikilia msimamo wa "vita hadi ushindi kamili" na hivi karibuni alitangaza operesheni mpya ya kijeshi.
Tangazo hilo limezua mshtuko miongoni mwa familia za mateka na kulaaniwa na washirika wengi wa kimataifa wa Israel.
Pia, limepingwa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), ambapo Mkuu wa Majeshi, Jenerali Eyal Zamir, ameripotiwa kuiambia serikali kwamba mashambulizi mapya yatawaweka mateka hatarini na kuzidisha janga la kibinadamu Gaza.
Zamir, aliyeteuliwa mwezi Machi baada ya mtangulizi wake kujiuzulu kwa tofautiana na Netanyahu, sasa anaripotiwa kuwa chini ya shinikizo la kujiuzulu.
Ripoti moja inasema:
"Amewekewa chambo cha kutimuliwa" kwa kupinga mpango wa waziri mkuu.
Mikononi mwa Mungu
Katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, nimekuwa nikisafiri baina ya pande mbili zinazogawanya Israel kuanzia kwa wanaharakati wa mrengo wa kushoto jijini Tel Aviv, wanaoandamana kimya kimya kupinga mauaji ya watoto wa Kipalestina, wakionesha kile ambacho Avrum Burg, Spika wa zamani wa Bunge, amekiita "kukata tamaa kwa kina kisaikolojia."
Na upande mwingine ukiwa na Waisraeli wanaoamini kwa dhati kuwa hatua za kijeshi dhidi ya Gaza zina haki ya kimsingi kutokana na mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba na kuendelea kwa kizuizi cha mateka.
Waziri Mkuu Netanyahu, akiwa bado anaungwa mkono na Donald Trump licha ya dalili za kuvunjika moyo, anapanga mashambulizi mapya huku akiwashutumu washirika wa Israel kwa chuki dhidi ya Wayahudi.
Kwa Wazayuni wa kidini wanaomuunga mkono, vita hivi vinaongozwa na mkono wa Mungu.
Katika Ukingo wa mto Jordan ama West bank, walowezi kama Aaron Katzoff wanaamini wanatimiza unabii, wakinywa divai kutoka kwa mizabibu waliyoikuza kwa mbinu za Kibiblia.
Kwao, waandamanaji wa Tel Aviv ni wa kale.
Sasa, mustakabali wa Israel uko mikononi mwao na mikononi mwa Mungu.
Wana uhakika: mwisho wake utakuwa mzuri.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid